UGONJWA WA BERIBERI:Sababu,dalili,matibabu,kuzuia

Maelezo ya jumla

Ugonjwa wa beriberi ni ugonjwa uletwao na ukosefu wa vitamini B1 mwilini (vitamini B1).

Nini dalili za ugonjwa wa beriberi?

Dalili za ugonjwa wa beriberi kavu (dry ) ni pamoja na:

 • Kupata shida kutembea
 • Kupoteza hisia kwenye mikono na miguu
 • Kupooza kwa miguu
 • Kuchanganyikiwa akili
 • Kupata shida kuongea
 • Maumivu
 • Macho kucheza cheza yenyewe bila sababu
 • Kuwashwa/mchonyota
 • Kutapika

Dalili za ugonjwa wa beriberi chepechepe (wet) ni pamoja na:

 • Kushtuka usiku toka usingizi kwa sababu ya kubanwa pumzi
 • Kuongezeka kwa kiwango cha mapigo ya moyo
 • Kuishiwa pumzi na kupata shida kupumua baada ya shughuli ndogo
 • Kuvimba kwa miguu

Ni nini husababisha ugonjwa wa beriberi?

Kuna aina kuu mbili:

 • Ugonjwa wa beriberi chepechepe (yenye maji) ambayo huathiri mfumo wa moyo.
 • Ugonjwa wa beriberi kavu na ”Wernicke-Korsakoff syndrome” ambayo huathiri mfumo wa neva.

Ugonjwa huu hauwapati watu kiurahisi, hii ni kwa sababu vyakula vingi vina vitamini ya kutosha. Ukila mlo wa kawaida tu,unakupatia vitamini ya thiamine ya kutosha mwilini. Siku hizi ugonjwa huu huwatokea zaidi walevi wa pombe. Kunywa pombe kwa kiasi kikubwa husababisha mtu kuwa na lishe duni, na unywaji wa pombe hufanya iwe vigumu kwa mwili kufyonza na kuhifadhi ”thiamine”.
Kuna watu wachache wanaorithi ugonjwa wa beriberi, hali hii inaitwa Beriberi ya kurithi (genetic). Watu hawa wenye beriberi ya kurithi hupoteza uwezo wa kufyonza thiamine kutoka kwenye vyakula tumboni. Hali hii hutokea polepole, na mara nyingi matatizo huanza kujitokeza katika umri wa utu uzima. Hata hivyo, kwa sababu madaktari mara nyingi hawategemei ugonjwa wa beriberi kwa mtu asiyekunywa pombe,watu hawa hawagunduliwi mapema, na kwa sababu hiyo tiba huchelewa sana.
Beriberi inaweza kumpata mtoto mdogo anayenyonya kama mwili wa mama hauna thiamine ya kutosha. Hali hii pia inaweza kuwathiri watoto wachanga ambao wanakunya maziwa mbadala (formula) ambayo hayana thiamine ya kutosha.
Mtu anayechujwa damu kwa mashine baada ya figo zake kuharibika (dialysis ) na kutumia kiwango cha juu cha madawa ya kupunguza maji mwilini ”diuretics” huongeza hatari ya kupata beriberi.

Utambuzi wa ugonjwa wa beriberi

Uchunguzi wa mwili unaweza kuonesha ishara za kushindwa kwa moyo kufanya kazi , ikiwa ni pamoja na:
Kupata shida kupumua na mishipa ya shingo ambayo imetuna na kutokeza kwa nje

 • Kupanuka kwa moyo
 • Mapafu kujaa maji
 • Mapigo ya moyo kwenda mbio
 • Kuvimba miguu yote miwili

Mtu aliye kwenye hatua za mwisho za beriberi, anaweza kuwa amechanganyikiwa au amepoteza kumbukumbu na anaweza kuwa na maono/imani za uwongo (kama dalili ya wazimu) . Mtu huyu anaweza pia kuwa na uwezo mdogo wa kuhisi mitetemo (vibrations).
Uchunguzi wa mfumo wa neva unaweza kuonesha ishara zifuatazo:

 • Mabadiliko kwenye mwendo/jinsi ya kutembea
 • Matatizo ya uratibu (Coordination problems)
 • Kupungua kwa matendohiari (reflexes)
 • Kuinama kwa kope

Vipimo vifuatavyo vinaweza kufanyika:

 • Vipimo vya damu hufanyika ili kupima kiasi cha thiamine katika damu
 • Vipimo vya mkojo ili kuona kama thiamine inatolewa kwenye mkojo

Ukiwa na ugonjwa wa beriberi ni wakati gani umwone daktari?

Ugonjwa wa beriberi ni nadra sana hapa nchini. Hata hivyo, kama unahisi chakula cha familia yako ni duni au sio mlo kamili, na wewe au watoto wana dalili za beriber, mwone mtoa huduma ya afya.

Uchaguzi wa matibabu

Kuiongeza mwilini thiamine ambayo mwili wako unakosa ndio lengo la matibabu. Hili linafanyika kwa kutumia virutubisho vyenye thiamine. Virutubisho vya thiamine hutolewa kwa njia ya vidonge au sindano.
Aina nyingine za vitamini pia zinaweza kupendekezwa.
Vipimo vya damu vinaweza kufanywa baada ya kupewa virutubisho vya thiamine ili kuona matokeo baada ya matibabu.

ugonjwa wa beriberiKuzuia

Kula chakula bora ambacho kina thiamine na vitamini nyingine kutazuia beriberi. Mama anayenyonyesha,  anapaswa kula mlo wenye vitamini zote na kuhakikisha kuwa maziwa mbadala anayotumia mtoto mchanga yana thiamine yakutosha.
Watu wanao kunywa sana pombe, wanapaswa kujaribu kupunguza kiasi au kuacha kabisa kunywa pombe, na kutumia vitamini B ili kuhakikisha mwili wao unanyonya na kuhifadhi vyema thiamine.

Nini cha kutarajia ?

Mara nyingi mgonjwa wa beriberi asipopata matibabu anaweza kufa. Lakini akipata matibabu mapema, dalili zake huondoka haraka sana.
Mara nyingi, uharibifu kwenye moyo unaosababishwa na beriberi unaweza kurekebika, na mgonjwa kupona kabisa. Lakini kama moyo utakua umefikia hatua ya kushindwa kufanya kazi (heart failure) matarajio huwa mabaya.
Uharibifu kwenye mfumo wa neva pia unaweza kurekebika kama utagunduliwa mapema. Kama hautagunduliwa mapema, dalili zingine (kama vile kupoteza kumbukumbu) zinaweza kubaki hata baada ya matibabu.

Matatizo yanayoweza kutokea

Vyanzo

https://medlineplus.gov/ency/article/000339.htm

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi