Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Mabusha (hydrocele) ni hali inayosababishwa na kujaa kwa maji katikati ya tabaka mbili za utando unaozunguka korodani na mrija unaobeba manii kutoka kwenye korodani kwenda nje.
Je! Nini dalili ya mabusha?
Kwa kawaida busha halisababishi maumivu yoyote, korodani huvimba na kuwa kama puto lililojaa maji. Busha linaweza kutokea kwa korodani moja au zote mbili.
Ni nini husababisha mabusha?
Ni jambo la kawaida sana kwa watoto wachanga kuzaliwa na mabusha. Mtoto anapokua tumboni mwa mama wakati wa ujauzito, korodani zake huwa tumboni, na huanza kushuka taratibu kupitia upenyo mdogo kwenye kinena mpaka kwenye mapumbu. Busha hutokea kama upenyo huu mdogo unaoruhusu korodani kushuka kwenye pumbu utashindwa kujifunga. Kwa sababu upenyo huu unashindwa kujifunga, maji hushuka kutoka tumboni na kujaa kwenye pumbu. Hii husababisha pumbu kukua na kuongeza ukubwa. Mabusha kwa watoto mara nyingi huisha yenyewe baada ya miezi kadhaa, lakini mwonekano wake huwatia wasiwasi sana wazazi. Kwa mara chache busha na ngiri hutokea kwa pamoja.
Mabusha yanaweza pia kusababishwa na kuvimba au jeraha kwenye korodani au kifuko cha kutunzia manii (epididymis). Inaweza pia kusababishwa na damu au maji kuziba mrija wa kubeba manii (spermatic cord). Aina hii ya busha inawapata zaidi wanaume watu wazima.
Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata mabusha?
Sehemu kubwa ya watu wenye mabusha huzaliwa nayo. Vinginevyo, waanaothirika zaidi ni watu walio na umri zaidi ya miaka 40.
Sababu zinazoongeza hatari ya kupata mabusha ni:
- Jeraha kwenye pumbu
- Maambukizi, hii ni pamoja na magonjwa ya zinaa
- Tiba mionzi
Wakati gani utafute matibabu ya haraka?
Mwone mtoa huduma wa afya kama una dalili za mabusha. Ni muhimu kufanya hivi ili kuondoa uwezekano wa kuwepo uvimbe mwingine kwenye korodani.
Ni dharura ya kimatibau kama una maumivu makali kwenye korodani au pumbu zako. Kama pumbu zimevimba na kuna maumivu tafuta huduma ya kimatibabu mapema iwezekanavyo.
Utambuzi wa mabusha
Wakati wa uchunguzi wa mwili, daktari hutarajia kuona mapumbu yaliyovimba lakini hayaumi. Wakati mwingine anaweza asizihisi korodani sababu ya majimaji mengi yanayozizunguka. Ukubwa na wingi wa maji mara nyingine unaweza kuongezeka na kupungua kwa kubonyeza na kuachia tumbo au pumbu.
Kama wingi wa maji unaongezeka na kupungua, kuna uwezekano mkubwa kuwa busha hilo limetokea sambamba na Mshipa wa ngiri.
Busha linaweza kutambuliwa kwa urahisi sana, kwa kumulika kurunzi (tochi) kwenye upande mmoja wa pumbu lililojaa maji, mwanga utapita na kutokea upande wa pili kwa sababu busha huwa limejaa maji pekee.
Ultrasound ya pumbu inaweza kufanyika ili kuthibitisha utambuzi.
Uchaguzi wa matibabu
Mara nyingi mabusha si hatari, na mara nyingi hutibiwa pale tu yanapoanza kusababisha shida, kuleta aibu, au kama yatakuwa makubwa sana hata kutishia kuharibu tishu zingine za korodani.
Chaguo moja wapo ni kuondoa maji yaliyomo kwenye mapumbu kwa kutumia sindano, mchakato huu huitwa aspiration. Hata hivyo, kwa ujumla upasuaji hupendelewa zaidi. Aspiration inaweza kuwa chaguo bora kwa watu ambao kwa namna moja au nyingine hawawezi kufanyiwa upasuaji.
Unaweza kuchomwa dawa ya kusababisha kovu kutengenezeka (sclerosing medication) ili kuziba upenyo unaoleta tatizo hili ili maji ya busha yasirudi tena baada ya aspiration.
Mabusha yanayoambatana na Ngiri yanapaswa kutibiwa kwa upasuaji mapema iwezekanavyo. Mabusha yasiyoisha yenyewe baada ya miezi kadhaa yanapaswa kutathminiwa na ikibidi upasuaji ufanyike. Aina ya upasuaji inayoitwa hydrocelectomy hufanyika ili kutibu mabusha.
Nini cha kutarajia ukiwa na mabusha?
Busha la kawaida huisha lenyewe bila upasuaji. Ikiwa ni muhimu ufanyiwe upasuaji, Â daktari aliyebobea atakufanyia upasuaji na matokeo yake huwa ni mazuri sana.
Matatizo yanayoweza kutokea
Matatizo yanaweza kutokana na matibabu ya busha.
Hatari zinazohusiana na upasuaji wa busha ni pamoja na:
- Madonge ya damu
- Maambukizi
- Kuumizwa au kuharibika kwa viungo vingine vilivyo kwenye mapumbu
Hatari zinazohusiana na aspiration na sclerosing ni pamoja na:
- Maambukizi
- Makovu makubwa
- Maumivu madogo au ya kadiri kwenye eneo la pumbu
- Busha linaweza kurudi tena
Kuzuia
Hakuna njia ya uhakika ya kuzuia mabusha kwa watu wazima au kwa wavulana wachanga. Kuepuka majeraha kwenye mapumbu kwa watu wazima kunaweza kupunguza uwezekano wa kupata Busha.
Leave feedback about this