Chakula cha nyongeza kwa mtoto baada ya miezi 6

Ulishaji wa chakula cha nyongeza

Ulishaji wa chakula cha nyongeza ni kumlisha mtoto vyakula au vinywaji vingine zaidi ya maziwa ya mama pale mtoto anapotimiza umri wa miezi sita. Vyakula hivi hujulikana kama vyakula vya nyongeza kwa sababu ni nyongeza kwa maziwa ya mama au mengine.

 • Mahitaji yake ya nishati lishe na virutubishi yameongezeka na maziwa ya mama pekee hayawezi kutosheleza mahitaji hayo.
 • Kuanzisha ulishaji wa vyakula vya nyongeza kabla ya umri wa miezi 6 kunaweza kusababisha kuongezeka kwa uwezekano wa mtoto kupata maambukizi hususani kuhara.
 • Kiumri wanakuwa tayari na uwezo wa kula vyakula vingine

Katika kipindi hiki maziwa ya mama bado yanaendelea kuwa chakula muhimu kwa mtoto hadi anapotimiza umri wa miaka miwili au zaidi. Kipindi hiki ni cha muhimu sana kwa afya, ukuaji na maendeleo ya mtoto na ni kipindi ambacho watoto wengi hupatwa na matatizo ya utapiamlo endapo hawatapatiwa chakula kilicho na ubora na cha kutosha kwa wakati unaofaa.

Vyakula vya nyongeza viwe vya kutosha na vyenye virutubishi vingi ili kumuwezesha mtoto kukua kimwili na kiakili kikamilifu. Maziwa ya mama huendela kuwa muhimu kwani huchangia kwa kiasi kikubwa mahitaji ya kilishe ya mtoto – ikiwa ni pamoja na vitamin na madini.

Hata hivyo, kama mtoto hanyonyi maziwa ya mama ni muhimu kumpatia maziwa ya aina nyingine hadi atimize umri wa miaka miwili au zaidi. Ni vigumu sana kutosheleza mahitaji ya kilishe ya mtoto chini ya umri wa miaka miwili kwa kutumia vyakula vya nyongeza pekee bila maziwa au aina nyingine ya chakula cha asili ya wanyama.mlo kwa mtoto

Taratibu za Ulishaji Vyakula vya Nyongeza kwa Mtoto Anayenyonyeshwa

Shirika la Afya Duniani linapendekeza kufuata taratibu zifuatazo za ulishaji watoto vyakula vya nyongeza:

 • Nyonyesha mtoto maziwa ya mama pekee hadi atimize umri wa miezi 6, na anza kumpa vyakula vya nyongeza anapokamilisha umri wa miezi 6 na aendelee kunyonya.
 • Endelea kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama kila anapohitaji hadi anapotimiza umri wa miaka 2 au zaidi.
 • Mtoto anapotimiza umri wa miezi 6 anza kumpa kiasi kidogo cha chakula, na ongeza kiasi cha chakula kadri anavyoendelea kukua, na endelea kumnyonyesha maziwa ya mama mara nyingi.
 • Zingatia taratibu za ulishaji shirikishi kwa kumlisha mtoto kwa uvumilivu na akiwa na furaha (epuka kumlazimisha kula chakula).
 • Zingatia usafi na usalama wa chakula wakati wa kutayarisha, kuhifadhi, na kumlisha mtoto.
 • Ongeza ugumu wa chakula taratibu pamoja na kumpa vyakula vya mchanganyiko kadiri anavyoongezeka umri, ukizingatia mahitaji yake na uwezo wake wa kula.
 • Ongeza idadi ya milo unayompa mtoto kadiri anavyoongezeka umri.
 • Mlishe vyakula vya mchanganyiko vyenye virutubishi kwa wingi ili kuhakikisha kuwa vinakidhi mahitaji yake.
 • Ongeza virutubishi vya vitamini na madini kwenye chakula cha mtoto iwapo vinapatikana
 • Mpe mtoto vinywaji na vyakula laini kwa wingi pamoja na kuendelea kumnyonyesha mara nyingi zaidi wakati wa ugonjwa. Baada ya kupona, mpe vyakula mara nyingi zaidi na mhamasishe ale chakula kingi zaidi.

Mlo Mchanganyiko Unaokidhi Mahitaji

Mlo mchanganyiko unaokidhi mahitaji unatafsiriwa kama mlo uliondaliwa kwa kutumia angalau vyakula kutoka kwenye makundi manne. Mlo mchanganyiko unaokidhi mahitaji ni muhimu kwa ajili ya ukuaji na maendeleo ya mtoto. Tathmini ya ulishaji wa mlo mchanganyiko unaokidhi mahitaji ya mtoto husaidia kutoa mapendekezo kuhusu ulishaji sahihi wa vyakula vya nyongeza. Vyakula vya kuandaa mlo mchanganyiko unaokidhi mahitaji ya mtoto vinayoweza kutoka katika makundi yafuatayo:

 • Vyakula vya asili ya nafaka, mizizi na ndizi za kupika
 • Vyakula vya asili ya wanyama na jamii ya mikunde
 • Matunda
 • Mbogamboga
 • Sukari, asali na mafuta (ongeza kwenye chakula kwa kiasi kidogo)

Vyakula vya Nyongeza na Nyongeza ya Vitamini na Madini

Vitamini na madini ya nyongeza kwa ajili ya matumizi ya mara moja yanaweza kuongezwa kwenye chakula cha nyongeza cha mtoto kilicho tayari kuliwa nyumbani, shuleni au sehemu nyingine. Vitamini na madini ya nyongeza huweza kuongezwa kwenye chakula cha mtoto bila kuathiri taratibu yake ya ulaji.

Jamii ambazo kiwango cha upungufu wa damu kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5 ni asilimia 20 au zaidi, Shirika la Afya Duniani linapendekeza kuongeza virutubishi kwenye chakula cha mtoto nyumbani hususani kwa watoto wadogo wenye umri wa miezi 6–23 ili kuboresha kiwango cha madini chuma mwilini mwao na kupunguza tatizo la upungufu wa damu.

Vyakula vya Nyongeza – Chakula Gani Kinafaa na Kwanini?

Vyakula vya nyongeza vinavyopaswa kulisha watoto baada ya kutimiza umri wa miezi 6 ni pamoja na:

 • Maziwa, bidhaa za maziwa – zenye madini ya chokaa kwa wingi
 • Vyakula vikuu, vinavyopatia mwili nishati lishe na utomwili
 • Vyakula vya asili ya wanyama pamoja na samaki – kwa ajili ya kupata vitamini A, madini chuma na utomwili
 • Mboga za majani zenye rangi ya kijani/njano – zenye vitamini A, na vitamini C kwa wingi
 • Matunda – yenye vitamini A na C kwa wingi

Vyakula vingine vya nyongeza anavyopaswa kupewa mtoto ni pamoja na:

 • Mbegu za mafuta – zenye nishati lishe na utomwili
 • Mikunde – inayotupatia utomwili
 • Mafuta – yanayotupatia nishati lishe na asidi za mafuta

Watoto wadogo wanahitaji vyakula vyenye nishati lishe na virutubishi kwa wingi. Uji ni chakula kinachotumiwa zaidi na watoto wachanga na wadogo, hata hivyo uji una kiasi kidogo cha nishati lishe na virutubishi vingine hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya mtoto.

Wakati wa mapishi, unga unaotumika kuandaa uji hufyonza maji mengi, na hivyo kuwa na uzito mkubwa ambao mtoto anaweza kushindwa kula. Endapo maji yataongezwa ili kulainisha uji mzito uwe mwepesi kwa lengo la kumfanya mtoto aweze kula, kiasi cha nishati na virutubishi hupungua zaidi.

Mtoto atahitaji kunywa uji mwingi ulio laini ili kukidhi mahitaji yake ya nishati na virutubishi, lakini kutokana na kuwa na tumbo dogo inakuwa vigumu kwake kula kiasi hicho kikubwa cha uji.

Mbinu za kuongeza nishati lishe na virutubishi kwenye uji na kumfanya mtoto aweze kula kwa urahisi ni pamoja na:

 • Kuongeza vyakula vyenye nishati lishe kwa wingi (mfano mafuta, jibini, samli) na kuongeza vyakula vyenye virutubishi vingi (kama vile unga wa karanga, mikunde, au mbegu za alizeti) kwenye uji
 • Kutengeneza uji kwa kutumia unga wa nafaka zilizooteshwa na kuchachushwa

Watoto wachanga wanaweza kupewa vitafunwa kama vile:

 • Matunda– embe, papai, ndizi, na parachichi
 • Mayai ya kuchemsha
 • Chapati au mkate na karanga zilizopondwa
 • Vipande vidogo vya mihogo iliyochemshwa, ndizi au magimbi
 • Mtindi na juisi ya matunda halisi

Mambo mengine ya kuzingatia katika ulishaji watoto vyakula vya nyongeza

Zingatia ugumu au ulaini wa chakula cha mtoto:

 • Ugumu au ulaini wa chakula cha mtoto hutegemea umri wake
 • Unapomwanzishia mtoto chakula cha nyongeza anza kumpa chakula laini
 • Kadri anavyoendelea kukua ongeza ugumu wa chakula ili apate virutubishi vya kutosha.
 • Chakula kisiwe majimaji au chepesi kwani kitakuwa na virutubishi kidogo visivyokidhi mahitaji ya mtoto.

Zingatia kiasi na idadi ya milo anayopewa mtotochakula cha nyongeza

 • Ongeza kiasi na idadi ya milo anayopewa mtoto kulingana na umri wake
 • Tumbo la mtoto ni dogo kwa hiyo anahitaji kula mara nyingi zaidi ili kukidhi mahitaji yake ya kilishe

Zingatia mchanganyiko wa makundi ya vyakula na aina mbalimbali ya vyakula

 • Ni muhimu kumpa mtoto mlo wenye vyakula kutoka makundi yote ya vyakula ili apate virutubishi vyote vinavyohitajika katika kufanya kazi mwilini.

Mlo wa mtoto unapokosa chakula kutoka katika mojawapo ya makundi haya inamaanisha kwamba mtoto huyo atakosa virutubishi muhimu kwa ajili ya afya yake, na hivyo anaweza kupata utapiamlo

Madhara ya kumuanzishia mtoto chakula cha nyongeza mapema

Endapo mtoto ataanzishiwa chakula cha nyongeza kabla hajatimiza umri wa miezi 6 madhara yafuatayo yanaweza kutokea:

 • Kiasi cha maziwa ya mama hupungua kwa kuwa mtoto atakuwa ameshiba vyakula vingine na hivyo kumfanya anyonye mara chache au ashindwe kunyonya. Kama mtoto hanyonyi mara kwa mara, kiasi cha maziwa ya mama yanayotengenezwa na mwili hupungua.
 • Chakula cha nyongeza huchukua nafasi ya maziwa ya mama ambayo yana virutubishi vingi ambavyo ni muhimu kwa ukuuaji na maendeleo ya mtoto.
 • Chakula anachokula mtoto hakiwezi kumeng’enywa ipasavyo tumboni kwa sababu mfumo wa chakula wa mtoto haujakomaa. Hivyo, mtoto anaweza akawa ameshiba lakini chakula alichokula hakiwezi kumeng’enywa kikamilifu hivyo hapati virutubishi vya kutosha. Katika hali hii inawezekana mtoto akapata utapiamlo
 • Mtoto anaweza kupata maradhi mara kwa mara kutokana na kupungua kwa kinga mwili zinazopatikana katika maziwa ya mama. Pia mtoto huweza kuhara kutokana na mfumo wake wa chakula kushindwa kumeng ‘enya chakula kikamilifu kwa kuwa bado ni mchanga.

Athari za kuchelewa kumuanzishia mtoto vyakula vya nyongeza

 • Mtoto hapati virutubishi vya kutosheleza mahitaji yake, hivyo hupunguza kasi ya ukuaji na maendeleo yake.
 • Mtoto atakuwa kwenye hatari ya kupata utapiamlo kwa kuwa maziwa ya mama pekee hayakidhi mahitaji yake kilishe kwa ukuaji na maendeleo kikamilifu.
 • Mtoto anaweza kuwa na tatizo la kujifunza kula chakula cha nyongeza au kukataa chakula na kupendelea kunyonya tu, hivyo kumuweka katika hatari ya kupata utapiamlo

Vyanzo

https://www.tfnc.go.tz/publications/9

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi