Lishe

UGONJWA WA KISUKARI: Mlo/Chakula/Ulaji unaofaa

kisukari

Last Updated on October 12, 2023 by Dr Mniko

Ugonjwa wa kisukari ni nini?

Ugonjwa wa kisukari ni hali ambayo hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu inayotokana na kongosho linaposhindwa kutengeneza kichocheo cha insulini au insulini iliyopo katika damu inaposhindwa kufanya kazi kwa ufanisi. Kichocheo cha insulini ndicho kinachodhibiti kiwango cha sukari katika damu. Kichocheo hiki ni muhimu sana katika kufanya sukari iweze kutumika mwilini ili kupata nishati-lishe. Ugonjwa wa kisukari unapompata mtu huwa ni wa kudumu, hivyo anahitaji kufuata matibabu na maelekezo atakayopewa na mtoa huduma ya afya kwa maisha yake yote.

kisukariAina za ugonjwa wa kisukar

Kuna aina mbili kuu za ugonjwa wa kisukari ambazo ni kisukari kinachotegemea insulini (type 1 diabetes) na kile kisichotegemea insulini (type 2 diabetes). Kuna aina nyingine ya kisukari ambayo huweza kutokea wakati wa ujauzito (gestational diabetes). ­

 • Kisukari kinachotegemea insulini (Ugonjwa wa kisukari aina ya 1) ambacho huwapata zaidi watoto na wenye umri chini ya miaka 35. Katika aina hii ya kisukari, seli za kongosho zinazotengeneza insulini huwa zimeharibika na hivyo kusababisha upungufu au ukosefu wa insulini mwilini. ­
 • Ugonjwa wa kisukari kisichotegemea insulini (Ugonjwa wa kisukari aina ya 2) ambacho huwapata zaidi watu wenye umri kuanzia miaka 45 na kuendelea. Katika aina hii ya kisukari, insulini ya kutosha inaweza ikatengenezwa katika kongosho lakini haifanyi kazi na hivyo mwili hushindwa kutumia sukari kwa ufanisi. ­
 • Kisukari cha mimba (ugonjwa wa kisukari wakati wa ujauzito) ni aina ya kisukari kinachotokea kwa baadhi ya wanawake wakati wa ujauzito. Hali ya ujauzito husababisha ongezeko la baadhi ya vichocheo kama Progesterone, Estrogen, na free Cortisol, ambavyo huongeza kiwango cha sukari katika damu, wakati huo huo kichocheo cha Human Placental Lactogen huzuia insulini kufanya kazi kwa ufanisi hivyo kusababisha kiwango cha sukari kuongezeka katika damu. Vichocheo hivyo huongezeka kadiri mimba inavyokua. Mwili unaposhindwa kutengeneza insulini ya kutosha kupambana na ongezeko la sukari katika damu kisukari cha mimba hutokea. Mara nyingi hutokea mimba ikiwa na umri wa miezi 5 au zaidi na kwa kawaida huisha wiki 6 baada ya mwanamke kujifungua.

Viashiria hatarishi vya kupata ugonjwa wa kisukari

Viashiria hivi huweza kuwekwa katika makundi kutegemeana na aina ya kisukari:

 • Kisukari kinachotegemea insulini ­(ugonjwa wa kisukari aina ya 1)
  • Kurithi katika familia; ­
  • Magonjwa ya kongosho (kama saratani au uambukizo) ambayo huweza kuua seli zinazotengeneza kichocheo cha insulini; ­
  • Mtoto kupewa maziwa mbadala (ya kopo au ya wanyama) au kumnyonyesha mtoto kwa muda mfupi; ­
  • Mtoto akizaliwa na uzito mkubwa kupita kiasi; na ­
  • Unene au uzito mkubwa utotoni.
 • Kisukari kisichotegemea insulini ­(Ugonjwa wa kisukari aina 2)
  • Uzito uliozidi na unene uliokithiri; ­
  • Shinikizo kubwa la damu; ­
  • Mtindo wa maisha usiofaa hususan kutokufanya mazoezi, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi na uvutaji sigara na bidhaa nyingine za tumbaku; ­
  • Kuwepo kwa historia ya kisukari katika familia; na ­
  • Umri zaidi ya miaka 45.
  • Kutokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha, vijana wengi wamekuwa na uzito mkubwa pamoja na kutofanya mazoezi hali ambayo inafanya tatizo hili kuongezeka katika umri mdogo.
 • Kisukari cha mimba (Ugonjwa wa kisukari wakati wa ujauzito)
  • Kuwepo na historia ya kuwa na kisukari katika familia; ­
  • Kuwahi kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa; ­
  • Mimba kuharibika mara kwa mara; ­
  • Historia ya kisukari cha mimba; ­
  • Mkojo kuwa na sukari mara kwa mara; ­
  • Kuzaa mtoto mfu; ­
  • Uzito au unene uliokithiri; ­
  • Shinikizo kubwa la damu la muda mrefu; ­
  • Umri zaidi ya miaka 35.

Dalili za ugonjwa wa kisukari

Dalili za ugonjwa wa kisukari ni pamoja na: ­

 • Kukojoa mara kwa mara; ­
 • Kuhisi kiu sana; ­ Kuhisi njaa sana; ­
 • Kuhisi uchovu wa mwili na kukosa nguvu bila ya kufanya kazi; ­
 • Kupungua kwa uzito wa mwili, na kuwa mdhaifu; ­
 • Kutoona vizuri; ­
 • Kuhisi kizunguzungu; ­
 • Kuwa na maambukizi ya ngozi na vidonda visivyopona haraka; na ­
 • Baadhi ya viungo vya mwili kama vidole vya miguu na mikono kufa ganzi.

Mapendekezo ya Ulaji kwa Mgonjwa wa Kisukari

Ugonjwa wa kisukari

Kumbuka kuwa mgonjwa wa kisukari hahitaji kula chakula maalum bali anashauriwa kuzingatia yafuatayo: Ni muhimu kufuata kanuni za ulaji unaofaa:

 1. Kula mlo kamili (angalau mara 3 kwa siku) kwa kuzingatia muda aliojipangia kwani haishauriwi kukaa na njaa kwa muda mrefu. Hii itamsaidia mgonjwa kuweza kudhibiti kiwango cha sukari katika damu na kiasi cha chakula kwani anapokuwa na njaa kali huweza kuongeza kiasi cha chakula anachokula.
 2. Kudhibiti kiasi cha nishati – lishe katika chakula. Kiasi kitegemee mahitaji ya mtu binafsi.
 3. Kuongeza ulaji wa vyakula vyenye makapi – mlo kwa wingi. Kiasi kikubwa cha nishati – lishe katika mlo kitokane na vyakula vyenye makapimlo kwa wingi ambavyo huyeyushwa na kufyonzwa na mwili taratibu (simple vs complex carbohydrates), na hivyo kasi ya kuongezeka sukari katika damu hupungua.
 4. Kupunguza kiasi cha mafuta. Epuka mafuta yenye asili ya wanyama na punguza kiasi cha mafuta mengine. Mafuta yanapaswa kuchangia asilimia 35 ya nishati – lishe inayohitajika kwa siku.
 5. Kupanga utaratibu wa kula chakula na matumizi ya dawa. Mgonjwa anayetumia insulini au dawa za kushusha sukari katika damu (oral hypoglycaemic agents), ni muhimu kupanga utaratibu maalum wa kula na kumeza dawa ili kuzuia kupungua kwa sukari katika damu. Aepuke kukaa kwa muda mrefu bila kula chakula.
 6. Kupunguza uzito kama umezidi au dhibiti uzito wa mwili. Ni muhimu kuwa na uzito unaoshauriwa kulingana na urefu wake.
 7. Kula vyakula vya aina mbalimbali, badili hata vile ambavyo viko kwenye kundi moja la chakula. Virutubishi vilivyo kwenye vyakula mbalimbali hutofautiana kwa kiasi na ubora.
 8. Kula mbogamboga kwa wingi katika kila mlo. Chagua mbogamboga ambazo hazina kabohaidreti kwa wingi, mfano mboga za majani, nyanya, matango na saladi.
 9. Kula tunda katika kila mlo. Kula kipande cha kadiri ambacho ni sawa na ngumi yako; mfano saizi ya kati ya chungwa, embe, kipande cha papai, tikiti-maji, au nanasi. Kula matunda kwa kiasi, kwa mfano kipande cha papai, embe au ndizi moja kwa kila mlo. Ni vyema kula tunda zima ambalo halijamenywa kama inawezekana na sio juisi
 10. Epuka kunywa pombe. Pia haishauriwi kunywa pombe kali kwani huweza kuleta madhara kwenye ini. Usinywe pombe kabla ya kula chakula kwani huweza kusababisha damu sukatiti.
 11. Epuka sukari na vyakula vyenye sukari nyingi kama soda, keki, biskuti, pipi na asali. Asilimia 80 ya asali in sukari

Vyanzo

https://www.tfnc.go.tz/publications/9

Leave feedback about this

 • Quality
 • Price
 • Service

PROS

+
Add Field

CONS

+
Add Field
Choose Image
Choose Video
X