CHUNUSI

 • August 13, 2020
 • 1 Like
 • 138 Views
 • 0 Comments

Maelezo ya jumla

Chunusi (acne) ni hali ya muda mrefu ya ngozi ambayo husababisha kutokea kwa vipele na madoa meupe na/au meusi.

Je, nini dalili za chunusi?

Chunusi kwa kawaida huto kea kwenye uso na mabega, lakini pia zinaweza kutokea kwenye kiwiliwili, mikono, miguu, na matako.    

 • Madoa meusi kwenye ngozi
 • Madoa meupe kwenye ngozi
 • Upele (uvimbe mwekundu)    
 • Kutatuta kwa sehemu ya ngozi yenye upele.
 • Kuwepo kwa uvimbe mdogo uliojaa maji (Cyst).
 • Malengelenge
 • Wekundu kuzunguka sehemu chunusi ilipojitokeza.
 • Kutokea kwa makovu kwenye ngozi   

Nini husababisha chunusi?

Chunusi hutokea kwa sababu ya kuziba kwa matundu/vishimo vidogo vilivyo kwenye ngozi.

 • Kila tundu huruhusu kinyweleo kuchomoza. Kinyweleo huundwa kwa unywele na tezi inayotengeneza mafuta. Mafuta haya yanayotengenezwa na tezi husaidia kusafisha ngozi na kusaidia kuondoa seli za ngozi za kale/zilizokufa.    
 • Tezi  zinapozalisha mafuta mengi zaidi, matundu ya ngozi huziba. Uchafu, bakteria, na seli zinazosababisha uvimbe hujaa hapo na kusababisha chunusi. Kuziba huku kwa vinyweleo huitwa “comedone” kitaalamu.    
 • Sehemu ya juu ya kizibo kilichoziba vinyweleo ,inaweza kuwa nyeupe na kusababisha madoa meupe au nyeusi na kusababisha madoa meusi kwenye ngozi ya mgonjwa.
 • Ikiwa uvimbe ni mkali na umechimba ngozi yako, upele unaweza kukua na kutengeneza uvimbe mdogo unaouma sana.

Chunusi ni tatizo la kuvimba, na sio tatizo linalosababishwa na bakteria. Mara nyingi chunusi huwapata watu waliotoka kwenye familia yenye historia ya kuwa na chunusi,mtu aliyetoka kwenye familia yenye chunusi nyingi  huwa na uwezekano pia wa kupata chunusi,kutokea kwa chunusi huchochewa na ;

 • Mabadiliko ya homoni kipindi cha hedhi, ujauzito, dawa za kupanga uzazi, au msongo wa mawazo.
 • Kutumia dawa za nywele na vipodozi vyenye shahamu (greasy) au mafuta mengi.   
 • Kutumia baadhi ya dawa kama vile steroids, testosterone, estrogen, na phenytoin   
 • Kiwango kikubwa cha unyevu na kutokwa jasho sana.

Licha ya imani maarufu ya kwamba chokoleti, karanga, na vyakula vyenye mafuta husababishia chunusi, utafiti haujathibitishi wazo hili. Lakini chakula chenye sukari  nyingi  ya viwandani inaweza kuhusiana na chunusi.

Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata chunusi?

Chunusi kwa kawaida huwatokea vijana walio kwenye balehe, lakini inaweza kumtokea mtu katika umri wowote, hata kwa mtoto mdogo sana.Vijana watatu kati ya wanne walio kwenye balehe wana chunusi. Mabadiliko ya homoni yanaweza kusababisha mafuta kuongezeka kwenye ngozi. Hata hivyo, watu wenye umri wa miaka 30 na 40 wanaweza kuwa na chunusi pia.

Utambuzi

Daktari wako anaweza kutambua kuwa una chunusi kwa kuangalia mwonekano wa ngozi yako. Vipimo mara nyingi havihitajiki.

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Mwone daktari wako au daktari bingwa wa ngozi (dermatologist) ikiwa:   

 • Umejaribu njia za kawaida za kujisaidia mwenyewe(self-care) na dawa za kununua duka la dawa muhimu bila nafuu kwa muda wa mwezi mzima au zaidi.
 • Chunusi zako ni kali sana (kwa mfano, kama kuna wekundu kuzunguka kipele au kuna uvimbe uliojaa maji)    
 • Chunusi zako zinazidi kuwa mbaya zaidi
 • Unapata makovu pale chunusi inapopona.

Mwone daktari/mtoa huduma ya afya ikiwa mtoto wako mdogo ana chunusi amabazo hazijapona ndani ya miezi mitatu.

Uchaguzi wa matibabu

JINSI YA KUJITUNZA MWENYEWE (SELF-CARE ) UKIWA NA CHUNUSI.

Ukifanya mambo yafuatayo yanaweza kusaidia;

 • Safisha ngozi yako polepole kwa sabuni.

Ondoa uchafu au vipodozi vyote. Osha mara moja au mbili kwa siku, ikiwa ni pamoja na baada ya kufanya mazoezi. Hata hivyo, jaribu kuepuka kusugua sana au kuosha ngozi mara nyingi.

 • Osha kwa Shampuu nywele zako kila siku, hasa ikiwa zina mafuta mengi. Chana nywele zako au zivutie nyuma ,ili kuziondoa usoni.

Usijaribu kufanya yafuatayo unapokua na chunusi;

 • Jitahidi usifinye, kukwaruza, kuminya,kutoboa, au kusugua vipele. Jitahidi ,ingawa vinashawishi kuvikuna,hii ni kwa sababu kuvikuna kunaweza kusababisha maambukizi kwenye ngozi na makovu.    
 • Epuka kuvaa mikanda/au vitu vinavyobana na kofia.
 • Jitahidi kuepuka kushika/kugusa uso wako kwa mikono yako au vidole.    
 • Epuka cream au vipodozi vyenye shahamu(greasy) na mafuta mengi. Ondoa urembo na vipodozi vyote wakati wa usiku. Tafuta na jaribu kutumia vipodozi vilivyotengezwa kwa maji zaidi(water-based).

Ikiwa hatua hizi zote hazijakusaidia , jaribu dawa za chunusi. Mara nyingi bidhaa/dawa  hizi hupakwa moja kwa moja kwenye ngozi .    

 • zinaweza kuwa zimetengenezwa kwa benzoyl peroxide, sulfur, resorcinol, au salicylic acid.    
 • zinafanya kazi kwa kuua bakteria, kukausha mafuta ya ngozi, au kwa kusababisha safu ya juu ya ngozi yako kubanduka.    
 • Zinaweza kusababisha wekundu au kubanduka kwa ngozi.

Kiwango kidogo cha miali ya jua kinaweza kuleta nafuu kidogo. Hata hivyo, miali na mwangaza wa jua haipendekezwi kwa sababu huongeza hatari ya kupata saratani ya ngozi.

DAWA ZINAZOTOLEWA KWA MAAGIZO YA DAKTARI.

Ikiwa bado chunusi ni tatizo kwako, mtoa huduma ya afya anaweza kuagiza upewe dawa kali zaidi na lakini pia anaweza kujadiliana na wewe kuhusu njia nyingine.

Antibiotics zinaweza kusaidia kutibu chunusi kwa watu fulani fulani:    

 • Dawa za kumeza kama vile tetracycline, doxycycline, minocycline, erythromycin, trimethoprim, na amoxicillin     
 • Dawa za kupaka kwenye ngozi kama vile clindamycin, erythromycin, au dapsone

Daktari anaweza kuagiza upewe creams au jeli za kupaka kwenye ngozi  kama vile:   

 • Retinoic acid cream or gel (tretinoin, Retin-A)
 • Prescription formulas of benzoyl peroxide, sulfur, resorcinol, or salicylic acid
 • Topical azelaic acid

Kwa wanawake ambao chunusi zao husababishwa au huongezeka zaidi kwa sababu ya homoni:   

 • Kidonge kinachoitwa spironolactone kinaweza kusaidia    
 • Vidonge vya kupanga uzazi vinaweza kusaidia katika baadhi ya kesi, ingawa kwa wengine vinaweza kufanya chunusi kuwa mbaya zaidi.

Operesheni ndogo au tiba ya mbadala inaweza pia kuwa na manufaa:   

 • Matibabu ya kutumia leza (laser)  yanayoitwa photodynamic therapy, leza ni chombo cha kukuza na kushadidisha miale kuelekea upande mmoja,na hutumia miale hiyo kutibu chunusi.   
 • Daktari wako anaweza pia kupendekeza kumenya na kuitoa sehemu ya juu ya ngozi yako kwa kutumia kemikali, anaweza pia kuondoa makovu (dermabrasion).

Watu ambao wana chunusi zenye majimaji ndani (cystic acne) wanaweza kujaribu dawa inayoitwa isotretinoin (Accutane). itahitajika kuangaliwa kwa karibu wakati unatumia dawa hii kwa sababu ya madhara yake.

Wanawake wajawazito HAWAPASWI kutumia accutane, kwa sababu inaweza kusababisha kasoro mbaya kwa mtoto aliye-tumboni. Wanawake wanaotumia Accutane wanapaswa kutumia aina mbili za njia za kuzuia mimba kabla hawajaanza dawa hizi.Daktari wako atafuatilia matumizi ya dawa hii na mara kadhaa utafanyiwa vipimo vya damu.

Nini cha kutarajia nikiwa na chunusi?

Chunusi kwa kawaida huisha/kupotea baada ya miaka ya vijana kubalehe, lakini pia chunusu zinaweza kudumu kuwepo mpaka katika umri wa kati. Chunusi mara nyingi hutibika vyema kwa matibabu baada ya wiki 6 hadi 8, inaweza pia kujirudia mara kadhaa kila baada ya kitambo kidogo.

Makovu yanaweza kutokea kama chunusi mbaya/kali hazikutibiwa. Watu fulani, hasa vijana wanaobalehe, wanaweza kuwa na huzuni sana /sonona ikiwa chunusi  hazitatibiwa vyema.

Dhana potofu kuhusu chunusi

Je! Unadhani tayari unajua yote kuhusu chunusi?  Unaweza kushangaa kwamba baadhi ya mambo unayoyasikia kuhusu chunusi ni uongo mtupu-

 • Ukiosha sana uso wako, chunusi zako zitapungua.

Ukweli ni kuwa Ingawa kuosha uso husaidia kuondoa uchafu na mafuta kutoka kwenye matundu ya ngozi yako, kuosha sana kunaweza kusababisha ngozi kuwa kavu sana na kusababisha chunusi zako kuongezeka zaidi. Pia jaribu kuepuka kusugua sana (scrub) uso wako. Kwa kawaida mtu mwenye chunusi anapaswa kusafisha uso wake taratibu kwa kutumia sabuni ya kawaida na maji mara mbili kwa siku na akimaliza kujipangusa kwa kitambaa laini.

 • Kutoboa/kuminya chunusi husaidia kuziondoa kwa haraka.

Ukweli ni kuwa kuminya chunusi kutaifanya ipungue na isionekane kwa muda tu,lakini kutaifanya iendelee kuwepo kwa muda mrefu zaidi. Kwa kuiminya chunusi unaweza kuingiza bakteria na mafuta yanayosababisha chunusi ndani zaidi,hii itasababisha chunusi kuvimba zaidi na kusababisha alama nyekundu au kahawia na kovu wakati wa kupona. Wakati mwingine alama inaweza kudumu kwa miezi kadhaa na makovu yanaweza kubaki milele.

 • Usijipodoe (make-up) kama unataka chunusi zipone .

Ukweli ni kuwa mtu mwenye chunusi akichagua vyema vipodozi anavyotumia vitasaidia kupunguza chunusi. Tena baadhi ya concealers siku hizi zina benzoyl peroxide or salicylic acid, ambayo husaidia kupambana na chunusi. Unaweza pia kujaribu creams zenye benzoyl peroxide zinazoficha chunusi na kuzitibu pia.

Ikiwa umepata chunusi kali sana, Ongea na daktari wako au daktari bingwa wa ngozi kuhusu vipodozi bora vya kutumia – anaweza pia kupendekeza kuepuka vipodozi kabisa au kutumia tu bidhaa fulani ili kupunguza uwezekano wa chunusi kuzidi kuongezeka.

 • Kama unaendelea kupata chunusi, tumia dawa nyingi za chunusi mpaka zitoweke.

Ukweli ni kuwa kwa sababu dawa za chunusi zina benzoyl peroxide na salicylic acid ambazo hukausha ngozi, ukizitumia kwa wingi sana zitasababisha kukauka sana kwa ngozi, na kusababisha chunusi kuongezeka zaidi.

Kama dawa za kutibu chunusi za kwenye duka la dawa muhimu hazisaidii, ongea na daktari wako au daktari bingwa wa ngozi. Pia, kama unatumia dawa za kutibu chunusi, hakikisha unafuata maelekezo ya daktari – baadhi ya dawa zinaweza kuchukua hadi wiki 8 ili kupata matokeo bora.

 • Dawa ya meno inaweza kuponya chunusi

Dawa ya meno ina baking soda, hydrogen peroxide, alcohol, menthol, essential oils, na triclosan, ambazo zinaweza kukausha chunusi, Lakini haikutengenezwa kwa ajili ya ngozi yako, kwa hiyo inaweza kusababisha harara na kuwashwa ngozi. Hii inamaanisha unaweza kupona chunusi ukapata tatizo lingine. Badala ya kutumia dawa ya meno,jaribu dawa ya kupaka yenye benzoyl peroxide.

 • Kuogelea kwenye swimming pool kunaponya chunusi

Inaweza kuonekana kama kuogelea kunasababisha chunusi zako kukauka, lakini huleta shida sawa na kutumia dawa ya meno. Chlorine iliyo kwenye maji inaweza kukausha chunusi, lakini inaweza pia kusababisha ngozi kuwasha na kusababisha chunusi zaidi. Hakikisha kuwa unaoga baada ya kuogelea, na tumia lotion isiyo na mafuta mengi ili kukabiliana na ukavu wa ngozi.

 • Msongo wa mawazo hauwezi kusababisha chunusi
  Msongo wa mawazo husababisha homoni kadhaa mwilini kuongezeka zaidi na kusababisha chunusi. Kwa hiyo ukiona chunusi zinamtokea bibi harusi siku kadhaa kabla ya harusi usishangae.                                                                                                              

Vyanzo                                    

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/ency/article/000873.htm

Leave Your Comment