DEGEDEGE

DEGEDEGE

 • January 19, 2021
 • 0 Likes
 • 85 Views
 • 0 Comments

Maelezo ya jumla

Degedege (seizuire) ni mabadiliko ya kimwili na tabia yanayotokea kunapokuweko na shughuli ya umeme isiyo ya kawaida kwenye ubongo.

Mtu anayepatwa na degedege hutikisika na kutupa tupa mikono na miguu kwa vurugu bila kujitambua, misuli yake hukaza na kulegea kwa kujirudia rudia. Aina fulani za degedege hazina dalili kali na hakuna kutikisika, kutetemeka au kutetereka.

Mambo ya kuzingatia

Inaweza kuwa ngumu kutambua mtu anapopata degedege. Aina fulani za degedege humfanya mtu kukodoa macho tu (staring spells). Aina hii unaweza hata usiione. Dalili za tatizo hili hutegemea ni sehemu gani ya ubongo iliyoathirika. Dalili hutokea ghafla na zinaweza kujumuisha:

 • Kutokujitambua kwa muda mfupi (kukata umeme kwa lugha ya mtaani) na kisha kuhisi kama hujielewi – Mtu hujihisi kuwa hakumbuki kilichotokea kwa dakika kadhaa)
 • Mabadiliko ya tabia, kama vile kuchokoa nguo zake
 • Kutokwa na mate au povu mdomoni
 • Macho kuchezacheza isivyo kawaida
 • Mkoromo na mguno
 • Kujikojolea au kujinyea
 • Mabadiliko ya tabia, kama kuwa na hasira za ghafla, woga, kushikwa na hofu kubwa ya ghafla na hata kutofikiria sawasawa ,kufurahi au kucheka bila sababu ya msingi inayoeleweka.
 • Kutetemeka au kutikisika mwili mzima
 • Kuanguka chini ghafla
 • Kuhisi ladha chungu au ya chuma mdomoni
 • Kuuma au kusugua meno
 • Kuacha kupumua kwa muda mfupi
 • Mkazo wa ghafla wa misuli na kutetema kwa miguu au mikono

Dalili zinaweza kupotea baada ya sekunde kadhaa au zinaweza kuendelea mpaka dakika 15. Mara chache sana dalili zinaweza kuendelea kwa zaidi ya dakiak 15.

Mtu anaweza kuwa na dalili za tahadhari kabla tukio la degedege halijatokea, kama vile:

 • Hofu au wasiwasi
 • Kichefuchefu
 • Vertigo (unahisi kana kwamba unazunguka au chumba kinazunguka)
 • Matatizo ya macho au kuona (kuona mwaga mkali, kivuli kwenye macho au misitari mbele ya macho yako.)

Sababu

Degedege za aina zote husababishwa na shughuli isiyo ya kawaida ya umeme kwenye ubongo. Sababu ni pamoja na:

 • Viwango visivyo vya kawaida vya sodiamu au sukari kwenye damu
 • Maambukizi ya ubongo, ambayo yanaweza kusababisha kuvimba kwa utando unaofunika uti wa mgongo na ubongo
 • Kumia au majeraha ya ubongo yanayotokea utotoni au wakati wa kuzaliwa
 • Matatizo ya ubongo yanayotokea kabla ya kuzaliwa (kasoro za ubongo za kuzaliwa nazo)
 • Uvimbe kwenye ubongo (kwa nadra)
 • Matumizi mabaya ya dawa
 • Mshtuko unaotokana na kupigwa shoti ya umeme
 • Kifafa
 • Homa (hasa kwa watoto wadogo)
 • Kuumia au majeraha ya kichwa
 • Ugonjwa wa moyo
 • Joto kali (kutovumilia joto)
 • Phenylketonuria (PKU), hili ni tatizo la kimetaboliki analozaliwa nalo mtoto na kusababisha degedege kwa watoto wachanga.
 • Sumu
 • Madawa ya kulevya kama vile cocaine, amphetamines na PCP
 • Kiharusi
 • Kifafa cha ujauzito
 • Sumu mwilini zinazosababishwa na kushindwa kwa ini au figo kufanya kazi ya kuzitoa
 • Sumu inayotokana na kuumwa na nyoka au wadudu
 • Kuacha kutumia pombe au madawa fulani baada ya kunywa au kutumia madawa kwa muda mrefu.

Wakati mwingine, hakuna sababu inayoweza kupatikana ya kutokea kwa tatizo hili. Mara nyingi aina hii huwapata zaidi watoto na vijana wadogo, lakini inaweza kutokea katika umri wowote. Kwa watu wanaopata degedege bila sababu ya msingi inayofahamika wanaweza kuwa na historia ya tatizo hili au kifafa kwenye familia.

Huduma nyumbani

 • Matukio mengi huisha tu yenyewe. Lakini wakati wa tukio la degedege mtu anaweza kuumia au kujeruhiwa.
 • Tukio la degedege linapotokea, lengo kuu ni kumlinda mtu huyo asiumie au kupata majeraha:
  • Jaribu kuzuia asianguke. Mlaze chini katika eneo salama. Ondoa viti, meza au vitu vingine vyenye ncha kali vinavyoweza kumuumiza.
  • Weka kitu laini chini ya kichwa chake, kitu kama mto au nguo iliyokunjwa ili kulinda kichwa chake
  • Legeza nguo zake zinazombana, hasa meneo ya shingoni au kifuani
  • Mgeuze alalie upande. Kama akitapika, hili litasaidia asipaliwe na matapishi
  • Kaa na mgonjwa mpaka atakapo pata nafuu au kumka au mpaka mtaalamu wa tiba atakapokuja au mpaka utakapomfikisha kituo cha afya.
  • Mambo ambayo rafiki au mwanafamilia wa mgonjwa HAPASWI KUFANYA:
  • USIMZUIE au kujaribu kumshikilia au kumkandamiza ili asitikisike
  • USIMWEKEE kitu chochote mdomoni au katikati ya meno wakati wa tukio la degedege (hii ni pamoja na vidole vyako)
  • USIMHAMISHE mtu huyo, isipokuwa kama yuko katika eneo lisilo salama au hatari.
  • USIJARIBU kumfanya mtu huyo aache kutikisika. Kwa wakati huo hawajitambui na hawawezi kujizuia.
  • USIMPE mtu huyo chochote mdomoni hadi degedege itakapokoma na mtu huyo yuko macho kabisa na anajitambua.
  • USIANZE kufanya CPR, isipokuwa kama degedege imekoma na mtu huyo hapumui au hana mapigo ya moyo.
 • Kama mtoto anapata degedege wakati wa homa kali, mpooze kwa kumwagia maji ya vuguvugu. USIMZAMISHE kwenye maji ya baridi. Mpeleke kituo cha afya au wasiliana na daktari akuambie nini cha kufanya baada ya hapo. Pia, muulize kama unaweza kumpatia paracetamol/ acetaminophen mara tu atakapokuwa macho.

Wakati gani umwone daktari

Mpigie simu daktari au mpeleke mgonjwa kituo cha afya kama:

 • Hii ni mara yake ya kwanza kupata degedege
 • Degedege inadumu kwa zaidi ya dakika 2 mpaka 5.
 • Mtu aliyepata degedege hataamuka au hajielewi baada ya tukio la degedege
 • Degedege nyingine imeanza mara baada tu ya ile ya kwanza kuisha
 • Mtu huyo amepata degedege ndani ya maji
 • Mtu huyo anayepata degedege ni mjamzito
 • Kuna chochote kigeni kwa degedege hii tofauti na matukio aliyowahi kupata huko nyuma

Unapaswa kuto taarifa ya matukio yote ya degedege kwa mtumishi wa afya. Daktari anaweza kuamua kubadili au kuongeza au kupunguza dozi ya dawa.

Utarajie nini unapokwenda kwa daktari?

Mtu ambaye amepata degedege kwa mara ya kwanza au aliyepata tukio kali la degedege humwona daktari kwenye chumba cha dharura. Dakitari atajaribu kutambua umepata degedege ya aina gani kutokana na dalili zako.

Vipimo vitafanyika ili kuhakikisha kuwa hakuna sababu nyingine inayosababisha tatizo hili. Matatizo kama kiharusi, kipanda uso, matatizo ya usingizi n.k.

Vipimo ni pamoja na:

 • Vipimo vya damu na mkojo
 • CT Scan ya kichwa au MRI ya kichwa
 • EEG (Kwa kawaida hii haifanyiki kwenye chumba cha dharura)
 • Kuchomwa sindano kwenye uti wa mgongo na kutoa maji yake kwa ajili ya kipimo-lumber puncture

Vipimo zaidi vinahitajika kama:

 • Ndio tukio la kwanza la degedege kwa mgonjwa na hakuna sababu maalumu inayofahamika
 • Kifafa (Hakikisha kuwa mgonjwa anatumia dawa sahihi)

Vyanzo

https://medlineplus.gov/seizures.html

 • Share:

Leave Your Comment