EBOLA

EBOLA

 • November 18, 2020
 • 0 pendwa
 • 10 Wameona
 • 0 Maoni

Maelezo ya jumla

Homa ya Ebola ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya ebola. Ugonjwa huu, huua zaidi ya 90% ya wagonjwa wanaoambukizwa. Japo asili ya virusi vya ebola haijulikani, popo hufikiriwa kuwa chanzo cha maambukizi. Unaweza kuambukizwa ebola kwa kugusa majimaji ya mwili yenye uambukizo. Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na: homa, kuhisi baridi, upele, uchovu, maumivu ya misuli, kutapika, kuhara, n.k. Watu wanaosafiri kwenda kwenye maeneo yenye mlipuko wa ebola, wanaoishi na wagonjwa wa ebola na watumishi wa afya, wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa huu, hasa kama hawatafuata njia za kujikinga zilizopendekezwa. Unapaswa kutafuta matibabu unapopata dalili zilizotajwa hapo juu. Maambukizi yanapaswa kuthibitishwa kwa vipimo vya maabara. Hakuna tiba ya homa ya Ebola, madaktari hujaribu kudhibiti dalili kwa kumwongezea mgonjwa maji au damu.

Ni nini husababisha Ebola?

Homa ya Ebola husababishwa na virusi vya ebola. Wanasayansi wamebainisha aina nne za virusi vya Ebola. Tatu zimeripotiwa kusababisha ugonjwa kwa wanadamu: Ebola-Zaire virus, Ebola-Sudan virus, na Ebola-Ivory Coast virus. Ugonjwa wa ebola, umekuwa ukiathiri sehemu kadhaa za afrika. Wanadamu wanaweza kuambukizwa kutoka kwa wanyama au bidhaa za wanyama. Unaweza pia kuambukizwa kwa kugusa majimaji ya mwili ya mtu aliyambukizwa, au sindano zilizoathirika hospitalini. Mtu mwenye maambukizi anaweza kuwaambukiza wengine pindi tu anapoanza kuonesha dalili.

Je, Ebola huambukizwaje?

Mtu huambukizwa virusi vya Ebola kwa njia zifuatazo:

 • Wanadamu huambukizwa Ebola kwa kugusa damu, uteute, bidhaa au majimaji mengine ya mwili yalioambukizwa. Afrika, maambukizi hutokea kwa kugusa mizoga ya nyani, tumbili, popo, paa na nungunungu waliokufa msituni. Ni muhimu kuepuka kukutana na mizoga au bidhaa za wanyama wa mwituni.
 • Mara tu mtu anapoambukizwa na mnyama aliye na Ebola, anaweza kuambukiza watu wengi kwenye jamii
 • Maambukizi hutokea kwa kugusa damu, kinyesi, mkojo, mate au shahawa za mtu aliyeambukizwa hasa ukiwa na kidonda kwenye ngozi.
 • Maambukizi yanaweza kutokea kama midomo, macho au ngozi yenye kidonda itagusa sehemu au vitu vyenye majimaji yaliyoambukizwa, mf; nguo zenye kinyesi, matandiko au sindano zilizotumika.
 • Watu wenye virusi kwenye damu wanaweza kuambukiza wengine. Ndio maana madaktari hufanya vipimo vya maabara ili kujiridhisha kuwa hakuna virusi kwenye damu kabla ya mgonjwa kuruhusiwa kurudi nyumbani. Watu wasio na virusi kwenye damu hawawezi kumwambukiza yeyote.

Je, nini dalili za Ebola?

Baada ya maambukizi, dalili za awali zinaweza kuanza siku ya 2 hadi 21, dalili za awali hujumuisha:

 • Homa inayoanza ghafla
 • Kuhisi baridi
 • Uchovu
 • Kukosa nguvu
 • Maumivu ya misuli
 • Maumivu ya mgongo
 • Maumivu ya kichwa
 • Yabisi kavu
 • Donda koo
 • Kutapika
 • Kuhara
 • Kichefuchefu
 • Upele wa ngozi

Dalili zinazotokea baadae ni pamoja na:

 • Figo kushindwa kufanya kazi
 • Ini kushindwa kufanya kazi
 • Kuvuja damu ndani na nje ya mwili
 • Kuvuja damu kwenye macho, masikio na pua
 • Kuvuja damu kutoka kwenye mfumo wa kumeng’enya chakula, mf; rektamu
 • Sonona
 • Kuvimba macho
 • Kuvimba kwa via vya uzazi
 • Mgonjwa huhisi maumivu akigusa-sensitive
 • Upele mwili mzima, mara nyingi upele huwa na damu ndani yake
 • Sehemu ya juu ya mdomo huonekana nyekundu
 • Degedege, koma, kuchanganyikiwa

Zaidi ya 90% ya wagonjwa hufa kutokana na ugonjwa huu.

Nani yuko kwenye hatari zaidi?

Watu walio katika hatari zaidi ya kuambukizwa Ebola ni pamoja na:

 • Wasafiri wanaokwenda kwenye maeneo yenye mlipuko wa Ebola mara kwa mara (kama Afrika ya Kati)
 • Wafanyakazi wa hospitalini/wanaowahudumia wagonjwa wa Ebola
 • Wanafamilia wanaoishi karibu na mtu aliyembukizwa
 • Watu wanaoshughulika na maiti wakati wa mazishi ya mtu aliyeambukizwa
 • Wawindaji wanaokutana na mizoga ya wanyama waliokufa

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Mtu anapaswa kutafuta huduma ya matibabu haraka kama:

 • Alisafiri kwenda katika eneo lenye mlipuko wa virusi vya ebola na anaona dalili za ebola
 • Umekutana na mtu ambaye anahisiwa kuwa na virusi vya ebola na ameanza kuonesha dalili
 • Kama unahisi umegusa majimaji ya mwili yanayohisiwa kuwa na maambukizi
 • Kama umeanza kuona dalili za homa ya ebola

Huduma ya matibabu ni muhimu ili kudhibiti dalili na kuenea kwa ugonjwa wa ebola.

Utambuzi

Maambukizi ya virusi vya Ebola yanaweza kutambuliwa kwa vipimo vya maabara tu. Vipimo vinavyotumika kutambua homa ya Ebola ni pamoja na:

 • Vipimo vya damu –Complete Blood Count huonesha:
 • Kiwango cha chini cha seli nyeupe za damu
 • Kiwango cha chini cha chembe sahani
 • Kiwango cha chini cha vimeng’enya (enzymes) vinavyotolewa na ini
 • Vipimo kupima uwezo wa damu kuganda- coagulation studies
 • Vipimo kutambua maambukizi ya virusi

Uchaguzi wa matibabu

Kwa sasa hakuna dawa maalumu ya kutibu homa ya Ebola. Baadhi ya wagonjwa hupona baada ya matibabu ya kina. Wagonjwa kwa kawaida hulazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi na hupewa msaada ufuatao:

 • Kuongezewa maji kwa wagonjwa walioishiwa maji mwilini
 • Watu wanaovuja damu wanaweza kuhitaji kuongezewa damu

Ili kupunguza kuenea kwa ugonjwa huu, watu wanaohisiwa kuwa wameambukizwa wanapaswa kutengwa, kutambuliwa na kutibiwa.

Nini cha kutarajia?

Zaidi ya  90% ya wagonjwa hufa kutokana na ugonjwa huu.

Matatizo yanayoweza kutokea

 • Kifo
 • Watu wanaopona wanaweza kupoteza nywele na uwezo wa kuhisi wanapoguswa hupungua sehemu sehemu.

Kuzuia

Jamii

Kwa sasa hakuna chanjo iliyoidhinishwa dhidi ya virusi vya Ebola. Njia pekee ya kuzuia maambukizi na kupunguza idadi ya vifo, ni kufahamu mambo yanayoongeza hatari na kufuata hatua za kijinga zilizopendekezwa, ambazo ni:

 • Fuata maelekezo yanayotolewa na Wizara ya Afya ya nchi yako
 • Nyama ya wanyama inapaswa kupikwa vizuri kabla ya kula
 • Kupunguza uwezekano wa kukutana na wanyama hatarishi msituni, kama vile
 • Popo
 • Nyani
 • Tumbili
 • Epuka kushughulika na wanyama au mizoga ya wanyama walioambukizwa, kama unahisi mnyama ameambukizwa usimguse.
 • Nawa mikono kwa sabuni mara kwa mara, hasa baada ya kumtembelea mgonjwa hospitalini. Hakikisha unanawa kwa sabauni, hasa baada ya kumgusa mgonjwa, majimaji ya mwili, vitu/vyombo au mazingira anayotumia mgonjwa.
 • Epuka kwenda kwenye maeneo yenye mlipuko.
 • Usiguse majimaji ya mwili ya mgonjwa bila kujikinga.
 • Vaa gauni, glavu na barakoa (mask) unapokuwa karibu na wagonjwa wa ebola
 • Hatua za kujikinga zinapaswa kuchukuliwa kwenye sehemu za mkusanyiko kama, hospitalini, kanisani na nyumbani.
 • Kama kuna mtu anahisiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya ebola, mhimize na kumshauri atafute msaada wa kitabibu.
 • Kama umenuia kumtunza na kumhudumia mgonjwa wa ebola nyumbani kwako, toa taarifa kwa watumishi wa afya ya umma ili upatiwe mafunzo, vifaa na maelekezo jinsi ya kumtunza na kujikinga wewe, familia na jamii kwa ujumla dhidi ya ebola.
 • Maiti za watu waliokufa kutokana na maambukizi ya virusi vya ebola, zinapaswa kuzikwa na watu wenye vifaa maalumu vya kujikinga.
 • Shahawa za wanaume waliopona, zinaweza kuwaambukiza washirika wao wa ngono mpaka wiki 7 baada ya kupona. Kwa sababu hii, ni muhimu kwa wanaume kuepuka kufanya ngono kwa angalau wiki 7 baada ya kupona au kuvaa kondomu kama watajamiana ndani ya wiki 7 baada ya kupona.

Wafanyakazi wa Huduma za Afya

Wafanyakazi wa huduma za afya wanaohudumia wagonjwa wanaohisiwa kuwa na maambukizi ya virusi ebola wako katika hatari zaidi ya kuambukizwa kuliko makundi mengine.

Mbali na tahadhari za kawaida zinazochukuliwa kila siku, wafanyakazi wa huduma za afya wanapaswa kuzingatia hatua maalumu za kuzuia maambukizi. Watahakikisha wanajikinga dhidi ya sindano, majimaji ya mwili, damu au mazingira yaliyochafuliwa na virusi vya ebola. Zaidi ya hayo ,wanapaswa:

 • Kutumia vifaa binafsi vya kujikinga kama gauni, glavu, barakoa na miwani ya kukinga uso
 • Usirudie kutumia vifaa au nguo za kujikinga zaidi ya mara moja, Isipokuwa kama zimesafishwa ipasavyo.
 • Tumia glavu mpya kila unapomuhudumia mgonjwa mwingine anayehisiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya ebola.
 • Fanya chini ya uangalizi mkali utaratibu, matibabu au upasuaji wowote unaoweza kuongeza uwezekano wa watu wengine kuambukizwa . wataarifu na watumishi wengine wawe chonjo.

Hatua za kujikinga zinazopendekezwa na WHO

Shirika la Afya Duniani (WHO) hutoa ushauri kwa jumuia za kimataifa kujiandaa na  kukabiliana na mlipuko wa Ebola.

Hatua zinazochukuliwa na  WHO ni pamoja na:

 • Ufuatiliaji wa ugonjwa wa ebola na utawanyaji wa habari kuhusu mlipuko kwa maeneo mengine
 • Kutoa msaada wa vifaa na watenda kazi ili kufanya uchunguzi na kudhibiti majanga
 • Kutoa ushauri juu ya njia za kujikinga na chaguzi za matibabu
 • Kusambaza wataalamu na vifaa vya kujikinga dhidi ya ebola kwa watumishi wa afya kama vitaitishwa na nchi husika.
 • Kutoa taarifa na elimu kuhusu asili na njia za kujikinga ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya virusi

Safari

Wakati wa mlipuko, shirika la afya duniani huchunguza hali ya kiafya ya umma na kutoa mapendekezo kuhusu kusitisha safari au biashara.

Hatari ya maambukizi kwa wasafiri ni ndogo sana ,hii ni kwa sababu maambukizi hutokana na kugusa majimaji ya mwili ya mgonjwa aliyeambukizwa.

Maelekezo ya jumla ya shirika la afya duniani kwa wasafiri;

 • Wasafiri wanapaswa kuepuka kukutana na wagonjwa walioambukizwa
 • Watumishi wa afya wanaosafiri kwenda katika maeneo yaliyoathirika, wanapaswa kufuata hatua za kujikinga zilizoainishwa na shirika la afya duniani.
 • Mtu yeyote aliyeishi, aliyekaa au aliyepitia katika eneo lenye mlipuko, anapaswa kuzifahamu dalili na ishara za maambukizi na anapaswa kutafuta msaada wa kitabibu pindi tu dalili zinapoanza kujitokeza.
 • Madaktari wanaowahudumia wasafiri wanaotoka katika maeneo yenye mlipuko, wanapaswa kuchukua tahadhari na kuchunguza uwezekano wa kuwepo maambukizi ya ebola kama dalili zinashabihiana.

Vyanzo

 • Shirikisha:

Leave Your Comment