Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Echocardiogram hutumia mawimbi ya sauti ili kuzalisha picha ya moyo. Kipimo hiki humruhusu daktari kuuchunguza moyo ukipiga na kusukuma damu. Daktari anaweza kutumia picha za Echo kutambua ugonjwa wa moyo.
Kulingana na taarifa anazohitaji daktari wako, unaweza kuhitajika kufanya aina moja au nyingine ya echocardiograms.
Kwa nini ufanye echocardiogram?
Daktari anaweza kupendekeza ufanye echo ili:
- Kuangalia kama kuna matatizo kwenye vali au vyumba vya moyo
- Kuchunguza kama dalili fulani imetokana na tatizo la moyo mf; kupata shida kupumua au maumivu ya kifua.
- Kuchunguza kasoro za moyo alizozaliwa nazo mgonjwa –hii hufanyika utotoni
Aina ya echocardiogram unayofanya hutegemea daktari anahitaji taarifa gani.
Baadhi ya aina za echocardiogram
Transthoracic echocardiogram
Hii ndio aina ya echo inayofanyika mara nyingi:
- Mtaalam hupakaza jeli kwenye kifaa (transducer).
- Mtaalamu hukandamiza taratibu kifaa hicho kilichopakwa jeli kwenye kifua
- Transducer hurekodi mwangwi wa mapigo ya moyo.
- Kompyuta hubadilishana mwangwi huo kuwa picha ya video .
Transesophageal echocardiogram
Kama daktari atahitaji picha zenye taarifa zaidi au kama picha iliyopigwa na echocardiogram ya kawaida haioneshi vyema moyo, daktari wako anaweza kupendekeza transesophageal echocardiogram.
Katika utaratibu huu:
- Koo lako litatiwa dawa ya ganzi.
- Kisha kifaa chenye transducer huingizwa kooni kupitia mdomoni mpaka kwenye umio.
- Transducer hurekodi mawimbi ya sauti ya moyo.
- Kompyuta hubadilisha mwangwi huo kuwa picha ya video ya moyo, ambayo daktari anaweza kuiangalia.
Echocardiogram ya doppler
Mawimbi ya sauti hubadili sauti (pitch) yanapogonga seli za damu zinazopita kwenye moyo na mishipa yake. Mabadiliko haya yanaweza kumsaidia daktari kupima kasi na mwelekeo wa damu kwenye moyo.
Mbinu hii ya doppler hutumiwa kutambua matatizo ya mtiririko wa damu na shinikizo la damu kwenye ateri za moyo.
Mzunguko wa damu unaooneshwa kwenye monitor huwa umetiwa rangi ili kumsaidia daktari kutambua matatizo vyema.
Stress echocardiogram
Matatizo mengine ya moyo – hasa yale ya mishipa ya moyo– hujitokeza wakati mgonjwa anapofanya shughuli nzito. Daktari wako anaweza kupendekeza ufanye stress echocardiogram ili kuchunguza matatizo ya ateri za moyo zinazopeleka damu kwenye misuli ya moyo. Hata hivyo, echocardiogram haiwezi kutoa taarifa kuhusu kuziba kwa mishipa ya moyo.
Watika wa stress echocardiogram:
- Picha za moyo huchukuliwa kabla na baada tu ya kufanya mazoezi (kukimbia,kutembea au kuendesha baiskeli kwenye chumba cha mazoezi )
- Kama hauwezi kufanya mazoezi, daktari anaweza kukuchoma sindano ili kuufanya moyo wako kusukuma damu haraka kama vile unafanya mazoezi.
Hatari ya kipimo cha echocardiogram
Hakuna hatari yoyote unapofanya echocardiogram ya kawaida (transthoracic). Transducer inaweza kukukera inapokandamizwa kifuani kwako. Ni muhimu transducer ikandamizwe ili kuzalisha picha bora za moyo.
Kama umefanya transesophageal echocardiogram, koo lako linaweza kuwa na maumivu kwa masaa machache. Kwa nadra sana, mpira unaobeba transducer unaweza kukwangua koo.
Wakati wa stress echo, mazoezi au dawa zinaweza kusababisha moyo wako kwenda mbio kuliko kawaida.
Jinsi ya kujiandaa na kipimo cha echocardiogram
Hakuna haja ya maandalizi yoyote maalum kabla ya echo ya kawaida (transthoracic). Unaweza kula, kunywa na kutumia dawa kama kawaida.
Kama unafanya transesophageal echo, daktari anaweza kukuagiza usile chochote kwa masaa kadhaa kabla ya kipimo.
Nini cha kutarajia
Wakati wa kupimo
Echocardiogram inaweza kufanyika ofisi kwa daktari au hospitalini.
- Kwa echocardiogram ya kawaida (transthoracic):
- Utavua nguo na kuacha kifua wazi na kisha utalala chali kwenye meza au kitanda cha kufanyia uchunguzi.
- Mtaalamu ataweka jeli kwenye transducer ili kuboresha unasaji wa mawimbi ya sauti.
- Mtaalamu ataitembeza transducer kifuani,juu,chini, kushoto na kulia ili kunasa mawimbi ya sauti na kuunda picha. Unaweza kusikia sauti “whoosh,” kutoka kwenye ultrasound ikirekodi mtiririko wa damu kwenye moyo wako.
- Kama unafanya transoesophageal echocardiogram:
- Koo lako litatiwa dawa ya ganzi.
- Kisha kifaa chenye transducer huingizwa kooni kupitia mdomoni mpaka kwenye umio.
- Transducer hurekodi mawimbi ya sauti ya moyo.
- Kompyuta hubadilisha mwangwi huo kuwa picha ya video ya moyo, ambayo daktari wako anaweza kuiangalia.
- Utahitaji si zaidi ya saa moja ili kufanya kipimo hiki. Baada ya kipimo daktari anaweza kukubakiza ofisini kwake au hospitalini ili kukuangalia kwa masaa kadhaa kabla ya kukuruhusu kwenda nyumbani.
Baada ya kipimo
Watu wengi wanaweza kuanza shughuli zao za kila siku baada ya echocardiogram.
Kama majibu ya echocardiogram ni ya kawaida, unaweza usihitajike kufanya vipimo zaidi. Kama majibu yako yatatia mashaka , daktari anaweza kukuagiza kwa daktari bingwa wa moyo kwa ajili ya vipimo zaidi.
Matokeo ya kipimo cha echocardiogram
Taarifa za echocardiogramm zinaweza kuonesha:
- Mabadiliko ya ukubwa wa moyo. Kuchoka au kuharibika kwa vali za moyo, shinikizo la juu la damu au matatizo mengine ya moyo yanaweza kusababisha moyo kupanuka na kuta za moyo kuwa nene kuliko kawaida.
- Uwezo wa kusukuma damu. Echocardiogram hupima asilimia ya damu inayosukumwa kutoka kwenye ventrikali za moyo na kiasi cha damu kinachosukumwa kwa dakika moja. Moyo ambao hausukumi damu ya kutosha kukidhi mahitaji ya mwili husababisha kuwepo kwa dalili za kushindwa kwa moyo -Heart failure.
- Kuharibika kwa misuli ya moyo. Echocardiogram humsaidia daktari kutambua kama misuli/sehemu zote za kuta za moyo huchangia kusukuma moyo. Maeneo ya ukuta wa moyo ambayo hayaonekani kusukuma damu vyema yanaweza kuwa yameharibika baada ya mshtuko wa moyo au hayapati oksijeni ya kutosha.
- Matatizo ya vali za moyo. Echocardiogram inaweza kumsaidia daktari kutambua kama vali za moyo zinafunguka na kufunga vyema ili kuruhusu damu kuingia na kutoka kwenye moyo bila kuvuja.
- Matatizo ya moyo. Echocardiogram inaweza kuonesha matatizo kwenye vyumba vya moyo, matatizo ya mishipa ya moyo na matatizo mengine ya moyo.
Leave feedback about this