KIPIMO CHA EKSIREI

Eksirei ni nini?

Kipimo cha eksirei (X-ray) ni kipimo cha picha ambacho kimetumika kwa miongo mingi. Kinamsaidia daktari kutazama ndani ya mwili wa mgonjwa bila ya kufanya upasuaji wowote. Hii inasaidia kutambua, kufuatilia, na kutibu hali nyingi za kitabibu.
Kuna aina nyingi tofauti tofauti za x-ray zinazotumika kwa madhumuni tofauti tofauti. Kwa mfano, daktari anaweza kuagiza ufanye mammogram kuchunguza matiti yako. Au anaweza kuagiza eksirei na barium enema kuangalia kwa ukaribu mfumo wako wa kumeng’enya chakula.
Kuna baadhi ya hatari zinazohusishwa na kufanya x-ray. Lakini kwa watu wengi, manufaa yake ni makubwa kuliko hatari hiyo. Ongea na daktari wako ili kujua nini kinachokufaa.eksirei

Kwa nini eksirei hufanyika?

Daktari anaweza kuagiza ufanye eksirei ili:

 • kuchunguza eneo unalopata maumivu au usumbufu
 • kufuatilia maendeleo ya ugonjwa, kama vile ugonjwa wa kudhoofika mifupa (osteoporosis)
 • Kuangalia kama dawa anayotumia mgonjwa inafanya kazi vizuri

Hali nyingine zinazoweza kuhitaji eksirei kufanyika ni pamoja na:

 • Saratani ya mifupa
 • Saratani ya matiti
 • Kupanuka kwa moyo
 • Kuziba kwa mishipa ya damu
 • Hali zinazoathiri mapafu
 • matatizo ya tumbo
 • Kuvunjika mifupa
 • maambukizi
 • osteoporosis (huu ni ugonjwa wa kudhoofika kwa mifupa)
 • yabisi kavu (arthritis)
 • Jino lililooza au kutoboka
 • Ili kutoa vitu vilivyokwama baada ya kumezwa (hasa kwa watoto)

Je, unapaswa kujiandaa vipi kabla ya kufanya eksirei?

Eksirei ni utaratibu wa kawaida. Katika hali nyingi, hauhitaji kuchukua hatua zozote maalum za kujiandaa. Kutegemea na eneo litakalopigwa picha, unaweza kuvaa nguo zisizobana. Madaktari wanaweza kukuomba ubadilishe nguo na kuvaa za hospitalini. Wanaweza pia kukuomba uondoe mapambo yako yote au vitu vyote vya chuma mwilini kabla ya kupiga picha ya eksirei.
Daima mwambie daktari wako kama una chuma au kipandikizi chochote mwilini mwako, hata kama kiliwekwa baada ya upasuaji uliofanyika miaka mingi iliyopita. Vyuma au vitu vilivyowekwa mwilini vinaweza kuharibu picha ya eksirei.
Katika hali nyingine, huenda ukahitajika kutumia au kunywa rangi inayotumika kutofautisha tishu za mwili (contrast dye) kabla ya kupigwa picha ya eksirie. Kulingana na sababu ya X-ray, rangi hii inaweza kutolewa kwa njia tofauti, ikiwa ni pamoja na:

 • Unaweza kunywa rangi hii kama kimiminika
 • Rangi inaweza kuchomwa moja kwa moja kwenye mshipa
 • Inaweza kuwekwa kupitia kwenye njia ya haja kubwa (enema) kabla ya kipimo.

Kama unapiga picha ya eksirei ili kuchunguza mfumo wa kumeng’enya chakula, daktari anaweza kukuagiza ufunge na usile chochote kwa muda fulani kabla ya kipimo. Unaweza pia kuepuka kunywa vinywaji fulani fulani. Katika hali nyingine, daktari anaweza pia kukuagiza utumie dawa ili kusafisha matumbo yako.

Eksirei inafanywaje?

Mtaalamu wa teknolojia ya mionzi anaweza kukupiga picha ya eksirei katika idara ya mionzi.
Baada ya kujiandaa, mtaalamu wa mionzi atakwambia namna ya kukaa ili kupata picha nzuri za eksirei. Mtaalamu anaweza kukuomba ulale chali, kifudifudi, ukae au usimame ili kupata picha nzuri. Wakati mwingine atazunguza mashine ya kupiga picha toka upande mmoja mpaka mwingine ili kupata picha za mahala anapohitaji huku ukiwa umetulia.
Ni muhimu kutulia wakati picha zinapopigwa. Hii itatoa picha nzuri zaidi.

Je, nini madhara ya Eksrei?

Eksirei hutumia kiwango kidogo sana cha mionzi ili kutengeneza picha za mwili wako. Kiwango cha mionzi inayotumika ni salama kwa watu wazima wengi, lakini si salama kwa mtoto anayekuwa tumboni mwa mama. Kama una ujauzito au unaamini kuwa unaweza kuwa na mimba, mwambie daktari wako kabla ya kupiga picha ya eksirei. Anaweza kupendekeza njia tofauti isiyotumia miozi kama MRI.
Kama unapiga picha ya eksirei ili kutambua au kutibu hali inayosababisha maumivu, kama vile mfupa uliovunjika, unaweza kuhisi maumivu au usumbufu wakati wa kipimo. Utatakiwa kuweka pozi mbalimbali wakati wa kupigwa picha. Hii inaweza kusababisha kujisikia vibaya au maumivu. Daktari anaweza kupendekeza utumie dawa za maumivu kabla ya kipimo.
Kama ukinywa rangi ya kutofautisha tishu za mwili kabla ya eksirei, inaweza kusababisha madhara kama yafuatayo:

Katika matukio machache sana, rangi inaweza kusababisha athari kali sana, kama mshtuko wa moyo au shinikizo la chini sana la damu. Kama unapata athari kali unapaswa kumwona daktari haraka iwezekanavyo.

Je! Nini kinachotokea baada ya eksirei?

Baada ya picha za eksirei kupigwa, kulingana na hali yako, daktari anaweza kukushauri kuendelea na shughuli zako au kujipumzisha wakati ukisubiria majibu. Majibu ya kipimo chako yanaweza kupatikana siku hiyo hiyo ya kipimo au baadae.
Daktari atachunguza picha zako za eksirei na ripoti ya mtaalamu wa mionzi na kuamua jinsi ya kuendelea. Kutegemea na majibu ya kipimo chako, daktari anaweza kuagiza vipimo vingine ili kuhakiki utambuzi. Kwa mfano daktari anaweza kuagiza vipimo vya damu, au vipimo vingine vya picha. Madaktari wanaweza pia kuagiza aina fulani ya matibabu.
Muulize daktari wako  akupe maelezo zaidi juu ya hali yako, utambuzi na uchaguzi wa matibabu.

Vyanzo

https://www.wikidoc.org/index.php/X-rays

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi