Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Homa ya dengue (dengue fever) ni ugonjwa unaosababishwa na virusi wanaoenezwa na mbu.
Je, nini dalili za homa ya dengue?
Homa ya dengue huanza na homa ya ghafla, joto la mwili linaweza kupanda hata kufikia nyuzi joto 40. Mgonjwa anaweza kutokewa na upele mwekundu siku 2-5 baada ya homa kuanza. Upele wa pili unaofanana kama wa surua (measles) hutokea baadaye.
Dalili nyingine ni pamoja na:
- Kuumwa kichwa (hasa nyuma ya macho)
- Uchovu
- Maumivu ya viungo
- Maumivu ya misuli
- Kichefuchefu
- Kuvimba kwa tezi za limfu – hii husababisha mtoki kwapani, shingoni au kwenye kinena
- Kutapika
Ni nini husababisha homa ya dengue?
Homa ya dengue husababishwa na moja ya virusi wanne tofauti wanaohusiana. Inaenezwa kwa kuumwa na mbu aliyeambukizwa, mbu aina ya Aedes aegypti ndiye huhusishwa zaidi na ugonjwa huu. Ugonjwa huu hupatikana zaidi katika maeneo ya kitropiki kama:
- Nchi zilizo kusini mwa jangwa la sahara, ikiwemo Tanzania, Kenya n.k.
- Kaskazini mashariki mwa Australia na visiwa vya Indonesia
- Amerika ya kusini na kati
- Asia ya kusini
Homa ya dengue huwapata zaidi watu wanaoishi au wanaosafiri kwenda katika maeneo yenye mlipuko
Homa ya dengue haipaswi kuchanganywa na homa ya dengue inayosababisha kuvuja damu (dengue hemorrhagic fever) , aina hii husababishwa na aina hiyohiyo ya virusi lakini dalili zake huwa ni kali sana.
Nani yuko kwenye hatari zaidi?
Kuishi au kusafiri kwenda katika eneo lenye mlipuko au uambukizi huongeza uwezekano wa kuambukizwa ugonjwa huu. Maeneo haya ni pamoja na:
- Nchi zilizo kusini mwa jangwa la sahara, ikiwemo Tanzania, Kenya n.k.
- Kaskazini mashariki mwa Australia na visiwa vya Indonesia
- Amerika ya kusini na kati
- Asia ya kusini
Kuwepo kwa vyombo vya kutunzia maji au madimbwi ya maji yaliyotwama karibu na nyumba huwaruhusu mbu kukua na kuongezeka, hii huongeza hatari zaidi.
Makundi ya watu walio katika hatari ya kupata ugonjwa wenye dalili kali za dengue ni pamoja na:
- Watoto wachanga na watoto wadogo
- Jinsi ya kike,
- Watu wenye kiwango kikubwa cha virusi
- Kisukari
- Pumu
- n.k
Ukiwa na homa ya dengue, ni wakati gani utafute matibabu haraka?
Mwone mtoa huduma wa afya kama unaishi au umesafiri kwenda katika eneo lenye mlipuko wa homa ya dengue na unahisi au kuona dalili za ugonjwa huu.
Utambuzi wa homa ya dengue
Vipimo vinavyoweza kufanyika ilikutambua hali hii ni pamoja na:
- Kupima kiwango cha kinga mwili kilichotengenezwa na mwili ili kupambana na virusi vya dengue- antibody titre for dengue fever virus
- Complete blood count – hesabu ya seli za damu
- Daktari anaweza pia kuagiza vipimo vingine zaidi ili kujiridhisha kuwa dalili hizo hazisababishwi na tatizo lingine mf. Vipimo vya malaria
Uchaguzi wa matibabu ya homa ya dengue
Hakuna matibabu maalum kwa homa ya dengue. Utahitaji kuongezewa maji mwilini kama utakuwa na ishara za kuishiwa maji mwilini. Acetaminophen (paracetamol) hutumiwa kutibu homa. EPUKA KUTUMIA ASPIRINI.
Magonjwa yenye dalili zinazofanana na homa ya dengue
Nini cha kutarajia?
Hali ya kuugua kwa ujumla hudumu kwa wiki moja au zaidi. Japo homa ya dengue hukufanya ujisikie vibaya, mara nyingi haisababishi kifo. Watu wengi walioambukizwa ugonjwa huu hupona kabisa baada ya muda. Baadhi ya wagonjwa hupata dalili kali na huhitajika kulazwa hospitalini.
Matatizo yanayoweza kutokea
Matatizo yanayoweza kutokea ni pamoja na:
- Degedege inayosababishwa na joto kali la mwili
- Upungufu mkubwa wa maji mwilini
- Kuvuja damu, hii ni pamoja na kuvuja damu tumboni hasa kama kinyesi ni cheusi kama lami
- Koma
Homa ya dengue inaweza kutishia maisha kwa watu wenye magonjwa sugu kama vile kisukari na pumu.
Kuzuia
- Vaa nguo zinazofunika mwili vizuri ili kujikinga na mbu mf. Nguo za mikono mirefu na suruali
- Jipake mafuta au dawa za kufukuza mbu kama unaishi maeneo hatarishi
- Lala chini ya chandarua kilichotiwa dawa ili usiumwe na mbu
- Safisha mazingira ya nyumba na funika madimbwi ili kupunguza mazalia ya mbu
- Kama unataka kusafiri kwenda maeneo hatarishi, fuata hatua za kujikina zilizowekwa.
Vyanzo
Leave feedback about this