Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Njia kuu ya maambukizi ya ugonjwa huu ni ngono isiyo salama. Hadi sasa, bado hakuna tiba ya ugonjwa wa Ukimwi, lakini kuna dawa zinazotumika kupunguza makali ya ugonjwa huu. Matumizi ya mapema ya dawa za kufubaza virusi ”ARV” yatakuwezesha kuishi ukiwa na afya njema. Ni muhimu kupima afya ili kujitambua na kuchukua hatua mapema.
Ingawa maarifa ya ugonjwa huu ni mengi, bado kumeendelea kuwepo na changamoto nyingi katika jamii yetu. Moja ya changamoto hizi ni imani potofu iliyojengeka katika jamii, inayopelekea uoga wa kupima kwa kuhofia unyanyapaa wa waathirika utakaofuata. Hali hii hurudisha nyuma harakati za mapambano dhidi ya ugonjwa huu.
Je, imani potofu juu ya ugonjwa wa Ukimwi ni zipi?
Zifuatazo ni baadhi ya imani potofu zinazoweza kurudisha nyuma hatua iliyopigwa katika mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya ukimwi;
- Kupata maambukizi ya ukimwi ndiyo mwisho wa maisha; Hii si kweli, kwa kupima, kujitambua na kuanza dawa za kufubaza virusi vya ukimwi ”ARV’ mapema, kutakupelekea kuishi maisha marefu yenye afya njema.
- Unaweza kumtambua muathirika kwa kumuangalia afya yake au muonekano wake kwa macho;Hauwezi kumtambua muathirika kwa kuangalia kwa macho. Watu wengi hawana dalili yoyote ya maambukizi ya ukimwi kwa miaka ya awali. Hivyo, njia pekee na ya uhakika kujua kama mwenza ana maambukizi ni kupima. Upimaji wa Virusi vya Ukimwi umerahisishwa na unatolewa bila gharama yoyote.
- Ukimwi unatibika;Hadi sasa bado hakuna tiba ya ugonjwa wa Ukimwi. ARV husaidia kupunguza makali ya virusi vya ukimwi. Hivyo , matumizi bora ya dawa za kufubaza virusi ”ARV” hupelekea virusi kufubaa na kushindwa kuzaliana na hivyo kumuwezesha mtu anayeishi na virusi vya ukimwi kuishi maisha marefu na yenye afya. Si kweli kwamba zinatibu na kuponya kabisa ugonjwa huu.
- Tohara kwa wanaume inazuia kabisa maambukizi ya ukimwi; Ukweli ni kuwa, tohara inapunguza hatari ya maambukizi ya virusi ya ukimwi kwa kiasi kikubwa, lakini si kweli kwamba inazuia maambukizi ya virusi vya ukimwi.
- Nikiwa nina VVU/Ukimwi sitakiwi kubeba ujauzito; Unao uwezo wa kupata mtoto ili mradi viwango vya virusi katika damu ”viral load” ipo chini na imechungwa vyema ndani ya miezi sita. Wenza ambao mmoja wao ana maambukizi na mwingine hana, wanao uwezo wa kutumia njia ya tendo kwa ajili ya kupata ujauzito lakini wanatakiwa kuzingatia viwango vya virusi ”viral load”. Hivyo, unashauriwa kupima na kuongea na daktaria au washauri nasaa watakaofuatilia wingi wa virusi na kukushauri muda muafaka wa kushika ujauzito.
Kuhusu UKIMWI, unapaswa kutambua kuwa:
Hauwezi kuambukizwa au kumuambukiza mtu virusi vya ukimwi kwa njia zifuatazo:
- Kuumwa na mbu
- Kwa jasho
- Kuchangia vyoo, sahani, vifaa vya gym.
- Kwenda shule pamoja au kuwa na rafiki mwenye virusi vya ukimwi.
- Kupiga chafya au kukohoa
- Kushikana mikono, kukumbatia au kupigana busu kavu na mtu mwenye virusi vya ukimwi.
- Kuvuta hewa moja na mtu mwenye virusi vya ukimwi.
Ni vizuri kupima bure maambukizi ya virusi vya ukimwi katika mojawapo ya vituo vya afya vya serikali. Na unapogundulika kuwa na maambukizi anza kutumia dawa za kufubaza virusi vya ukimwi mapema ili afya isidhoofike.
Pia, kama unaishi na mwathirika wa ugonjwa huu usimnyanyapae au kumtenga. Unapaswa kumwonesha upendo na kuwa msaada kwake katika kuhakikisha wanapata huduma ya dawa za kufubaza virusi na kufuata maelekezo yote anayopatiwa na wataalamu wa afya.
Imeandaliwa na: Gekura Mataro – Clinician, counselor
Vyanzo
https://www.healthline.com/health/hiv-aids/misconceptions-about-hiv-aids
Leave feedback about this