KICHOMI

 • August 19, 2020
 • 2 Likes
 • 620 Views
 • 0 Comments

Maelezo ya jumla

Kichomi ni maumivu ya kifua yanayotokea hasa wakati wa kuvuta pumzi ndani au kukohoa,maumivu haya husababishwa na kuvimba kwa utando mdogo (pleural) unaofunika kifua na mapafu.

Je! Nini dalili za kichomi?    

Dalili kuu ya kichomi ni maumivu kifuani. Mara nyingi maumivu hutokea unapovuta pumzi ndani au kukohoa. Watu wengine wanaweza kuhisi maumivu kwenye bega.

Kuvuta pumzi ndani ,kukohoa na mjongeo wowote wa kifua hufanya maumivu kuwa mabaya zaidi.

Kuvimba kwa utando unafunika mapafu (pleural) kunaweza kusababisha maji kujikusanya ndani ya kifua. Hii inaweza kusababisha kupumua kwa shida na kusababisha dalili zifuatazo:    

 • Ngozi kuwa na rangi ya bluu (cyanosis)    
 • Kukohoa    
 • Kupumua kwa shida   
 • Kupumua haraka haraka (tachypnea)

Kichomi husababishwa na nini?

Kichomi hutokea mapafu yanapovimba kwa sababu ya maambukizi kama nimonia (pneumonia) au kifua kikuu (tuberculosis). Mara nyingi kichomi ni ishara ya kuwepo maambukizi ya virusi kwenye mapafu.

Pia,maumivu ya kichomi yanaweza kusababishwa na:

 • Magonjwa yanayosababishwa na asibesiti (asbestos)    
 • Saratani fulani    
 • Jeraha/kuumia kifuani    
 • Magonjwa ya yabisi-baridi (Rheumatic diseases)

Nani yuko kwenye hatari zaidi?

Ikiwa una ugonjwa wa mapafu, kama vile nyumonia au kifua kikuu, uko katika hatari kubwa ya kupata kichomi.

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Mwone mtoa huduma wa afya ikiwa una dalili za kichomi. Kama unapata shida kupumua au ngozi yako inageuka bluu, tafuta huduma ya matibabu haraka sana.

Utambuzi

Unapokuwa na kichomi, utando laini unaofunika mapafu na kifua unakuwa mgumu na unaoparura. Tando hizi mbili husuguana kila unapovuta pumzi na inaweza kutoa sauti ya mpapruro anayoweza kuisikia daktari kwa kutumia kifaa cha kusikiliza kifua (stethoscope).

Mtoa huduma ya afya anaweza kufanya vipimo vifuatavyo:    

 • Complete blood count – kipimo hiki hufanyika ili kutambua kama kuna maambukizi kwenye damu,
 • Thoracentesis – kipimo hiki hufanyika ili kupunguza maji kifuani au kwa ajili ya kuyapima ,hili hufanyika kwa kuchoma sindano ndefu kwenye kifua ili kupunguza maji hayo   
 • Ultrasound ya kifua –  kipimo hiki hutumia nguvu ya mawimbi ya sauti kupiga picha ya kifua
 • Eksirei ya kifua – picha ya eksirei husaidia kutambua sababu ya kichomi

Uchaguzi wa matibabu

 • Mtoa huduma wa afya anaweza kuondoa maji kwenye mapafu kwa thoracentesis na kuyachunguza kuangalia  kama kuna ishara za maambukizi.
 • Matibabu yanategemea kinachosababisha kichomi. Maambukizi ya bakteria yanatibiwa kwa antibiotics. Maambukizi mengine ya bakteria yanaweza kuhitaji upasuaji ili kutoa maji yote yenye uambukizo.
 • Kichomi kinachosababishwa na maambukizi ya virusi kwa kawaida hupona tu chenyewe bila bila dawa. Wagonjwa mara nyingi wanaweza kudhibiti maumivu ya kichomi kwa dawa za maumivu kama vile paracetamol au ibuprofen.

Nini cha kutarajia?

Kupona kwa kichomi hutegemea kimesababishwa na nini.

Matatizo yanayoweza kutokea   

 • Kupata shida kupumua    
 • Kuharibika kwa mapafu kwa sababu ya jeraha baada ya thoracentesis    
 • Matatizo yanayotokana na ugonjwa uliosababisha kichomi

Kuzuia

Kutibu mapema maambukizi ya bakteria kwenye njia ya hewa itasaidia kuzuia kichomi.

Vyanzo

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/article/001371.htm

Leave Your Comment