KIFAFA

KIFAFA

 • August 15, 2020
 • 0 Likes
 • 117 Views
 • 0 Comments

Maelezo ya jumla

Kifafa (epilepsy) ni ugonjwa wa ubongo unaotokea kama muundo na shughuli za neva kwenye ubongo umevurugika .Ugonjwa wa kifafa unaweza kusababishwa na majeraha ya kichwa, kiharusi na magonjwa mengine ya mishipa ya damu, uvimbe kwenye ubongo, maambukizi kwenye ubongo yanayoweza kusababisha uvimbe wa tando za uti wa mgongo na ubongo (meningitis), uvimbe wa ubongo (encephalitis), ulevi wa pombe uliopindukia, homa kali kwa watoto, au uzazi mgumu.

Dalili hutofautiana kulingana na aina ya Kifafa, wengine wanakodoa tu kwa muda mfupi,wengine wanapoteza fahamu na wengine wanatupatupa mikono na miguu kwa vurugu (degedege). Kwa kawaida dalili hujumuisha kuchanganyikiwa kwa muda mfupi, kukodoa kwa kitambo kidogo, kurusharusha mikono na miguu kusikoweza kudhibitiwa, na hata kupoteza fahamu kabisa.

Electroencephalogram ni kipimo kinachotumiwa mara nyingi kugundua kifafa. Vipimo vya picha kama vile CT au MRI vinaweza kusaidia kupata sababu ya ugonjwa huu. Uchaguzi wa aina ya matibabu hutegemea sababu ya kifafa . Matibabu ni pamoja na dawa za kudhibiti kifafa  na upasuaji. Wagonjwa wengi wenye kifafa wanaishi maisha ya kawaida.

Nini dalili za kifafa?

Dalili hutofautiana kulingana na aina ya kifafa, kuanzia wengine kukodoa kwa muda bila kujitambua mpaka kupoteza fahamu na degedege. Katika hali nyingi, mgonjwa mwenye kifafa huwa na aina sawa ya degedege kila wakati.        

 • Kuchanganyikiwa kwa muda        
 • Kukodoa kwa muda bila kujitambua   
 • Mkukutuo/degedege/Kutupatupa miguu na mikono kwa vurugu usiyoweza kudhibitiwa.
 • Kupoteza fahamu kabisa.

Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata kifafa?      

 • Watu waliopata majeraha ya kichwa        
 • Wagonjwa wa kiharusi na magonjwa mengine ya mishipa        
 • Kuwa na uvimbe kwenye ubongo
 • Kuwa na mambukizi kwenye ubongo yanayoweza kusababisha uvimbe wa tando za uti wa mgongo na ubongo (meningitis) au uvimbe wa ubongo (encephalitis)        
 • Kuutia ubongo sumu, kama vile pombe
 • Homa kali kwa watoto        
 • Mtoto anayezaliwa kwa shida, hasa anayepata ugumu kupita kwenye via vya uzazi wakati wa kuzaliwa.
 • Kuwepo kwa historia ya kifafa kwenye familia
 • Wanaume

 Ni wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Ikiwa unajisikia unapata mojawapo ya dalili zifuatazo, unahitaji kupata huduma ya afya haraka iwezekanavyo:        

 • kupata mshtuko/degedege kwa mara ya kwanza        
 • kupata Mshtuko/degedege iliyodumu kwa muda mrefu zaidi kuliko hapo awali.
 • Kupata mshtuko/degedege mara nyingi au mara kwa mara kuliko kawaida.
 • Kifafa kikali (Status epilepticus)

Kabla mgonjwa anayepata degedege hajapelekwa kwenye idara ya magonjwa ya dharura, mambo yafuatayo yanaweza kusaidia.

 • Tulia usiwe na papara.
 • Usimshikilie mgonjwa, weka kitu laini kama mto au nguo chini ya kichwa cha mgonjwa.
 • Ondoa vitu vyote vigumu vinavyoweza kuharibika au kumuumiza mgonjwa kama vile miwani,au mkoba, na legeza nguo zozote zinazobana shingo.        
 • Kaa na mgonjwa, liangalie hilo tukio linavyotokea na kisha utamueleza daktari yaliyotokea kabla, wakati, na baada ya degedege ukufika kituo cha afya.

Utambuzi

Lengo la vipimo vifuatavyo ni kutambua sababu ya kifafa chako.

 • Uchunguzi wa mwili hufanyika kuangalia mfumo wako wa neva: Daktari anaweza kuulizia kuhusu hali yako wakati wa kuzaliwa, ukuaji wako na kama ulishawahi kupata majeraha yoyote kichwani. Uchunguzi wa mwili wa mfumo wa neva unahitajika kutambua sababu ya kifafa.        
 • Vipimo vya damu: Hivi hutumiwa kuchunguza dalili za maambukizi au sumu.
 • Vipimo vya neva na saikolojia (Neuropsychological): Majaribio haya yanajumuisha ukaguzi wa IQ (uwezo wa kufikiria), kumbukumbu na uwezo wa kuzungumza. Majaribio haya humsaidia daktari kuchunguza sababu ya kifafa.
 • Electroencephalogram (EEG): Hiki ni kipimo kinachofanyika kugundua kifafa. kinaweza kurekodi shughuli ya umeme unaopita kwenye ubongo wako, na kama umeme huo umevurugika itaonekana. Jaribio hili linaweza kumsaidia daktari wako kujua ni aina gani ya kifafa uliyo nayo.
 • Computerized tomography (CT): CT Scan ni kipimo kinachofanyika mara nyingi kwa wagonjwa wenye kifafa. kinaweza kumsaidia daktari kutofautisha sababu za kifafa, hii ni pamoja na uvimbe kwenye ubongo, majeraha, uvimbe uliojaa maji (cysts) au kiharusi.        
 • Magnetic resonance imaging (MRI): MRI Scan hutumia nguvu ya sumaku kupiga picha ubongo na kutoa picha tofuti na ile ya CT Scan, picha hii inayopigwa na MRI humpatia taarifa za nyongeza daktari ili kutambua sababu ya kifafa.

Uchaguzi wa matibabu

Uchaguzi wa matibabu hutegemea sababu ya kifafa. Matibabu yake ni dawa na upasuaji.     

 • Watafiti wanashauri kuwa mtoto mwenye kifafa, atumie chakula chenye mafuta mengi na chenye wanga kidogo ,hii itapunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kupata degedege mara kwa mara.
 • Tiba kwa ajili ya tatizo linalosababisha kifafa inahitajika , kama vile: dawa aina ya antibiotics zinahitajika kutibu maambukizi kwenye ubongo, upasuaji au tiba ya mionzi  vinahitajika kutibu uvimbe/saratani kwenye ubongo. Kama sababu za kifafa zitatibiwa na kudhibitiwa vyema, mshtuko/degedege itapungua au kuacha kabisa.        
 • Madawa: Lengo la dawa za kudhibiti kifafa (anti-epileptic ) ni kupunguza au kutokomeza kabisa kutokea kwa degedege. Wagonjwa wengi hatimaye wanaweza kuacha kutumia dawa baada ya miaka miwili au zaidi bila kupata mshtuko/degedege. Dawa zote za kudhibiti mshtuko/degedege zina madhara, kama vile uchovu, kizunguzungu, kuongezeka uzito au kupoteza wiani wa mfupa.        
 • Upasuaji: Upasuaji unapendekezwa kwa kawaida ili kuondoa sehemu ndogo ya ubongo, sehemu hii ndogo ya ubongo inayokatwa na kuondolewa huwa imechunguzwa na kugundulika kuwa ndiyo inayosababisha degedege

Magonjwa yenye dalili sawa na kifafa

 • Degedege itokanayo na homa kali sana
 • Kuzirai/kuzimia (Syncope)        
 • Matatizo ya moyo        
 • Kusikwa na hofu (Panic attack)
 • Hali ya kuwa na kiwango kidogo cha glukosi mwilini (Hypoglycaemia )       
 • Kuanguka chini kusiko na sababu(Idiopathic drop attacks)
 • Mtetemo wa kineva (Tics)        

Jinsi ya kujikinga/kuepuka Kifafa

 • Epuka kuumia/kupata majeraha ya kichwa, linda kichwa chako unapokua maeneo hatarishi
 • Epuka mfumo mbaya wa maisha, kuepuka matumizi ya pombe        
 • Tibu homa zote haraka iwezekanavyo kwa watoto        
 • Kuepuka changamoto na uzazi mgumu wakati mtoto anapozaliwa, maandalizi ya kujifungua yafanywe mapema.

Nini cha kutarajia?

Wagonjwa wengi wenye kifafa wanaishi maisha ya kawaida. Lakini baadhi yao, hasa watoto, wanaweza kupata matatizo ya kitabia na kihisia. Wanaweza kuchukiwa/kunyanyaswa/kuonewa na wenzao au kutengwa shuleni na kwenye jamii.

Vyanzo

 

 • Share:

Leave Your Comment