KIFUA KIKUU

 • August 15, 2020
 • 0 Likes
 • 127 Views
 • 0 Comments

Maelezo ya jumla

Kifua kikuu (Tuberculosis) ni maambukizi ya bakteria yanayoua zaidi ya watu milioni 1.8 kote duniani. Takribani watu milioni 10.4 duniani wameambukizwa kifua kikuu. Kifua kikuu ni ugonjwa unaoweza kuua 60% ya watu walioambukizwa kama hawatatibiwa, lakini wakitibiwa 90% ya wagonjwa walioambukiza hupona kabisa. Watu wengi ambao wameambukizwa Kifua kikuu wana kifua kikuu fiche. Hii ina maana kwamba bakteria wa kifua kikuu wanadhibitiwa na mfumo wa kinga ya mwili. Watu wenye Kifua kikuu fiche hawana dalili yoyote na hawawezi kuambukiza kifua kuu kwa watu wengine. Kulingana na shirika la afya duniani, mwaka 2015, tiba ya kifua kikuu iliokoa maisha ya watu takribani milioni 3 kote duniani.

Nini dalili za kifua kikuu?

Wakati wa Kifua kikuu fiche, bakteria hujificha kwenye alveoli za mapafu. Bakteria hawa waliojificha kwenye alveoli, wanapotoka na kuenea kwenye tishu za mapafu na viungo vingine husababisha Kifua kikuu hai. Dalili za kifua kikuu hutofautiana kulingana na viungo vilivyoathiriwa. Mara nyingi katika hatua ya mwanzo ya kifua kikuu hakuna dalili.                                                                              Dalili za kifua kikuu hujumuisha

 • Kikohozi sugu, hasa kinapokuwepo zaidi ya wiki mbili
 • Kutokwa jasho usiku
 • Kukohoa damu
 • Kutokwa jasho jingi, hasa usiku
 • Uchovu
 • Homa
 • Kupungua kwa uzito
 • Kupumua kwa shida
 • Maumivu ya kifua
 • Kukorota

Dalili za ugonjwa wa TB katika sehemu nyingine za mwili zitategemea eneo lililoathirika.

Kifua Kikuu husababishwa na?

Kifua kikuu husababishwa na bakteria anayeitwa Mycobacterium tuberclosis. Bakteria huyu mara nyingi huharibu mapafu ya mgonjwa, lakini anaweza pia kufanya uharibifu sehemu nyingine ya mwili kama vile figo, mgongo, na ubongo. Ikiwa hautatibiwa vizuri, ugonjwa wa kifua kikuu unaweza kusababisha kifo.

Kifua Kikuu sugu husababishwa na?

Kifua kikuu sugu (Multidrug-Resistant Tuberculosis) hakisikii dawa. Husababishwa na bakteria mycobacterium tuberculosis ambaye hasikii dawa, dawa za kawaida za kifua kikuu zinashindwa kumuua bakteria huyu.Usugu kwa dawa za kifua kikuu unaweza kusababishwa na utumiaji mbaya wa dawa za kifua kikuu,Kwa mfano:

 • Mgonjwa anaposhindwa kukamilisha kipimo kamili (dose) cha dawa alichoandikiwa na daktari.
 • Mhudumu wa afya anapoandika na kumpatia mgonjwa dawa isiyosahii, au kumpatia dawa atumie kwa muda mrefu zaidi kuliko inavyotakiwa.
 • Madawa yanapokuwa hayapatikani muda wote
 • Madawa yanapokuwa na ubora duni

Nani yuko katika hatari zaidi ?

Kifua kikuu huenea kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kwa njia ya hewa (kukohoa, kupiga chafya).

Watu walio katika makundi yafuatayo wako kwenye hatari kubwa ya kupata kifua kikuu hai:

 • Wazee
 • Watoto
 • Watu wenye upungufu wa kinga ya mwili (watu wenye UKIMWI, wanaotumia Tibakemikali (chemotherapy), wagonjwa wa kisukari, au wanaotumia dawa fulani)

Hatari ya kuambukizwa kifua kikuu huongezeka ikiwa:

 • Unakaa/unaishi na mtu mwenye kifua kikuu
 • Lishe yako ni duni
 • Unaishi katika eneo lenye msongamano mkubwa wa watu au usafi duni

Sababu zifuatazo zinaweza kusababisha kuongezeka kwa kiwango cha maambukizi  katika jamii

 • Kuongezeka kwa maambukizi ya VVU
 • Kuongezeka kwa idadi ya watu wasio na makazi
 • Kutokea kwa uzao wa mycobacterium unaosababisha kifua kikuu sugu

Kifua Kikuu sugu

Kifua kikuu sugu huwapata zaidi watu ambao:

 • Hawatumii dawa zao za kifua kikuu mara zote kama walivyoelekezwa
 • Hawatumii dawa zote kama walivyoelekezwa na daktari au muuguzi
 • Wamepata ugonjwa wa kifua kikuu kwa mara nyingine tena baada ya kumaliza kutumia dawa za kifua kikuu.
 • Wametokea sehemu/mahali ambapo kuna kifua kikuu sugu kwa wingi.
 • Wamekaa/kuishi na mtu anayejulikana kuwa ana kifua kikuu sugu

Ni wakati gani utafute msaada wa haraka?

Mwone mtoa huduma wa afya ikiwa:

 • Unahisi uko kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa kifua kikuu au umesafiri kwenda katika eneo ambalo kuna hatari kubwa ya kukuambukizwa kifua kikuu.
 • Umeanza kupata dalili za kifua kikuu
 • Dalili zako zinaendelea japo unatibiwa
 • Kuna dalili mpya zinajitokeza

Utambuzi wa kifua kikuu

Utambuzi wa kifua kikuu hai unaweza kufanyika kwa kutumia dalili, historia ya mgonjwa ,vipimo vya kifua kikuu, na picha za x-rays.

Kifua kikuu fiche kinaweza kuonekana baada ya wiki 6-8 baada ya kuambukizwa. Kuna vipimo/majaribio mawili ambayo yanaweza kutumika kusaidia kuchunguza maambukizi ya kifua kikuu:

 • Kipimo cha ngozi ili kugundua kifua kikuu
  • Sindano ndogo hutumiwa kuchoma dawa ya kupimia inayoitwa tuberculin chini ya ngozi yako.
  • Baada ya siku 2-3, mgonjwa anapaswa kurudi hospitalini na mhudumu wa afya atakagua kuona kama kuna majibu (reaction)
  • Uchunguzi wa ngozi hautumiki sana katika maeneo mengi ya Afrika, hii ni kwa sababu watu wengi afrika  hupewa chanjo ya kifua kuu na hii chanjo husababisha majibu yasiyo sahihi. 
 • Kipimo cha damu ili kugundua kifua kikuu
  • Kipimo cha damu hutumiwa kupima maambukizi ya kifua kikuu
  • Kipimo cha damu hupima jinsi mfumo wa kinga ya mwili unavyoathiriwa na bakteria wanaosababisha kifua kikuu.

Kifua kikuu sugu hupimwa kwa kipimo cha kupima usugu kwa dawa (drug susceptibility test ). Ili kuhakikisha kuwa mtu ana ugonjwa kifua kikuu, vipimo vingine vinahitajika:

 • X-ray ya kifua – Picha ya x-ray ya kifua huonesha mapafu yenye vijishimo au vidonda ambavyo kawaida huonekana kwa mtu mwenye kifua kikuu pekee
 • Makohozi kwa ajili ya kupima

Ni muhimu kumwambia mtoa huduma wa afya kama umewahi kuwa na majibu “chanya” kwenye vipimo vya kupima kifua kikuu na kama umeshawahi kutibiwa kifua kikuu.

Uchaguzi wa matibabu

Matibabu ya kawaida huhusisha kutumia dawa (antibiotic) kwa miezi kadhaa. Matibabu ya kifua kikuu yanachukua muda mrefu. Baada ya wiki mbili za matibabu mgonjwa hawezi kuambukiza watu wengine. Baadhi ya dawa zinazotolewa kwa ajili ya kutibu kifua kikuu zina madhara, hasa zikichanganywa na madawa mengine. Kwa sababu hizi, wagonjwa wengine wanaona vigumu kutumia dawa zao kwa muda unaohitajika. Hata hivyo, kutokutumia dawa vizuri kunaweza kusababisha bakteria kuwa sugu na kufanya tiba kuwa ngumu zaidi  hapo baadaye. Matibabu ya kifua kikuu sugu ni tofauti na mara nyingi matarajio ya kupona si mazuri sana.

Kifua Kikuu sugu

 • Kifua kikuu ni ugonjwa unaotibika na kupona. Kabla ya kuanza matibabu ya kifua kikuu sugu, mgonjwa atahitajika kufanyiwa vipimo ili kuhakikisha usugu wa bakteria kwa dawa za kifua kikuu (drug-susceptibility testing). Hata hivyo, kipimo hiki kinaweza kuchukua wiki kadhaa kukamilika, kwa hiyo matibabu yanapaswa kuanza kulingana na ushauri wa mtaalamu mara tu kifua kikuu sugu kinapohisiwa.
 • Baada ya matokeo ya vipimo kujulikana, utaratibu wa matibabu unapaswa kurekebishwa kwa mujibu wa matokeo, Wagonjwa wanapaswa kufuatiliwa kwa karibu sana ili kuhakikisha wanafuata mpango wa matibabu.
 • Matibabu ya kawaida ya kifua kikuu sugu yanajumuisha angalau aina tano za madawa, ambayo yamethibitishwa kwa vipimo kuwa yanaweza kuua bakteria wanaosababisha kifua kikuu sugu.
 • Matibabu kwa kawaida yamegawanywa katika awamu mbili: awamu ya awali na awamu mwendelezo.
 • Dawa aina ya Fluoroquinolone inahitajika katika kutibu wagonjwa wenye kifua kikuu sugu.
 • Kumsimamia mgonjwa kila anapotumia dawa ,itasaidia kuhakikisha mgonjwa mwenye kifua kikuu sugu anafuata vyema mpango wa matibabu.

Makundi malumu ya kuzingatia

Watu walioambukizwa VVU

 • Matibabu ya kifua kikuu sugu kwa watu wenye maambukizi ya VVU na wasio na VVU ni sawa.
 • Matibabu ya kifua kikuu na ukimwi, yanahitaji mtaalamu mwenye ujuzi wa kutibu ukimwi na kifua kikuu.
 • Watoa huduma wanapaswa kufuatilia  matumizi ya ARVs, hii itasaidia kugundua mapema kama kuna mwingiliano wa dawa unaoweza kuleta madhara.
 • Haupaswi kutumia Rifampin na madawa ya ARV kwa pamoja. Rifabutin, ambayo ina Muingiliano mdogo na madawa mengine inaweza kutumika badala ya Rifampin.

Watoto

 • Matibabu kwa watoto wenye ugonjwa wa kifua kikuu baada ya kuambukizwa au wanahisiwa kuambukizwa kifua kikuu na mtu mwenye kifua kikuu sugu, mpango wa matibabu unapaswa kupangwa kwa kuongozwa na matokeo ya vipimo vya mtu aliyemwambukiza kifua kikuu.
 • Kama chanzo cha maambukizi hakifahamiki na hali ya mambo inaashiria hatari ya kuwepo kifua kikuu sugu, watoto wanapaswa kutibiwa kwa mpango wa matibabu wa awali unaotumia dawa nne mpaka matokeo ya vipimo vyake yatakapojulikana.
 • Kama kuna uwezekano kuwa kuna usugu kwa dawa aina ya Isoniazide, Ethambutol inaweza kutumika (15-20 mg / kg kwa siku)
 • Dawa kama Streptomycin, kanamycin, au amikacin zinaweza kuchaguliwa katika hizo dawa nne.
 • Matumizi ya muda mrefu ya fluoroquinolones kwa watoto hayajaidhinishwa. Hata hivyo, wataalamu wengi wanakubaliana kuwa madawa haya yanahitajika kwa matibabu ya watoto wenye kifua kikuu sugu.
 • Ushauri kutoka kwa daktari bingwa wa kutibu kifua kikuu kwa watoto unapendekezwa.

Wanawake wajawazito

 • Kushauriana na wataalamu ni muhimu kabla ya kuanza matibabu kwa wanawake wajawazito wenye kifua kikuu sugu, kwa sababu sehemu kubwa ya madawa yanayotumiwa kutibu kifua kikuu sugu yana madhara kwa mtoto aliye tumboni.
 • Pyrazinamide haipaswi kutumiwa na wanawake wajawazito.
 • Ushauri kuhusu madhara yanayoweza kumpata mtoto aliye tumboni unapaswa kutolewa.

Watu waliokaribu na wagonjwa wa kifua kikuu sugu

 • Kwa watu ambao wanaishi karibu na wagonjwa wenye kifua kikuu sugu kisichosikia /kisichoweza kutibiwa na dawa aina ya Isoniazid (Drug restant tb), na wamegunduliwa au wanahisiwa kuwa na kifua kikuu fiche, inapendekezwa kuwa watibiwe kwa dozi ya kila siku ya Rifampin kwa muda wa miezi 4.
 • Ikiwa Rifampin haiwezi kutumika kwa sababu yoyote, rifabutin inaweza kutumika kama mbadala.
 • Kwa watu wanaohisiwa kuwa na kifua kikuu sugu kisichoweza kutibiwa na Isoniazid na Rifampin (mult-drug resistance tb) , dawa mbadala zinaweza kutumika kwenye mpango wa matibabu.
 • Mpango mbadala wa matibabu ni lazima ujumuishe madawa mawili ambayo yanaweza kutibu aina hiyo ya kifua kikuu, kulingana na matokeo ya vipimo vya kupima usugu (susceptiblity tests).
 • Mpango wa matibabu unaofaa unapaswa kujumuisha fluoroquinolone kila siku

Nini cha Kutarajia?

Baada ya wiki 2 – 3 za matibabu dalili huanza kupoa. Ikiwa kifua kikuu kitatambuliwa mapema na matibabu kuanza haraka, matarajio huwa mazuri sana.

Kifua Kikuu sugu

Matarajio ya kifua kikuu sugu kupona ni mabaya zaidi kuliko yale ya kifua kikuu cha kawaida. Kwa hiyo kuna ulazima wa kufanya vipimo vya kupima usugu (drug susceptibility test) na kumwangalia mgonjwa anapotumia dawa ili kuhakikisha anazingatia mpango wa matibabu, hii itasaidia kuzuia maambukizo mapya ya kifua kikuu sugu na kuhakikisha matokeo bora ya tiba.

Matatizo yatokanayo na kifua kikuu

Kifua kikuu inaweza kusababisha uharibifu wa kudumu kwenye mapafu ikiwa matibabu hayatafanyika mapema. Madawa yanayotumika kutibu kifua kikuu yanaweza kuleta madhara, ikiwa ni pamoja na matatizo ya ini. Madhara mengine ni pamoja na:

 • Kusababisha matatizo ya kuona
 • Machozi na mkojo wenye rangi ya machungwa au rangi ya kahawia
 • Upele

Vipimo vya macho vinaweza kufanyika kabla hujaanza matibabu, ili daktari aweze kufuatilia kama kuna mabadiliko yoyote katika macho yako unapoendelea na tiba.

Kuzuia/kujikinga dhidi ya kifua kikuu

Kwa mtu binafsi, kufunika mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya kunapunguza maambukizi. Kwa kiwango kikubwa, kukaa katika eneo au nyumba yenye hewa safi na kupunguzwa kwa maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu, inaweza pia kupunguza maambukizi. Kama ilivyo kwa magonjwa yote ya kuambukiza, kugundua mapema ugonjwa huu ni muhimu ili kuuzuia kuenea. Watu wenye kifua kikuu fiche wanaweza kutibiwa kwa isoniazid kabla ugonjwa hauajaendelea na kuwa hai.

 Dawa ya Isoniazid inapaswa kutolewa kwa watu ambao:

 • Wana kifua kikuu fiche
 • Wanakaa/Wanaishi karibu na watu wenye kifua kikuu
 • Wanaishi katika nchi, wilaya au eneo ambalo  ugonjwa wa kifua kikuu umeenea sana.
 • Wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa kifua kikuu

Chanjo inayoitwa BCG inazuia kuenea kwa kifua kikuu kutoka kwenye mapafu na kwenda katika sehemu nyingine za mwili, lakini haizuii maambukizi. Inashauriwa tu kwa watoto wachanga katika nchi zinazojulikana kuwa na viwango vya juu vya kifua kikuu kama Tanzania. Chanjo ya kifua kikuu (BCG) husababisha vipimo vya ngozi kutoa majibu ya uongo na hivyo kusababisha kutafutwa njia nyingine za kupima kifua kikuu. Kifua kikuu hakienei kwa:

 • Kumpa mtu mkono
 • Kula au kunywa pamoja
 • Kugusa matandiko ya mgonjwa au nguo
 • Kutumia mswaki mmoja
 • Kubusu

Kifua Kikuu sugu

Ili kuzuia kifua kikuu kisichoweza kutibiwa na dawa za kawaida, sheria zifuatazo zinapaswa kuzingatiwa:

 • Tumia dawa zote kama ilivyoagizwa na mtoa huduma ya afya
 • Usivuke hata dozi moja na haupaswi kuacha kutumia dawa mapema.
 • Wagonjwa wanapaswa kuwaambia watoa huduma wa afya ikiwa wanapata shida wanapotumia dawa
 • Ikiwa wagonjwa wanatarajia kusafiri, wanapaswa kuzungumza na watoa huduma wa afya na kuhakikisha kuwa wana dawa za kutosha wanapokuwa safarini
 • Epuka mazingira yanayokuweka katika hatari ya kuambukizwa kifua kikuu sugu,kwa mfano maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu kama vile hospitalini na magerezani:
 • Kwa kesi ya wafanyakazi wa afya, hatari ni kubwa sana ya kukutana na wagonjwa wenye kifua kikuu sugu, ni muhimu mazingira yaboreshwe na vifaa binafsi vya kujikinga vitumike mf: barakoa (mask)

Wahudumu wa afya wanaweza kusaidia kuzuia kifua kikuu sugu kwa:

 • Kutambua mapema kifua kikuu na kuanza matibabu haraka
 • Kuhakikisha wanafuata miongozo ya kimatibabu iliyopendekezwa na wizara ya Afya
 • Kufuatilia matokeo ya matibabu   
 • Kuhakikisha kuwa mgonjwa anafuata mpango na kumaliza nmatibabu

Vyanzo

Leave Your Comment