KIHARUSI

 • August 14, 2020
 • 0 Likes
 • 142 Views
 • 0 Comments

Maelezo ya jumla

Kiharusi (stroke) ni hali inayomtokea mtu kunapokuwepo na kizingiti kinachozuia damu kufika katika sehemu fulani ya ubongo.Wakati mwingine kiharusi huitwa “shambulio la ubongo.”

Je! Nini dalili za kiharusi?

Dalili za kiharusi hutegemea mahali na eneo la uharibifu wa ubongo.Eneo dogo la ubongo linapoathiriwa na kiharusi inaweza kusababisha dalili yoyote. Kwa mujibu wa Taasisi ya Taifa ya Matatizo ya mfumo wa neva na kiharusi nchini marekani (NINDS), kuna dalili tano kuu za kiharusi, kama zifuatazo.

 • Kutokea kwa ghafla ganzi na kulegea/udhaifu wa uso, mkono, au mguu (hasa kwa upande mmoja wa mwili)
 • Kuchanganyikiwa kwa ghafla, kushindwa kuzungumza vizuri au kushindwa kuelewa kinachozungumzwa na wengine.
 • Kushindwa ghafla kuona/upofu wa jicho moja au macho yote mawili
 • Kupata shida ya kutembea ghafla, kizunguzungu, kupoteza usawa au uratibu wakati wa kutembea/kusimama.
 • Kuumwa kichwa kikali ghafla bila sababu inayojulikana

Magonjwa mengine yenye dalili sawa na hizo  ni:

 • Saratani ya ubongo
 • Jipu kwenye ubongo
 • Kipandauso (migraine headache)
 • Kuumia/jeraha la kichwa
 • Uvimbe wa tando za uti wa mgongo na ubongo(meningitis)
 • Uvimbe wa ubongo ( encephalitis)
 • Kuzidisha kiasi cha dawa kinachohitajika.
 • Ukosefu wa usawa wa electrolyte kama sodiamu au glukosi mwilini.

Ni nini kinachosababisha Kiharusi?

Kiharusi ni hali ya dharura. Kuna aina mbili za kiharusi, aina ya kwanza husababishwa na ubongo kukosa damu ya kutosha. Hii hutokea kwa sababu ya kunywea au kuziba mishipa ya ubongo na kushindwa kutiririsha damu ya kutosha kufika kwenye ubongo.

Aina ya pili hutokea baada ya mishipa inayopeleka damu kwenye ubongo kupasuka na damu kuvuja kwenye ubongo.

Karibu asilimia 80 ya viharusi husababishwa na kuziba kwa mishipa,na kusababisha damu kutokufika kwenye ubongo. Tafiti za kitabibu zinaonesha kuwa sababu kubwa zinazoongeza hatari ya kupata kiharusi ni shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa kisukari, kitambi na uvutaji wa sigara.

Matibabu ya kiharusi kinachosababishwa na kuziba mishipa ya ubongo ni pamoja na madawa ya kuzuia kuganda kwa damu (anti-platelets,anticoagulants) . Kwa wagonjwa wenye kiharusi kinachosababishwa na kuvuja damu kwenye ubongo, upasuaji unaweza kupendekezwa kutibu au kuzuia shambulio lingine.

Wagonjwa huhitaji mazoezi ili kupona na kukarabati viungo /sehemu za mwili zisizofanya kazi vyema baada ya shambulio.

Hatima ya matibabu ya kiharusi hutegemea ukubwa wa eneo la ubongo lililoharibika,muda aliotumia mgonjwa toka alipopata shambulio mpaka alipofika kwenye idara ya magonjwa ya dharura, matatizo yatokanayo na shambulio na matokeo ya ukarabati wa viungo.

Yafuatayo huongeza hatari ya kupata kiharusi

 • Shinikizo la juu la damu
 • Ugonjwa wa moyo, kama vile ugonjwa wa mishipa/ateri za moyo na ugonjwa wa yabisi-baridi ya moyo (rheumatic heart disease)
 • Kisukari
 • Kuwa na kiwango cha juu cha mafuta (cholesterol) mwilini.
 • Uvutaji wa sigara
 • Kuwa na umri mkubwa

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Kiharusi ni dharura ya kimatibabu. Mtu yeyote anayedhaniwa kuwa na kiharusi anapaswa kupelekwa kituo cha matibabu mara moja kwa ajili ya tathmini na matibabu.

Utambuzi kuwa una kiharusi

 • Uchunguzi wa kimwili, hasa uchunguzi wa mfumo wa neva.
 • CT scan: Ili kutambua sababu ya kiharusi, Picha ya CT scan ya ubongo hufanyika. CT scan hutumia  mionzi kutambua damu iliyovujaau uvimbe ndani ya ubongo. CT Scan inaweza pia kusaidia kutofautisha kiharusi na magonjwa mengine ya ubongo, kama vile saratani au jipu kwenye ubongo,magonjwa yana baadhi ya dalili zinazoshabihiana na kiharusi.
 •  MRI scan: Hutumia nguvu ya sumaku kupiga picha ya ubongo. Inaweza kutoa maelezo zaidi kuliko yale ya CT scan, lakini MRI sio kipimo cha kwanza wakati wa kiharusi,kwa sababu inaweza kuchukua mpaka saa moja kupiga picha ya MRI na hii itachelewesha matibabu.

Uchaguzi wa matibabu

Matibabu hutegemea ni aina gani ya kiharusi.Kila aina ya kiharusi ina matibabu maalumu na haitakiwi kuyachanganya.Tiba ya aina moja ya kiharusi inaweza KUUA mgonjwa wa aina ya ili. Daktari atanapaswa kufanya CTscan ili kujua kwa uhakika ni aina gani kabla hajatoa matibabu

Matibabu ya kiharusi kinachosababishwa na kuziba kwa mishipa ya ubongo.
Lengo la matibabu ni kurejesha mtiririko wa damu kwenye ubongo wa mgonjwa haraka iwezekanavyo. Matibabu  ya haraka sio tu yanaongeza uwezekano wa kuokoa maisha, lakini pia yanaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa matatizo/athari zitokanazo na kiharusi.

 • Madawa: Dawa kama aspirini, warfarin au heparini, zinaweza kutolewa kwa haraka baada ya kiharusi ili kupunguza uwezekano wa kuwa na kiharusi kingine.

Tissue plasminogen activator (TPA) ni dawa yenye nguvu sana inayosaidia kuvunja vunja madonge ya damu yaliyoganda na kuziba mishipa ya damu kwenye ubongo. Dawa hii husaidia watu wengi kupona kabisa na ni MARUFUKU kutumiwa na watu wenye kiharusi kinachosababishwa na kuvuja damu kwenye ubongo.

 • Upasuaji: Upasuaji unafanyika kufungua ateri zilizoziba.
  • Carotid endarterectomy: Katika operesheni hii, daktari wa upasuaji hufungua ateri ya karotidi iliyoziba na kuondoa utando ulioiziba. Operesheni hii inaweza kupunguza hatari ya mgonjwa kupata kiharusi.
  • Angioplasty na stents: Katika operesheni  hii daktari hujaribu kuurekebisha mshipa wa damu ulioharibika pia huweka bomba ndogo kupanua sehemu ya ateri iliyopungua upana ili kuruhusu damu kupita. Stent hubaki ndani ya mwili kuzuia kujirudia kwa tatizo.

Matibabu ya kiharusi kinachosababishwa na kuvuja damu kwenye ubongo

Viharusi vingi vinavyosababishwa na kuvuja damu kwenye ubongo huhusishwa na perema (aneurysm ) na matatizo ya kimuundo ya mishipa ya damu. Upasuaji hupendekezwa kutibu haya matatizo au kuyazuia. Operesheni ya kawaida hupunguza ukubwa wa perema na kurekebisha matatizo ya kimuundo ya mishipa ya damu.

Kurejesha na kukarabati mwili(Rehab)

Daktari atakusaidia kurejesha ujuzi ambao umepotea baada ya shambulio, kama vile kutembea, kuwasiliana au uratibu. Ukarabati ni muhimu sana kwa sababu huamua ubora wa maisha atakayoishi mgonjwa yeye mwenyewe na familia yake baada ya kutoka hospitalini.

Dawa za kuepuka kama una kiharusi

Wagonjwa wanaopatikana na kiharusi wanapaswa kuepuka kutumia dawa zifuatazo:

 • Almotriptan
 • Alteplase
 • Eletriptan
 • Eptifibatide
 • Esterified estrogens
 • Frovatriptan
 • Phentermine
 • Prasugrel
 • Streptokinase
 • Urokinase
 • Vorapaxar
 • Abciximab

Ikiwa umegundulika kuwa una kiharusi, shauriana na daktari wako kabla ya kuanza au kuacha kutumia hizo dawa .

Jinsi ya Kuzuia/Kujikinga dhidi ya kiharusi

 • Kufuata mfumo wa maisha mzuri: Epuka kuvuta sigara, uwe na lishe bora na fanya mazoezi ili kudhibiti uzito wako.
 • Zingatia matibabu ya shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa kisukari na magonjwa mengine ya ateri.
 • Tumia dawa za kuzuia kiharusi kama uko kwenye hatari sana ya kupata kihrusi
  • Anti-platelets, kama vile aspirin, clopidogrel au ticlopidine
  • Anticoagulants, kama heparin na warfarin

Nitarajie nini baada ya kupata kiharusi?

Matarajio baada ya kugundulika kuwa una kiharusi hutegemea mambo yafuatayo:

 • Eneo la ubongo lililopata uharibifu: Ikiwa kuna eneo kubwa lililoathiriwa na kiharusi kinachosababishwa na kuvuja damu kwenye ubongo,mgonjwa huwa katika hatari kubwa ya kupoteza maisha.
 • Muda uliotumika kumfikisha mgonjwa katika idara ya dharura tangu alipopata dalili za mwanzo za kiharusi: Mgonjwa anapofikishwa mapema kwenye kituo cha afya uwezekano wa kupata matokeo bora unaongezeka,lakini anapochelewa sana matokeo ya matibabu huwa ya wasiwasi.
 • Ikiwa ugonjwa wa kiharusi umeambatana na matatizo/athari kubwa zitokanazo na shambulio,matarajio ya maisha bora yanapungua.
 • Athari ya matibabu ya ukarabati: Matibabu ya ukarabati yakifanyika vyema huongeza uwezekano wa kuishi maisha bora zaidi baadae.Ukarabati hufanyika kurudisha kazi za viungo zilizopotea au kudhoofu baada ya shambulio.

Matatizo/athari zinazoweza kutokea baada ya kiharusi.

 • Chakula kuingia kwenye mfumo wa hewa ,hii inaweza kuwa hatari.
 •  Kupungua kwa muda wa kuishi (hufupisha maisha)
 • Ugumu wa kuwasiliana,mgonjwa hushindwa kuongea vyema.
 • Kuvunjika kwa mifupa ya mwili (Fractures
 • Utapia mlo  
 • Kukakamaa kwa misuli
 • Ubongo kukoma kabisa kufanya kazi yake
 • Kupoteza kabisa uwezo wa kuhisi sehemu moja ya mwili au zaidi,na tatizo hili linaweza kuwa la kudumu.
 • Matatizo yatokanayo na kushindwa kujongea, ikiwa ni pamoja na viungo vya mwili kukakamaa na vidonda vitokanavyo na kulala sana.
 • Kupungua kwa uwezo wa kufanya kazi au kujitunza mwenyewe.
 • Kupungua kwa ushiriki katika mambo ya kijamii
 • Madhara yatokanayo na dawa anazotumia mgonjwa.

Vyanzo

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/stroke.html

http://www.ninds.nih.gov/disorders/stroke/stroke.htm

Leave Your Comment