Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Kipindupindu (cholera) ni ugonjwa unasababishwa na maambukizi ya bakteria aina ya vibrio cholerae. Mara nyingi maambukizi huwa ya kawaida na yanaweza yasisababishe dalili yoyote. Lakini wakati mwingine yanaweza kuwa hatari sana. Takribani mtu moja kati ya 20 wanaoambukizwa kipindupindu, huwa na dalili kali, dalili hizi ni pamoja na kuhara majimaji na kutapika. Wagonjwa wa kipindupindu hupoteza maji mengi kwa haraka sana, hii husababisha kuishiwa maji mwilini. Bila matibabu, kifo kinaweza kutokea ndani ya masaa machache.
Je, nini dalili za kipindupindu?
Ifuatayo ni orodha ya dalili za kipindupindu:
- Maumivu ya tumbo
- Kukauka kwa midomo
- Ngozi kavu
- Kuwa na kiu sana
- Macho yaliyoingia/yaliyorudi ndani
- Kushindwa kutoa machozi
- Uchovu
- Mkojo kidogo
- Upungufu wa maji mwilini
- Mapigo ya moyo yanayoenda mbio
- Kubonyea kwa utosi wa mtoto mchanga
- Kuchoka sana kuliko kawaida
- Kutapika
- Kuhara kinyesi kama majimaji ya mchele yenye kiharufu cha “samaki”
Kipindupindu husababishwa na nini?
Kipindupindu husababishwa na bakteria aina ya vibrio cholerae. Bakteria hawa hutoa sumu ambayo husababisha kutolewa kwa maji mengi ndani ya utumbo, ambayo husababisha kuhara. Kipindupindu hutokea zaidi katika maeneo yenye usafi duni, yenye msongamano mkubwa wa watu, vita na ukame. Maeneo yanayopata kipindupindu mara wa mara ni pamoja na:
- Afrika
- Asia
- India
- Mexico
- Amerika ya Kusini na Kati
Watu hupata maambukizi baada ya kula vyakula au kunywa maji yenye bakteria.
Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata kipindupindu?
Kuna uwezekano mkubwa wa kupata kipindupindu kama:
- Utakunywa wa maji yaliyochafuliwa au yasiyochemshwa au kutibiwa
- Unaishi au unasafiri kwenda katika maeneo yenye kipindupindu
- Watu wengi watapoteza makazi yao kutokana na janga i (k.m., tetemeko la ardhi, vimbunga, makambi ya wakimbizi, nk)
Utambuzi wa kipindupindu
Vipimo vinavyoweza kufanyika ni pamoja na:
- Culture ya damu
- Culture ya kinyesi
*Culture- Katika kipimo hiki, sampuli hupandwa katika sahani maalumu ili kuruhusu vimelea waliomo kukua haraka ili watambuliwe kwa urahisi.
Wakati gani utafute matibabu haraka?
Mwone mtoa huduma wa afya kama:
- Unaharisha uharo kama majimaji
- Una ishara za kuishiwa maji mwilini, kama:
- Midomo mikavu
- Ngozi kavu
- Macho yaliyorudi/ yaliyodumbukia ndani
- Uchovu
- Hakuna machozi
- Mapigo ya moyo yanayonda mbio
- Kupunguza au hakuna mkojo
- Kiu kikali
- Unahisi uchovu sana au kama unasinzia sinzia
Uchaguzi wa matibabu ya kipindupindu
Kipindupindu hutibiwa kwa urahisi na kwa ufanisi kwa kumwongezea mgonjwa maji na chumvi aliyopoteza baada ya kuharisha. Wagonjwa wanaweza kutibiwa kwa kunywa oral rehydration salt (ORS) (Huu ni mchanganyiko maalumu wa chumvi na sukari unaopaswa kuchanganywa na maji safi kabla ya kunywa.) Unapaswa kunywa kiasi kikubwa cha mchanganyiko huu ili kufidia chumvi na maji yanayopotea kwa kuharisha. Mchanganyiko huu hutumika duniani kote kutibu kuhara. Watu wenye hali mbaya zaidi, wataongezewa maji kupitia kwenye mishipa yao. Wagonjwa wa kipindupindu wakiongezewa maji mwilini mapema iwezekanavyo,zaidi ya 99% hupona kabisa. Dawa za antibiotiki husaidia kupunguza makali ya ugonjwa, lakini kuongezewa maji mwilini ni muhimu zaidi.
Nini cha kutarajia?
Upungufu mkubwa wa maji mwilini unaweza kusababisha kifo. Baada ya kupewa maji ya kutosha, watu wengi hupona kabisa.
Matatizo yanayoweza kutokea
Kuzuia kipindupindu
Japo chanjo ya kipindupindu inapatikana, haitolewi katika nchi nyingi duniani. Wakati wa mlipuko wa kipindupindu, jitihada zinapaswa kuelekezwa kupata maji safi, chakula, na usafi wa mazingira, hii ni kwa sababu chanjo haifai sana wakati wa mlipuko. Wasafiri na watu wanaoishi katika maeneo yenye kipindupindu wanapaswa kufanya mambo yafuatayo:
- Kunywa maji yaliyochemshwa au kutibiwa kwa klorini au iodini. Vinywaji vingine vilivyo salama ni pamoja na chai na kahawa iliyotengenezwa kwa maji yaliyochemshwa na na vinywani vya chupa.
- Kula vyakula ambavyo vimepikwa vizuri na vikiwa vya moto
- Kula matunda uliyomenya mwenyewe
- Epuka kula samaki wabichi au ambao hawajaiva vyema
- Hakikisha kila mbogazimepikwa vyema, epuka kula kachumbari/saladi.
- Epuka kula vyakula na vinywaji kutoka kwa wachuuzi wa mitaani.
MAELEZO ZAIDI KWA UFUPI KUHUSU KIPINDUPINDU
Maelezo ya jumla
Ni ugonjwa mkali unaosababishwa na vibrio cholerae
Sababu
Vibrio cholerae
Epidemiolojia
Kumetokea milipuko kadhaa ya ugonjwa huu katika sehemu mbalimbali duniani na wakati mwingine kuwa janga.
Umbukizo
kwa kula chakula au kunywa maji yaliyochafuliwa na kinyesi au matapishi ya mtu alaiyeambukizwa
Muda mpaka dalili kuanza kuonekana
Masaa machache mpaka siku 5, kwa kawaida ni siku 2-3.
Muda wa uambukizo
Mgonjwa anaweza kuendelea kuambukiza wengine wakati wote kinyesi chake kinapokuwa na vimelea, hii mara nyingi ni mpaka siku chache baada ya kupona. Kutumia dawa za antibiotiki zinafupisha muda wa uambukizo.
Dalili
- Kuhara kwa ghafla kinyesi cha majimaji; kinyesi kinaonekana kama maji ya mchele
- Kwa visa vikali, kiasi cha lita kadhaa za maji yanayaweza kupotea kutoka mwili kwa masaa machache tu na kusababisha mshtuko
- Wagonjwa wenye ugonjwa mkali, midomo inabadilika rangi kuwa bluu, macho na mashavu yandumbukia ndani, tumbo linarudi ndani, ngozi inalegea na mapigo ya moyo yanaweza yasisikike kabisa.
- Upotevu wa maji mwilini unaendelea kwa siku 1-7
Utambuzi
- Unafanyika kwa kuangalia dalili na ishara
- Kupandikiza kinyesi – culture – kunafanyika ili kuhakikisha
Matibabu
- Kuongeza haraka maji na chumvi chumvi zilizopotea ktoka mwilini
- Kumwongezea mgonjwa maji kupitia mishipa haraka
- Dawa za antibiotiki kama tetracycline hupunguza haraka kuhara na kusababisha iwe rahisi kupona
Kuzuia
- Kutibu wagonjwa mapema
- Kutumia vyema choo na kudhibiti nzi
- Uwepo wa maji safi na salama kwa wanajamii
- Kunawa mikono na usafi unaposhughulika na chakula
- Kudhibiti na kutibu watu wanaoishi au waliokutana na mgonjwa
Leave feedback about this