KISONONO

KISONONO

 • November 22, 2020
 • 0 Likes
 • 279 Views
 • 0 Comments

Maelezo ya jumla

Kisonono (Gonorrhea) ni ugonjwa wa zinaa.

Je, Nini dalili za kisonono?

Dalili za kisonono huanza kuonekana siku 2 – 5 baada ya kuambukizwa. Hata hivyo, kwa wanaume, dalili zinaweza kuchelewa mpaka mwezi. Watu wengine hawapati dalili kabisa. Wanaweza kuwa hawajui kabisa kwamba wameambukizwa ugonjwa huu, na kwa sababu hiyo hawatafuti matibabu. Hii huongeza uwezekano wa kupata matatizo na hatari ya kuambukiza wengine.

Dalili kwa wanaume ni pamoja na:

 • Maumivu wakati wa kukojoa
 • Kukojoa mara kwa mara au kushindwa kuzuia mkojo (mgonjwa akibanwa mkojo, ni lazima akakojoe haraka sana)
 • Kutoa uchafu kwenye uume (uchafu unaweza kuwa mweupe, njano, au rangi ya kijani)
 • Wekundu au kuvimba kwa urethra (huu ni mrija unaobeba mkojo kutoka kwenye kibofu kwenda nje)
 • Kuvimba na kuuma kwa korodani
 • Maumivu kwenye koo

Dalili kwa wanawake zinaweza kuwa ndogo sana na zisizo maalam, na huenda zikachanganywa na dalili za maambukizi mengine.

Dalili kwa wanawake ni pamoja na:

 • Kutoa uchafu ukeni
 • Maumivu wakati wa kukojoa
 • Kukojoa mara kwa mara/mara nyingi
 • Maumivu kwenye koo
 • Maumivu wakati wa ngono
 • Maumivu makali kwenye sehemu ya chini ya tumbo (kama maambukizi yataenea mpaka kwenye mirija ya uzazi)
 • Homa (Kama maambukizi yataenea mpaka kwenye mirija ya uzazi au eneo zima la tumbo)

Kama maambukizi yataenea kwenye damu, homa, kuwashwa, na dalili kama za yabisi kavu zinaweza kutokea.

Kisonono husababishwa na nini?

Kisonono husababishwa na bakteria anayeitwa  Neisseria gonorrhoeae. Mtu yeyote anayefanya ngono ya aina yoyote anaweza kuambukizwa kisonono. Maambukizi yanaweza kuenezwa kwa mdomo, uke, uume au mk*ndu. Bakteria  huyu hukua kwenye maeneo ya joto na yenye unyevu, hii ni pamoja na mrija unaotoa mkojo mwilini (urethra). Kwa wanawake, bakteria hupatikana kwenye via vya uzazi ( hii hujumuisha mirija ya uzazi, mji wa mimba, na mlango wa mji wa mimba). Bakteria hawa wanaweza kukua hata machoni.

Nani yuko kwenye hatari zaidi?

Kuna uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi ya kisonono kama:

 • Una washirika wengi wa ngono
 • Una mpenzi mwenye historia ya kupata magonjwa ya zinaa
 • Hautumii kondomu wakati wa ngono
 • Wewe ni mwanaume unayefanya ngono na mwanaume mwingine
 • Unatumia madawa ya kulevya

Utambuzi

 • Kisonono hutambuliwa baada ya sampuli ya tishu au uchafu unaotoka ukeni/ kwenye uume kutiwa rangi (gram stain) na kisha kuchunguzwa chini ya darubini. Japo njia hii ya utambuzi ni ya haraka, si ya kuaminika sana. Sampuli kwa ajili ya gram stain huchukuliwa:
  • Kwenye mlango wa kizazi cha mwanamke
  • Uchafu unaotoka kwenye uume wa mwanaume
  • Majimaji kutoka kwenye maungio ya mwili-joints
 • Culture (sampuli huchukuliwa na kupandwa kwenye sahani maalumu ya maabara, njia hii huwaruhusu bakteria kukua – utambuzi hufanyika kwa urahisi wakikua ), njia hii ni ya kuaminika zaidi. Sampuli kwa ajili ya culture huchukuliwa:
  • Kwenye kizazi na mlango wa kizazi cha mwanamke
  • Uchafu unaotoka kwenye uume wa mwanaume
  • Kooni kwa wanaume na wanawake
  • Mk*nduni kwa wanaume na wanawake
  • Majimaji kutoka kwenye maungio ya mwili- joints
  • Damu

Matokeo ya awali ya culture hutoka baada ya masaa 24 na matokeo thabiti ndani ya masaa 72.

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Kama una dalili za kisonono unapaswa kumwona daktari mapema iwezekanavyo.

Uchaguzi wa matibabu

Kuna malengo mawili katika kutibu magonjwa ya zinaa, hasa ambayo yanaenea kwa urahisi kama kisonono. La kwanza ni kutibu maambukizi ya mgonjwa. La pili ni kuwatafuta na kuwapima watu wengine wote ambao wamefanya ngono na mgonjwa, ili kuwatibu na kuzuia maambukizi zaidi. Usijitibu mwenyewe bila kuonwa na daktari kwanza. Mtoa huduma wa afya ataamua ni matibabu gani yaliyo bora zaidi. Matibabu yanayopendekezwa ni pamoja na:

 • Sindano moja ya ceftriaxone 125 mg au kumeza dozi moja ya cefixime 400mg.
 • Dozi moja ya Azithromycin 2g inaweza kutumika kwa watu wenye mzio kwa ceftriaxone, cefixime, au penicillin.

Mgonjwa anapaswa kurejea hospitalini baada ya siku 7. Vipimo vitafanywa tena, kuhakikisha maambukizi yamekwisha. Watu wote waliofanya ngono na mgonjwa wanapaswa kutafutwa ili wapimwe na kutibiwa. Hii hupunguza kuenea kwa kisonono.

Nini cha kutarajia?

Kwa karibu mara zote, maambukizi ya kisonono ambayo hayajaenea kwenye damu au maeneo mengine hupona vyema baada ya kutumia antibiotiki. Kisonono ambayo imeenea ni tatizo kubwa, lakini pia hupona baada ya matibabu.

Matatizo yanayoweza kutokea

Matatizo yanayoweza kutokea kwa wanawake ni pamoja:

 • Kuharibika kwa mirija ya uzazi (salpingitis ) – hii inaweza kusababisha ashindwe kupata mimba au kusababisha mimba itungwe nje ya mji wa mimba (ectopic pregnancy).
 • Ugumba (kukosa uwezo wa kuwa mjamzito)
 • Maumivu wakati wa ngono
 • Wanawake wajawazito wenye kisonono wanaweza kuwaambukiza watoto wao wakiwa tumboni au wakati wa kuzaliwa

Matatizo kwa wanaume ni pamoja na:

 • Mgonjwa anaweza kupata makovu yanayoweza kusababisha kuziba kwa njia ya mkojo (urethra)- hii inaweza kusababisha shida wakati wa kukojoa
 • Jipu (usaha kwenye urethra)
 • Matatizo wakati wa kukojoa
 • Maambukizi kwenye njia ya mkojo
 • Kushindwa kwa figo kufanya kazi

Matatizo yanayoweza kuwapata wanaume na wanawake ni pamoja na:

 • Kusambaa kwa maambukizi mwili mzima- hii inaweza kuwa hatari sana
 • Kama mgonjwa hatatibiwa mapema, anaweza kuwa na maumivu ya muda mrefu ya maungio (joints).
 • Maambukizo ya vali za moyo
 • Kuvimba kwa tando za uti wa mgongo au ubongo

Vyanzo

http://wikidoc.org/index.php/Gonorrhea

 • Share:

Leave Your Comment