Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Kisukari aina ya 1 huwapata zaidi watoto na vijana wadogo. Kisukari ni ugonjwa ambao mgonjwa huwa na kiwango cha juu cha sukari kwenye damu kuliko kawaida.Mwili wa mgonjwa wa kisukari aina ya 1 hautengenezi insulini. Mfumo wa kinga ya mwili hushambulia na kuharibu seli za kongosho zinazozalisha insulini. Insulini ni homoni inayohitajika kuingiza sukari iliyo kwenye damu ndani ya seli za mwili ili kutumika kama nishati. Sababu za kisukari aina ya 1 ni tofauti na zile za kisukari aina ya 2. Kisukari aina ya 1 hudhaniwa kuanza baada ya tukio fulani la kimazingira, kama maambukizi ya virusi yanayopelekea mfumo wa kinga ya mwili kushambulia na kuharibu seli za kongosho.
Dalili za kisukari aina ya 1
Mtu anayedhani ana kisukari anapaswa kumwona daktari ili atambuliwe. Mgonjwa wa kisukari anaweza asiwe na dalili yoyote au anaweza kuwa na moja ya dalili zifuatazo:
- Kukojoa mara kwa mara
- Kuhisi kiu kikali
- Kupungua kwa uzito bila sababu ya msingi
- Kuhisi njaa kali
- Mabadiliko ya ghafla ya uwezo wa kuona
- Ganzi kwenye mikono au miguu
- Uchovu
- Ngozi kavu sana
- Vidonda vinavyochelewa kupona
- Maambukizi ya mara kwa mara kuliko kawaida
- Kichefuchefu, kutapika au kuumwa tumbo
Magonjwa yenye dalili sawa
- Kisukari aina ya 2
- Ugonjwa unaosababisha mgonjwa kukojoa sana unaoitwa diabetes inspidus unaotokana na kupungua kwa homoni ya ADH (antiduretic hormone)
- Kisukari wakati wa ujauzito
Ni nini husababisha kisukari aina ya 1
Kuna aina kadhaa za ugonjwa wa kisukari. Kisukari aina ya 1 inaweza kutokea katika umri wowote, lakini hutambuliwa zaidi kwa watoto na vijana wadogo.
Insulini ni homoni inayozalishwa na seli maalum za kongosho zinazoitwa beta. Kongosho ni kiungo kinachopatikana nyuma ya tumbo. Insulini huhitajika ili kuingiza sukari ndani ya seli ili kutunzwa na kutumika kama nishati. Kwa wagonjwa wa kisukari aina ya 1 seli hizi huzalisha insulini kidogo au hazizalishi kabisa insulini.
Bila ya insulini ya kutosha, glukozi/sukari hurundikana kwenye damu badala ya kuingia kwenye seli za mwili. Mwili unapokosa chanzo chake cha nishati, huanza kuonesha dalili za kisuakri.
Ndani ya miaka 5-10, seli za beta zinazozalisha insulini huharibika kabisa na kushindwa kabisa kuzalisha insulini.
Sababu halisi ya kisukari aina ya 1 haijulikani, lakini mara nyingi huwapata watu wenye jeni (gene) hatarishi baada ya kupata virusi au mabadiliko ya kimazingira yanayosababisha mfumo wa kinga ya mwili kuharibu seli za kongosho. Seli nyeupe za damu huharibu seli za kongosho kwa bahati mbaya wakati wa harakati za kudhibiti virusi hivyo.
Ni nani aliye katika hatari zaidi ya kisukari aina ya 1?
Mambo yanayoongeza hatari ya kupata kisukari aina ya 1 hayako bayana sana kama ilivyo kwa kisukari aina ya 2, lakini kinga ya mwili, jeni na mazingira huhusishwa na kutokea kwa kisukari aina ya 1.
Wakati gani utafute matibabu ya haraka?
Kwa nini ni muhimu kudhibiti kisukari ?
Baada ya miaka mingi, ugonjwa wa kisukari unaweza kusababisha matatizo makubwa ya macho, figo, neva, fizi na meno. Lakini tatizo kubwa zaidi linalosababishwa na ugonjwa wa kisukari ni ugonjwa wa moyo. Unapokuwa na ugonjwa wa kisukari, unakuwa na hatari mara mbili zaidi ya kupata ugonjwa wa moyo au kiharusi ukilinganisha na watu wasio na kisukari. Ukiwa na kisukari hatari ya kupata mshtuko wa moyo ni sawa na ya mtu aliyekwisha kupata mshtuko wa moyo. Unaweza hata usiwe na dalili za kawaida za mshtuko wa moyo. Unaweza kupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa wa moyo kwa kudhibiti kiwango cha shinikizo la damu na mafuta mwilini. Acha kuvuta sigara kama unavuta.
Mtu yeyote mwenye umri wa miaka 45 au zaidi anapaswa kupimwa ili kuangalia kama ana kisukari, hasa kama ana uzito mkubwa. Kama una miaka chini ya 45 lakini una uzito mkubwa na una moja au zaidi ya mambo yanayoongeza hatari, unapaswa kupima pia.
Unapaswa kutafuta msaada wa kitabibu haraka iwezekananvyo kama kiwango cha sukari yako kiko juu sana au chini sana kabla haujapoteza fahamu au kuingia kwenye koma.
Utambuzi wa kisukari aina ya 1
Kisukari hutokea wakati mwili unaposhindwa kudhibiti sukari katika damu, sukari inaporundikana katika damu yaweza kufikia viwango vya hatari, ili kujua viwango vya sukari katika damu vipimo vya sukari hufanyika,na vipimo vifuatavyo huonesha kama mgonjwa ana kisukari
- Kipimo cha sukari kinapoonesha zaidi ya 7.0 mmol/L baada ya kufunga bila kula kwa muda wa saa nane (fasting blood glucose).
- Kipimo cha sukari kipimwacho wakati wowote (random blood glucose) kinapoonesha zaidi ya 11.1 mmol/L ,huku kukiwepo na dalili zozote za kisukari.
Ukibainika una kiwango cha juu cha sukari katika damu yako na daktari hajaridhika na majibu, anaweza kupendekeza kurudia kipimo hicho siku inayofuata, itapendeza zaidi kama utafunga kwa muda wa saa nane kabla ya kipimo ili kujiridhisha na matokeo.
Kulingana na shirika la afya duniani (WHO), watu wenye viwango vya glukosi kutoka 6.1 hadi 6.9 mmol /L baada ya kufunga masaa manane,wako kwenye hatari ya kupata kisukari na magonjwa ya moyo
Uchaguzi wa matibabu ya kisukari aina ya 1
Lengo kuu la matibabu ni kudhibiti kiwango cha sukari katika damu ili kupunguza uwezekano wa kupata matatizo yatokanayo na kisukari. Watu wenye kisukari wanapaswa kumwona mtumishi wa huduma ya afya ili kupata elimu jinsi ya kudhibiti kisukari. Watu wenye kisukari aina ya 1 huhitaji kuchomwa sindano ya insulini ili kudhibiti viwango vya sukari kwenye damu.
Kuishi kwa afya
Kula kwa afya, kufanya mazoezi ya kimwili, na kupima kiwango cha sukari kwenye damu, ndiyo tiba ya msingi zaidi kwa wagonjwa wa kisukari aina ya 1. Watu wenye ugonjwa wa kisukari wanapaswa kuchukua jukumu la kujihudumia siku hadi siku, na kuhakikisha kiwango cha sukari hakishuki chini sana au hakipandi juu sana. Kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu ndiyo muhimili mkuu wa tiba na maisha ya mtu mwenye kisukari. Kipimo cha sukari hukuambia kiwango cha sukari kwenye damu kwa wakati huo. Tunza kumbukumbu (record) ya viwango vya sukari kila unapopima. Unapopeleka record ya aina hii kwa daktari, humsaidia kupata picha kamili ya juhudi zako na humsaidia kuweka sawa mpango wako wa kudhibiti kisukari. Kupima mara kwa mara, hukusaidia kutambua ni dawa gani au kitu gani kinachosaidia hali yako kuwa njema au mbaya zaidi. Taarifa hizi zitatumika kufanya marekebisho katika mpango wa tiba ili kudhibiti vyema kisukari.
Je, unapimaje sukari kwenye damu?
Unatoboa kidole chako kwa kifaa maalumu kinachoitwa lancet ili kupata tone la damu kwa ajili ya kipimo. Kuna aina maalumu za lancet zenye spring zinazosaidia kupunguza maaumivu wakati wa kujitoboa. Kabla haujatumia lancet kujitoboa, nawa mikono vizuri kwa sabuni na maji. Vifaa vya kupimia sukari (blood glucose meters) husoma kiwango cha sukari kwenye damu pindi tu unapoweka tone la damu. Katika aina zote za mashine, kiwango cha sukari huonekana kama namba kwenye skrini (kama ilivyo kwenye kikokotoo/calculator). Hakikisha kuwa madaktari au manesi wanakufundisha vizuri namna ya kutumia mashine yako.
Kwa mara chache, unaweza kuhitajika kupima kiwango cha ketoni (ketones) kilicho kwenye mkojo wako. Ketoni kwenye mkojo ni ishara kuwa mwili unatumia mafuta badala ya glukozi kama nishati kwa sababu hakuna insulini ya kutosha kuingiza glukozi kwenye seli. Si ajabu kukuta ketoni kwenye mkojo wa wagonjwa wenye aina ya 1 ya kisukari.
Insulini
Ndani ya kongosho, seli za beta huzalisha insulini. Baada ya mlo, seli za beta huzalisha insulini ili kuusaidia mwili kutumia glukozi/sukari inayopatikana kutoka kwenye chakula. Watu wenye kisukari aina ya 1 hawazalishi insulini ya kutosha. Baadhi ya watu wenye kisukari huhitaji kuchomwa sindano za insulini ili kusaidia miili yao kutumia glukozi kama nishati.
Insulini haiwezi kumezwa kama kidonge. Insulini inapaswa kuchomwa kwenye utando wa mafuta ulio chini ya ngozi ili iweze kuingia kwenye damu. Kuna aina nyingi za insulini zinazotumika katika mazingira tofauti na kwa mifumo tofauti ya maisha. Aina hizi za insulini hutofautiana kwa jinsi zinavyotengenezwa, zinavyofanya kazi mwilini na bei.
Mengineyo
Kwa wakati fulani wagonjwa watahitajika kuonana na madaktari bingwa wa mfumo wa homoni (endocrinologists), madaktari bingwa wa macho (ophthalmologists) kwa ajili ya vipimo vya macho, Madaktari wa miguu (podiatrists) kwa huduma ya miguu na waelimishaji kuhusu ugonjwa wa kisukari.
Watu wazima wenye ugonjwa wa kisukari wana hatari kubwa ya kupata magonjwa ya moyo. Kama 65% ya wagonjwa wa kisukari hufa kutokana na magonjwa ya moyo au kiharusi. Kudhibiti kisukari ni zaidi ya kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu – ni muhimu pia kudhibiti shinikizo la juu la damu na kiwango cha lehemu mwilini kwa kula chakula chenye afya, kufanya mazoezi na matumizi ya dawa kama zitahitajika. Kwa kufanya hivyo, watu wenye kisukari wanaweza kupunguza hatari hii. Ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo, daktari anaweza kupendekeza matumizi ya dawa za aspirini na kuacha kuvuta sigara.
Madawa ya kuepuka
Nini cha kutarajia
Kushuka kwa kiwango cha sukari kwenye damu (hypoglycaemia) kunaweza kutokea hata kama unafanya kila kitu unachotakiwa kukifanya ili kudhibiti kisukari. Kwa hiyo, japo mara nyingi hauwezi kuepuka hali hii, unaweza kuitibu mapema kabla haijawa mbaya zaidi.
Dalili za kushuka kwa kiwango cha sukari katika damu ni pamoja na:
- Kutetemeka
- Kizunguzungu
- Kutokwa jasho
- Kuhisi njaa
- Maumivu ya kichwa
- Mabadiliko ya ghafla ya tabia na hali ya mgonjwa, kama vile kulialia bila sababu maalumu
- Degedege
- Kushindwa kuzingatia mambo au kuchanganyikiwa
Njia ya haraka ya kupandisha sukari kwenye damu ni kwa kutumia sukari, kama vile vidonge vya glukozi (unaweza kununua hizi duka la dawa), juisi ya matunda au pipi.
Kupanda kwa kiwango cha sukari kwenye damu hutokea kunapokuwa hakuna kiwango cha kutosha au hakuna kabisa insulini mwilini. Kama una aina ya 1 ya kisukari, mwili wako hautengenezi insulini kabisa. Kupanda kwa sukari kunaweza kutokana na kula zaidi ya kiwango unachotakiwa au kufanya mazoezi kidogo sana kuliko inavyotakiwa. Msongo unaotokana na ugonjwa kama mafua unaweza kuwa sababu pia. Sababu nyingine za msongo kama vile, matatizo ya kifamilia au shule au ya kimahusiano, yanaweza pia kupandisha sukari mwilini.
Ishara na dalili za kupanda kwa kiwango cha sukari mwilini ni pamoja na:
- Kiwango cha sukari kwenye damu huongezeka (ukipima damu)
- Kunakuwa na kiwango kikubwa cha sukari kwenye mkojo (mkojo unakuwa mtamu)
- Mgonjwa hukojoa mara kwa mara
- Mgonjwa huhisi kiu kikali
Ni muhimu kushusha kiwango cha sukari haraka iwezekanavyo la sivyo mgonjwa anaweza kupata tatizo hatari linaloitwa kitaalamu ketoacidosis ambalo linaweza kupelekea mgonjwa kuingia kwenye koma na hatimae kifo. Ketoacidosis hutokea wakati mwili hauna insulini ya kutosha.
Mara nyingi, unaweza kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu kwa kufanya mazoezi. Kupunguza kiasi cha chakula unachokula husaidia pia. Ni muhimu kujifunza ni nini kinachopandisha sana sukari yako na kukidhibiti.
Ketoacidosis ni hali ya hatari inayotishia maisha na inahitaji matibabu ya haraka. Inaweza kutokea kama ongezeko la kiwango cha sukari halitadhibitiwa.
Dalili za ketoacidosis ni pamoja na:
- Kuishiwa pumzi
- Pumzi inayonukia kama matunda (harufu ya pumzi ya mgonjwa inanukia vizuri kama tunda tamu)
- Kichefuchefu na kutapika
- Kukauka kwa midomo na kinywa
Matatizo yanayoweza kutokea
Magonjwa ya moyo na kiharusi
Watu wenye ugonjwa wa kisukari wako kwenye hatari zaidi ya kupata magonjwa ya moyo na magonjwa yanayoathiri mishipa ya damu. Ugonjwa wa kisukari huongeza maradufu hatari ya kupata mshtuko wa moyo, kiharusi na matatizo yanayotokana na mzunguko usio mzuri wa damu kwenye mwili. Watu 2 kati ya 3 wenye kisukari hufa kwa ugonjwa wa moyo au kiharusi. Matibabu ya kisukari ni zaidi ya kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu. Watu wenye kisukari wanapaswa kudhibiiti shikizo la damu, kiwango cha lehemu (cholesterol) na kuongea na watumishi wa afya ili kujifunza jinsi ya kupunguza uwezekano wa kupata mshtuko wa moyo au kiharusi. Pia, mabadiliko ya mfumo wa maisha kama vile kuchagua chakula bora, na kufanya mazoezi, na kutumia dawa za kisukari husaidia. Watu wengi wakibadilisha aina ya chakula wanachokula huleta mabadiliko makubwa ya kiwango cha sukari kwenye damu, shinikizo la damu na hata kiwango cha lehemu (cholesterol) mwilini.
Magonjwa ya figo
Kisukari kinaweza kuharibu figo, figo zinaweza kuharibiwa na kushindwa kabisa kufanya kazi ya kuchuja uchafu. Kisukari kinaweza kuharibu na kupunguza uwezo wa figo kuchuja damu. Kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu husababisha figo kuchuja damu nyingi zaidi kuliko kawaida. Kazi hii ya ziada huelemea figo na kusababisha baada ya miaka mingi kuanza kuvuja. Protini ambayo ni muhimu mwilini huanza kupotea kwenye mkojo. Hali ya kuwepo kwa kiwango kidogo cha protini kwenye mkojo huitwa microalbuminuria.
Ugonjwa wa figo ukigundulika mapema hasa kipindi cha microalbuminuria matibabu kadhaa yanaweza kusaidia figo zisiharibike zaidi. Kukiwa na kiwango kikubwa cha protini kwenye mkojo huitwa macroalbuminuria. Ugonjwa wa figo unapogunduliwa wakati wa macroalbuminuria uwezekano wa kurejesha figo katika hali njema huwa mdogo sana.
Mara nyingi figo zilizofikia katika hatua hii hushindwa kabisa kufanya kazi hapo baadae. Hali hii ya kushindwa kwa figo ni hatari sana. Mgonjwa mwenye figo iliyoshindwa kufanya kazi huhitaji kupandikiziwa figo nyingine (kidney transplant) au kuchujwa damu kwa mashine (dialysis) mara kwa mara. Magonjwa ya figo yanayotokana na kisukari yanaweza kuzuiwa kwa kudhibiti vyema kiwango cha sukari katika damu
Matatizo ya Macho
Watu wenye ugonjwa wa kisukari wana uwezekano wa zaidi ya 40% wa kupata ugonjwa wa glakoma (ugonjwa unaotanua mboni ya jicho na kutatiza kuona) kuliko watu wasio na kisukari. Kadri umri wa kuishi na ugonjwa kisukari unavyoongezeka ndivyo na uwezekano wa kupata glakoma unavyoongezeka. Glakoma hutokea shinikizo linapoongezeka ndani ya jicho, uwezo wa kuona hupungua polepole kwa sababu ya kuharibiwa retina (sehemu ya jicho inayopokea mwanga) na neva. Japo watu wengi wasio na kisukari hupata ugonjwa wa mtoto wa jicho (cataracts), watu wenye kisukari wana ongezeko la zaidi ya 60% la kupata tatizo hili. Watu wenye kisukari hupata tatizo hili katika umri mdogo na uwezo wao wa kuona hupotea haraka sana. Mtu anapokuwa na ugonjwa wa mtoto wa jicho lenzi ya jicho hujaa ukungu na kuzuia mwanga kuingia jichoni kwa urahisi.
Watu wanaodhibiti vyema kiwango cha sukari katika damu hupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya macho na hata wakipata, matatizo hayawi makubwa sana.
Matatizo ya mfumo wa neva
Mojawapo ya matatizo yanayotokea sana kwa wagonjwa kisukari ni matatizo ya mfumo wa neva yatokanayo na sukari. Uharibifu wa mishipa ya fahamu inayounganisha uti wa mgongo na misuli, ngozi, mishipa ya damu na viungo vingine. Kuna ina mbili za uharibifu wa mishipa ya fahamu. Ya kwanza huitwa peripheral neuropathy, hii husababisha maumivu, ganzi, au kuishiwa nguvu kwenye miguu au mikono. Aina ya pili huitwa autonomic neuropathy, hii husababisha:
- Matatizo ya mfumo wa kumeng’enya chakula, mgonjwa hujihisi ameshiba muda wote
- Kichefuchefu, kutapika, kuharisha au kufunga choo
- Matatizo ya kibofu
- Matatizo wakati wa kujamiiana
- Kizunguzungu au kuzirai/kuzimia
- Mgonjwa hushindwa kutambua ishara za kawaida za onyo za wakati wa mshtuko wa moyo
- Mgonjwa hushindwa kutambua ishara au dalili za onyo za kushuka kwa kiwango cha sukari mwilini.
- Kutokwa jasho sana au kutotoka jasho kabisa
- Mabadiliko ya jinsi macho yako yanavyopokea mwanga na giza
Watu wenye ugonjwa wa kisukari wanaweza pia kuwa na kile kinachojulikana kama focal neuropathy. Katika aina hii, neva au kundi fulani la neva huharibika na kusababisha shida ya ghafla au maumivu. Inaweza kusababisha kuona vitu viwili viwili, kupooza upande mmoja wa uso (Bell’s palsy), au maumivu ya sehemu ya mbele ya paja au sehemu nyingine yoyote ya mwili. Watu wenye ugonjwa wa kisukari wako kwenye hatari ya mishipa ya fahamu kukandamizwa. Kitu chochote mwilini kinaweza kukandamiza neva yoyote na kuizuia kutuma ishara (signal). Carpal tunnel syndrome ni mojawapo ya matatizo yanayotokea baada ya neva zinazopita katika kifundo cha mkono kukandamizwa na kusababisha ganzi, maumivu na udhaifu wa misuli ya vidole. Kudhibiti kiwango cha sukari katika damu husaidia kuzuia matatizo haya yasitokee au kupunguza dalili
Matatizo ya Miguu
Japo inaweza kuleta maumivu, uharibifu wa neva hupunguza uwezo wa kuhisi maumivu, joto na baridi. Kupungua kwa uwezo wa kuhisi humaanisha unaweza usijue ukiumia mguuni. Unaweza usijue kuwa umeumia mpaka unapopata kidonda. Uharibifu wa neva unaweza pia kusababisha mabadiliko ya mwonekano (shape) wa mguu na vidole.
Vidonda mara nyingi hutokea kwenye kisigino cha mguu au upande wa chini wa dole gumba la mguu. Kupuuza vidonda kunaweza kusababisha maambukizi yanayoweza kusababisha ukatwe mguu. Kwa sababu mzunguko wa damu hauko vyema, uwezo wa kupona na kupambana na maambukizo hupungua.
Ugonjwa wa kisukari husababisha mishipa ya damu ya mguu kuwa myembamba na iliyokakamaa. Unaweza kudhibiti baadhi ya mambo yanayoweza kuharibu mtiririko wa damu katika mishipa ya damu. Acha kuvuta sigara, kuvuta sigara husababisha mishipa ya damu kugangamara mapema. Kuna uwezekano mkubwa sana wa watu wenye kisukari kukatwa mikono au miguu ukilinganisha na watu wasio na kisukari.
Watu wenye kisukari wana magonjwa ya mishipa inayozuia mtiririko mzuri wa damu kwenda kwenye miguu. Pia, watu wengi wenye kisukari wana magonjwa ya neva yanayopunguza uwezo wa kuhisi. Kwa pamoja, matatizo haya mawili husababisha iwe rahisi kupata vidonda na maambukizi yanayoweza kupelekea ukatwe mguu au mkono. Moja ya tishio kubwa kwa miguu yako ni uvutaji wa sigara. Uvutaji wa sigara huathiri mishipa midogomidogo ya damu. Hupunguza mtiririko wa damu kwenye miguu na kusababisha vidonda kupona polepole. Watu wengi wenye kisukari wanokatwa miguu au mikono wanavuta sigara. Acha kuvuta sigara.
Matatizo ya tumbo
Wagonjwa wa kisukari aina ya 1 na ya 2 hupata matatizo ya tumbo yanayoitwa kitaalamu gastroparesis. Chakula huchukua muda mrefu kusafiri kutoka kwenye tumbo (chakula hukaa tumboni kwa muda mrefu isivyo kawaida). Tatizo hili husababishwa na kuharibika kwa neva zinazopeleka taarifa tumboni. Neva inayoitwa Vagus hudhibiti mjongeo wa chakula kwenye mfumo wa kumeng’enya chakula. Kama neva ya vagus ikiharibika, misuli ya tumbo na utumbo haifanyi kazi vizuri, kwa sababu hiyo mjongeo wa chakula tumboni/utumboni hupungua au kusimama kabisa.
Gastroparesis inaweza kusababisha udhibiti wa sukari kwa wagonjwa wa kisukari kuwa mgumu zaidi. Chakula kilichocheleweshwa tumboni kinapoingia kwenye utumbo na kunyonywa/kufyonzwa husababisha kiwango cha sukari kwenye damu kupanda. Chakula kinapokaa muda mrefu tumboni huchacha na kusababisha bakteria kukua sana. Pia, chakula kinaweza kushikamana na kusababisha mabonge magumu yanayoweza kusababisha kichefuchefu, kutapika na hata kuziba kwa tumbo. Ni tatizo kubwa na hatari tumbo linapoziba na kusababisha chakula kushindwa kujongea kuingia kwenye utumbo.
Matatizo mengine
- Kushindwa kusimamisha wakati wa kujamiiana
- Maambukizi ya ngozi, via vya uzazi vya wanawake, na njia ya mkojo
Kuzuia
Hakuna njia inayofahamika ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa kisukari aina ya 1
Leave feedback about this