Magonjwa ya ndani ya mwili

KISUKARI AINA YA 2:Sababu,dalili,matibabu

Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko

Maelezo ya jumla

Mgonjwa wa kisukari huwa na kiwango cha juu cha sukari kwenye damu kuliko ilivyo kawaida. Kisukari aina ya 2, ndiyo aina ya kisukari inayowapata watu wengi zaidi, karibia 90-95% za wagonjwa wote wanaotambuliwa kuwa na kisukari huwa na aina hii ya kisukari. Wagonjwa wa aina ya 2 ya kisukari hawatengenezi insulini ya kutosha mwilini au kama wanatengeneza insulini, miili yao huipuuza/ haiitikii mchocheo unaosababishwa na homoni hii.
Insulini ni muhimu sana, kwa sababu huusaidia mwili kutumia sukari iliyomo mwilini kama nishati kwa shughuli zake za kila siku. Unapokula chakula, mwili humeng’enya na kuvunjavunja wanga zote mwilini kuwa sukari/glukozi, ambayo hutumiwa na seli zote mwilini kama nishati. Kama sukari haitatumika na kuachwa imetwama kwenye damu, inaweza kusababisha matatizo ya aina mbili, Mwanzoni, seli za mwili hukosa chanzo chao cha nishati na baadae kadri kiwango cha sukari kinavyoongezeka huanza kuharibu macho, figo, mishipa ya fahamu au moyo

Dalili za kisukari aina ya 2

Kisukari kinapokunyemelea

Kabla watu hawajapata ugonjwa wa kisukari aina ya 2, karibu mara zote hupitia wakati wa kisukari nyemelezi ”pre- diabetes”. Katika kipindi hiki, kiwango cha sukari kwenye damu kinakuwa kiko juu lakini kinakuwa bado hakijafikia viwango vya kuitwa kisukari. Karibu 11% ya watu walio katika hatua za kunyemelewa na kisukari huugua ugonjwa wa kisukari kila mwaka. Tafiti nyingine zinaonesha kuwa watu wengi zaidi wenye kunyemelewa na kisukari wanaishia kuugua kisukari ndani ya miaka 10. Tafiti nyingine zinaonesha kuwa, matatizo ya muda mrefu yanayosababishwa na kisukari yanaweza kuwa yameanza tayari katika kipindi cha kunyemelewa na kisukari.

Dalili za kisukari aina ya 2

Watu wenye ugonjwa wa kisukari wanaweza wasioneshe dalili yoyote au wanaweza kuonesha baadhi ya dalili zifuatazo:

 • Kukojoa mara kwa mara
 • Kiu kikali kuliko kawaida
 • Kupungua kwa uzito wa mwili bila sababu yoyote ya msingi
 • Kuhisi njaa kali sana
 • Kubadilika ghafla kwa uwezo wako wa kuona
 • Kuhisi ganzi au kuhisi kama vitu (visindano) vinakuchomachoma mikononi au miguuni
 • Uchovu
 • Ngozi kavu sana
 • Vidonda ambavyo huchukua muda mrefu sana kupona
 • Kupata maambukizi mara nyingi kuliko kawaida

Matatizo yenye dalili sawa na kisukari aina ya 2

 • Ugonjwa wa kisukari aina ya 1
 • Ugonjwa unaosababisha mgonjwa kukojoa sana na kupoteza maji kwa wingi unaoitwa ”diabetes inspidus”
 • Kisukari cha wakati wa ujauzito

Nini sababu ya kisukari aina ya 2?

Ugonjwa wa kisukari hutokea kunapokuwepo na tatizo kwenye mfumo wa utengenezaji na utumizi wa nisulini mwilini. Insulini inahitajika kwa ajili ya kuhamisha/kuingiza sukari ndani ya seli za mwili kutoka kwenye damu kwa ajili ya matumizi ya baadae.
Unapokuwa na ugonjwa wa kisukari aina ya 2, mwili wako hauitikii vyema vichocheo vya insulini. Mgonjwa wa aina hii, anasemekana kuwa na usugu dhidi ya insulini. Usugu kwa insulini humaanisha kuwa mafuta, ini, na seli za misuli haziitikii kwa usahihi vichocheo vinavyotolewa na insulini. Na matokeo yake sukari iliyomo kwenye damu haingii kwenye seli za mwili kwa ajili ya matumizi.
Sukari inaposhindwa kuingia ndani ya seli za mwili, kiwango chake huongezeka sana kwenye damu. Kiwango cha sukari kinapoongezeka kwenye damu, kinasababisha kongosho kuzalisha insulini kwa wingi zaidi na zaidi, lakini hata hivyo bado insulini inayozalishwa haitoshi kukidhi mahitaji ya mwili. Watu wenye uzito mkubwa wako kwenye hatari zaidi ya kuwa na Usugu kwa insulini kwa sababu mafuta ya mwili yanaathiri uwezo wa kutumia insulini.
Watu wengi wenye ugonjwa huu wana uzito mkubwa kuliko kawaida, lakini hii haimaanishi kuwa watu wembaba hawawezi kuupata. Kutokea kwa kisukari aina ya 2 kunahusishwa sana na historia ya kifamilia na maumbile ”genetics”. Kutokufanya mazoezi, chakula kisicho bora na uzito mkubwa wa mwili huongeza maradufu uwezekano wa kupata kisukari aina ya 2.

Nani aliye kwenye hatari zaidi ya kupata kisukari aina ya 2?

Sababu zinazoongeza hatari ya kupata kisukari aina ya 2 ni pamoja na:

 • Uzee
 • Kitambi au kuwa na uzito mkubwa sana
 • Kuwepo kwa historia ya kifamilia ya ugonjwa wa kisukari
 • Kuwa na historia ya kupata kisukari wakati wa ujauzito – hii ni aina ya kisukari inayowapata wanawake wajawazito na hupona mara tu baada ya kujifungua.
 • Au kama ameshawahi kuzaa mtoto mwenye kilo zaidi ya 4Kg
 • Karibu asilimia 40 ya wanawake wenye historia ya kupata ugonjwa wa kisukari wakati wa ujauzito hupata kisukari aina ya 2 baadae
 • Shinikizo la juu la damu zaidi ya 140/90 mmHg
 • Kuwa na kiwango kikubwa cha lehemu kwenye damu
 • Kutofanya mazoezi ya mwili (kutofanya mazoezi angalau mara 3 kwa wiki)
 • Asili

Wamarekani wenye asili ya Afrika, walatino, Wahindi, na watu wa Asia wana hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kisukari aina ya 2.

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Mtu yeyote mwenye umri wa miaka 45 au zaidi anapaswa kupimwa kama ana ugonjwa wa kisukari, hasa kama ana kitambi/uzito mkubwa sana. Kama una miaka chini ya 45, lakini una uzito mkubwa na una mojawapo ya mambo mengine yanayoongeza hatari ya kupata kisukari, unapaswa kupimwa.
Pia, kama kiwango cha sukari kwenye damu kitakuwa juu sana au chini sana, unahitaji huduma ya kitabibu ili kuzuia kupoteza fahamu au kuingia kwenye koma inayosababishwa na kisukari.

Utambuzi wa kisukari aina ya 2

Kisukari kinatokea kwa sababu mwili umeshishindwa kudhibiti uzalishaji na matumizi ya sukari, sukari inaporundikana kwenye damu inaweza kufikia viwango vya hatari, ili kujua viwango vya sukari katika damu vipimo vya sukari hufanyika, na vipimo vifuatavyo huonesha kama mgonjwa ana kisukari

 • Kipimo cha sukari kinapoonesha zaidi ya 7.0 mmol/L baada ya kufunga bila kula kwa muda wa saa nane ”fasting blood glucose”.
 • Kipimo cha sukari kipimwacho wakati wowote ”random blood glucose” kinapoonesha zaidi ya 11.1 mmol/L ,huku kukiwepo na dalili zozote za kisukari.

Ukibainika una kiwango cha juu cha sukari katika damu yako na daktari hajaridhika na majibu, anaweza kupendekeza kurudia kipimo hicho siku inayofuata, itapendeza zaidi kama utafunga kwa muda wa saa nane kabla ya kipimo ili kujiridhisha na matokeo.,

Uchaguzi wa matibabu

Lengo kuu la matibabu ni kudhibiti kiwango cha sukari kilicho kwenye damu ya mgonjwa ili aweze kuishi maisha marefu yasiyo na matatizo yatokanayo na kisukari.  Watu wenye ugonjwa wa kisukari wanapaswa kumwona mtoa huduma ya afya, atakayefuatilia udhibiti wa sukari katika damu na kuwasaidia kujifunza jinsi ya kuishi na ugonjwa wa kisukari. Aidha, watu wengi wenye ugonjwa wa kisukari aina ya 2 wanahitaji dawa za kumeza, insulini, au zote mbili ili kudhibiti viwango vya glukozi kwenye damu.

Kuishi kwa afya

Kula kwa afya, kufanya mazoezi ya kimwili, na kupima kiwango cha sukari kwenye damu, ndiyo tiba ya msingi zaidi kwa wagonjwa wa kisukari aina ya 2. Watu wenye ugonjwa wa kisukari wanapaswa kuchukua jukumu la kujihudumia siku hadi siku, na kuhakikisha kiwango cha sukari hakishuki chini sana au hakipandi juu sana.
Kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu ndiyo muhimili mkuu wa tiba na maisha ya mtu mwenye kisukari. Kipimo cha sukari hukuambia kiwango cha sukari kwenye damu kwa wakati huo. Tunza kumbukumbu ya viwango vya sukari kila unapopima. Unapopeleka kumbukumbu za aina hii kwa daktari, unamsaidia kupata picha kamili ili kuweka sawa mpango mpya wa kudhibiti kisukari.
Kupima sukari mara kwa mara, kunasaidia kutambua ni dawa gani au kitu gani kinachosaidia hali yako kuwa bora au mbaya zaidi. Taarifa hizi zitatumika kufanya marekebisho katika mpango wa tiba ili kudhibiti vyema kisukari.

Je, unapimaje sukari kwenye damu?

Unatoboa kidole chako kwa kifaa maalumu kinachoitwa ”lancet” ili kupata tone la damu kwa ajili ya kipimo. Kuna aina maalumu za ”lancet zenye spring zinazosaidia kupunguza maaumivu wakati wa kujitoboa. Kabla haujatumia lancet kujitoboa, nawa mikono vizuri kwa sabuni na maji.
Vifaa vya kupimia sukari (blood glucose meters) husoma kiwango cha sukari kwenye damu pindi tu unapoweka tone la damu. Katika aina zote za mashine, kiwango cha sukari huonekana kama namba kwenye skrini (kama ilivyo kwenye kikokotoo/calculator). Hakikisha kuwa madaktari au manesi wanakufundisha vizuri namna ya kutumia mashine yako.
Kwa mara chache, unaweza kuhitajika kupima kiwango cha ketoni (ketones) kilicho kwenye mkojo wako. Ketoni kwenye mkojo ni ishara kuwa mwili unatumia mafuta badala ya glukozi kama nishati kwa sababu hakuna insulini ya kutosha kuingiza glukozi kwenye seli. Si ajabu kukuta ketoni kwenye mkojo kwa wagonjwa wenye aina ya 1 ya kisukari.

Insulini ni nini?

Homoni ya insulini hutengenezwa na seli zinazoitwa beta zilizo ndani ya kongosho. Kwa kila mlo, seli za beta hutengeneza insulini ili kuusadia mwili kutumia au kutunza sukari iliyo kwenye damu inayotokana na chakula. Watu wenye ugonjwa wa kisukari aina ya 2 hutengeneza insulini, lakini miili yao haitikii vyema mchocheo wa insulini hiyo. Baadhi ya watu wenye kisukari aina ya 2 huhitaji dawa za kisukari au sindano za insulini ili kuusaidia mwili kutumia sukari kama nishati.
Insulini haiwezi kumezwa kama kidonge. Insulini inapaswa kuchomwa kwenye utando wa mafuta ulio chini ya ngozi ili iweze kuingia kwenye damu. Kuna aina nyingi za insulini zinazotumika katika mazingira tofauti na kwa mifumo tofauti ya maisha. Aina hizi za insulini hutofautiana zinavyotengenezwa, zinavyofanya kazi mwilini na bei.

Madawa ya kutibu kisukari

Mara nyingi, matibabu ya kwanza ya kisukari aina ya 2 ni kula chakula bora, kupunguza uzito, na mazoezi. Wakati mwingine, hatua hizi hazitoshi kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu. Na hatua inayofuata ni kumeza vidonge (dawa) vinavyosaidia kushusha kiwango cha sukari kwenye damu. Kuna makundi matano ya dawa hizi za kisukari: sulfonylureas, meglitinides, biguanides, thiazolidinediones, na alpha-glucosidase inhibitors. Kila moja ya makundi haya matano hufanya kazi kwa njia tofauti ili kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu.
Dawa za kisukari hazimsaidii kila mtu. Dawa za kisukari hufanya kazi bora zaidi zikitumiwa sambamba na mlo bora na mazoezi ya kutosha. Kwa njia hii unatumia njia tatu kwa pamoja kudhibiti kiwango cha sukari.  Uwezo wa dawa za kisukari kufanya kazi hupungua baada ya mika 10 au zaidi ya kuishi na kisukari au kama anatumia unit 20 za insulini kila siku.
Kwa upande mwingine, uwezekano wa dawa hizi kufanya kazi ni mkubwa kama umepata kisukari hivi karibuni au unatumia kiwango kidogo cha insulini kudhibiti sukari yako.  Kwa mara chache, dawa za kisukari huacha kufanya kazi baada ya kuzitumia kwa miezi au miaka kadhaa. Hata kama dawa za kisukari zinadhibiti sukari yako vyema, unaweza kutakiwa kutumia sindano ya insulini pia kama una maambukizi au umepangwa kufanywa upasuaji. Vidonge vinaweza visiweze kudhibiti kiwango cha sukari yako katika kipindi hiki cha msongo. Pia, kama unapanga kuwa mjamzito, utahitaji kudhibiti sukari yako kwa kula mlo maalumu, mazoezi au insulini. Si salama kwa wanawake wajawazito kutumia dawa za kisukari.

Mengineyo

Kwa wakati fulani wagonjwa watahitajika kuonana na madaktari bingwa wa mfumo wa homoni (endocrinologists), madaktari bingwa wa macho (ophthalmologists) kwa ajili ya vipimo vya macho, Madaktari wa miguu (podiatrists) kwa huduma ya miguu na waelimishaji kuhusu ugonjwa wa kisukari.
Watu wazima wenye ugonjwa wa kisukari wana hatari kubwa ya kupata magonjwa ya moyo. Kama 65% ya wagonjwa wa kisukari hufa kutokana na magonjwa ya moyo au kiharusi. Kudhibiti kisukari ni zaidi ya kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu – ni muhimu pia kudhibiti shinikizo la juu la damu na kiwango cha lehemu mwilini kwa kula chakula chenye afya, kufanya mazoezi na matumizi ya dawa kama zitahitajika.
Kwa kufanya hivyo, watu wenye kisukari wanaweza kupunguza hatari hii. Ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo, daktari anaweza kupendekeza matumizi ya dawa za aspirini na kuacha kuvuta sigara.

Nini cha kutarajia ukiwa na kisukari aina ya 2

Kushuka kwa kiwango cha sukari

Kwenye damu kunaweza kutokea hata kama unafanya kila kitu unachotakiwa kukifanya ili kudhibiti kisukari. Kwa hiyo, japo mara nyingi hauwezi kuepuka hali hii, unaweza kuitibu mapema kabla haijawa mbaya zaidi.
Dalili za kushuka kwa kiwango cha sukari katika damu ni pamoja na:

Njia ya haraka ya kupandisha sukari kwenye damu ni kwa kutumia sukari, kama vile vidonge vya glukozi (unaweza kununua hizi duka la dawa), juisi ya matunda au pipi.

Kupanda kwa kiwango cha sukari kwenye damu

Kiwango cha sukari kinaweza kupanda kunapokuwa hakuna kiwango cha kutosha au hakuna kabisa insulini mwilini au kama mwili unashindwa kutumia insulini iliyopo kwenye damu. Kama una aina ya 2 ya kisukari, unaweza kuwa na insulini ya kutosha kabisa, lakini mwili usiweze kuitumia vizuri kama inavyopaswa.
Kupanda kwa sukari kunaweza kutokana na kula zaidi ya kiwango unachotakiwa au kufanya mazoezi kidogo sana kuliko inavyotakiwa. Msongo unaotokana na ugonjwa kama mafua unaweza kuwa sababu pia. Sababu nyingine za msongo kama vile, matatizo ya kifamilia au shule au ya kimahusiano, yanaweza pia kupandisha sukari mwilini.
Ishara na dalili za kupanda kwa kiwango cha sukari mwilini ni pamoja na:

 • Kiwango cha sukari kwenye damu huongezeka (ukipima damu)
 • Kunakuwa na kiwango kikubwa cha sukari kwenye mkojo (mkojo unakuwa mtamu)
 • Mgonjwa hukojoa mara kwa mara
 • Mgonjwa huhisi kiu kikali

Ni muhimu kushusha kiwango cha sukari haraka iwezekanavyo la sivyo mgonjwa anaweza kupata tatizo hatari linaloitwa kitaalamu ketoacidosis ambalo linaweza kupelekea mgonjwa kuingia kwenye koma na hatimae kifo. Ketoacidosis hutokea wakati mwili hauna insulini ya kutosha.
Mara nyingi, unaweza kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu kwa kufanya mazoezi. Kupunguza kiasi cha chakula unachokula pia husaidia. Ni muhimu kujifunza ni nini kinapandisha sana sukari yako na kukidhibiti.

Matatizo yanayoweza kutokea ukiwa na kisukari aina ya 2

Magonjwa ya moyo na kiharusi

Watu wenye ugonjwa wa kisukari wako kwenye hatari zaidi ya kupata magonjwa ya moyo na magonjwa yanayoathiri mishipa ya damu. Ugonjwa wa kisukari huongeza maradufu hatari ya kupata mshtuko wa moyo, kiharusi na matatizo yanayotokana na mzunguko usio mzuri wa damu kwenye mwili.
Watu 2 kati ya 3 wenye kisukari hufa kwa ugonjwa wa moyo au kiharusi. Matibabu ya kisukari ni zaidi ya kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu. Watu wenye kisukari wanapaswa kudhibiiti shinikizo la damu, kiwango cha lehemu na kuongea na watumishi wa afya ili kujifunza jinsi ya kupunguza uwezekano wa kupata mshtuko wa moyo au kiharusi.
Pia, mabadiliko ya mfumo wa maisha kama vile kuchagua chakula bora, na kufanya mazoezi, na kutumia dawa za kisukari husaidia. Watu wengi wakibadilisha aina ya chakula wanachokula huleta mabadiliko makubwa ya kiwango cha sukari kwenye damu yao, shinikizo la damu na hata kiwango cha lehemu mwilini.

Magonjwa ya figo

Kisukari kinaweza kuharibu figo, figo zinaweza kuharibiwa na kushindwa kabisa kufanya kazi ya kuchuja uchafu. Kisukari kinaweza kuharibu na kupunguza uwezo wa figo kuchuja damu. Kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu husababisha figo kuchuja damu nyingi zaidi kuliko kawaida. Kazi hii ya ziada huelemea figo na kusababisha figo kushindwa kazi kabisa baada ya miaka mingi kuanza kuvuja.
Protini ambayo ni muhimu mwilini hupotea kwenye mkojo. Hali ya kuwepo kwa kiwango kidogo cha protini kwenye mkojo huitwa ”microalbuminuria”. Ugonjwa wa figo ukigundulika mapema hasa kipindi cha ”microalbuminuria” matibabu kadhaa yanaweza kusaidia figo zisiharibike zaidi. Kukiwa na kiwango kikubwa cha protini kwenye mkojo huitwa ”macroalbuminuria”. Ugonjwa wa figo unapogunduliwa wakati wa ”macroalbuminuria” uwezekano wa kurejesha figo katika hali njema huwa mdogo sana.
Mara nyingi figo zilizofikia katika hali hii hushindwa kabisa kufanya kazi hapo baadae. Hali hii ya kushindwa kwa figo ni hatari sana. Mgonjwa mwenye figo iliyoshindwa kufanya kazi huhitaji kupandikiziwa figo nyingine ”kidney transplant” au kuchujwa damu kwa mashine ”dialysis” mara kwa mara.  Magonjwa ya figo yanayotokana na kisukari yanaweza kuzuiwa kwa kudhibiti vyema kiwango cha sukari katika damu

Matatizo ya Macho

Watu wenye ugonjwa wa kisukari wana uwezekano wa zaidi ya 40% wa kupata ugonjwa wa glakoma (ugonjwa unaotanua mboni ya jicho na kutatiza kuona) kuliko watu wasio na kisukari. Kadri umri wa kuishi na ugonjwa kisukari unavyoongezeka ndivyo na uwezekano wa kupata glakoma unavyoongezeka.
Glakoma hutokea shinikizo linapoongezeka ndani ya jicho, uwezo wa kuona hupungua polepole kwa sababu ya kuharibiwa retina (sehemu ya jicho inayopokea mwanga) na neva. Japo watu wengi wasio na kisukari hupata ugonjwa wa mtoto wa jicho, watu wenye kisukari wana ongezeko la zaidi ya 60% la kupata tatizo hili. Watu wenye kisukari hupata tatizo hili katika umri mdogo na uwezo wao wa kuona hupotea haraka sana. Mtu anapokuwa na ugonjwa wa mtoto wa jicho lenzi ya jicho hujaa ukungu na kuzuia mwanga kuingia jichoni kwa urahisi.
Watu wanaodhibiti vyema kiwango cha sukari katika damu hupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya macho na hata wakipata, matatizo hayawi makubwa sana.

Matatizo ya mfumo wa neva

Mojawapo ya matatizo yanayotokea sana kwa wagonjwa kisukari ni matatizo ya mfumo wa neva yatokanayo na sukari. Uharibifu wa mishipa ya fahamu inayounganisha uti wa mgongo na misuli, ngozi, mishipa ya damu na viungo vingine. Kuna ina mbili za uharibifu wa mishipa ya fahamu. Ya kwanza huitwa ”peripheral neuropathy”, hii husababisha maumivu, ganzi, au kuishiwa nguvu kwenye miguu au mikono. Aina ya pili huitwa ”autonomic neuropathy”, hii husababisha:

 • Matatizo ya mfumo wa kumeng’enya chakula, mgonjwa hujihisi ameshiba muda wote
 • Kichefuchefu, kutapika, kuharisha au kufunga choo
 • Matatizo ya kibofu
 • Matatizo wakati wa kujamiiana
 • Kizunguzungu au kuzirai/kuzimia
 • Mgonjwa hushindwa kutambua ishara za kawaida za onyo za wakati wa mshtuko wa moyo
 • Mgonjwa hushindwa kutambua ishara au dalili za onyo za kushuka kwa kiwango cha sukari mwilini.
 • Kutokwa jasho sana au kutotoka jasho kabisa
 • Mabadiliko ya jinsi macho yako yanavyopokea mwanga na giza

Watu wenye ugonjwa wa kisukari wanaweza pia kuwa na kile kinachojulikana kama ”focal neuropathy”. Katika aina hii, neva au kundi fulani la neva huharibika na kusababisha shida ya ghafla au maumivu. Inaweza kusababisha kuona vitu viwili viwili, kupooza upande mmoja wa uso ”Bell’s palsy”, au maumivu ya sehemu ya mbele ya paja au sehemu nyingine yoyote ya mwili.

Matatizo ya Miguu

Japo inaweza kuleta maumivu, uharibifu wa neva hupunguza uwezo wa kuhisi maumivu, joto na baridi. Kupungua kwa uwezo wa kuhisi humaanisha unaweza usijue ukiumia mguuni. Unaweza usijue kuwa umeumia mpaka unapopata kidonda. Uharibifu wa neva unaweza pia kusababisha mabadiliko ya mwonekano wa mguu na vidole.
Vidonda mara nyingi hutokea kwenye kisigino cha mguu au upande wa chini wa dole gumba la mguu. Kupuuza vidonda kunaweza kusababisha maambukizi yanayoweza kusababisha ukatwe mguu. Kwa sababu mzunguko wa damu hauko vyema, uwezo wa kupona na kupambana na maambukizo hupungua.
Ugonjwa wa kisukari husababisha mishipa ya damu ya mguu kuwa myembamba na iliyokakamaa. Unaweza kudhibiti baadhi ya mambo yanayoweza kuharibu mtiririko wa damu katika mishipa ya damu. Acha kuvuta sigara, kuvuta sigara husababisha mishipa ya damu kugangamara mapema. Kuna uwezekano mkubwa sana wa watu wenye kisukari kukatwa mikono au miguu ukilinganisha na watu wasio na kisukari.
Watu wenye kisukari wana magonjwa ya mishipa inayozuia mtiririko mzuri wa damu kwenda kwenye miguu. Pia, watu wengi wenye kisukari wana magonjwa ya neva yanayopunguza uwezo wa kuhisi. Kwa pamoja, matatizo haya mawili husababisha iwe rahisi kupata vidonda na maambukizi yanayoweza kupelekea ukatwe mguu au mkono.
Moja ya tishio kubwa kwa miguu yako ni uvutaji wa sigara. Uvutaji wa sigara huathiri mishipa midogomidogo ya damu. Hupunguza mtiririko wa damu kwenye miguu na kusababisha vidonda kupona polepole. Watu wengi wenye kisukari wanokatwa miguu au mikono wanavuta sigara. Acha kuvuta sigara.

Matatizo ya tumbo

Wagonjwa wa kisukari aina ya 1 na ya 2 hupata matatizo ya tumbo yanayoitwa kitaalamu ”gastroparesis”. Chakula kinachukua muda mrefu kusafiri kutoka kwenye tumbo (chakula hukaa tumboni kwa muda mrefu isivyo kawaida). Tatizo hili linasababishwa na kuharibika kwa neva zinazopeleka taarifa tumboni. Neva inayoitwa ”Vagus” hudhibiti mjongeo wa chakula kwenye mfumo wa kumeng’enya chakula. Kama neva ya vagus ikiharibika, misuli ya tumbo na utumbo haifanyi kazi vizuri, kwa sababu hiyo mjongeo wa chakula tumboni/utumboni hupungua au kusimama kabisa.
Gastroparesis inaweza kusababisha udhibiti wa sukari kwa wagonjwa wa kisukari kuwa mgumu zaidi. Chakula kilichocheleweshwa tumboni kinapoingia kwenye utumbo na kunyonywa/kufyonzwa husababisha kiwango cha sukari kwenye damu kupanda. Chakula kinapokaa muda mrefu tumboni huchacha na kusababisha bakteria kukua sana. Pia, chakula kinaweza kushikamana na kusababisha mabonge magumu yanayoweza kusababisha kichefuchefu, kutapika na hata kuziba kwa tumbo. Ni tatizo kubwa na hatari tumbo linapoziba na kusababisha chakula kushindwa kujongea kuingia kwenye utumbo.kisukari aina ya 2

Kuzuia kisukari aina ya 2

Tafiti kadhaa zimeonesha kuwa mazoezi ya mara kwa mara na mlo mzuri hupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya kupata kisukari aina ya 2. Ugonjwa wa kisukari aina ya 2 huhusishwa sana na kitambi. Kama ukipenda unaweza kujaribu kufanya moja ya yafutayo kupunguza uzito:

 • Jaribu kupunguza mafuta unayokula (punguza kula nyama zenye mafuta, ngozi za nyama ya ndege (kama kuku/bata), siagi, maziwa, jibini, mafuta ya mitende, mafuta ya nazi  na mafuta ya kondoo n.k.
 • Chagua kula nyama yenye mafuta kidogo mfano: usile kuku au bata mzinga na ngozi yake, kula nyama ya nguruwe iliyoondolewa mafuta.
 • Badili aina ya bidhaa za maziwa unazotumia, kunywa maziwa yenye kiwango kidogo cha mafuta  – soma label za bidhaa kabla hujanunua
 • Kula kwa wingi kadri uwezavyo matunda na mbogamboga
 • Punguza kula vyakula vyenye lehemu kwa wingi kwa mfano: kiini cha mayai, nyama yenye mafuta mengi, nyama ya ndege na bidhaa za maziwa zenye kiwango kikubwa cha mafuta.
 • Chagua aina ya mafuta yanayoweza kusaidia kupunguza kiwango cha lehemu mwilini, kama vile mafuta ya mzeituni , mafuta ya canola. Karanga pia zina mafuta mazuri.
 • Kula samaki mara mbili au tatu kwa wiki, chagua aina ya samaki yenye mafuta yanayoukinga moyo (sadini (samaki mdogo kama dagaa ambao hupikwa na kutiwa makoponi), jodari, heringi (aina ya samaki majichumvi), samaki wa jamii ya bangala , samoni (samaki mkubwa mwenye mnofu mwekundu).
 • Pika kwa njia zisizohitaji utumie mafuta mengi kama vile kuoka, kubanika au kuchoma n.k
 • Kula chakula chenye nyuzinyuzi kwa wingi kama maharagwe, mbaazi, matunda na mbogamboga n.k
 • Punguza kiwango cha chumvi kwenye chakula
 • Punguza kiwango cha kalori na mafuta.
 • Fanya mazoezi zaidi ya unayofanya sasa

Vyanzo

Leave feedback about this

 • Quality
 • Price
 • Service

PROS

+
Add Field

CONS

+
Add Field
Choose Image
Choose Video
X