KISUKARI

KISUKARI

 • October 25, 2020
 • 0 Likes
 • 118 Views
 • 0 Comments

Maelezo ya jumla

Kisukari (diabetes) ni ugonjwa unaoleta matatizo ya kimetaboliki ambayo husababisha kuwepo kwa viwango vya juu vya sukari katika damu kwa muda mrefu. Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na kukojoa mara kwa mara, kuwa na kiu sana, na kuhisi njaa sana. Bila kutibiwa, ugonjwa wa kisukari unaweza kusababisha matatizo mengi. Matatizo haya yanaweza kuwa matatizo ya muda mfupi au matatizo makubwa ya muda mrefu ambayo ni pamoja na ugonjwa wa moyo, ugonjwa wa figo, vidonda vya miguu, na uharibifu wa macho.

Kisukari husababishwa na kongosho kushindwa kuzalisha insulini ya kutosha ili kuingiza sukari kwenye seli za mwili na kwa sababu hii sukari hubakia kwenye damu na kuleta madhara makubwa. Seli za mwili zinaposhindwa kuitikia msisimo unaotolewa na insulini husababisha kisukari pia, hili husababishwa na usugu wa seli kwa insulini.

Kuna aina 3 kuu za ugonjwa wa kisukari:

Kisukari aina ya 1 ,husababishwa na kongosho kushindwa kuzalisha insulini ya kutosha kutokana na kupungua kwa seli za beta ambazo huzalisha insulini mwilini. Sababu ya kupungua kwa seli hizi haifahamiki vyema.

Kisukari aina ya 2, humpata mtu mwenye seli za mwili zenye usugu kwa insulini, hali hii husababisha seli za mwili kutoitikia vyema msisimuo unaotolewa na homoni ya insulini. Sababu kuu ya kupata aina hii ya kisukari ni unene wa mwili uliopitiliza na mazoezi yasiyotosha.

Kisukari cha Ujauzito, aina hii ya kisukari huwapata wanawake wajawazito na baada ya kujifungua hupona kabisa,na mara nyingi hawana historia ya kuwa na ugonjwa wa kisukari hapo awali.

Kinga na matibabu ya kisukari huhusisha kudumisha mlo ulio bora na mazoezi ya mwili ya mara kwa mara kudumisha uzito wa mwili unaofaa.

Kisukari aina ya 1 ni lazima itibiwe kwa sindano za insulini. kisukari aina ya 2 inaweza kutibiwa kwa dawa pekee au kwa dawa na insulini. Kisukari cha ujauzito kwa kawaida hupona baada ya mtoto kuzaliwa.

Kufikia mwaka wa 2015, watu milioni 415 ulimwenguni kote walidhaniwa kuwa na ugonjwa wa kisukari, kati ya wagonjwa wote 90% walikuwa na kisukari aina ya 2, idadi hiyo inawakilisha 8.3% ya idadi ya watu wazima wote duniani. [1]

Kufikia mwaka wa 2014, mwenendo ulipendekeza kuwa kiwango hicho kitaendelea kuongezeka. Ugonjwa wa kisukari unaongeza mara mbili hatari ya mtu kufa mapema. Kuanzia mwaka 2012 -2015, kumetokea vifo kati ya milioni 1.5 -5.0 kila mwaka kwa sababu ya ugonjwa wa kisukari. na gharama za kiuchumi za kisukari duniani kote mwaka 2014, ilikadiriwa kuwa bilioni 612 US$. [2]

Ishara na dalili za kisukari

Dalili za mgonjwa wa kisukari asiyekuwa kwenye tiba ni pamoja na: kupoteza uzito haraka, kukojoa sana,kuwa na kiu sana, na kuwa na hamu ya kula sana. Dalili za kisukari zinaweza kujitokeza kwa haraka sana (wiki au miezi) kwa kisukari aina ya 1, lakini kwa Kisukari aina ya 2 dalili hujitokeza taratibu na polepole,wakati mwingine zaweza kuwepo kidogo sana au zisiwepo kabisa.

Kuna dalili nyingine na ishara zinazoweza kuashiria mwanzo wa ugonjwa wa kisukari ingawa si maalum sana kwa ugonjwa huu, mgonjwa anaweza kuona maluweluwe, kichwa kuuma, uchovu, vidonda hupona polepole, na kuwashwa ngozi. Kiwango cha sukari katika damu kikiwa juu kwa muda mrefu husababisha lenzi ya jicho kuharibika na kusababisha matatizo ya macho.

Dharura ya kisukari     

kiwango cha sukari katika damu kinaposhuka saana (hypoglycemia) kinaweza kuwa hatari. Dalili hutofautiana kwa kila mtu,wengine hujihisi vibaya tu, wengine kutokwa kijasho chembamba, kutetemeka, na kuongezeka kwa hamu ya kula,hii ni kwa tukio lisilo kali sana,  katika tukio lililo kali sana, athari huwa  kubwa zaidi, kama vile kuchanganyikiwa akili, mabadiliko ya tabia kama vile ugomvi, kupoteza fahamu, degedege, na kwa mara chache uharibifu wa ubongo wa kudumu au kifo.

Kama tukio sio kali sana, mgonjwa anaweza kujitibu mwenyewe kwa kula au kunywa kitu chenye sukari nyingi. Kwa tukio kali linaloweza kusababisha fahamu kupotea, mgonjwa anapaswa kutibiwa hospitalini kwa kuongezewa maji maalumu yenye sukari au sindano (intravenous glucose or injections with glucagon).

Wagonjwa (hasa wenye kisukari aina ya 1) wanaweza kupata ketoacidosis, tatizo la kimetaboliki linalosababisha mgonjwa kuwa na kichefuchefu, kutapika, maumivu ya tumbo, pumzi yenye harufu tamu ya matunda (acetone), kupumua kwa shida na mara nyingine kupoteza fahamu.

Tukio lingine la nadra lakini hatari pia huitwa hyperglycemic hyperosmolar state, tukio hili huwapata zaidi watu wenye Kisukari aina ya 2 kwa sababu ya kupungua kwa maji mwilini.

Athari za kisukari

Aina zote za kisukari huongeza hatari ya kupata matatizo ya muda mrefu. Matatizo haya hutokea baada ya miaka mingi (10-20).

Athari za muda mrefu huhusishwa na uharibifu wa mishipa ya damu na kuongeza hatari ya kupata ugonjwa wa moyo na mishipa ya damu.

Athari nyingi za ugonjwa wa kisukari hutokana na uharibifu wa mishipa midogo ya damu ya macho, figo na neva. Uharibifu wa mishipa midogo ya damu katika retina ya macho husababisha uwezo wa kuona kupungua na hatimaye upofu. Ugonjwa huu pia huongeza hatari ya kupata glakoma, mtoto wa jicho, na matatizo mengine ya jicho. Wagonjwa wa kisukari wanashauriwa kumwona daktari wa macho angalau mara moja kwa mwaka. Kuharibika kwa tishu za figo kunaweza kusababisha protini kupotea kwenye mkojo, na hatimaye figo kushindwa kufanya kazi.  Wagonjwa wenye figo zilizoshindwa kufanya kazi huhitaji mashine maalumu kuchuja damu badala ya figo (dialysis) au kupandikiza figo.

Ugonjwa wa kisukari mara nyingi huharibu mishipa ya fahamu ya mwili. Mgonjwa huhisi ganzi, maumivu na kutokuhisi maumivu.

Wagonjwa wa kisukari wana hatari kubwa ya kupata matatizo ya miguu kama vile vidonda na maambukizi. Inaweza kuwa vigumu kutibu matatizo haya na wakati mwingine unaweza kukatwa sehemu ya mguu ili upone.

Kisukari husababishwa na nini ?

Kisukari aina ya 1

Kisukari aina ya 1 husababishwa na kupungua kwa seli za beta zinazozalisha insulini kwenye kongosho, na kusababisha uhaba wa insulini. Kinga ya mwili huziharibu seli hizi za beta baada ya kuzifananisha na kitu kigeni kilichouvamia mwili, kitaalamu hali ya aina hii huitwa Autoimmune attack, lakini pia kwa mara nyingi sababu ya kupungua seli hizi haijulikani (Idiopatic).

Kisukari aina ya kwanza inakadiriwa kuathiri 10% ya kesi zote za kisukari duniani. Watu wengi walioathirika na ugonjwa huu huwa na afya njema wanapogunduliwa.

Japo kisukari aina ya kwanza huwaathiri zaidi watoto, watu wazima pia hupata ugonjwa huu.

Watu wanaorithi jeni zinazoongeza hatari ya kupata kisukari aina ya 1 kama vile HLA, huwa na uwezekano mkubwa kupata ugonjwa huu.

Kwa watu waliorithi jeni hizi ,kuanza kwa ugonjwa wa kisukari kunaweza kusababishwa na sababu moja au zaidi za kimazingira, kama vile maambukizi ya virusi fulani au chakula anachokula. Virusi kadhaa vimehusishwa na kusababisha kisukari lakini hadi sasa hakuna ushahidi wa uhakika wa kuunga mkono dhana hii. Japo namna haieleweki, takwimu zinaonesha kwamba gliadin (protini iliyopo katika gluten) inaweza kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya ugonjwa wa kisukari aina ya 1.

Kisukari aina ya 2

Kisukari aina ya 2 husababishwa na usugu wa mwili kwa insulini, seli za mwili wa mgonjwa haziitikii vyema mchocheo unaotolewa na insulini na kwa kiasi kidogo kupungua kwa utengenezaji wa insulini.

Kisukari aina ya 2, husababishwa na mfumo mbaya wa maisha na urithi wa jeni zenye kubeba kisukari toka kwa wazazi wa kuzaliwa.

Sababu kadhaa ni muhimu ili kutokea kwa kisukari aina ya 2 , hii ni pamoja na kitambi,ukosefu wa mazoezi ya kutosha, lishe mbaya na msongo wa mawazo.

Mafuta mengi katika chakula pia huongeza hatari ya kupata kisukari. Kula kwa wingi mchele na nafaka zingine zilizokobolewa na kusindikwa huongeza hatari pia.

Kisukari cha ujauzito

Kisukari cha ujauzito hufanana na aina ya 2 kwa namna kadhaa, seli za mwili huwa na usugu kwa insulini ,lakini pia utengenezaji wa insulini hupungua.

Inatokea katika asilimia 2-10 ya mimba zote na mara nyingi hupona kabisa baada ya kujifungua. Hata hivyo takribani 5-10% ya wanawake wenye kisukari cha ujauzito hubakia na aina ya 2. [3]

Kisukari cha ujauzito hutibiwa kikamilifu, lakini mgonjwa anahitaji uangalifu wa matibabu wakati wote wa ujauzito. Matibabu yanaweza kujumuisha mabadiliko ya mlo, upimaji wa mara kwa mara wa kiwango cha sukari mwilini, na wakati mwingine sindano ya insulini.

Ingawa ugonjwa huu unaweza kuwa wa muda mfupi,usipotibiwa unaweza kuharibu afya ya mama na mtoto tumboni. Mtoto anaweza kuzaliwa akiwa na uzito mkubwa sana (macrosomia) na kuongeza changamoto wakati wa kujifungua, matatizo ya moyo au matatizo ya mfumo wa neva na misuli.

Kiwango cha insulini kinapoogezeka katika damu ya mtoto tumboni mwa mama hupunguza uzalishaji wa surfactant ambayo husaidia katika upumuaji hivyo kusababisha mtoto kupumua kwa shida.

Pathofisiolojia

Insulini ni homoni ambayo husaidia kuingiza glukosi kwenye seli za mwili kutoka kwenye damu. Insulini inapopungua au kunapokuwepo na usugu kwa insulini, sukari hurundikana kwenye damu na kusababisha madhara.

Mwili hupata glukosi kutoka vyanzo vikuu vitatu: kufyonza chakula toka tumboni, kuvunjavunja glycogen iliyopo katika ini kutengeneza glukosi, au kuvunjavunja vyanzo vingine visivyo wanga vilivyo mwilini kutengeneza glukosi (gluconeogenesis).

Insulini ina jukumu muhimu la kusawazisha kiwango chya glukosi mwilini. Insulini inaweza kuzuia kuvunjwavunjwa kwa glycogen au mchakato wa gluconeogenesis, inaweza kuchochea kuingia kwa glukosi kwenye seli, na inasaidia pia kuchochea uhifadhi wa glukosi kwa njia ya glycogen ili kupunguza kiwango cha sukari katika damu.

Insulini hutengenezwa na seli za beta, zinazopatikana kwenye kongosho ili kukabiliana na  ongezeko la glukosi kwenye damu baada ya kula.

Kiwango cha insulini kinachotolewa na seli za beta hupungua pindi tu kiwango cha glukosi katika damu kinapopungua, hii husababisha mwili kuvujavunja glycogen iliyotunzwa katika ini kutengeneza glukosi kufidia upungufu huo. Utaratibu huu wa kutengeneza glukosi kutoka kwa glycogen hudhibitiwa na homoni iitwayo glucagon ambayo hufanya kazi kwa kukinzana na insulini.

Kama kiwango cha insulini hakitoshi, au seli za mwili haziitikii vyema mchocheo wa insulini, au kama insulini yenyewe ina kasoro, glukosi haiwezi kuingizwa ndani ya seli za mwili na matokeo yake, sukari hulundikana ndani ya damu na kuleta madhara.

Sukari inapoongezeka kwenye damu, figo hushindwa kuinyonya yote na hivyo kiwango kidogo cha sukari hutoka kwenye mkojo (glycosuria). Sukari kwenye mkojo huvutia maji mengi kwenye mkojo na kuongeza uzalishaji wa mkojo (polyuria), na kwa sababu ya hili kiwango cha maji yanayopotea kwenye mkojo huongezeka. Kupotea kwa maji husababisha mtu kuishiwa maji mwilini na hivyo kuhisi kiu ya maji isio ya kawaida (polydipsia).

Utambuzi

Kisukari hutokea wakati mwili unaposhindwa kudhibiti sukari katika damu, sukari inaporundikana katika damu yaweza kufikia viwango vya hatari, ili kujua viwango vya sukari katika damu vipimo vya sukari hufanyika,na vipimo vifuatavyo huonesha kama mgonjwa ana ugonjwa huu

 • Kipimo cha sukari kinapoonesha zaidi ya 7.0 mmol/L baada ya kufunga bila kula kwa muda wa saa nane (fasting blood glucose).
 • Kipimo cha sukari kipimwacho wakati wowote (random blood glucose) kinapoonesha zaidi ya 11.1 mmol/L ,huku kukiwepo na dalili zozote za kisukari.

Ukibainika una kiwango cha juu cha sukari katika damu yako na daktari hajaridhika na majibu, anaweza kupendekeza kurudia kipimo hicho siku inayofuata,itapendeza zaidi kama utafunga kwa muda wa saa nane kabla ya kipimo ili kujiridhisha na matokeo.

Kulingana na shirika la afya duniani (WHO), watu wenye viwango vya glukosi kutoka 6.1 hadi 6.9 mmol /L baada ya kufunga masaa manane,wako kwenye hatari ya kupata kisukari na magonjwa ya moyo.

Kuzuia kisukari

Hakuna njia inayojulikana ya kujikinga na Kisukari aina ya 1.

Kisukari aina ya 2 huathiri kiasi cha 85-90% ya wagonjwa wote wa kisukari duniani, aina hii inaweza kuzuiwa kwa kupunguza uzito wa mwili, kufanya mazoezi, na kula mlo bora. [4]

Kubadilisha kile unachokula husaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia ugonjwa wa kisukari. Chagua kula vyakula vya nafaka isiyokobolewa, na epuka kutumia mafuta mengi kwenye chakula, mafuta yanayotokana na karanga, mbogamboga na samaki yanafaa zaidi. Punguza kunywa vinywaji vya sukari na punguza ulaji wa nyama nyekundu. Kuacha kuvuta sigara hupunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kupata ugonjwa huu.

Matibabu ya kisukari

Ugonjwa wa kisukari hauwezi kutibiwa na kupona kabisa. Mgonjwa kisukari hutumia dawa za kudhibiti sukari maisha yake yote. Matibabu ya kisukari hujaribu kurudisha kiwango cha sukari katika kiwango cha kawaida. Hii inawezekana kwa kula mlo bora, kufanya mazoezi, kupunguza uzito, na kutumia vyema dawa (insulini pekee kwa mgonjwa wa Kisukari aina ya 1, na dawa za kumeza pekee au pamoja na insulini kwa mgonjwa wa Kisukari aina ya 2).

Mgonjwa anapaswa kujifunza kuhusu ugonjwa huu na kushiriki kikamilifu katika matibabu ili kudhibiti kisukari ipasavyo. Mgonjwa anapaswa kuacha kuvuta sigara, kupunguza kiwango cha lehemu mwilini, kupunguza uzito wa mwili na kufanya mazoezi.

Mfumo wa Maisha

Watu wenye ugonjwa huu wanapaswa kupewa elimu kuhusu ugonjwa wa kisukari na matibabu yake, wanapaswa kula mlo bora ili kuweka uzito wa mwili sawa na kufanya mazoezi ya mwili ili kudhibiti kiwango cha sukari mwilini. Kubadili mfumo wa maisha husaidia kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo na kudhibiti shinikizo la damu. Hakuna mlo maalumu uliothibitishwa unaowafaa watu wenye kisukari, mlo wowote utakaokula na kufanikiwa kupunguza uzito wa mwili unafaa.

Madawa

Udhibiti wa glukosi

Ukweli usiopingika ni kuwa, mgonjwa anaedhibiti vyema viwango vya glukosi katika damu kwa kutumia dawa vyema, hupunguza maradufu uwezekano wa kupata athari mbaya zitokanazo na kisukari, kwa mfano matatizo ya figo, macho n.k.

Kuna makundi kadhaa ya dawa za kudhibiti ugonjwa huu. Baadhi hupatikana kama vidonge,mfano metformin,na zingine kwa njia ya sindano kama vile GLP-1 agonists. Kisukari aina ya 1 hutibiwa kwa insulini pekee.

Metformin hupendekezwa kama tiba ya mwanzo ya ugonjwa wa kisukari aina ya 2, hufanya kazi kwa kupunguza uzalishaji wa glukosi wa ini. Makundi mengine kadhaa ya dawa hutumika kutibu kisukari aina ya 2,dawa hizi husaidia kuongeza kiwango cha insulini inayotengenezwa mwilini, zingine hupunguza kiwango cha sukari kinachofyonzwa kutoka tumboni, na nyingine hupunguza usugu wa seli kwa insulini.

Shinikizo la damu

Wagonjwa wa kisukari wanapaswa kudhibiti kiwango cha shinikizo la juu la damu. Wataalamu wanapendekeza kiwango cha juu cha shinikizo la damu kuwa chini ya 130/80 mmHg ili kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo na kiharusi.

Upasuaji

Upasuaji wa kupunguza uzito (Weight loss surgery) huwasaidia baadhi ya wagonjwa wenye kisukari aina ya 2. Wengi wao huweza kudhibiti kiwango cha sukari kwa kutumia dawa kidogo au bila dawa kabisa baada ya upasuaji. Japo vifo vya muda mrefu hupungua baada ya upasuaji, 1% ya wagonjwa hufa kutokana na athari za upasuaji. Inashauriwa kuwa kufanyiwa upasuaji iwe chaguo la mwisho kabisa, pale tu mgojwa anaposhindwa kupunguza uzito na kushindwa kabisa kudhibiti sukari chini ya viwango vilivopendekezwa. [5]

Epidemiolojia

Mnamo mwaka 2016, watu milioni 422 walikua na ugonjwa huu duniani, hili lilikua ongezeko kutoka kwa watu milioni 382 mwaka 2013 na kutoka milioni 108 mwaka 1980. Ugonjwa wa kisukari unaathiri zaidi ya 8.5% ya watu wazima, karibu mara mbili ya kiwango cha 4.7% cha mwaka 1980.  90% ya kesi hizo ni za kisukari aina ya 2. Shirika la Afya duniani linakadiria kuwa ugonjwa wa kisukari ulisababisha vifo milioni 1.5 mwaka 2012, na ni namba 8 kwa kusababisha vifo duniani. [6]

Vifo vingine milioni 2.2 hutokea ulimwenguni kote kwa sababu ya athari kubwa za kisukari mfano: ugonjwa wa moyo, kusinyaa na kukakamaa kwa mishipa, kuharibika kwa figo n.k. Kisukari hutokea duniani kote, lakini kisukari aina ya 2 hupatikana zaidi katika nchi zilizoendelea. Ongezeko la kesi za kisukari aina ya 2 linaonekana katika nchi zenye uchumi wa chini na za kati, ambako zaidi ya 80% ya vifo vya kisukari hutokea. Kwa sababu ya ongezeko hili, asilimia kubwa ya watu wenye kisukari watakuwa Afrika na Asia kufikia mwaka 2030. Hii ni kwa sababu ya kubadilika kwa mwenendo wa maisha (mlo, starehe, kazi zisizohitaji kutumia nguvu n.k) unaoletwa na kukua kwa uchumi na maendeleo. [6]

Marejeleo

 1. Shi Y, Hu FB (June 2014). “The global implications of diabetes and cancer”. Lancet. 383
 2. IDF DIABETES ATLAS (PDF) (6th ed.). International Diabetes Federation. 2013. p. 7. ISBN 978-2930229850. Archived from the original (PDF) on 9 June 2014.
 3. “National Diabetes Clearinghouse (NDIC): National Diabetes Statistics 2011”. U.S. Department of Health and Human Services. Archived from the original on 17 April 2014. Retrieved 22 April 2014.
 4. “The Nutrition Source”. Harvard School of Public Health. 2012-09-18. Archived from the original on 25 April 2014. Retrieved 24 April 2014.
 5. Colucci RA (January 2011). “Bariatric surgery in patients with type 2 diabetes: a viable option”. Postgraduate Medicine. 123 (1): 24–33. doi:10.3810/pgm.2011.01.2242. PMID 21293081.
 6. “Global Report on Diabetes” (PDF). World Health Organization. 2016. Retrieved 20 September 2018.

https://medlineplus.gov/ency/article/001214.htm

 

 • Share:

Leave Your Comment