KITANZI CHENYE MADINI YA SHABA

Kitanzi Chenye Madini ya Shaba ni Nini?

Kitanzi chenye madini ya shaba ni kiplastiki kilichozungushiwa madani ya shaba. Mtoa huduma ya afya aliyepata mafunzo maalum huingiza kitanzi ndani ya kizazi cha mwanamke kupitia uke na mlango wa kizazi.

 • Karibu aina zote za vitanzi zina nyaya au nyuzi mbili, zilizozungushiwa na kufungwa. Nyaya hizo huning’inia kupitia seviksi kwenda kwenye uke.
 • Hufanya kazi kwa kusababisha mabadiliko ya kikemikali ambayo huharibu mbegu za kiume na yai kabla hayajakutana.

Mambo Muhimu kuhusu kitanzi chenye madini ya shaba

 • Kinga ya muda mrefu ya kuzuia mimba. Kimeonekana kufanya kazi vizuri sana kwa miaka 12, na kikitolewa mwanamke huweza kushika mimba haraka.
 • Huingizwa kwenye kizazi na mtoa huduma aliyepata mafunzo maalum.
 • Mteja hatakiwi kufanya lolote mara kitanzi kinapokuwa kimewekwa.
 • Mabadiliko ya hedhi ni ya kawaida. Kwa kawaida, hupata hedhi ya damu nyingi na mkakamao wa misuli ya tumbo au maumivu wakati wa hedhi, hasa katika miezi 3 ya mwanzo

Kitanzi chenye madini ya shaba Ufanisi Kiasi Gani?

Moja ya njia zenye mafanikio makubwa na kwa muda mrefu:

 • Inawezekana kupatikana chini ya mimba 1 kwa wanawake 100 wanaotumia kitanzi kwa mwaka wa kwanza (mimba 6 hadi 8 kwa wanawake 1,000). Hii ina maana kuwa wanawake 992 hadi 994 katika kila 1,000 wanaotumia kitanzi hawatapata mimba.
 • Inabakia kuwepo hatari kidogo ya mimba kwa zaidi ya mwaka wa kwanza na inaendelea kuwepo wakati wote mwanamke anapotumia kitanzi.
 • Kwa miaka 10 ya kutumia kitanzi: Karibu mimba 2 kwa wanawake 100.
 • Tafi ti zimegundua kuwa TCu-380A kinafanya kazi vizuri kwa miaka 12.

Kurudi kuwa na uwezo wa kushika mimba baada ya kutumia kitanzi: Bila kuchelewa

Kuhusu Athari za kitanzi chenye madini ya shaba

Madhara yanayofahamika zaidi  Mabadiliko katika mpangilio wake wa hedhi: Hedhi kuchukua muda mrefu na kuwa na damu nyingi, Hedhi isiyotabirika, Mkakamao wa misuli na maumivu wakati wa hedhi
Ufafanuzi kuhusu madhara haya Mabadiliko ya hedhi si dalili za ugonjwa
Kawaida hupungua baada ya miezi michache ya mwanzo baada ya kuwekwa kitanzi
Mteja anaweza kurudi ili kupata msaada kama atakuwa na matatizo yanayomsumbua.

 

Faida, Hasara na Athari za kutumia kitanzi chenye madini ya shaba

Faida za Kiafya

 • Husaidia kutoa kinga dhidi ya:
  • Hatari ya kupata mimba
 • Kinaweza kusaidia kukinga dhidi ya:
  • Saratani ya kizazi

Hasara Kiafya

 • Zisizo za kawaida:
  • Kinaweza kuchangia kusababisha anemia kama mwanamke tayari ana kiwango kidogo cha madini ya chuma kwenye damu kabla ya kuwekwa kitanzi na kitanzi kikasababisha kutokwa damu nyingi.
 • Nadra:
  • Ugonjwa wa uvimbe wa nyonga unaweza kutokea kama mwanamke ana chlamydia au kisonono wakati akiwekwa kitanzi.

Athari

Nadra:

 • Kutobolewa kwa ukuta wa kizazi na kitanzi au kifaa kinachotumika kuingiza kitanzi. Kawaida hupona bila tiba.
 • Kuharibika kwa mimba, kuzaa kabla ya wakati, au maambukizi mara chache mwanamke anapopata mimba wakati akiwa na kitanzi.

Nani Anaweza Kutumia Kitanzi Chenye Madini ya Shaba

Wanawake wengi wanaweza kutumia kitanzi kwa usalama na ufanisi, ikiwa ni pamoja na wanawake ambao:

 • Wanao au hawajawahi kuwa na watoto
 • Hawajaolewa
 • Wa umri wowote, pamoja na vijana na wanawake wenye umri zaidi ya miaka 40
 • Ndiyo kwanza wametoa mimba au mimba zimeharibika (kama hakuna ushahidi wa maambukizi)
 • Wananyonyesha
 • Wanafanya kazi ngumu za kutumia nguvu
 • Walikuwa na mimba zilizotunga nje ya kizazi
 • Walikuwa na maambukizi sehemu za ukeni
 • Wana anemia
 • Wameambikizwa VVU, au wanatumia dawa za kupunguza makali ya UKIMWI na wanaendelea vizuri

Wanawake wanaweza kuanza kutumia Vitanzi:

Nani hawezi kutumia kitanzi chenye madini ya shaba?

Ikiwa jibu ni “Ndio”, kwa maswali yafuatayo, haupaswi kutumia kitanzi chenye madini ya shaba

 1. Je tangu ujifungue ni zaidi ya saa 48 lakini chini ya wiki 4 zilizopita? NDIYO – Chelewa kuweka Kitanzi mpaka zipite wiki 4 au zaidi baada ya kujifungua
 2. Je umewahi kupata maambukizi baada ya kujifungua au kutoa mimba? NDIYO- Kama kwa sasa ana maambukizi ya via vya uzazi katika wiki 6 za mwanzo baada ya kujifungua (puerperal sepsis) au amepata maambukizi yanayotokana na kutoa mimba kwenye kizazi (septic abortion), usimweke kitanzi. Mpatie tiba au mpatie rufaa kama bado hajaanza kupata huduma. Msaidie kuchagua njia nyingine au mpatie kinga. Baada ya tiba, fanya tena uchunguzi kuhusu uwezekano wa kutumia kitanzi.
 3. Je unapata hedhi isiyo kawaida kwako? NDIYO – Iwapo anapata hedhi isiyo kawaida ambayo inaonyesha dalili ya mimba au hali ya ugonjwa, kutumia kitanzi kunaweza kuleta ugumu wa kufanya uchunguzi na ufuatiliaji wa matibabu ya aina yoyote utakuwa na ugumu zaidi. Msaidie achague njia atakayotumia wakati akifanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu (lakini isiwe kitanzi chenye vichocheo, sindano zenye kichocheo kimoja, au vipandikizi). Baada ya matibabu, fanya tena uchunguzi juu ya uwezekano wa kutumia kitanzi.
 4. Je una hali au matatizo yoyote ya kike (hali au matatizo ya kina mama au uzazi) kama vile saratani ya kizazi au tibii ya nyonga? Kama ndivyo, matatizo gani? NDIYO- Inajulikana ana saratani ya kizazi, endometriu au ovari; ugonjwa wa trofoblasti ya mimba (gestational trophoblast disease); tibii ya nyonga: Usimweke kitanzi. Mpatie tiba au rufaa kwa ajili ya huduma ya afya kama alikuwa hapati. Msaidie kuchagua njia nyingine. Iwapo atakuwa na tibii ya nyonga, mfanyie uchunguzi tena kama ni salama kutumia kitanzi.
 5. Je una ugonjwa wa UKIMWI? NDIYO -Usimwekee kitanzi kama ana UKIMWI isipokuwa kama ana hali nzuri kwa kutumia dawa za kupunguza makali ya UKIMWI. Kama ameambukizwa VVU lakini hana UKIMWI, anaweza kutumia kitanzi. Iwapo mwanamke mwenye kitanzi atapata UKIMWI, anaweza kuendelea kuwa na kitanzi
 6. Chunguza kama yupo katika hatari kubwa ya kupata kisonono au chlamydia. Wanawake ambao wapo kwenye hatari kubwa ya kupata kisonono au chlamydia wasiwekwe kitanzi

Kwa kawaida, mwanamke mwenye hali yoyote kati ya hzi inafaa asiwekwe kitanzi. Katika mazingira maalum, hata hivyo, kunapokuwa hakuna njia nyingine sahihi au zinazokubalika kwake, mtoa huduma mwenye ujuzi wa kutosha anaweza kuchunguza kwa makini hali ya mwanamke na mazingira na kuamua kuwa anaweza kutumia kitanzi. Mtoa huduma anapaswa kuzingatia ugumu wa hali na, hali mbalimbali, aangalie kama ataweza kufanya ufuatiliaji.

Kuwachunguza Wanawake Hatari za Magonjwa Ya Ngono

Mwanamke mwenye kisonono au chlamydia wakati wa kupima hatawekwa kitanzi. Ukiwa na magonjwa yanayoambukizwa kwa ngono wakati wa kuwekwa kitanzi inawezekana kuongeza hatari ya kupata ugonjwa wa uvimbe wa nyonga (PID).

Magonjwa haya ya ngono yanaweza kuwa na ugumu kuyachunguza kwa kuangalia na vipimo vinavyoaminika vinachukua muda mrefu, ghali, na mara nyingi hakuna sehemu za kupima. Kwa sababu ni ngumu kupima, njia pekee ya kufahamu kama mwanamke anaweza kuwa na ugonjwa tayari ni kwa kuangalia tabia yake kama inamweka kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi. Kama hatari ni kubwa sana ni vyema asiwekwe kitanzi.

Ili kuangalia hatari ya kupata magonjwa ya ngono, watoa huduma wanajadiliana na mteja kuhusu tabia zao na hali ilivyo kwenye jumii zao.

Mtoa huduma:

 1. Atakueleza kuwa, mwanamke aliye kwenye hatari kubwa ya kupata magonjwa ya ngono hafai kuwekewa kitanzi..
 2. Atakuomba ufikirie hatari uliyonayo na kama unadhani unaweza kuwa na ugonjwa wa ngono. Mara nyingi mwanamke mwenyewe ni mwamuzi mzuri kuhusu hatari iliyopo.

Baadhi ya mambo yanayoonesha hatari ni kubwa ni pamoja na:

 • Mwenzi wako anaweza kuwa na dalili za ugonjwa wa ngono kama vile maumivu, kidonda au usaha kutoka kwenye uume
 • Wewe au mwenza wako alipimwa akakutwa na ugonjwa wa ngono hivi karibuni.
 • Umekuwa ukijamiiana na zaidi ya mtu mmoja hivi karibuni.
 • Una mwenza ambaye alikuwa na wenza wengi aliojamiiana nao siku za karibuni.

Pia, mtoa huduma anaweza kutaja mazingira mengine yenye hatari kubwa zaidi ambazo zipo mahali husika ili kukusaidia kuamua.

 1. Kama baada ya kufikiria umeona hatari iliyopo ya kupata magojwa ya ngono ni ndogo, mtoa huduma atakuwekea kitanzi.

Kama utaona hatari ni kubwa ya kupata magonjwa ya ngono, mtoa huduma atakusaidia kuchagua njia nyingine itakayokufaa.

Kumbuka: Kama bado unahitaji kitanzi japo hatari ni kubwa ya kuwa na kisonono au chlamydia, na amepima na kuonekana hana maambukizi anaweza kuwekwa kitanzi. Mwanamke atakayepatikana na ugonjwa anaweza kuwekwa kitanzi mara baada ya kumaliza matibabu

Uwekaji wa Kitanzi

Mwanamke anaweza kuwekewa kitanzi chenye madini ya shaba wakati wowote anapotaka kama kuna uhakika wa kutosha kuwa hana mimba. Hakuna haja ya kutumia njia nyingine ya kuzuia ujauzito.

Hali ya mwanamke (Maalumu) Aanze lini kutumia
Asiyepata hedhi Mwanamke anaweza kuwekewa kitanzi chenye madini ya shaba wakati wowote anapotaka kama kuna uhakika wa kutosha kuwa hana mimba. Hakuna haja ya kutumia njia nyingine ya kuzuia ujauzito.
Aliyejifungua Mwanamke anaweza kuwekewa kitanzi chenye madini ya shaba wakati wowote (hata baada tu ya kujifungua) anapotaka kama kuna uhakika wa kutosha kuwa hana mimba. Hakuna haja ya kutumia njia nyingine ya kuzuia ujauzito.
Kitanzi kisiwekwe kama mwanamke ana maambukizi baada ya kujifungia
Baada ya kutoa au mimba kuharibika Kitanzi kinaweza kuweka ndani ya siku 7 (hata baada tu ya mimba kutoka).
Kitanzi kisiwekwe kama mwanamke ana maambukizi baada ya kujifungia
Kubadili kutoa njia nyingine ya uzazi wa mpango Mwanamke anaweza kuwekewa kitanzi chenye madini ya shaba wakati wowote anapotaka kama kuna uhakika wa kutosha kuwa hana mimba. Hakuna haja ya kutumia njia nyingine ya kuzuia ujauzito.

 

Kama njia ya dharura kuzuia mimba Ndani ya siku 5 baada ya ngono bila kinga.
Wakati muda wa yai kupevuka unapoweza kukisiwa, anaweza kuwekwa kitanzi hadi siku 5 baada ya yai kupevuka. Wakati mwingine hii inaweza kuwa zaidi ya siku 5 baada ya ngono bila kinga.
Baada ya kumeza vidonge vya dharura kuzuia mimba Kitanzi kinaweza kuwekwa siku hiyo ambayo amemeza vidonge vya dharura kuzuia mimba. Hakuna haja ya kutumia kinga.

Kama mtoa huduma ya afya hatokuwa na uhakika kuwa mwanamke hana ujauzito, atapaswa kupewa njia mbadala mpaka pale atakapokuwa na uhakika kuwa hana ujauzito.

Namna ya Kuweka Kitanzi

Kabla ya kuweka kitanzi
 • Mtaalamu atakuelekeza utaratibu wa kuweka kitanzi.
 • Atakuonesha spekulamu, tenakulamu, na kitanzi na kifaa cha kuingizia.
 • Atakueleza kuwa utajisikia vibaya au misuli kukakamaa wakati wa kuweka, na kuwa hili ni la kutarajiwa.
 • Atakuomba umwambie wakati wowote utakapojisikia vibaya au maumivu.
 • Wakati mwingine atakupatia Iburprofen (200-400 mg), paracetamol (325-1000 mg), au dawa yoyote ya kupunguza maumivu dakika 30 kabla ya kuweka kitanzi ili kusaidia kupunguza kukakamaa kwa misuli na maumivu.
Wakati wa kuweka kitanzi
 • Mtoa atakueleza kila kinachoendelea, hatua kwa hatua.
 • Atakujulisha kabla ya kuanza hatua ambayo itasababisha maumivu au mshtuko.
 • Atakuuliza  kila wakati kama anasikia maumivu

Kufafanua Utaratibu wa kuweka Kitanzi

Mwanamke ambaye amechagua kutumia kitanzi anahitaji kujua kutatokea nini wakati wa kukiweka.

 1. Mtoa huduma anafanya uchunguzi wa nyonga ili kujua kama anaweza kuitumia. Kwanza mtoa huduma anafanya uchunguzi kwa macho na kisha kuingiza spekulamu kwenye uke ili kukagua seviksi.
  • Je kuna aina yoyote ya kidonda kwenye vulva, uke au shingo ya kizazi (seviksi)? – NDIYO Inawezekana una ugonjwa wa ngono
  • Je anasikia maumivu kwenye tumbo lake la chini unapochezesha shingo ya kizazi?NDIYO – Inawezekana mimba imetunga nje ya kizazi
  • Je anapata maumivu kwenye kizazi, ovari, au mrija wa fallopio (maumivu ya adneksa)?- NDIYO -Inawezekana mimba imetunga nje ya kizazi.
  • Je anatokwa usaha kutoka kwenye shingo ya kizazi?NDIYO – Inawezekana ugonjwa wa ngono au mimba imetunga nje ya kizazi.
  • Je Shingo ya kizazi inatoa damu kirahisi ikiguswa? NDIYO Inawezekana ugonjwa wa ngono au saratani ya shingo ya kizazi.
  • Je kuna mabadiliko yasiyo kawaida ya anatomia ya mvungu wa uterasi ambayo yatakwamisha kuweka kwa usahihi kitanzi? NDIYO Iwapo mabadiliko yasiyo kawaida ya anatomia yamevuruga mvungu wa uterasi, itashindikana kuweka vizuri kitanzi. Msaidie kuchagua njia nyingine.
  • Je ulishindwa kujua ukubwa na/au mahali ilipo uterasi (mji wa mimba)? NDIYO Kujua ukubwa na mahali ilipo uterasi kabla ya kuweka kitanzi ni muhimu ili kuhakikisha unaweka vizuri kitanzi na kupunguza hatari ya kuichana. Iwapo itashindikana kujua ukubwa na mahali ilipo uterasi, usiweke kitanzi. Msaidie kuchagua njia nyingine.
 1. Mtoa huduma anasafi sha seviksi na uke kwa kutumia dawa za kuua vijidudu.
 2. Mtoa huduma anaingiza taratibu tenakulamu kupitia spekulamu na kufunga tenakulamu ili iweze kushikilia vizuri seviksi na uterasi.
 3. Mtoa huduma kwa taratibu anapitisha kipima uterasi kupitia kwenye seviksi ili kupima kina na mahali ilipo uterasi.
 4. Mtoa huduma anaweka kitanzi kwenye kifaa cha kuingizia wakati vyote vikiwa kwenye paketi iliyofungwa iliyotasishwa.
 5. Mtoa huduma kwa taratibu anaingiza kitanzi na kuondoa kifaa cha kuingizia.
 6. Mtoa huduma anakata nyaya zilizo kwenye kitanzi na kuacha karibu sentimeta 3 zikining’inia kwenye seviksi.
 7. Baada ya kuweka kitanzi, mwanamke apumzike. Abaki kwenye meza ya uchunguzi mpakaatakapojisikia yupo tayari kuvaa nguo.

Maelekezo Maalum baada ya kuwekewa kitanzi

Tarajia misuli kukakamaa na maumivu Tarajia mkakamao wa misuli na maumivu kwa siku chache baada ya kuwekwa kitanzi.
Unaweza ktumia iburprofen (200-400 mg), paracetamol (325-1000 mg), au dawa nyingine za kupunguza maumivu.
Pia, tarajia kupata hedhi au matone matone mara baada ya kuwekwa kitanzi. Hii inaweza kuendelea kwa miezi 3 hadi 6.
Unaweza kuangalia nyaya Kama unataka, unaweza kukagua nyaya za kitanzi chako mara kwa mara, hasa katika miezi michache ya mwanzo na baada ya hedhi ili kuthibitisha kuwa kitanzi chako bado kipo mahali pake.
Muda wa kinga kuzuia mimba Ni vizuri kujadili namna ya kukumbuka tarehe ya kurudi kliniki.
Unaweza ukapewa kadi yenye taarifa ifuatayo kwa maandishi kwenye kadi ya kukumbushia: Aina ya kitanzi ulichonacho, Tarehe ya kuweka kitanzi, Mwezi na mwaka kitanzi kitakapotakiwa kutolewa au kubadilishwa; Uende wapi kama utakuwa na matatizo au maswali kuhusu kitanzi chako

Sababu za kurudi kituo cha afya

 • Rudi kama unafikiri kitanzi kinaweza kuwa kimetoka. Kwa mfano:
  • Unahisi nyaya hazipo.
  • Unahisi plastiki ngumu ya kitanzi imetoka nje kiasi fulani.
 • Una dalili za ugonjwa wa uvimbe wa nyonga (PID) (maumivu yanayozidi kuongezeka au makali tumboni, maumivu wakati wa kufanya ngono, kutokwa uchafu usio wa kawaida ukeni, homa, kuhisi baridi, kichefuchefu, na kutapika), hasa katika siku 20 za mwanzo baada ya kuwekwa kitanzi.
 • Unafikiri unaweza kuwa na mimba.
 • Ushauri wa afya kwa ujumla

Kuondoa Kitanzi

MUHIMU: Mtoa huduma hawezi kumkatalia au kumchelewesha mwanamke anapotaka kutolewa kitanzi, bila kujali sababu zake, hata kama ni sababu binafsi au za kiafya. Watalamu wote wa afya wanafahamu kuwa, haipaswi kushinikzwa au kulazimishwa kuendelea kutumia kitanzi.

Iwapo utaona ugumu kuvumilia athari za kitanzi, jadili matatizo unayopata na daktari. Atakusaidia kuangalia kama ingefaa ujaribu kushughulikia tatizo au utolewe kitanzi mara moja.

Kazi ya kutoa kitanzi kawaida ni rahisi. Inaweza kufanyika wakati wowote wa mwezi. Utoaji unaweza kuwa rahisi zaidi wakati wa hedhi, wakati shingo ya kizazi inapokuwa imelainika.

Maelezo ya Taratibu za Utoaji wa Kitanzi

Kabla ya kutoa kitanzi, mtaalamu atakuelekeza kutatokea nini wakati wa kukitoa:

 1. Mtoa huduma ataingiza spekulamu ili kuona shingo ya kizazi (seviksi) na nyaya za kitanzi na kusafisha kwa makini seviksi na uke kwa kutumia dawa ya kuua vijidudu, kama vile iodine.
 2. Mtoa huduma atamwomba mwanamke avute ndani hewa taratibu na kutulia na aseme kama anasikia maumivu wakati wa kutoa kitanzi.
 3. Kwa kutumia koleo nyembamba, mtoa huduma atavuta waya za kitanzi taratibu na kwa makini mpaka kitanzi kitoke kabisa nje ya shingo ya kizazi (seviksi).

Imani potofu kuhusu Vitanzi

Vitanzi:

 • Mara chache husababisha ugonjwa wa uvimbe wa nyonga.
 • Haviongezi hatari ya kupata magonjwa yaambukizwayo kwa ngono, pamoja na VVU.
 • Haviongezi hatari ya mimba kuharibika wakati mwanamke anaposhika mimba baada ya kitanzi kuondolewa.
 • Haviwasababishi wanawake wagumba.
 • Havisababishi mtoto kuzaliwa na kasoro.
 • Havisababishi saratani.
 • Haviendi kwenye moyo au akili.
 • Havisababishi kukosa raha au maumivu kwa mwanamke wakati wa kujamiiana.
 • Kiasi fulani hupunguza hatari ya mimba kutunga nje ya kizazi

Vyanzo

https://medlineplus.gov/birthcontrol.html

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi