Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Kiungulia (heartburn) ni hali ya kuhisi mchomo (maumivu kama moto) unaotokea nyuma ya mfupa wa kidari. Kwa kawaida maumivu haya huanzia kwenye umio (oesophagus) na kupanda kifuani na yanaweza kuenea mpaka kwenye shingo au koo.
Ni nini husababisha kiungulia?
Karibu kila mtu hupatwa na kiungulia kwa wakati fulani katika maisha yake. Kama unapata kiungulia mara kwa mara, unaweza kuwa na ugonjwa unaosababishwa na kucheua mara kwa mara unaoitwa gastroesophageal reflux disease. Katika hali ya kawaida, chakula kinapoingia tumboni, ukanda wa misuli ulio mwishoni mwa umio hukaza na kukifungia chakula tumboni. Ukanda huu huitwa  lower esophageal sphincter. Kama ukanda huu hautafunga vyema au kulegea, asidi zinazosaidia kumeng’enya chakula zilizo tumboni, zinaweza kurudi juu kwenye umio na kusababisha hisia ya mchomo.
Nani yuko katika hatari zaidi ya kupata kiungulia?
Ujauzito na dawa nyingi zinaweza kusababisha kiungulia.
Kiungulia hutokea kwa sababu mtoto anayekua hujaza fumbatio la mama na kusukuma tumbo juu zaidi kuliko kawaida. Asidi zilizo kwenye tumbo la mama zinazosaidia katika umeng’enyajiwa chakula husukumwa juu kwenye umio lake na kusababisha hisia ya mchomo. Ni muhimu kumhakikishia mama mjamzito kuwa tatizo hili litakwisha baada ya kujifungua.
Madawa yanayoweza kusababisha kiungulia ni pamoja na:
- Anticholinergics (mf, dawa za kuzuia mtu kutapika au kuugua akiwa kazini )
- Beta-blockers kwa ajili ya kudhibiti shinikizo la juu la damu au kutibu ugonjwa wa moyo
- Calcium channel blockers hutumika kutibu shinikizo la juu la damu
- Dawa kama dopamine zinazotumika kutibu ugonjwa wa parkinson
- Dawa aina ya progestin zinazotumika kutibu matatizo ya hedhi au uzazi wa mpango
- Madawa yanayotumika kudhibiti wasiwasi, au kutibu insomnia (dawa za usingizi)
- Theophylline (Dawa za kutibu pumu au magonjwa mengine ya mapafu)
- Dawa za kudhibiti sonona/kushuka moyo
Kama unafikiri moja ya dawa zako inasababisha kiungulia , ongea na daktari. USIBADILI au KUACHA kutumia dawa bila kuzungumza na daktari.
Wakati gani utafute matibabu ya haraka?
Pata matibabu ya haraka kama:
- Unatapika matapishi yenye damu au yanayoonekana kama kahawa
- Kinyesi chako ni cheusi (kama lami) au cha rangi ya damu ya mzee
- Unahisi mkandamizo au kuungua kifuani mwako. Wakati mwingine watu wanaweza kudhani kuwa wanakiungulia kumbe wanapata mshtuko wa moyo
Mwone daktari kama:
- Unapata kiungulia mara kwa mara au unapata kiungulia muda wote
- Unapungua uzito bila sababu maalumu
- Unapata shida kumeza (unahisi kama chakula kinakwama kooni)
- Una kikohozi au mkoroto (wheeze) usioisha
- Dalili zako huwa mbaya zaidi ukitumia dawa za kupunguza asidi tumboni
- Unadhani moja ya dawa zako inasababisha kiungulia. USIBADILI au KUACHA kutumia dawa mwenyewe, bila kuzungumza na daktari kwanza
Utambuzi wa kiungulia
Kwa kawaida, kutambua kiungulia ni rahisi sana kutokana na dalili utakazomweleza daktari. Daktari wako atafanya uchunguzi wa mwili na kuuliza maswali kadhaa kuhusu tatizo lako, kama vile:
- Ilianza lini?
- Kikianza kinadumu kwa muda gani?
- Je! Hii ni mara ya kwanza kupata kiungulia?
- Je, unakula chakula gani? Kabla ya kuhisi kiungulia, je, umekula chakula chenye viungo vingi au mafuta?
- Je! Unakunywa kahawa nyingi, vinywaji vingine vyenye kafeini, au pombe?
- Je! Unavuta sigara?
- Je! Unavaa nguo zinazobana sana tumbo au kifua?
- Je! una maumivu kwenye kifua, taya, mkono, au mahali pengine?
- Je, unatumia dawa yoyote kwa sasa? Ni ipi?
- Je! Unatapika damu au matapishi meusi?
- Je, kuna damu kwenye kinyesi chako?
- Je! Una kinyesi cheusi?
- Je, kuna dalili nyingine zozote zinazoambatana na kiungulia chako?
Vipimo vifuatavyo vinaweza kufanyika:
- Daktari anaweza kutumia kamera ndogo kuchunguza sehemu ya ndani ya umio na koo (Esophagogastroduodenoscopy)
Uchaguzi wa matibabu ya kiungulia
Unapaswa kutibiwa kiunguli hasa kama kinatokea mara kwa mara. Kama kiungulia kitakuwepo kwa muda mrefu, asidi zinaweza kuharibu utando ute wa ndani ya umio na kusababisha matatizo makubwa. Habari njema, ni kuwa ukibadilisha tabia na mfumo wa maisha unaweza kuzuia kiungulia au kupunguza dalili.
Vidokezo vifuatavyo vinaweza kusaidia kuzuia kingulia. Kama hatua hizi hazitafanikiwa kupunguza dalili zako, mwone daktari.
Kwanza, jaribu kuepuka vyakula na vinywaji vinaweza kusababisha ucheue, kama vile:
- Pombe
- Kafeini
- Vinywaji vyenye kaboni-mf; soda
- Chokoleti
- Matunda na juisi za jamii ya mchungwa,mlimau, mdimu n.k
- Vyakula vyenye viungo vingi, mafuta, na bidhaa za maziwa
- Nyanya na sosi za nyanya
Kisha, jaribu kubadili tabia ya ulaji wako:
- Epuka kuinama au kufanya mazoezi baada tu ya kula.
- Epuka kulala masaa 3 – 4 baada ya kula. Kulala tumbo likiwa limejaa husababisha chakula kusukuma kwa nguvu ukanda unaozuia chakula
- Kula chakula kidogo.
Fanya mabadiliko mengine katika maisha yako kama inavyohitajika:
- Epuka kuvaa mikanda au nguo zinazobana sana kiuno na tumbo. Hii inaweza kubana tumbo na kusababisha chakula kupanda juu.
- Punguza uzito kama wewe ni mnene. Kitambi huongeza shinikizo ndani ya tumbo. Shinikizo hili linaweza kusukumia chakula na asidi kwenye umio.
- Lala kichwa kikiwa kimenyanyuliwa kwa angalau kwa sentimeta 3 hivi. Kulala kichwa kikiwa juu kidogo kuliko tumbo husaidia kuzuia chakula kilichomeng’enywa kurudi nyuma. Weka vitabu, tofali au mito chini ya godoro kwenye maeneo ya kichwa. Kulalia mito mingi haisaidii kupunguza kiungulia kwa sababu unaweza kuteleza na kutoka kwenye mto usiku. Weka mito chini ya godoro ili kulinyanyua.
- Acha kuvuta sigara, kemikali katika moshi wa sigara hulegeza ukanda unaofunga sehemu ya chini ya umio.
Kama bado haujapata nafuu vizuri, jaribu kutumia dawa.
- Dawa za kupunguza asidi tumboni (Antacids), husawazisha asidi iliyo tumbo.
- H2 blockers, kama Pepcid AC, Tagamet, na Zantac, hupunguza uzalishaji wa asidi tumboni.
- Proton pump inhbitors, kama Prilosec OTC, hupunguza uzalishaji wa asidi tumboni.
Nini cha kutarajia ukiwa na kiungulia?
Kama dalili zako hazijapungua baada ya kujihudumia nyumbani, daktari atakupatia dawa za kupunguza asidi tumboni. Matarajio ni mazuri.
Leave feedback about this