Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Kizunguzungu ni hali ya kuhisi kama unataka kuzimia, unatetereka, unapoteza balance au kuhisi kama wewe au chumba ulichomo kinazunguka. Sababu nyingi hazitishii maisha na hupoa zenyewe baada ya muda fulani au baada ya matibabu.
Ni nini husababisha kizunguzungu?
Kizunguzungu hutokea ubongo unapokosa damu ya kutosha. Hili hutokea kama shinikizo la damu litashuka kwa ghafla au kama umepata upungufu wa maji mwilini kwa sababu ya kutapika, kuhara, homa au sababu nyingine. Watu wengi, hasa wazee, hupata kizunguzungu wanaposimama haraka kutoka walipolala au walipokaa. Tatizo hili mara nyingi hutokea sambamba na mafua, kushuka kwa kiwango cha sukari kwenye damu au mzio.
Matatizo mengine makubwa yanayoweza kusababisha tatizo hili ni pamoja na matatizo ya moyo (kama vile mshtuko wa moyo), kiharusi na kushuka sana kwa shinikizo la damu. Kama matatizo haya makubwa yatakuwepo kutakua na dalili nyingine kama vile, maumivu ya kifua, mapigo ya moyo yanayoenda mbio, kushindwa kuona vyema na dalili nyingine.
Japo ni kwa nadra, kizunguzungu kinaweza kusababishwa na kiharusi, kifafa, uvimbe kwenye ubongo au kuvuja damu kwenye ubongo. Matatizo kama haya huambatana na dalili nyingine.
Nani yuko kwenye hatari zaidi?
Watu wenye matatizo ya moyo, kiharusi, kifafa, uvimbe kwenye ubongo na ”vertigo” (ugonjwa huu husababisha kizunguzungu unapobadilisha mkao wa kichwa chako) wako kwenye hatari zaidi ya kupata tatizo hili.
Wakati gani utafute huduma ya matibabu?
Fika katika kituo cha afya kama mtu mwenye kizunguzungu ana shida zifuatazo
- Kama ameumia/ amepata jeraha la kichwa
- Homa zaidi ya 38 ° C, maumivu ya kichwa, au shingo iliyokakamaa
- Degedege au kutapika
- Maumivu ya kichwa, maumivu ya kifua, kuongezeka kwa mapigo ya moyo, kushindwa kupumua, uchovu, kushindwa kusogeza mkono au mguu au kushindwa kuona u kushindwa kuongea.
- Kuzimia na kupoteza fahamu kwa zaidi ya dakika kadhaa
Mwone daktari kama:
- Umepata tatizo hili kwa mara ya kwanza
- Dalili unazoona sasa zinatofautiana na zile unazoziona kila siku (Kwa mfano, kama unapata tatizo hili kwa muda mrefu zaidi, au kizunguzungu kikali zaidi kuliko kawaida au kama shida hii inavuruga mfumo wako wa maisha)
- Unadhani kizunguzungu kimesababishwa na madawa unayotumia. Ongea na mtoa huduma ya afya kabla ya kubadili dawa hizo.
- Umepoteza uwezo wa kusikia
Utambuzi wa kizunguzungu
Daktari atafanya uchunguzi wa mwili, ataangalia moyo, kichwa, masikio, na mfumo wa neva, na atakuuliza maswali kama:
- Je! Unajihisi kama unataka kuzimia, unatetereka, unapoteza balance au kuhisi kama wewe au chumba ulichomo kinazunguka?
- Je! Kizunguzungu chako kinatokea baada ya kubadilisha mkao wako?
- Je! Ni dalili gani nyingine zinazojitokeza wakati unapohisi kizunguzungu?
- Ulianza kupata lini shida hii?
- Je! Unapata kizunguzungu muda wote au kinakuja na kuondoka?
- Kizunguzungu hudumu kwa muda gani (dakika, masaa)?
- Je! Kuna tatizo jingine linalojitokeza kabla au baada ya kupata kizunguzungu? Baada ya muda gani?
- Je! Unapata kichefuchefu au kutapika?
- Je! Una msongo au wasiwasi mwingi-anxiety?
Vipimo vinavyoweza kufanyika ni pamoja na:
- Vipimo vya kuangalia shinikizo la damu
- ECG
- Vipimo vya masikio
- Vipimo vya mfumo wa neva
- Unaweza kufanya vipimo vya kuangalia balance yako
- MRI
Uchaguzi wa matibabu
- Kama unapata kizunguzungu kila mara unaposimama, jaribu kusimama kwa hatua na polepole.
- Kama unakiu na unahisi kizunguzungu, kunywa maji. Kama unashindwa kunywa maji au unatapika au kuhara, unaweza kuhitaji kuongezewa maji kwenye mishipa. Hili la kuongezewa maji kwenye mishipa hufanyika hospitalini.
- Matatizo ya kizunguzungu yanayosababishwa na vertigo (kisulisuli) huisha yenyewe baada ya wiki kadhaa. Wakati wa mashambulio ya kisulisuli yanayotokana na shida yoyote, jaribu kupumzika. Epuka kubadili mkao wako kwa ghafla na epuka mwanga mkali. Kuwa makini unapoendesha gari au kutumia mashine.
- Wakati mwingine dakitari anaweza kushauri utumie madawa au kufanya mazoezi ili kukusaidia kujihisi vizuri.
- Madawa hayo ni pamoja na ”antihistamines”, dawa za usingizi au dawa za kupunguza kichefuchefu. Kwa baadhi ya matatizo upasuaji unaweza kuhitajika.
Kuzuia kizunguzungu
- Tibu mapema maambukizi ya sikio, mafua na maambukizi mengine ya mfumo wa kupumua.
- Kama una mafua au ugonjwa mwingine unaosababishwa na virusi, kunywa maji ya kutosha kuzuia upungufu wa maji mwilini.
Nini cha kutarajia unapokua na kizunguzungu?
- Sababu nyingi za kizunguzungu sio kubwa na hupona zenyewe baada ya muda fulani au baada ya matibabu.
Leave feedback about this