Magonjwa ya ndani ya mwili

KOMA :Dalili, Sababu, Matibabu, Kuzuia

Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko

Maelezo ya jumla

Koma (coma) si ugonjwa. Ni hali ya kuwa na usingizi mzito sana, mgonjwa huzimia kwa muda mrefu na hawezi kuhisi chochote.

Koma inaweza kusababishwa na kiharusi, jeraha/kuumia kichwani, Degedege, uvimbe kwenye ubongo, maambukizi kwenye ubongo, upungufu wa oksijeni mwilini unaosababishwa na kukosa hewa au kushindwa kupumua, kiwango cha juu cha sukari kwenye damu hasa kwa mtu mwenye kisukari isiyodhibitiwa vyema na kiwango cha chini cha sukari katika damu.

Dalili kuu ni kupoteza fahamu. Historia ya mgonjwa, uchunguzi wa kimwili, tathmini ya mfumo wa fahamu na picha za kichwa zinaweza kusaidia kupata sababu ya tatizo hili. Wagonjwa walio kwenye koma wanahitaji matibabu ya haraka ili kuepuka madhara makubwa na ya hatari.

Matibabu ni pamoja na kutibu tatizo la msingi lilosababisha koma, kudumisha hali nzuri ya kimwili, kuzuia maambukizi, na mazoezi ya mwili. Matarajio ya mgonjwa kupona yanategemea sababu ya kutokea kwa tatizo hili, mahali na kiwango cha uharibifu katika mfumo wa neva. Mtu anaweza kupona, lakini mwingine anaweza kubaki bila kurudiwa na fahamu kwa kitambo sana.

Ni nini dalili za koma?koma

Koma si ugonjwa, bali ni hali ambayo inaweza kusababishwa na matatizo mengi.   

  • Kasi ya kutokea kwa koma hutegemea imesababishwa na nini:
  • Kabla hajaingia kwenye koma mgonjwa huonesha dalili za awali, dalili hizi hutofautiana kulingana na sababu ya msingi ya tatizo hili:
    • Ikiwa imesababishwa na matumizi mabaya ya pombe au aina fulani ya madawa ya kulevya, mgonjwa atahisi kuchanganyikiwa na atashikwa na lepe la usingizi.
    • Ikiwa imesababishwa na maambukizi ya ubongo, wagonjwa wanaweza kuumwa kichwa, wanaweza kuwa na homa, au kizunguzungu kabla mgonjwa hajapoteza kabisa fahamu.
    • Katika hali nyingine, tatizo hili linaweza kutokea kwa haraka sana kiasi kwamba wagonjwa au wanafamilia hawapati muda wa kuziona dalili hizi.    
  • Ishara za koma
    • Kupoteza fahamu        
    • Kutetemeka
    • Macho kuchezacheza isivyo kawaida
    • Kama misuli ya kupumua imeathirika, mgonjwa atapata shida kupumua
    • Mgonjwa hashtuki hata akiitwa, akishikwa au akiumizwa.
  • Magonjwa yafuatayo yanazo dalili zinazofanana na za koma:

Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kuingia kwenye koma? 

Wagonjwa wenye matatizo yafuatayo wako kwenye hatari kubwa ya kuingia kwenye koma kwa sababu ya ugonjwa wenyewe au matibabu yake.      

  • Kiharusi      
  • Kuumia kichwani        
  • Kifafa       
  • Uvimbe kwenye ubongo        
  • Maambukizi ya ubongo        
  • Ukosefu wa oksijeni mwilini kwa muda mrefu
  • Matatizo ya kimetaboli kama vile, kiwango cha juu cha sukari mwilini kwa mtu mwenye kisukari au kiwango cha chini cha sukari katika damu.
  • Sumu, ikiwa ni pamoja na pombe na madawa ya kulevya kama amphetamines, cocaine         
  • Ini au Figo kushindwa kufanya kazi

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Unapomkuta mtu kwenye koma, mwahishe kwenye kituo cha afya kilicho karibu haraka iwezekanavyo.

Utambuzi

Lengo la vipimo vifuatavyo ni kutambua sababu ya koma.        

  • Historia ya mgonjwa, uchunguzi wa mwili na tathmini ya mfumo wa neva: Vipimo hivi ni  muhimu sana ili  kupata sababu ya koma.        
  • Uchunguzi wa macho: Husaidia kutambua kama tatizo lililosababisha koma liko kwenye ubongo.        
  • Vipimo vya maabara: Vipimo vya kupima kazi ya ini na figo , kiwango cha sukari mwilini, kazi ya tezi dundumio (thyroid functions),na hata uwepo sumu yoyote mwilini. Matokeo ya vipimo mbalimbali vya maabara yanaweza kusaidia kutambua magonjwa mengine ya kimetaboliki ambayo yanaweza kusababisha koma.        
  • Uchunguzi kwa kutumia picha kama CT scan ya kichwa na MRI : Picha hizi hupigwa kwa kutumia nguvu ya mionzi au sumaku, zinampa nafasi daktari ya kuchunguza kama tatizo lililosababisha koma liko kwenye ubongo. Kwa mfano; uvimbe ubongoni,kiharusi.       
  • Electroencephalography (EEG): Kipimo hiki kinaweza kuonesha shughuli ya umeme kwenye ubongo wa mgonjwa na hutumiwa kugundua kama kuna degedege au la.

Uchaguzi wa matibabu

Wagonjwa walio kwenye koma wanahitaji matibabu ya haraka ili kuepuka madhara makubwa. Matibabu hutegemea sababu iliyoyasababisha.        

  • Matibabu ya magonjwa yaliyosababisha, kama vile
    • Upasuaji wa dharura kwa kiharusi kinachosababishwa na kuvuja damu ubongoni
    • Viuavijasumu (antibiotics) kwa maambukizi ya ubongo
    • Udhibiti wa sukari kwa wagonjwa wa kisukari
    • Dialisisi (usafishaji wa damu kwa mashine) baada ya figo kushindwa kufanya kazi.        
  • Kudumisha hali nzuri ya kimwili, kutoa lishe bora.        
  • Kuzuia maambukizo, kama vile nyumonia na kidondamalazi (bedsore).        
  • Tiba ya mazoezi itasaidia kuzuia kukakamaa kwa viungo,mifupa na misuli.

Kuzuia koma        

  • Kutibu mapema magonjwa ya ubongo        
  • Kwa wagonjwa wa kisukari, kudhibiti kiwango cha sukari mwilini
  • Epuka kukutana na sumu

Nini cha kutarajia?

Wagonjwa wengine walio kwenye koma wanaweza kupona, wengine wanaweza kubaki bila kurudiwa na fahamu kwa muda mrefu.

Matarajio ya kupona hutegemea:        

  • Sababu ya msingi iliyosababisha koma        
  • Makali ya koma (madaktari wanazo njia za kupima makali)       
  • Eneo la mfumo wa neva liloharibiwa

Matatizo yanayoweza kutokea

  • Mgonjwa anaweza kubaki bila kurudiwa na fahamu kwa muda mrefu    
  • Kifo

Vyanzo

https://medlineplus.gov/coma.html#:~:text=A%20coma%20is%20a%20deep,injuries%2C%20such%20as%20brain%20injury.

 

Leave feedback about this

  • Quality
  • Price
  • Service

PROS

+
Add Field

CONS

+
Add Field
Choose Image
Choose Video
X