Magonjwa ya ndani ya mwili

KONDOMU YA KIKE NA KIUME

kondomu

Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko

1. Kondomu ya kiume

Kondomu ni kiwambo chembamba kinachovaliwa kwenye uume wakati wa kujamiiana. Ukitumia kondomu itasaidia :

Kondomu ya kiume ni kiwambo chembamba kinachovaliwa na kufunika uume uliosimama. Zinatengenezwa kwa kutumia:

 • Ngozi ya wanyama (Aina hii ya kondomu haikulindi dhidi ya maambukizi.)
 • Ulimbo wa mpira (latex rubber)
 • Polyurethane – hii ni plastiki

Kondomu ndio njia pekee ya uzazi wa mpango kwa wanaume isiyo ya kudumu. Kondomu za kiume zinaweza kununuliwa kwenye maduka ya kawaida ya dawa, nyumba za wageni, hospitalini, maduka ya kawaida na hazina gharama sana.

Kondomu huzuiaje ujauzito?

Kama manii ya mwanaume yaliyo kwenye shahawa yakiufikia uke wa mwanamke, anaweza kupata ujauzito. Kondomu hufanya kazi ya kuzuia manii kumwagika ukeni.
Kama itatumiwa kwa usahihi kila wakati wa kushiriki ngono, hatari ya kupata ujauzito hupungua mpaka kufikia mara 3 kwa kila mara 100 unapofanya ngono. Hata hivyo, uwezekano wa kupata ujauzito ni mkubwa zaidi kama:

 • Haitumiwi kwa usahihi wakati wa kushiriki ngono
 • Ikipasuka au kutoboka wakati wa matumizi

Japo njia nyingine za kupanga uzazi zina ufanisi zaidi wa kuzuia mimba kuliko matumizi ya kondomu, lakini ni heri kutumia kuliko kutotumia kabisa.
Kondomu zingine zina kemikali zinazoua manii, zinazoitwa spermacide. Hizi zinaweza kufanya kazi ya kuzuia mimba vyema zaidi.
Pia huzuia kuenea kwa virusi kadhaa na bakteria ambao husababisha magonjwa.
Unaweza kuambukizwa ugonjwa unaosababisha malengelenge (herpes) hata kama umevaa kondomu kama uume utagusa sehemu ya nje ya uke. Kondomu haizui kabisa kuenea kwa sundosundo ”warts”.

Jinsi ya kutumia kondomu ya kiumekondomu

 • Kondomu ni lazima ivaliwe kabla uume haujagusa sehemu ya nje ya uke au kuingia ukeni. La sivyo:
  • Maji maji yanayotoka kwenye uume kabla ya kufika kileleni yanaweza kuwa na manii na yanaweza kusababisha ujauzito.
  • Maambukizi yanaweza kusambazwa.
 • Kondomu ni lazima ivaliwe kwenye uume uliosimama, hakikisha inavaliwa kabla uume haujagusana na uke.
 • Kuwa mwangalifu usiichane au kuitoboa wakati wa kuifungua au wakati wa kuitoa ndani ya kifuko chake.
 • Kama ina chuchu ndogo kwa mbele (hukusanya shahawa), weka kondomu kwenye kichwa cha uume na uifungue kwa kuibiringisha juu ya shina la uume.
 • Kama yako haina chuchu hakikisha unaacha nafasi kidogo kati ya kichwa cha uume na kondomu. Vinginevyo, shahawa zinaweza kusukumwa kwenye pande za kondomu na kutokea upande wa nyuma kabla ya kuitoa.
 • Hakikisha kuwa hakuna hewa yoyote kati ya uume na kondomu. Hii inaweza kusababisha ipasuke.
 • Watu wengine wanapendelea kuifungua kidogo kondomu kabla ya kuibiringisha kwenye uume. Hii huwasaidia kuacha nafasi kubwa ya shahawa kujikusanya. Vile vile huzuia kondomu kujikaza sana kwenye uume.
 • Baada ya kutokwa na shahawa kileleni, chomoa uume kutoka ukeni. Njia nzuri ya kuondoa kondomu ni kuishika sehemu ya nyuma na kuuvuta uume toka ndani. Epuka kumwaga au kudondosha manii ukeni.

Mambo muhimu ya kujua

 • Hakikisha kuwa unazo karibu unapozihitaji. Kama hakuna karibu, unaweza kushawishika kushirika ngono bila kondomu. Tumia kila moja mara moja tu.
 • Hifadhi mahali pakavu pasipo na joto kali mf: mbali na jua au moto.
 • Usizibebe kwenye wallet yako kwa muda mrefu. Zibadilishe kila mara baada ya muda fulani. Kuchakaa kwake kunaweza kusababisha vitundu vitundu kwenye kondomu. Lakini, bado ni bora kutumia ambayo imekaa ndani ya wallet yako kwa muda mrefu kuliko kutotumia kabisa.
 • Usitumie ambayo imekakamaa, inanata, au ambayo rangi yake imebadilika. Hizi ni ishara za kuzeeka, na ina uwezekano mkubwa wa kupasuka/kutoboka.
 • Usiitumie kama kifungashio kimeharibika, inaweza kuwa imeharibika pia.
 • Usitumie vilainishi na kondomu hasa vilivyotokana na petrol, kama vile Vaselini. Aina hizi za vilainishi huharibu mpira ”latex” inayotumika kutengeneza kondomu.
 • Kama unahisi imepasuka wakati wa ngono, ACHA mara moja na uvae ingine mpya. Kama shahawa zitamwagika ukeni baada ya kondomu kupasuka:
  • Unaweza kuweka jelly inayoua manii (spermicide) ili kupunguza uwezekano wa kupata mimba.
  • Mwone daktari au fika duka la dawa ili upate dawa za dharura za kukukinga na mimba-zinaitwa morning-after pills

Matatizo ya kutumia kondomu

Baadhi ya malalamiko au shida zinazotolewa na watumiaji ni pamoja na:

 • Japo matokeo mabaya ya mzio yanayotokana na latex ni adimu, huwa yanatokea. (Kubadilisha na kutumia zilizotengenezwa kwa ”polyurethane” au viwambo vya wanyama)
 • Msuguano wa kondomu hupunguza raha na starehe (Kutumia zenye mafuta mengi zinaweza kupunguza shida hii.)
 • Tendo la ngono linaweza lisifurahiwe pia kwa sababu mwanaume anapaswa kuchomoa uume baada tu ya kumwaga.
 • Kuvaa kondomu kunaweza kukatiza mshawasha wa tendo la ngono.
 • Mwanamke hukosa ile raha ya maji maji ya moto kumwingia mwanaume anapomwaga (hii ni muhimu kwa baadhi ya wanawake, sio muhimu kwa wengine).

2. Kondomu ya kike

 • Ni kifaa kinachotumiwa kupanga uzazi. Kama ilivyo kwa kondomu ya kiume, inazuia manii kulifikia yai.
 • Kondomu ya kike inazuia ujauzito. Pia inakulinda dhidi ya magonjwa ya ngono ikiwemo UKIMWI. Hata hivyo, za kiume zinadhaniwa kufanya kazi vyema zaidi ya kuzuia maambukizi kuliko za kike
 • Kondomu ya kike imetengenezwa kwa plastiki nyembamba, inayoitwa ”polyurethane”. Toleo jipya la kondomu za kike linalogharimu kidogo hutengenezwa kwa ”nitrile”
 • Kondomu hizi huingizwa ndani ya uke na huwa na pete mbili, moja kila upande.
 • Pete ambayo huingizwa ukeni hufunika sehemu ya juu ya mlango wa kizazi kwa mpira wake. Pete hiyo nyingine ina uwazi na hubakia nje ya uke na kuifunika kuma.

Ina ufanisi kiasi gani?

 • Kondomu ya kike ni ufanisi kwa 75% hadi 82% kwa matumizi ya kawaida. Inapotumiwa kwa usahihi wakati wote, kondomu za kike zinafaa kwa 95%.
 • Kondomu za kike zinaweza kushindwa kufanya kazi vyema kwa sababu zile zile sawa za kiume, hii ni pamoja na:
  • Kama kuna tobo au kuchanika (Hii inaweza kutokea kabla au wakati wa kujamiiana.)
  • Kama haijawekwa vyema kabla ya uume kugusa uke.
  • Kama hautumii kila wakati unaposhiriki ngono.
  • Kama kuna kasoro wakati wa kutengenezwa (hii ni adimu).
  • Kama shahawa zilizo kwenye kondomu zikimwagika ukeni wakati wa kuitoa

Je, zitakufaa?

 • Kondomu za kike zinapatikana kwa urahisi
 • Bei ni rahisi (ingawa ni ghali kuliko za kiume).
 • Unaweza kununua kondomu za kike katika maduka ya dawa, kliniki za magonjwa ya zinaa, na kliniki za uzazi wa mpango.
 • Unahitaji kuwa na kondomu wakati wa kushiriki ngono. Japo za kike zinaweza kuvaliwa/kuwekwa masaa 8 kabla ya kujamiiana.

Faida za kondomu ya kike

 • Zinaweza kutumika wakati wa hedhi, ujauzito, au baada tu ya kujifungua.
 • Inawaruhusu wanawake kujikinga dhidi ya mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya ngono bila kutegemea kondomu ya kiume.
 • Kinga dhidi ya ujauzito na magonjwa ya zinaa.

Maudhi ya kondomu ya kike

 • Msuguano wa kondomu hupunguza mchechemuo wa kinembe na kupunguza ute unaolainisha. Hii inaweza kusababisha usifurahie ngono au hata kukukera, ingawa matumizi ya vilainishi husaidia.
 • Unaweza kuwashwa au kupata mjibizo mbaya wa mzio
 • Kondomu inaweza kusababisha kelele (kutumia kilainishi inaweza kusaidia). Matoleo mapya hayana kelele sana.
 • Hakuna mawasiliano ya moja kwa moja kati ya uume na uke.
 • Mwanamke hukosa ile raha ya maji maji ya moto kumwingia mwanaume anapomwaga (hii ni muhimu kwa baadhi ya wanawake, sio muhimu kwa wengine).

Jinsi ya kutumia kondomu ya kikekondomu

 • Itafute pete ya ndani ya kondomu, na kisha ishike kwa kidole chako cha kati na gumba..
 • Ifinye pete ya ndani na kisha iingize ndani ukeni kwa kadri unavyoweza.
 • Iacha pete ya nje nje ya uke.
 • Hakikisha kuwa kondomu haijajipinda.
 • Weka matone kadhaa ya kilainishi kwenye uume kabla ya kuingiza uume au wakati wa kujamiiana.
 • Baada ya kujamiiana, na kabla ya kusimama, finya na kisha izungushe pete ya juu ili kuhakikisha shahawa hazimwagiki.
 • Ondoa kondomu kwa kuvuta polepole. Tumia mara moja tu.
 • Usitupe kondomu kwenye choo za kisasa, kwa sababu haziwezi ku-flush , zitupe kwenye shimo la taka, la sivy litaziba choo.

Mambo muhimu ya kujua

 • Kuwa mwangalifu usiitoboe kwa kucha zako au mapambo.
 • USITUMIE kondomu ya kike na kiume kwa wakati mmoja. Msuguano kati yao utafanya zichanike au zikunjamane.
 • USITUMIE kilainishi kilichotokana na petrol kama vile mafuta ya Vaselini. Aina hii ya vilainishi huharibu mpira.
 • Kama kondomu inachanika au kupasuka, pete ya nje hukandamizwa sana kwenye sehemu ya juu ya uke au kondomu hukunjama sana wakati wa kujamiiana. Iondoe mara moja na ingiza nyingine.
 • Hakikisha zinapatikana na zinafaa. Hii itasaidia kukupunguzia vishawishi vya kushiriki ngono bila kondomu.
 • Ondoa tampon kabla ya kuingiza kondomu.
 • Kama ikipasuka au kuchanika na shahawa kumwagika ukeni au kama zimemwagika ndani wakati wa kuitoa, mwone daktari kwa ajili ya dawa za dharura za kuzuia mimba.
 • Kama unatumia kondomu kila mara kwa ajili ya kuzuia mimba, mwone daktari na muulize njia mbadala za kukusaidia kama kondomu itapasuka
 • Tumia kila moja mara moja tu.

Vyanzo

Leave feedback about this

 • Quality
 • Price
 • Service

PROS

+
Add Field

CONS

+
Add Field
Choose Image
Choose Video
X