Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Sababu kubwa zaidi inayosababisha kucha zenye mwonekano mbaya ni mambukizi ya fangasi. Mara nyingi fangasi wanathiri zaidi kucha za miguu, hasa miguu inayotokwa jasho au kama haikauki vizuri baada ya kuiosha. lakini pia , kucha zinaweza kupata maambukizi kwa sababu ya unyevunyevu unaojificha chini ya kucha za kubandika.
Ukucha unakuwa mnene, unamomonyoka kwa urahisi na unabadilika rangi na kuwa mweupe /manjano. Ukucha unakua ukiwa na sura mbaya au umbo ambalo halipendezi au unakua ukiwa umenyanyuka na haugusi sakafu ya ukucha.
Matatizo mengine ni kama vile kuwa na kucha kavu, ngumu na zinazokatika au kuchanika kwa urahisi, baadhi huwa na madoadoa meupe kwenye kucha ambayo hutokea baada ya kuumia kucha. Wengine huwa na kucha zenye mikunjo mikunjo, hii utaipata zaidi kwa wazee. Kwa baadhi ya nyakati, mabadiliko kwenye kucha yanaweza kuashiria kuwa una ugonjwa mwingine ndani ya mwili.
Wakati gani umwone daktari
Ni vizuri kupanga kumwona daktari kama:
- Unadhani una maambukizi ya fangasi kwenye kucha
- Kama unaona kuna mabadiliko ya umbo kwenye kucha, kama vile kujikunja kwa kucha au kuwa na kucha zinazosababisha ncha za vidole zionekane kama rungu au kama unaona kuna vishimo shimo kwenye uso wa kucha
Unachoweza kufanya nyumbani ukiwa na kucha zenye mwonekano mbaya
Unaweza kujaribu kufanya mambo yafuatayo kama una kucha ngumu, zinazokatika kiurahisi, na kama una maambukizi ya fangasi. Ni vizuri pia kufuata matibabu aliyokuandikia daktari.
- Nawa mikono vizuri baada ya kushika ukucha ambao una maambukizi, kwa sababu ukishika ukucha mwingine unaweza kuhamishia maambukizi huko.
- Usitembee peku peku karibu na maeneo ya kuogelea au maeneo ya kuogea kama una maambukizi kwenye kucha, unaweza kuwaambukiza wengine
- Vaa soksi safi zilizotengenezwa kwa pamba na zibadilishe kila siku. Vaa viatu vinavyokutosha vizuri, vilivyotengenezwa kwa bidhaa asili ili visitunze unyevu. Kama miguu inatoa jasho, vua viatu wakati wa mchana, kama ikiwezekana vaa viatu vya wazi.
- Zitunze kucha kwa kuzihudumia, zipatie matunzo mazuri, sio lazima uende kutengenezwa kucha na mtaalamu “pedicure”
Namna ya kukata kucha vizuri
- fanya mambo ya kawaida tu, kama yafuatayo, yatakusaidia sana:
- Ukifuatilia utaratibu huu utasaidia kuweka kucha kuwa zenye afya na kupunguza uwezekano wa kuvunjika au kukatika
- Kwanza, Kata kucha mara kwa mara ili ziwe mraba kwenye pande zake na ziwe kwa mzunguko sehemu ya juu. Ni vizuri kukata kucha ambazo ni ngumu au zilizokakamaa baada ya kuziloweka au baada ya kutoka kuoga
- Pili, Sawazisha kucha baada ya kuzikata, unapaswa kuzisawazisha kutoka upande mmoja kwenda mwingine taratibu, yani kama unaranda mbao, usisugue kama unatumia msumeno kukata mbao (kutoka upande mmoja na upande mwingine), mbinu hii inasababisha ukucha uwe dhaifu.
-
- Tatu, usikwangue au kukata sehemu ya nyama inayokuwa kwenye shina la kucha (kucha inapokuwa inatokeza huwa kuna ukuta wa nyama huwa unatokeza), unaitwa cuticle kwa kiingereza, baadhi ya watu huwa wanaukata, lakini njia hii sio nzuri. Loweka kucha zako kisha chukua kifaa chenye ncha isiyochoma, jaribu kuzirudisha nyuma kadri unavyoweza
- Nne, Wakati wa kulala, jipake mafuta kwenye kucha na ngozi inayoizunguka. Ni vizuri kujipaka mafuta kila baada ya kunawa au kushika maji kwa muda mrefu
Mambo mengine unayoweza kufanya kulinda kucha ni:
- Unaweza kuvaa glavu unapokuwa unafanya kazi ndogo ndogo za nyumbani ili kukinga mikono na maji, kwa mfano kufua, kuosha vyombo au unapokuwa unasafisha nyumba kwa kutumia kemikali mbalimbali
- Kuna bidhaa za urembo ambazo unaweza kuzipaka kwenye kucha mara moja kwa wiki ili kuzitia nguvu, unaweza kutafuta moja ya hizo badhaa ukazitumia. Na ni vizuri usipachike au kubandika kucha za bandia au kupaka rangi ya kucha kama una tatizo kwenye kucha.
- Kama kuna mikunjo mikunjo kwenye kucha, unaweza kukwangua mara moja moja ili kuunyoosha, lakini kuwa makini usikwangue sana ukafanya ukucha kuwa mwepesi sana au ukajiumiza
Ukiwa na kucha zenye mwonekano mbaya mwone daktari kama;
Ni vizuri kumwona daktari kama matatizo ya kucha yataendelea kuwepo au kama utaanza kuona dalili nyingine ambazo hauzielewi
Leave feedback about this