KUCHANGIA DAMU:sababu na namna ya kujiandaa

Maelezo ya jumla

Kuchangia damu (blood donation) ni utaratibu wa hiari unaoweza kuokoa maisha ya wengine. Kuna aina kadhaa za uchangiaji wa damu, unaosaidia kukidhi mahitaji mbalimbali ya kitabibu.

Aina za uchangiaji damu

Kuna aina mbili za uchangiaji wa damu, kuchangia damu nzima au apheresis

Kuchangia damu nzima

Hii ndio aina ya uchangiaji damu inayofanywa na watu wengi. Mchangiaji huchangia chupa kadhaa za damu nzima. Baadae damu hii hugawanywa katika sehemu zake- seli nyekundu za damu, chembe sahani na plazima.

Apheresis

Ni aina nyingine ya utoaji damu ambayo haifanyiki sana kwenye nchi zetu.  Mtoaji huwekwa kwenye mashine ambayo hutoa damu mwilini mwa mfadhili na kuigawanya katika sehemu zake, hii ni pamoja na seli nyekundu, plazima na chembe sahani na kisha kumrudishia aina ya seli zisizohitajika.

 • Kuchangia chembe sahani – mfadhili huchangia chembe sahani za damu- chembe sahani husaidia kufanya damu kuganda kwa kutengeneza vizibo kwenye mishipa Watu wenye saratani ya damu,  wanaopata tibakemikali na watoto wenye maambukizi makali huongezewa chembe sahani zinapopungua.
 • Kuchangia seli nyekundu za damu– Aina hii ya uchangiaji humwezesha mchangiaji kuchangia seli nyekundu za damu mara mbili ya kiasi ambacho angechangia kama angechangia damu nzima .

Watu wenye mahitaji ya seli nyekundu za damu ni pamoja na watu wanaovuja damu, kama waliopata ajali au kuumia na wenye upungufu wa damu mwilini.

 • Kuchangia plazima– huchangia sehemu ya majimaji ya damu (plazima). Plazima husaidia damu kuganda na huwa na protini na vitu vingine vinavyosaidia mwili kufanya kazi yake vyema . Watu wenye matatizo ya ini ,  watu walioungua na moto na watu wenye maambukizi makali ya bakteria kwenye damu huhitaji kuongezewa plazima.

Kwanini ni muhimu kuchangia damu

Unakubali damu yako itolewe na kupewa mtu mwingine anayehitaji kuongezewa damu. Watu mamilioni wanahitaji kuongezewa damu kila mwaka. Wengi wanaitegemea baada ya ajali au kwa sababu wana ugonjwa unaohitaji damu. Uchangiaji wa damu hufanya mambo yote haya kuwezekana. Hakuna mbadala wa damu- damu yote inayotumika inatoka kwa wachangiaji.

Kuna hatari yoyote wakati wa kuchangia damu

Kuchangia damu ni utaratibu salama kabisa. Vifaa vipya, safi na salama hutumika kuchukua damu kutoka kwa kila mchangiaji. Kwa hiyo hakuna hatari ya kuambukizwa magonjwa wakati wa kuchangia.
Kama wewe ni mtu mzima mwenye afya njema, unaweza kuchangia chupa ya damu bila kuhatarisha maisha yako. Ndani ya masaa 24 mwili wako hurejesha kiasi cha kimiminika kilichotolewa. Na baada ya wiki kadhaa, mwili wako hutengeneza na kurejesha seli nyekundu ulizotoa.

Maandalizi kabla ya kuchangia damu

Je unakidhi vigezo?

Inabidi kukidhi vigezo kadhaa kabla ya kuchangia damu nzima, plazima au chembe sahani.
Unapaswa kuwa:

 • Katika hali njema ya kiafya
 • Angalau na umri wa miaka 16 au 17, hii hutegemea sheria za nchi
 • Uzito wa angalau kilo 50
 • Kupita tathmini ya kimwili na kihistoria inayofanywa na mtoa huduma

Vigezo hutofautiana kidogo kwa kila aina ya uchangiaji damu na kwa kila kituo cha kuchangia damu. Kabla haujachangia uliza ili kupata maelekezo zaidi.

Chakula na dawa

Kabla ya kuchangia damu:

 • Pata usingizi wa kutosha usiku wa kuamkia siku ya kuchangia damu
 • Kula mlo bora na wenye afya kabla ya kuchangia damu
 • Epuka kula vyakula vyenye mafuta mengi kama vile hamburgers, chips au ice cream kabla ya kuchangia. Vipimo vinavyofanyika kwa damu zote zinazochangiwa vinaweza kuathiriwa na mafuta haya.
 • Kunywa maji mengi zaidi kuliko kawaida au vinywaji vingine kabla ya kuchangia
 • Kama unachangia chembe sahani pekee, usitumie aspirini kwa angalau siku 2 kabla ya kuchangia.

Nini cha kutarajia

Kabla ya changia damu

Kabla ya kuchangia damu, utaombwa kujaza fomu au kujibu maswali kadhaa kuhusu historia yako ya kitabibu na kuhusu tabia zinazoongeza hatari ya kupata maambukizi yanayoweza kuambukizwa kwa kupitia damu. Taarifa hizi zinahifadhiwa kwa siri.
Kwa sababu kuna hatari ya magonjwa kusambaa kupitia damu, sio kila mtu anaruhusiwa kuchangia damu. Makundi ya watu wafuatayo hayastahiki kuchangia damu kwa sababu wako kwenye hatari kubwa ya kuwa na magonjwa yanayoweza kuambukizwa kupitia damu:

 • Mtu yeyote ambaye amewahi kujidunga madawa ya kulevya au madawa ambayo hayakuruhisiwa na daktari.
 • Wanaume ambao wameshiriki ngono na wanaume wenzao ndani ya kipindi cha miezi 12.
 • Mtu yoyote mwenye tatizo la damu kushindwa kuganda
 • Mtu yoyote mwenye maambukizi ya VVU
 • Wanaume au wanawake waliowahi kufanya ngono kwa ajili ya pesa au madawa (wanaojiuza)
 • Mtu yeyote ambaye kwa miezi 12 iliyopita amekuwa karibu au ameishi au kushiriki ngono na mtu mwenye ugonjwa wa homa ya ini

Utafanyiwa uchunguzi mfupi wa mwili, hii ni pamoja na kupimwa shinikizo la damu, mapigo ya moyo na joto la mwili. Utatobolewa kwenye kidole kwa sindano ili kuangalia kiwango cha haemoglobin. Kama haemoglobin inatosha utaruhusiwa kuchangia damu.

Wakati wa kuchangia damu

Unalala au unakaa kwenye kiti kilichoinama na kuweka mkono kwenye armrest. Mkono wako utafungwa kwa tourniquet ili mishipa yako ionekane vyema kabla ya kuingiza sindano. Sehemu ya ngozi itakapowekwa sindano itasafishwa vyema.
Sindano mpya na safi itaingizwa kwenye mshipa wa mkono. Sindano hii huwa imeungwa kwenye mrija ulioungwa kwenye mfuko wa kukusanya damu. Baada ya hapo utapaswa kukunja ngumi na kusaidia damu kutoka kwenye mishipa na kuujaza mfuko.  Mara nyingi sindano inabakia hapo kwa dakika 10 hivi. Baada ya mfuko kujaa, sindano itaondolewa na bandeji ndogo itafungwa kwenye sehemu iliyotobolewa kuzuia damu kuvuja.
Njia nyingine ya kutoa damu ambayo umaarufu wake haujaongezeka sana nchini kwetu ni apharesis.  Wakati wa apharesisi damu hutolewa kwenye mkono mmoja na kuingia kwenye mashine ambayo hupembua seli zinazohitajika , kama vile chembe sahani na kisha kuirudisha mwilini kupitia mkono mwingine.  Aina hii ya utoaji damu humruhusu mchangiaji kuchangia component anayotaka na kisha kurudishiwa component zingine. Aina hii ya uchangiaji huchukua muda mrefu zaidi kuliko uchangiaji wa kawaida. Inaweza kuchukua mpaka masaa 2.

Baada ya kuchangia damu

Baada ya kuchangia,  utakaa katika eneo la uangalizi, ambapo utapumzika na kula vitafunio au vinywaji. Baada ya dakika 15, unaweza kuondoka.
Baada ya kuchangia damu:

 • Kunywa maji ya ziada kwa siku mbili zinazofuata
 • Epuka shughuli nzito au kunyanyua vitu vizito ndani ya masaa 5 baada ya kuchangia damu
 • Kama unahisi kizunguzungu au unahisi kuzirai lala chini na nyanyua miguu yako mpaka utakapojihisi vizuri.
 • Bendeji uliyowekewa jaribu kuiacha hapo kwa angalu masa 5 ili ikauke
 • Kama bado unavuja damu baada ya kuondoa bendeji, bana sehemu inayovuja na kisha nyanyua mkono wako mpaka damu itakapokoma.
 • Kama damu imevia ndani ya ngozi, weka barafu mara kwa mara kwa angalu masaa 24 ya mwanzo
 • Kama mkono wako unauma, meza dawa ya maumivu kama paracetamol. Epuka kumeza Asprin au ibuprofen kwa masaa 24 mpaka 48 ya mwanzo.

Wasiliana na kituo cha kuchangia damu au daktari kama umesahau kuwataarifu kuhusu swala lolote muhimu kabla ya kuchangia damu au kama umepata tatizo lolote baada ya kuchangia damu.
Unapaswa pia kuwasiliana na kituo cha kuchangisha damu kama:

 • Unaendelea kuhisi kichefuchefu, kizunguzungu au kuhisi kuzirai baada ya kupumzika, kula na kunywa vinywaji.
 • Unaona kuna uvimbe , unaendelkea kuvuja damu au maumivu makali kwenye eneo ulilochomwa sindano.
 • Una hisi maumivu yanayosambaa kutoka mkononi mpaka kwenye vidole vya mkono
 • Unajihisi kuumwa na dalili za mafua kama homa, kichwa kuuma au maumivu kwenye koo, ndani ya siku nne baada ya kuchangia damu. Maambukizi ya bakteria yanaweza kusababisha mtu anayeongezewa damu yako kuugua , kwa hiyo toa taarifa ili damu yako isitumike.

Upimaji

Damu yako itapimwa ili kutambua aina ya damu yako – iliyoainishwa kama A, B, AB au O – na Rh factor. Neno Rh humaanisha uwepo au kutokuwepo kwa antijeni fulani – Antijeni huuchachawisha mwili kutengeneza kinga ya mwili- kwenye damu. Damu ya mtu huainishwa kama chanya kama ina antijeni hizi au hasi kama hakuna antijeni hzo. Taarifa hizi ni muhimu kwa sababu, ili kumwongezea mtu mwingine damu yako, ni lazima damu zenu zifanane.
Damu yako itapimwa pia kuangalia magonjwa kama vile homa ya ini, Virusi vya Ukimwi na kaswende. Kama vipimo hivi ni hasi, damu hutumika kuongezea wengine. Kama ni Chanya damu yako hutupwa.

Vyanzo

https://medlineplus.gov/bloodtransfusionanddonation.html

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi