Magonjwa ya ndani ya mwili

KUFUNGA CHOO

kufunga choo

Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko

Maelezo ya jumla

Kufunga choo (constipation) ni hali ya kushindwa kupata kinyesi (kunya) kwa angalau mara tatu kwa wiki. Mtu akifunga choo, kinyesi huwa kigumu, kidogo, na kigumu kutoka. Baadhi ya watu hupata maumivu  wakati wa kupata kinyesi, hujikamua sana wakiwa chooni na huwa na hisia ya tumbo kujaa.
Watu wengine hufikiri kuwa wamefunga choo wakikosa choo kwa siku moja tu. Lakini hiyo sio kweli, kwa kawaida mtu anaweza kupata choo mara tatu kwa siku au mara tatu kwa wiki.
Kufunga choo ni dalili, sio ugonjwa. Karibu kila mtu hufunga choo katika kipindi fulani katika maisha yake, na mara nyingi mlo usio kamili ndio chanzo. Hali hii ya kufunga choo mara nyingi si hatari ni ya muda tu. Kutambua sababu yake, jinsi ya kuizuia, na matibabu yake itasaidia watu wengi kupata nafuu.

Nini dalili za Kufunga choo?

Mtu aliyefunga choo hupata kinyesi mara chache isivyo kawaida, kinyesi huwa kigumu na huhitajika kujikamua sana ili kitoke. Kinyesi kinaweza kuwa kigumu na kikubwa hivyo kuchana njia ya haja kubwa, hasa kwa watoto. Hali hii inaweza kusababisha kutokwa damu na hata ufa kwenye njia ya haja kubwa.

Nini sababu ya kufunga choo?kufunga choo

Kuelewa jinsi mfumo wa kumeng’enya chakula unavyofanya kazi husaidia kuelewa jinsi kufunga choo kunavyotokea. Maji hunyonywa toka kwenye chakula kinapopita kwenye utumbo mpana ili kutengeneza kinyesi. Misuli kwenye utumbo mpana hukaza na kusukuma kinyesi kuelekea kwenye rektamu. Kinyesi kinapofika kwenye rektamu huwa kimeshakuwa kigumu tayari, hii ni kwa sababu, sehemu kubwa ya maji huwa imenyonywa na kurudishwa mwilini.
Kufunga choo hutokea kama utumbo mpana umenyonya maji mengi zaidi kutoka kwenye kinyesi na kukiacha kigumu na kikavu au kama misuli ya utumbo mpana imepata matatizo na kushindwa kusukuma kinyesi kuelekea kwenye rektamu, hii husababisha maji mengi zaidi kunyonywa, matokeo yake mtu hupata kinyesi kigumu na kikavu sana. Zifuatazo ni sababu za kufunga choo

  • Mlo usio na nyuzinyuzi za kutosha
  • Kutokuwa na mazoezi ya kutosha
  • Madawa
  • Maziwa
  • Mabadiliko katika maisha kama vile ujauzito, kuzeeka, au safari
  • Kutumia vibaya dawa za kulainisha kinyesi (laxative)
  • kupuuza hamu ya kwenda chooni/ kuchelewa kwenda choo.
  • Kutokunywa maji ya kutosha
  • Magonjwa au hali maalum, kama vile kiharusi
  • Matatizo ya utumbo mpana (koloni) au rektumu

Mlo usiokuwa na nyuzinyuzi za kutosha

Watu wanaokula mlo wenye nyuzinyuzi nyingi kwa kawaida hawako kwenye hatari ya kufunga choo. Sababu kubwa ya kufunga choo ni kula mlo wenye kiwango kidogo cha nyuzinyuzi au mlo wenye kiwango kikubwa cha mafuta, kama vile jibini, mayai, au nyama.
Nyuzinyuzi (fiber)- ni sehemu ya matunda, mbogamboga, na nafaka ambayo mwili hauwezi kuimeng’enya. Uzito na ulaini wa nyuzinyuzi hizi husaidia kuzuia kinyesi kuwa kigumu, kikavu na kugumu kutoka.
Watu wengi hula vyakula vilivyokobolewa na  kusafishwa viwandani. Vyakula hivi vya viwandani hundolewa nyuzinyuzi zote.
Vyakula vyenye kiwango cha chini cha nyuzinyuzi huchangia sana kufunga choo, hasa kwa wanaokula vyakula vya kiwandani ambavyo ni rahisi kupika au kununua.

Maji yasiyotosha

Utafiti unaonyesha kuwa ingawa kuongeza kiwango cha maji unayokunywa haisaidii mara zote unapokuwa umefunga choo, watu wengi hupata nafuu wanapokunywa maji na vinywaji kwa wingi. Vinywaji huongeza majimaji kwenye utumbo mpana na kuongeza uzito wa kinyesi, hii husaidia kinyesi kupita kwa urahisi. Watu wenye shida ya kufunga choo wanapaswa kunywa maji kwa wingi kila siku. Hata hivyo, vinywaji vyenye kafeini, kama vile kahawa na vinywaji vya cola vinaweza kuongeza tatizo. Vinywaji kama vile  pombe vinaweza kupunguza maji mwilini na kuongeza tatizo. Ni muhimu kunywa vinywaji vinavyoongeza maji mwilini hasa unapokuwa unatumia vinywaji vyenye kafeine au pombe.

Kutofanya mazoezi ya kutosha

Japo wataalamu hawajui kwa nini, kutofanya mazoezi ya kutosha kunaweza kusababisha kufunga choo. Kwa mfano,kufunga choo hutokea mara tu baada ya ajali au wakati wa kuugua, wakati ambao mgonjwa huwa amelazwa kitandani na hafanyi mazoezi yoyote. Kutofanya mazoezi ndio sababu kuu ya kufunga choo kwa wazee wengi.

Madawa

Madawa mengine yanaweza kusababisha kufunga choo, hii ni pamoja na:

  • Dawa za maumivu
  • Dawa za kupunguza asidi tumboni zenye aluminiamu na kalsiamu
  • Dawa za kudhibiti shinikizo la juu damu (calcium channel blockers)
  • Dawa za kudhibiti ugonjwa wa parkinson (ugonjwa wa kutetemeka/kukakamaa kwa mwili)
  • Dawa za kudhibiti sonona (anti-depressants)
  • Dawa zenye virutubisho vya chuma
  • Dawa za kupunguza maji mwilini (diuretics)
  • Dawa za kudhibiti degedege (anticonvulsants)

Mabadiliko katika maisha

  • Wakati wa ujauzito, wanawake wanaweza kufunga choo kwa sababu ya mabadiliko ya homoni au kwa sababu ya utumbo kubanwa na mji wa mimba (uterasi).
  • Uzee pia unaweza kuathiri utendaji kazi wa utumbo, hii ni kwa sababu shughuli za kimetaboliki hupungua uzeeni na kusababisha misuli ya utumbo kulegea.
  • Watu hufunga choo pia wakiwa safarini, hii ni kwa sababu, utaratibu wao wa mlo huvurugika sana wakati wakiwa safarini

Kutumia vibaya dawa za kulainisha kinyesi

Imani potofu kuwa mtu anapaswa kupata kinyesi kila siku imesababisha watu kutumia dawa za kulainisha kinyesi (laxatives) mara kwa mara bila ushauri wa daktari. Japo watu hawa huhisi nafuu baada ya kutumia dawa hizi, kwa kawaida kila mara huhitaji kuongeza dozi ya dawa wanayotumia ili kupata kinyesi, hii ni kwa sababu mwili huizoea dawa hii kila mara wanapoitumia. Mwishowe watu hawa, huwa tegemezi kabisa kwa dawa hizi.

Kupuuza hamu ya kwenda chooni

Watu wanaopuuza hamu ya kwenda chooni mwishowe hufunga choo. Watu hupuuza hamu ya kwenda chooni kwa sababu tofauti tofauti, wengine hawapendi kutumia vyoo vya uma hivyo husubiri mpaka wakirudi nyumbani mwao. Wengine hupuuza hamu ya kupata choo kwa sababu ya msongo wa mawazo au kazi nyingi sana (busy).

Magonjwa maalum

Magonjwa yanayosababisha kufunga choo ni pamoja na magonjwa ya mfumo wa neva, matatizo ya kimetaboliki, na hali zinazoathiri mifumo ya mwili. Matatizo haya yanaweza kupunguza kasi ya kinyesi kupita kwenye koloni, rektum, na njia ya haja kubwa.
Matatizo yanayoweza kusababisha kufunga choo ni pamoja na:

  • Matatizo ya mfumo wa neva
    • Multiple sclerosis– huu ni ugonjwa wa kukakamaa kwa tishu za mwili
    • Parkinson’s disease – Ugonjwa huu husababisha kutetemeka/kukakamaa kwa mwili
    • kiharusi
    • Majeraha ya uti wa mgongo
  • Hali za kimetaboliki
    • kisukari
    • Uremia- hii ni hali ya kuwepo kwa kiwango kikubwa cha urea ndani ya damu –urea ni taka mwili inayotengenezwa baada ya shughuli za kimetaboliki na inapaswa kutolewa mwilini kupitia kwenye figo.
    • Hypercalcemia– hali ya kuwapokwa kiwango kikubwa cha kalisi mwilini
    • Hypothyroidism– hali ya kuwepo kwa kiwango kidogo cha homoni zinazotolewa na tezi dundumio
  • Matatizo ya mfumo
    • Amyloidosis-ugonjwa huu husababisha aina ya protini inayoitwa amyloid kurundikana mwilini na kusababisha ini, figi, bandama na tishu zingine kushindwa kufanya kazi yake.
    • Lupus erythematosus– ni hali inayosababisha kuvimba na madoa doa mekundu kwenye ngozi
    • Scleroderma– ni hali inayosababisha kukakamaa kwa ngozi ya mgonjwa, ngozi huwa ngumu na nzito, kukakamaa huku kunaweza kutokea kwenye ngozi yote au sehemu tu ya ngozi

Matatizo ya utumbo mpana na rektum

Kuziba kwa utumbo mpana, makovu, uvimbe na kusinyaa kwa utumbo mpana, au saratani inaweza kubana na kupunguza kipenyo cha utumbo na kupunguza njia ya kinyesi kupita hivyo kusababisha kufunga choo.

Nani yuko katika hatari zaidi ya kufunga choo?

Kufunga choo ni mojawapo ya tatizo linalowapata watu wengi.

  • Wanaoripoti tatizo hili zaidi ni wanawake wenye umri wa miaka 65 na zaidi.
  • Wanawake wajawazito wanaweza kuwa na tatizo hili pia
  • Kufunga choo ni tatizo la kawaida baada ya kujifungua au baada ya upasuaji.

 Utambuzi wa kufunga choo

Vipimo atakavyofanya daktari hutegemea muda na makali ya hali yako, umri na kama kuna damu kwenye kinyesi. Watu wengi waliofunga choo hawahitaji vipimo vingi, na mara nyingi hutibiwa kwa mazoezi na mabadiliko ya mlo tu. Kwa mfano, mara nyingi ni historia na uchunguzi wa mwili tu unaohitajika kufanya utambuzi kwa vijana.

Historia

Daktari anaweza kumwomba mgonjwa kuelezea hali yake, Hii ni pamoja na:

  • Muda wa dalili
  • ugumu wa kinyesi,
  • Kama kuna damu kwenye kinyesi
  • Anapata kinyesi mara ngapi kwa wiki
  • Anakula chakula cha aina gani
  • Madawa anayotumia
  • Kama anafanya mazoezi ya kutosha

Maelezo haya yatamsaidia daktari kufanya utambuzi wa sababu ya kufunga choo.
Mtu hesemekana amefunga choo kama ana dalili mbili kati ya zifuatazo kwa angalau wiki 12 – sio lazima ziwe kwa mfuatano- ndani ya miezi 12 iliyopita;

  • Kujikamua ili kinyesi kitoke
  • Kinyesi kigumu na kikavu
  • Hisia kuwa kinyesi hakijatoka chote baada ya kujisaidia
  • Hisia kuwa kuna kitu kinaziba rektamu au mkundu
  • Kupata kinyesi chini ya mara tatu kwa wiki

Uchunguzi wa mwili

Uchunguzi wa mwili unaweza kujumuisha uchunguzi wa rektamu kwa kidole kilichopakwa kilainishi ili kupima mkazo wa misuli ya njia ya haja kubwa (anal sphincter) -na kutambua kama kuna maumivu, kuziba au damu eneo hilo.
Katika hali nyingine, vipimo vya damu na vipimo vya tezi dundumio vinaweza kuhitajika ili kutambua kama kuna;

  • Ugonjwa wa tezi dundumio
  • kiwango kikikubwa cha kalisi kwenye damu
  • Matatizo ya kimetaboliki na
  • Matatizo mengine

Vipimo vikubwa mara nyingi hufanyika kwa wagonjwa wenye dalili kali, kwa mfano wenye damu kwenye kinyesi.
Kwa sababu kuna hatari ya kuwepo kwa saratani ya njia ya haja kubwa kwa wazee, daktari anaweza kuagiza vipimo vifuatavyo ili kujiridhisha kuwa hakuna saratani:

  • Barium enema x-ray
  • sigmoidoscopy au colonoscopy

Ukiwa na tatizo la kufunga choo ni wakati gani utafute matibabu haraka?

Mwone daktari kama:

  • Umefunga choo ghafla, tumbo linauma sana na hujambi (USINYWE dawa za kulainisha kinyesi-laxatives)
  • Maumivu makali ya tumbo, hasa kama tumbo limejaa
  • Damu kwenye kinyesi
  • Kufunga choo kunakofuatiwa na kuhara na kisha kufanga choo tena
  • Kinyesi chembamba sana kama kalamu- hii humaanisha sehemu ya utumbo imeziba
  • Maumivu ya rektamu
  • Kupungua kwa uzito usioelezeka

Mwone daktari kama:

  • Mtoto mwenye umri chini ya miezi 2 amefunga choo
  • Mtoto (isipokuwa wale wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee) asipopata kinyesi kwa siku 3 – mwone daktari mara moja kama mtoto anatapika pia

Uchaguzi wa matibabu baada ya kufunga choo

Ingawa matibabu hutegemea sababu, makali, na muda mgonjwa aliofunga bila kupata choo, mara nyingi mabadiliko ya mlo na mfumo wa maisha husaidia sana kuleta nafuu.
Mlo wenye nyuzinyuzi za kutosha husaidia mwili kutengeneza kinyesi laini na kizito. Vyakula vyenye nyuzinyuzi za kutosha ni pamoja na maharage, nafaka kama mahindi, ngano n.k, matunda, na mbogamboga kama kabichi, karoti n.k.
Watu walio kwenye hatari ya kufunga choo, wanapaswa kuepuka vyakula visivyo na nyuzinyuzi kama ice cream, jibini, nyama na vyakula vya viwandani vilivyokobolewa.
Mabadiliko mengine ambayo yanaweza kusaidia kutibu na kuzuia kufunga choo ni pamoja na kunywa maji na vinywaji vya kutosha, kama vile juisi za matunda na mbogamboga ili kuongeza maji mwilini na kufanya mazoezi kila siku.
Watu wengi wenye dalili za kawaida hawahitaji dawa za kulainisha kinyesi (laxatives). Hata hivyo, kwa wale ambao wamefanya mabadiliko ya mfumo wa maisha na mlo, na bado hawapati nafuu, daktari anaweza kupendekeza dawa za kulainisha kinyesi au enemas kwa muda mfupi.
Daktari ataamua ni wakati gani mgonjwa atahitaji laxative na ni aina gani inayomfaa mgonjwa. Watu walio na utegemezi wa dawa za kulainisha kinyesi (laxatives) wanahitaji kupunguza matumizi taratibu mpaka watakapoacha kabisa. Daktari anaweza kusaidia katika mchakato huu. Kwa watu wengi, kuacha kutumia dawa hizi hurejesha vyema uwezo wa asili wa koloni kusukuma kinyesi.
Matibabu Mingine
Matibabu ya kufunga choo yanaweza kuelekezwa kwa chanzo chake maalumu. Kwa mfano, daktari anaweza kupendekeza usitishe matumizi ya dawa inayohisiwa kusababisha ttizo lako, anaweza pia kupendekeza kufanya upasuaji ili kurekebisha matatizo kwenye koloni au rektamu.

Dawa za kuepuka

Wagonjwa waliofunga choo wanapaswa kuepuka kutumia dawa zifuatazo:

  • Alosetron

Kama umefunga choo unapaswa kuwasiliana na daktari kabla ya kuanza au kuacha kutumia dawa hizi.

Kuzuia kufunga choo

Kuzuia kufunga choo ni rahisi zaidi kuliko kutibu:

  • Kula mlo wenye nyuzinyuzi kwa wingi
  • Kunywa maji ya kutosha kila siku (angalau glasi 8 za maji kwa siku).
  • Fanya mazoezi mara kwa mara.
  • Nenda chooni unapopata hamu ya kujisaidia. Usisubiri.

Vyanzo

Leave feedback about this

  • Quality
  • Price
  • Service

PROS

+
Add Field

CONS

+
Add Field
Choose Image
Choose Video
X