KUHARA

KUHARA

 • October 25, 2020
 • 0 Likes
 • 90 Views
 • 0 Comments

Maelezo ya jumla

Kuhara (Diarrhea) ni hali ya kupata kinyesi chepesi chenye majimaji mengi. Kwa kawaida, mtu mwenye kuhara hupata kinyesi zaidi ya mara tatu kwa siku. Kuharisha ni tatizo linalowapata watu wengi na linaweza kudumu kwa siku 1 au 2 na kisha kupungua bila matibabu yoyote. Kuharisha kwa muda mrefu kunakoendelea zaidi ya siku 2 kunaweza kuashiria tatizo kubwa zaidi na kunaweza kusababisha upungufu wa maji mwilini. Kuhara kunaweza kusababisha upungufu wa maji mwilini, hii inamaanisha mwili inakosa maji ya kutosha kufanya kazi vizuri. Ukosefu wa maji mwilini ni hatari sana, hasa kwa watoto wadogo na wazee, ni muhimu kupata matibabu ya haraka ili kuepuka matatizo makubwa ya kiafya. Mtu wa umri wotewote anaweza kuharisha na kwa wastani mtu mzima huhara kama mara nne kwa mwaka. Nchini Marekani, kila mtoto atakuwa atakua amepata matukio saba ya kuhara anapofikia umri wa miaka 5.

Je, nini dalili za Kuharisha?

Kuhara kunaweza kuambatana na kujaa tumbo, kichefuchefu, kubana, kukaza au maumivu ya tumbo. Kulingana na sababu iliyosababisha kuhara, mtu anaweza kuwa na homa au kupata kinyesi chenye damu.

Ni nini sababu za Kuharisha?

Kuharisha kwa muda mfupi mara nyingi husababishwa na maambukizi ya bakteria, virusi, au vimelea. Kuharisha kwa muda mrefu mara nyingi huhusiana na matatizo ya kimuundo ya mfumo wa chakula kama irritable bowel syndrome au inflammatory bowel disease.

Zifuatazo ni sababu chache zinazosababisha kuhara:

 • Maambukizi ya bakteria. Mtu anapokula chakula au kunywa maji yalichafuliwa na aina fulani za bakteria husababisha kuhara. Bakteria hawa ni pamoja na Campylobacter, Salmonella, Shigella, na Escherichia coli (E. coli).
 • Maambukizi ya virusi. Aina za virusi nyingi husababisha kuhara, hii ni pamoja na rotavirus, virusi vya Norwalk, cytomegalovirus, virusi vya herpes simplex, na viral hepatitis.
 • Kula vyakula usivyoweza kustahimili (food intolerance). Mfumo wa chakula wa watu wengine hauwezi kumeng’enya aina fulani za vyakula na kwa sababu hiyo wanapokula vyakula hivi husababisha kuharisha. Vyakula kama maziwa na sukari za viwandani ni mfano mzuri.
 • Vimelea (parasites). Vimelea wanaweza kuingia mwilini kwa njia ya chakula au maji na kuishi kwenye utumbo. Vimelea wanaosababisha kuhara ni pamoja na Giardia lamblia, Entamoeba histolytica, na Cryptosporidium.
 • Kuhara kunakosababiswa na madawa anayotumia mgonjwa. Madawa kama Antibiotics, madawa ya kupunguza shinikizo la damu, dawa za saratani, na antacids zenye magnesiamu zinaweza kusababisha kuhara.
 • Magonjwa ya tumbo. Kuna magonjwa ya tumbo kadhaa yanayoweza kusababisha kuhara ,hii ni pamoja na Inflammatory bowel disease, colitis, Crohn’s disease, na celiac disease.

Watu wengine huharisha baada ya upasuaji wa tumbo au kuondolewa kwa mfuko wa nyongo (gallbladder). Sababu inaweza kuwa mabadiliko ya kasi ya chakula kinapopita kwenye mfumo wa kumeng’enya chakula baada ya upasuaji au kuongezeka kwa kiasi cha nyongo kwenye utumbo  baada ya upasuaji wa mfuko wa nyongo.

Watu wanaotembelea nchi za kigeni wako kwenye hatari ya kuharisha,  hii husababishwa na kula chakula au kunywa maji yaliyochafuliwa na bakteria, virusi au vimelea. Kuhara kunakowapata wasafiri (traveler’s diarrhea) ni tatizo linalowapata watu wanaotembelea nchi zinazoendelea.

Kwa kesi nyingi za kuhara, sababu haipatikani. Kama kuharisha kutakoma bila kutumia dawa yoyote, si lazima kufanya vipimo vingi ili kujua sababu yake.

Nani yuko kwenye hatari zaidi ya Kuharisha?

Mtu yeyote anaweza kuharisha. Tatizo hili linaweza kudumu kwa siku moja,siku mbili, miezi na hata miaka, kulingana na sababu. Watu wengi hupona bila kutumia dawa yoyote, lakini kuhara kunaweza kuwa hatari kwa watoto wachanga na wazee ikiwa  hawataonezewa maji waliyopoteza. Watu wengi duniani hufa baada ya kuhara kutokana na kiasi kikubwa cha maji na chumvichumvi kilichopotea.

Utambuzi

Vipimo mbalimbali vinaweza kufanyika ili kubaini sababu ya kuhara kwako, vinaweza kujumuisha:

 • Historia na uchunguzi wa mwili. Daktari atauliza kuhusu ulaji wako na madawa unayotumia na atachunguza mwili wako kuangalia dalili za ugonjwa.
 • Uchunguzi wa kinyesi. Sampuli ya kinyesi itachukuliwa na kupelekwa kwenye maabara kwa ajili ya uchunguzi. Kwenye maabara mtaalamu atachunguza ili kujua kama bakteria, vimelea, magonjwa mengine au maambukizi ndiyo sababu ya kuhara.
 • Vipimo vya damu. Vipimo vya damu vinaweza kusaidia kutambua aina fulani za magonjwa.
 • Kufunga kula chakula. Ili kutambua kama kuharisha kumesababishwa na kushindwa kuhimili aina fulani ya chakula au mzio wa chakula, daktari anaweza kupendekeza usile aina fulani ya vyakula kama maziwa/laktosi, wanga, ngano, au vyakula vingine ili kuona kama kuhara kutakoma baada ya mabadiliko ya mlo.
 • Sigmoidoscopy. Kwa kipimo hiki, daktari hutumia kifaa maalum kuchunguza sehemu ya ndani ya rektum na sehemu ya chini ya utumbo mpana.
 • Colonoscopy. Kipimo hiki ni sawa na sigmoidoscopy, na humruhusu daktari kuchunguza utumbo mpana .
 • Vipimo vya picha. Vipimo hivi vinaweza kugundua matatizo ya kimuundo ya mfumo wa kumeng’enya chakula

Wakati gani utafute matibabu ya haraka

Katika hali ya kawaida kuhara si hatari, lakini inaweza kuwa hatari au kuasharia tatizo kubwa zaidi. Unapaswa kumwona daktari ikiwa utapatwa na lolote kati ya yafuatayo:

Uchaguzi wa matibabu

Katika matukio mengi ya kuhara, kuongeza maji mwilini ndiyo tiba muhimu zaidi. Madawa ya kuzuia kuhara yanaweza kusaidia, lakini hayapendekezwi kwa ugonjwa uliosababishwa na maambukizi ya bakteria au vimelea. Ukizuia kuharisha kabla bakteria na vimelea waliosababisha kuhara kutolewa nje, bakteria na vimelea hao hubaki tumboni, na inaweza kusababisha ugonjwa kuwa mbaya zaidi. Badala yake, mara nyingi madaktari huagiza mgonjwa kupewa antibiotics kama tiba ya kwanza. Maambukizi ya virusi yanaweza kutibiwa kwa dawa au kuachwa yapone yenyewe ,hii ni kulingana na ukali na aina ya virusi.

Vidokezo Kuhusu Chakula

Jaribu kuepuka kafeini, bidhaa za maziwa, na vyakula vyenye mafuta, nyuzinyuzi ,na sukari nyingi mpaka kuhara kutakapokoma. Vyakula hivi vinaweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi.

Kadri hali inavyoimarika unaweza kula vyakula laini kama ndizi,wali,viazi vya kuchemsa, mkate, karoti zilizopikwa, na kuku iliyeokwa bila mafuta.

Madawa yakuepuka

Wagonjwa wanaoharisha wanapaswa kuepuka kutumia dawa zifuatazo:

 • Ethacrynic acid

Ikiwa unaharisha, wasiliana na daktari wako kabla ya kuanza au kuacha kutumia dawa hizi.

Kuzuia Kuhara

 • Osha mikono yako mara kwa mara, hasa baada ya kutoka chooni na kabla ya kula.
 • Wafundishe watoto wasiweka vitu vichafu kinywani.
 • Tumia vitakasa mikono (gel)  kusafisha mikono mara kwa mara.

Kuhara kunakowapata watu wanaosafiri (traveller’s diarrhea) husababishwa na kula chakula au kunywa maji yaliyochafuliwa na bakteria,virusi au vimelea. Unaweza kuchukua tahadhari zifuatazo ili kuzuia kuhara unaposafiri:

 • Usinywe maji ya bomba au kuyatumia kupiga mswaki.
 • Usinywe maziwa ambayo hayajachemshwa au bidhaa za maziwa zisizo salama.
 • Usitumie barafu iliyotengenezwa kwa maji ya bomba.
 • Epuka kula matunda na mboga mboga ambazo hazijapikwa, hii ni pamoja na kachumbari. Unaweza kula matunda baada ya kuyamenya mwenyewe,kama tunda haujalimenya mwenyewe usilile. .
 • Usile nyama au samaki wabichi/bila kupika
 • Usila nyama au samaki waliopoa/ kula chakula kikiwa cha moto.
 • Usile chakula kutoka kwa wachuuzi wa mitaani/ maman’tilie.

Unaweza kuwa salama kwa kunywa maji ya chupa, maji yaliyochemshwa vyema au maji yaliyotiwa dawa ya kusafisha maji. Unaweza pia kunywa vinywaji vingine vilivyo kwenye chupa kama juice au soda na vinywaji vya moto kama chai au kahawa.

Nini cha kutarajia

Matarajio ni mazuri kwa mtu anayeharisha. Kuhara ni hali ya kawaida na mara nyingi hupona bila dawa yoyote, isipokuwa inapokua dalili ya ugonjwa mwingine sugu. Ni muhimu kuongeza maji yaliyopotea mwilini kwa sababu ya kuhara,bila kufanya hivyo mwili utaishiwa maji na hali inaweza kuwa mbaya zaidi.

Vyanzo

http://digestive.niddk.nih.gov/ddiseases/pubs/diarrhea/

 • Share:

Leave Your Comment