Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Kuingiliwa na kitu sikioni ni tatizo. Kama kitu kitaingia na kung’ang’ania ndani ya sikio kinaweza kusababisha usumbufu na kusababisha ushindwe kusikia kwa kitambo kama kitaziba njia nya sikio. Kama ni kitu chenye ncha kali kinaweza kutoboa ngoma ya sikio. Watoto wadogo wakati fulani wanaweza kuweka vitu masikioni. Vitu kama mbegu, vidude vya kuchezea au vipande vya karatasi. Kama hujaona wakiweka masikioni, inaweza kuwa ngumu kujua kuwa wameweka mpaka utakapoona wakilalamika maumivu sikioni, uchafu unatoka sikioni au wanashindwa kusikia vizuri. Watu wazima hubakiza vipande vya pamba kwenye sikio wakati wa kusafisha. Utaratibu huu wa kusafisha masikio kwa kutumia vijiti vyenye pamba haushauriwi na madaktari, kwa sababu unaweza kuleta madhara. Kwa mara chache wadudu wanaweza kuingia na kukwama ndani ya sikio, hii inaweza kushtua, hasa kwa mtoto.
Mwone daktari kama
Panga kumwona daktari mapema kama kitu kilichoingia kwenye sikio hakijatoka chenyewe baada ya kuinamisha sikio au kama umeshindwa kumwondoa mdudu aliyeingia sikioni kwa kutumia utaratibu ufuatao
Unachoweza kufanya wewe mwenywe
Kuna hatua kadhaa unazoweza kuchukua ili kushughulika na kitu au mdudu aliyeingia sikioni. Kama njia hizi hazitasaidia ni bora kumwona daktari akusaidie.
- Egemeza kichwa huku sikio likiwa linaangalia chini, kisha jaribu kulitikisa ili kuona kama kitu au mdudu ataanguka.
- Kama kuna mdudu kwenye sikio, tulia. Geuza kichwa kiweke ili sikio lenye mdudu liangalie juu na subiri uone kama atatoka mwenyewe. Mdudu hufuata mwanga, msubiri anaweza kutoka. Kama asipotoka tumia maji kumwinua ili atoke. Fuata utaratibu ufuatao:
- Kama mdudu ameingia kwenye sikio, mwombe mtu mwingine msaada. USITUMIE njia hii ya kuweka maji sikioni kutoa kitu cha aina nyingine yoyote isipokuwa mdudu. Baadhi ya vitu ukiviwekea maji vinavimba na inaweza kusababisha ikawa ngumu kuviondoa.
- Weka maji ya uvuguvugu tayari na ikiwezekana uwe na kifaa cha kudondoshea maji kwenye sikio ‘’dropper’’
- Mwambie mgonjwa alale huku sikio lenye mdudu likielekea juu na mwambie atulie
- Weka maji kwenye sikio kwa kutumia kifaa cha kuweka matone ‘’ dropper’’ taratibu. Hii itafanya mdudu kuelea juu ya maji na itakuwa rahisi kumtoa
- Baada ya hapo, geuza kichwa sikio lenye maji lielekee chini ili maji yamwagike kutoka sikioni
- Kama bado mdudu hajatoka baada ya kujaribu njia hii, USIJARIBU njia nyingine kumtoa, Tafadhali nenda kamwone daktari.
- Usijaribu kuondoa au kutoa kitu kilichoingia au kung’ang’ania masikioni kwa kuchokonoa na vidole, kutumia vidude vya kushikia ‘’tweezers’’ au vijiti vya kusafishia masikio ‘’cotton swab’’, hata kama unakiona. Kuna uwezekano mkubwa utakisukuma kwenda ndani zaidi. Unaweza kuharibu au kuumiza sikio au/na ngoma ya sikio.
Omba msaada wa daktari kama
Tafuta msaada wa daktari haraka kama, baada ya kuondoa au kutoa kitu masikoni
- Bado unahisi kuwa kuna kitu masikioni au unajihisi kama kuna kitu kimebakia masikioni
- Kama uwezo wa kusikia umepungua
- Kama una maumivu kwenye sikio au kama una majimaji au uchafu unatoka kwenye masikio
Leave feedback about this