Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Kukoroma (snoring) ni hali ya kupumua kwa nguvu au kutoa sauti kubwa yenye mkwaruzo usingizini.
Kukoroma husababishwa na nini ?
Unapokuwa umelala, misuli ya koo hulegea, ulimi wako hurudi nyuma na koo lako hupungua upana na kulegea. Unapovuta pumzi ndani, kuta za koo hutetema na kusababisha sauti ya kukoroma. Kadri kipenyo cha koo kinavyopungua nd ivyo na sauti ya kukoroma inavyoongezeka. Wakati mwingine kuta za koo huanguka ndani na kuziba koo kabisa, hii husababisha mgonjwa kushindwa kupumua, hali hii hatari huitwa sleep apnoea.
Kwa watu wengi, sababu ya kukoroma haijulikani. Baadhi ya sababu ni pamoja:
- Uzee – uzee kwa kawaida husababisha misuli ya koo kulegea –hii husababisha kukoroma
- Unene – unapokuwa mnene,tishu kwenye shingo huongezeka na zinaweza kubana njia ya hewa.
- Kuziba kwa pua kunakosababishwa na mafua au mzio, hasa kama yatadumu kwa muda mrefu
- Matatizo ya anatomia kwenye pua na koo, kama vile:
- Kuvimba kwa paa la kinywa (soft palate) au kidakatonge/ kimeo
- Kuziba kwa njia ya hewa kunakosababishwa na mafindomafindo au kuvimba kwa nyama za puani kunakosababishwa na maambukizi fulani.
- Kuvimba au kujaa kwa eneo lililo chini ya ulimi
- Ulimi mkubwa kuliko kinywa
- Matumizi ya dawa za usingizi, au pombe wakati wa kulala husababisha kulegea kwa misuli ya koo na kusababisha kukoroma
- Jinsi mtu anavyolala, kama vile, kulalia mgongo- kunaweza kusababisha kukoroma kwa baadhi ya watu
Nini dalili za kukoroma?
- Watu wanaokoroma hutoa sauti yenye mitetemo, mikwaruzo na kelele wakati wa kupumua wakiwa usingizini.
- Kukoroma ni hali ya kawaida kwa watu wazima, na mara nyingi, sio ishara ya ugonjwa.
- Wakati mwingine, kukoroma kunaweza kuwa ishara ya tatizo linalotokea usingizini linaloitwa sleep apnea.
- Mtu mwenye tatizo hili, huacha kabisa kupumua kwa sekunde zaidi ya 10 akiwa usingizini.
- Baada ya kipindi cha kuacha kupumua kupita, mgonjwa hutweta na kutoa mkoromo mkubwa wa ghafla, kisha huanza kupumua tena na kuendelea kukoroma
- Hii inaweza kutokea mara nyingi wakati wa usiku.
- Kukoroma ni tatizo linalotambulika kijamii. Watu wanaolala kitanda kimoja na mtu anayekoroma hupata shida sana kupata usingizi.
 Wakati gani utafute matibabu ya haraka?
- Japo kukoroma ni jambo la kawaida sana kwenye jamii, ni watu wachache sana wenye tatizo hatari la kuacha kupumua usingizini (sleep apnoea). Ongea na daktari kama una dalili zifuatazo:
- Unasinzia sinzia sana mchana
- Kichwa kinakuuma mara kwa mara asubuhi
- Uzito wa mwili wako umeongezeka hivi karibuni
- Unaamka asubuhi ukiwa umechoka, unajihisi kuwa hujapumzika
- Unaamka usiku na kujihisi kuchanganyikiwa au kutokujitambua vizuri
- Umakini wa kufanya mambounapungua na kama kumbukumbu yako inaathirika
- Una vipindi vya kuacha kupumua ukiwa usingizini: – Mtu anayelala chumba kimoja nawe, anaweza kukuambia kama hili linatokea –si rahisi wewe mwenyewe kugundua
- Watoto wanaokoroma kwa muda mrefu wanapaswa kuchunguzwa kama wana tatizo la kuacha kupumua usingizini.
- Kwa watoto, matatizo ya kuacha kupumua usingizini huhusishwa na:
- Matatizo ya ukuaji
- Matatizo ya kukosa usikivu, uangalifu na umakini kwa watoto – Attention Deficit Hyperactive Disorder
- Kufanya vibaya kwenye masomo shuleni
- Ukojozi/kikojozi
- Shinikizo la juu la damu
- Watoto wengi wanaokoroma hawana tatizo la kuacha kupumua usingizini (apnea), kumchunguza mtoto akiwa usingizini ndiyo njia pekee ya kulitambua
Utambuzi
- Watu wanaokoroma mara nyingi hawatambui kuwa wanakoroma, hivyo huwategemea watu wa karibu yao kuwaambia kuwa wana tatizo. Baadhi ya watu wanaokoroma hugutuka kutoka usingizini wakitweta na kufakamia hewa kama mtu aliyepaliwa, lakini hii hutokea mara chache. Kama umewahi kuambiwa kuwa unakoroma na kusumbua watu, au una dalili kama zilizotajwa hapo juu mwone daktari
- Daktari atakuuliza maswali kadhaa ili kutathmini tatizo lako, kisha atafanya uchunguzi wa mwili, hasa koo, kinywa na shingo.
- Maswali yafuatayo yanaweza kuulizwa (baadhi ya maswali yatapaswa kujibiwa na mwenzi wako):
- Je, unakoroma kwa sauti kubwa?
- Je! Hutokea zaidi ukilalia upande gani?
- Je! Kuna wakati wowote unakoroma mpaka unaamka toka usingizini?
- Je! Unakoroma mara ngapi? Kila usiku?
- Je! unakoroma usiku mzima? Au ni kwa masaa kadhaa ?
- Je! Kuna kipindi unaacha/unakoma kupumua ukiwa usingizini?
- Je! Una dalili nyingine, kama kusinzia mchana, kichwa kuuma asubuhi, kukosa usingizi, au kupoteza kumbukumbu?
- Wakati mwingine unaweza kupewa rufaa kuonana na mtaalamu wa usingizi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Uchaguzi wa matibabu ya kukoroma
- Watu wanaokoroma kidogo tu au kwa mara chache, wanaoamka asubuhi wakiwa safi bila uchovu na wanaofanya kazi zao bila matatizo wakati wa mchana, wanaweza kujaribu mambo yafuatayo nyumbani kabla ya kumwona daktari.
- Epuka kunywa pombe kwa angalau masaa manne au kula vyakula vizito masaa matatu kabla ya kulala
- Epuka kutumia vitu vingine vya kulevya mf; dawa kabla ya kulala.
- Usilale chali/ usilalie mgongo. Kama unaweza, lala upande. Madaktari wengine hupendekeza ushonee kitenesi kwenye nguo mgongoni, ili ukijaribu kulala chali ujisikie vibaya, hii husaidia kukukumbusha ulale upande. Hatimaye, kulala upande huwa tabia na huhitaji kukumbushwa.
- Punguza uzito, kama uzito wako ni mkubwa.
- Kutegemea na matokeo ya uchunguzi wa daktari, daktari anaweza kupendekeza machaguo kadhaa ya matibabu, machaguo hayo ni pamoja na:
-
- Kurekebisha mfumo wa maisha (kwa mf. Kuepuka mambo yanayoongeza hatari yaliyotajwa hapo juu, kulala upande badala ya chali kama itawezekana, kutibu mzio,n.k.)
- Kufanyiwa upasuaji ( hasa sehemu ya nyuma ya koo, paa/sehemu ya juu ya kinywa au pua kama itahitajika)
- Vifaa (vifaa hivi mara nyingi hupendekezwa na daktari wa meno, mf.vifaa vya kuzuia ulimi kuanguka nyuma na kuziba njia ya hewa au vifaa vya kupanua pua)
- CPAP (Continuous positive airway pressure appliances ) –hiki ni kifaa chenye barakoa/mask anayovaa mgonjwa usoni kabla ya kulala. Kifaa hiki hupuliza hewa kwenda ndani ya koo ili kuzuia koo kuziba. Hii ndio njia inayotumika kutibu watu wenye tatizo la kuacha kupumua usingizini (sleep apnoea). Kama umetambuliwa kuwa na tatizo hili ni muhimu kutibiwa, La sivyo, mfumo wako wa maisha na kazi zako wakati wa mchana zinaweza kuvurugika kabisa.
- Daktari wako ataongea nawe kwa kirefu kuhusu njia zote zilizoorodheswa hapo juu na kupendekeza njia bora zaidi inayokufaa kulingana na hali yako
Leave feedback about this