KUPANDIKIZA MOYO :Sababu, Matibabu, Kuzuia

Maelezo ya jumla

Kupandikiza moyo (heart transplant) ni upasuaji unaofanyika ili kuondoa moyo ulioharibika au mgonjwa na badala yake kupandikiza moyo wenye afya wa mtoaji (mfadhili).

 • Kupata moyo kwa ajili ya kupandikiza inaweza kuwa ngumu. Moyo ni lazima utolewe kwa mfadhili (donor) ambaye ubongo-wake umekoma kufanya kazi, lakini moyo huo unatakiwa kuwa na uwezo wa kuendeleza maisha ya mpokeaji. Moyo wa mfadhili lazima ufanane kwa kadri iwezekanavyo na aina ya tishu za mpokeaji ili kupunguza uwezekano wa mwili kuukataa.
 • Utawekwa kwenye usingizi mzito baada ya kuchomwa sindano ya nusu kaputi, na kisha Daktari atafanya upasuaji katika sehemu ya mfupa wa kidari.
 • Damu yako itapitishwa kwenye mashine inayoitwa ”heart-lung bypass machine” wakati daktari akishughulika na moyo wako, mashine hii itafanya kazi ya kusukuma damu na okisijeni kuipeleka katika sehemu zote za mwili badala ya moyo wakati wa upasuaji. Katika kipindi chote cha upasuaji, moyo utasimamishwa kudunda ili kumpa nafasi daktari kufanya kazi yake.
 • Moyo ulioharibika/mgonjwa utaondolewa na moyo wa mfadhili utawekwa na kushonewa mahala pake. Baada ya hilo, mashine ya kusukuma damu (heart-lung bypass machine) itazimwa na kuruhusu damu kuanza kupita tena katika moyo huu mpya uliopandikizwa.
 • Tyubu/bomba nyembamba itaingizwa kwenye kifua, ili kuruhusu damu na majimaji yaliyobakia kwenye kifua baada ya upasuaji kutoka nje ,tyubu hii hukaa hapo kwa siku kadhaa na kisha kutolewa, tyubu hii itasaidia kuruhusu mapafu kupanuka kikamilifu baada ya upasuaji.

Kwa nini Utaratibu wa kupandikiza moyo unafanyika?

 • Upandikizaji wa moyo unaweza kufanyika ili kutibu:
  • Chembe ya moyo au angina kali (ugonjwa wa moyo unaosababisha maumivu kifuani) ambayo haiwezi tena kutibiwa na dawa au upasuaji wa aina mwingine.
  • Moyo kushindwa kufanya kazi kama madawa, matibabu mengine na upasuaji havisaidii tena
  • Matatizo makubwa ya muundo wa moyo ya kuzaliwa nayo ambayo hayawezi kutibiwa kwa upasuaji wa aina nyingine.
  • Mapigo ya moyo yasiyo sawa yanayoweza kutishia maisha na kama hakuna njia nyingine za matibabu zinazoweza kusaidia.
 • Upandikizaji wa moyo HAUPASWI kufanyika kwa wagonjwa ambao:
  • Wana utapiamlo
  • Wana umri mkubwa, umri zaidi ya miaka 55 – 60
  • Wamepata kiharusi au wana ugonjwa wa akili (dementia)
  • Wamewahi kuwa na kansa
  • Wameambukizwa VVU
  • Wana magonjwa kama vile homa ya ini (hepatitis) ambayo iko hai.
  • Wana kisukari kinachotegemea insulini kama tiba na viungo vingine ambavyo havianyi kazi kwa usahihi.
  • Wana ugonjwa wa figo, mapafu, neva, au ugonjwa wa ini.
  • Hawana msaada wa kifamilia na wasiofuata vyema mpango wa  matibabu
  • Wana magonjwa mengine yanayoathiri mishipa ya damu ya shingo na miguu.
  • Wana shinikizo la juu la damu kwenye mapafu, hii husababishwa na kukakamaa kwa mishipa ya damu ya kwenye mapafu.
  • Wanavuta sigara au walevi wa pombe au madawa ya kulevya au aina yoyote ya mtindo wa maisha utakaopelekea kuharibika kwa moyo mpya.
 • Daktari anaweza kupendekeza mgonjwa asipandikiziwe moyo, ikiwa mgonjwa huyo hataweza kumudu ziara nyingi za kufika hospitalini na ofisini kwa daktari ili kufuatiliwa maendeleo ya afya, kama hataweza kumudu vipimo, na dawa zinazohitajika kuweka/kuutunza moyo mpya usiharibike.

Kupandikiza Moyo kuna hatari gani?

Hatari itokanayo na dawa za nusu kaputi ni pamoja na:

Hatari itokanayo na upasuaji ni pamoja na:

Hatari zitokanazo na kupandikiza moyo ni pamoja na:

 • Madonge ya damu iliyoganda yanaweza kukwama kwenye mishipa ya mguu na kusababisha maumivu makali – deep venous thrombosis
 • Kuharibika kwa figo, ini, au viungo vingine, kunakosababishwa na dawa za kuutunza moyo (anti-rejection medications- dawa hizi hupunguza uwezekano wa mwili kuukataa moyo mgeni)
 • Madawa yanayozuia kuharibika/kukataliwa kwa moyo yanayotumiwa na mpokeaji,yanaweza kusababisha kutokea kwa saratani.
 • Shambulizi la moyo au kiharusi
 • Tatizo la kuwa na mapigo ya moyo yasiyo sawa.
 • Viwango vya juu vya lehemu, ugonjwa wa kisukari, na kuponda mifupa kunakotokana na matumizi ya dawa za kuutunza moyo usiharibike.
 • kuongezeka kwa hatari ya kupata maambukizi mbalimbali kunakotokana na dawa za kuutunza moyo (dawa hizi hupunguza kinga ya mwili, na kupunguza uwezekano wa mwili kuukataa moyo mgeni).
 • Kukataliwa kwa moyo (baada ya kupandikiza moyo, kuna hatari kuwa mwili utaukataa moyo huu mgeni,mgonjwa anapaswa kutumia dawa za kuutunza moyo ili kupunguza uwezekano wa kukataliwa).
 • Maambukizi kwenye kidonda/jeraha

Kabla ya upasuaji wa kupandikiza moyo

 • Daktari atakuelekeza kwenye kituo cha kupandikiza, utafanyiwa uchunguzi na timu itakayofanya upasuaji. Watahitaji kuhakikisha na kujiridhisha kwamba wewe ni mteuliwa unaefaa kupandikiziwa moyo. Utakwenda mara kadhaa hospitalini kwa kipindi cha wiki kadhaa au hata miezi. Utahitaji kutolewa damu kwa ajili ya vipimo na utapigwa picha za eksirei mara kadhaa.

Yafuatayo yanaweza pia kufanyika:

 • Vipimo vya damu au ngozi kuangalia kama kuna maambukizi
 • Vipimo vya kuangalia figo na ini.
 • Vipimo vya moyo wako, kama EKG, echocardiogram, na cardiac catheterization.
 • Vipimo vya kuangalia kama una kansa.
 • Vipimo vya tishu na damu, ili kuhakikisha kuwa mwili wako hautakataa/kuuharibu moyo utakaopandikizwa kwako toka kwa mfadhili.
 • Utahitaji kuangalia kituo kimoja au zaidi cha kupandikiza ili kuona na kuchagua ni kipi kinakufaa:
  • Waulize wanafanya upasuaji kwa watu wangapi kwa mwaka kwa ajili ya kupandikiza moyo, waulize kati ya hao wanaofanyiwa upasuaji ni wangapi wanaishi. linganisha namba hizi na idadi kutoka vituo vingine, na kisha chagua.
  • Uliza kuhusu gharama za dawa utakazohitaji kutumia baada ya upasuaji.
 • Ikiwa timu ya kupandikiza inaamini wewe ni mteuliwa unaefaa, utawekwa kwenye orodha ya taifa ya kusubiri moyo (kwa nchi nyingi za Afrika mfumo huu haujawekwa vyema):
  • Mahali pako kwenye orodha hii hutegemea mambo kadhaa. Sababu muhimu zaidi ni pamoja na aina na ukali wa ugonjwa wako wa moyo, na uwezekano wa upandikizaji wa moyo kufanikiwa.
  • Kiasi cha muda unachotumia katika orodha ya kusubiri, kwa kawaida sio sababu ya kupata haraka moyo, isipokuwa kwa watoto.
  • Wengi, lakini sio wote, wa wagonjwa ambao wanasubiri kupandikiziwa moyo ni wagonjwa sana na wanahitaji kuwa hospitalini. Wengi  wao watahitaji aina fulani ya kifaa ili kusaidia moyo wao kusukuma damu ya kuutosha mwili.

Je, nitazamie nini baada ya kupandikizwa Moyo?

 • Unapaswa kutarajia kukaa hospitalini kwa siku 7 hadi 21 baada ya kupandikiza moyo. Masaa 24 hadi 48 ya kwanza utakuwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi. Katika siku chache za kwanza baada ya kupandikiza, utahitaji kuangaliwa kwa karibu ili kuhakikisha kwamba hupati maambukizi yoyote na kama moyo wako mpya unafanya kazi vyema.
 • Kipindi cha kujiuguza ni karibu miezi 6. Mara nyingi, timu yako ya kupandikiza itakuomba kuishi karibu na hospitali kwa miezi mitatu ya kwanza. Utahitajika kufanyiwa uchunguzi mara kwa mara na vipimo vya damu, x-ray, na echocardiograms kwa miaka mingi.
 • Kupambana na mwili kuukataa moyo wako mpya ni mchakato utakaoendelea milele. Mfumo wa kinga ya mwili unauona moyo huu mgeni uliopandwa kama maambukizi na kupigana nao. Kwa sababu hii, wagonjwa wa kupandikiza Moyo wanapaswa kutumia madawa ili kupunguza kinga ya mwili, hili hupunguza uwezekano wa kinga ya mwili kuuharibu moyo. Kwa hiyo,kutumia dawa na kufuata maelekezo ya daktari kwa makini ni muhimu sana kuzuia kukataliwa kwa moyo.
 • Biopsies (sampuli ndogo ya nyama kwa ajili ya vipimo), huchukuliwa kwenye misuli ya moyo angalau kila mwezi kwa kipindi cha miezi 6 hadi 12 ya mwanzo baada ya kupandikiza, na kisha mara chache zaidi baada ya hapo. Hii humsaidia daktari wako kutambua kama mwili wako unaukataa moyo wako mpya, hata kabla ya kuwepo dalili.
 • Ni muhimu utumie madawa yanayozuia kukataliwa kwa moyo uliopandikizwa kwa maisha yako yote. Utalazimika kuelewa jinsi ya kutumia dawa hizi, na kujua madhara yake.
 • Unaweza kurudi kwenye shughuli zako za kawaida mara tu unapohisi vizuri, na baada ya kuzungumza na daktari wako. lakini, jaribu kuepuka shughuli nzito.
 • Ili kuhakikisha kwamba hupati ugonjwa wa mishipa ya moyo, utafanyiwa cardiac catheterization kila mwaka.
 • Kupanda moyo hurefusha maisha ya wagonjwa ambao vinginevyo wangekufa. Karibia 80% ya wagonjwa waliopandikiza moyo huwa hai miaka 2 baada ya operesheni. Baada ya miaka 5, 70% ya watu watakuwa bado hai baada ya kupandikiza moyo.
 • Tatizo kuu, kama ilivyo kwa kesi nyingine za kupandikiza, ni kukataliwa kwa moyo. Ikiwa kukataliwa kunaweza kudhibitiwa vyema, muda wa kuishi unaongezeka hadi zaidi ya miaka 10.

Vyanzo

https://medlineplus.gov/ency/article/003003.htm

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi