Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Kupata shida kukojoa kwa wanaume wengi huaanza uzeeni na husababiswa na kuongezeka ukubwa wa tezi dume. Tezi dume ni tezi inayopatikana chini kidogo ya kibofu. Mara nyingi tatizo hili huwa sio kwa sababu ya saratani, lakini kwa baadhi ya nyakati linaweza kuambatana na saratani. Kadri tezi dume inapoendelea kukua inabana kibofu na kusababisha matatizo kama vile kushindwa kuzuia mkojo, mgonjwa hawezi kusubiri kabla ya kwenda kukojoa, akichelewa anajikojolea. Anapata hamu ya kukojoa mara kwa mara (hii ni pamoja na usiku); Mkojo unakuwa hauna nguvu unapotoka, unadondoka miguuni na unatoka kwa matone; na unakuwa na hisia kuwa haujakojoa mkojo ukaisha kabisa
Kupata shida kukojoa – mwone daktari haraka kama
Tafuta usaidizi wa kitabibu haraka sana kama:
- Ukianza kuhisi tumbo linauma na kuvimba na unashindwa kukojoa/ mkojo hautoki
Panga kumwona daktari mapema iwezekanavyo kama:
- Una matatizo kupata shida kukojoa, hasa kama kuna damu kwenye mkojo au unahisi maumivu kama ya kuungua wakati wa kukojoa
- Unatumia dawa uliyopewa duka la dawa na unadhani kuwa inasababisha shida kuwa kubwa zaidi, madawa kama ya mafua ‘’decongestants’’ au madawa ya kudhibiti ugonjwa wa sonona ‘’antidepressant’’ yanaweza kusababisha ukapata shida zaidi.
Kupata shida kukojoa – Unachoweza kufanya mwenyewe
Unaweza kufanya mambo yafuatayo ukiwa nyumbani ili kutegemeza matibabu aliyokupatia daktari ili kusaidia kupunguza dalili
- Kunywa maji angalau glass 6-8 kwa siku ili mkojo usiwe mzito sana ‘’concentrated’’ ukaleta karaha wakati wa kukojoa. Epuka kunywa maji mengi sana kwa wakati mmoja, kwa sababu ukifanya hivi itasababisha upate hamu ya kukojoa wakati huo huo.
- Kojoa pale tu utakapo hisi kibofu kimejaa mkojo. Kojoa taratibu bila haraka ili mkojo utoke wote kwenye kibofu. Wakati mwingine kama una choo cha kukaa inasaidia.
- Kama unaamka mara nyingi sana usiku, kunywa vinywaji kidogo wakati wa jioni na epuka kunywa vinywaji masaa machache kabla ya kulala. Kojoa kwanza kabla ya kwenda kulala.
- Punguza matumizi ya kahawa, chai, cola na pombe. Vinywaji hivi vinasababisha kibofu kujaa haraka na kusababisha uhisi hamu ya kukojoa kwa ghafla
- Epuka vinywaji vya viwandani vyenye kaboni kama vile soda, matunda ya jamii ya Mdimu na juisi zake. Epuka pia vyakula vyenye pilipili nyingi au viungo vingi vinaweza kuwasha kibofu.
Kuzuia
Unaweza kufanya mabadiliko yafuatayo kwenye mfumo wa maisha ili kupunguza matatizo wakati wa kukojoa kwa wanaume. Mambo haya yakifanyika yanaweza kuboresha na kupunguza dalili kadri muda unavyokwenda
- Punguza uzito, uzito mkubwa unaongeza shinikizo kwenye kibofu, punguza uzito kama inahitajika
- Kufanya mazoezi mara kwa mara kunaweza kusaidia kupunguza dalili zinazosababishwa na kuongezeka ukubwa wa tezi dume. Kama ukikaa bila mazoezi dalili zinaweza kuongezeka zaidi
Mwone daktari kama
Ni vizuri kuongea na daktari mara tu unapoanza kuona dalili zinazotokana na kuongezeka ukubwa wa tezi dume
Leave feedback about this