Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Kuumia maungio ‘’sprain/strain’’ ni jambo la kawaida kwenye michezo. Wakati mwingine kano ‘’ligaments’’ za kwenye maungio kama vile kifundo cha mguu huumia kwa sababu ya kuvutwa sana. Hii inatokea kama mifupa itavutwa ghafla kwa nguvu na kusababisha kuachia au kuchanika kwa tishu zinazozunguka maungio. Kwa baadhi ya matukio, maungio yakivutika sana yanaweza kusababisha misuli na kano kuchanika au kukatika. Dalili za kuumia kwenye maungio ni pamoja na maumivu, kuvimba na kuvia kwa damu eneo la maungio lililoathirika. Inaweza kuwa ngumu kuutumia mguu au mkono ulioumia au uliovutwa sana. Inaweza kuchukua siku kadhaa tu kuanza kujisikia vizuri, lakini inaweza kuchukua wiki kadhaa kupona kabisa.
Tafuta msaada wa daktari -Kuumia maungio
Panga kumwona daktari kama:
- Una maumivu makali, au kama umesikia sauti ‘’pop’’ wakati unaumia – yawezekana umeteguka/ kuvujika
- Hauwezi kusimama au kuuwekea uzito mkono au mguu ulioumia au kama eneo lililoumia linaonekana limevunjika
- Unadhani au una wasiwasi kuwa jeraha ulilopata ni kubwa na linahitaji matibabu
Unachoweza kufanya wewe mwenyewe baada ya kuumia maungio
- Unaweza kujitibu mwenyewe baada ya kuumia maungio kidogo kwa kutumia njia zifuatazo. Anza matibabu haraka iwezekanavyo ili kupunguza dalili na kuongeza kasi ya kupona.
- Fuata utaratibu ufuatao ili kupunguza maumivu na kupunguza uvimbe.
- Pumzisha mguu ulioumia. Epuka kufanya shughuli yoyote inayoleta maumivu au kufanya yawe makali zaidi. Kaa au lala ukiwa umeweka mguu mahala pazuri
- Weka barafu ili kupunguza uvimbe na maumivu. Unaweza kuchukua barafu iliyopondwa kwenye mfuko ukaifunika na kitambaa chepesi kisha ukaweka eneo lililoumua, au chukua taulo chovya kwenye maji ya barafu, likamue kisha funga eneo lililoumia. Fanya hivi kwa dakika 10
- Funga eneo lililoumia. Unaweza kufunga kwa kutumia ‘’elastic bandage’’ sehemu iliyoumia, hakikisha kuwa haukazi sana na kuzuia damu kupita. Bonyeza ukucha wa kidole kimoja mpaka rangi inapopotea kisha uachie, kama rangi ya damu itarudi haraka, ina maanisha damu inapita vizuri.
- Nyanyua mguu wako. Kunyanyua mguu kunapunguza mzunguko wa damu kwenda eneo liloumia na kupunguza damu kuvia mahali hapo. Unaweza kuunyanyua mguu wako kwa kuuweka juu ya kiti au mto. Jitahidi usiutumie mguu wako kwa masaa kadhaa ya mwanzo
- Tumia dawa za maumivu. Madawa ya maumivu kama ‘’acetaminophen’’ na ‘’ibuprofen’’inayoweza kupunguza uvimbe pia. Unaweza kutumia dawa zakupunguza maumivu wewe mwenyewe, lakini haupaswi kumtibu mtu mwingine.
- Iache ‘’bandage’’ iliyofunga mguu kwa masaa 48 ya mwanzo, unaweza kuifungua wakati wa usiku. Baada ya ‘’bandage’’ kuondolewa unaweza kuanza kujongesha mguu taratibu mpaka unapohisi maumivu. Kama maumivu hayajapungua baada ya siku 2 – 3, ni vizuri kuomba ushauri wa kitabibu.
Angalia pia: Maumivu ya miguu
Leave feedback about this