LISHE KWA WANAFUNZI: Mlo/chakula/lishe

Lishe kwa Wanafunzi

Umri wa kwenda shule (Miaka 6-12) ni kipindi cha mwendelezo wa ukuaji wa mwili na ukuaji wa haraka wa akili na fikra. Katika kipindi hiki watoto wa kike huanza kupata mabadiliko ya ukuaji wa kimwili. Magonjwa na matatizo ya kilishe hujitokeza sana katika kipindi hiki na kusababisha madhara ya muda mrefu. Matatizo ya kilishe yanayowapata watoto wa shule ni pamoja na:

Udumavulishe kwa wanafunzi

Watoto wengi walio dumaa katika umri huu inawezekana walipata lishe duni wakati wakiwa watoto wadogo. Ingawa kiwango cha udumavu huongezeka katika umri huu, uboreshaji wa lishe na mazingira wanayoishi inaweza kuchochea ukuaji kadiri mtoto anavyoendelea kukua.

Uzito pungufu

Uzito pungufu katika umri huu unaweza kusababishwa na kukosa virutubishi vinavyotakiwa kutokana na ulaji duni, magonjwa ya kuambukiza na kukosa matunzo stahiki.

Ukondefu

Ukondefu sio tatizo linalojitokeza kwa kiwango kikubwa kwa watoto wenye umri wa kwenda shule kama udumavu na uzito pungufu. Hata hivyo, ukosefu wa chakula au kukaa na njaa unaweza kusababisha hali hiyo. Uzoefu unaonyesha kuwa idadi kubwa ya watoto wanatoka nyumbani bila kupata kifungua kinywa na wanashinda na njaa kwa sababu ya kukosa huduma ya chakula cha mchana shuleni.

Uzito uliozidi

Maendeleo na ukuaji wa haraka wa miji pamoja na mabadiliko ya taratibu za ulaji, husabisha ongezeko la watoto wenye uzito uliozidi na kiriba tumbo hasa katika nchi za uchumi wa kati na mdogo. Hii husababisha watoto hawa kuwa na uwezekanao mkubwa wa kupata magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza katika maisha yao ya baadae pamoja na unyanyapaa katika jamii.lishe kwa wanafunzi

Watoto walio katika umri wa shule wanahitaji vyakula vya mchanganyiko na asusa zenye virutubishi. Watoto hawa huwa wanatakiwa kula milo 4 hadi 5 kwa siku pamoja na asusa kwa sababu ya ongezeko la mahitaji ya kilishe kutokana na ukuaji wa haraka. Tabia nyingi za ulaji Kama kupenda mfano vyakula vyenye mafuta na sukari kwa wingi kama chips, chokoleti, soda, juisi za bandia, biskuti au kutopenda baadhi ya vyakula mfano mboga za majani, matunda, maziwa huanzia katika umri huu na huchangia udumavu, uzito pungufu na uzito uliozidi.

Upungufu wa Vitamini na Madini kwa Wanafunzi

Wanafunzi wapo kwenye hatari ya kupata upungufu wa vitamini na madini kwa sababu ya kuongezeka kwa mahitaji ya nishati lishe na virutubishi vingine mwilini. Ifuatayo ni mitindo ya maisha ambayo inaongeza hatari za upungufu wa madini na vitamini.

  • Kula milo michache
  • Uangalizi duni wa wazazi na walezi
  • Tabia ya kupenda au kutokupenda baadhi ya chakula.
  • Maambukizi ya magonjwa kama minyoo, kichocho na kuhara.

Vyanzo

https://www.tfnc.go.tz/publications/9

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi