Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Dhana ya uzito pungufu
Mtoto aliyezaliwa na uzito chini ya kilogramu 2.5 (gramu 2500) ana uzito pungufu wa kuzaliwa. Akizaliwa na uzito chini ya kilogramu 1.5 anakuwa amezaliwa akiwa na uzito pungufu uliokithiri. Hii hutokea mara nyingi kwa wakina mama wajawazito wenye lishe duni na maradhi ya mara kwa mara. Watoto wenye uzito pungufu wa kuzaliwa wana uwezekano mkubwa wa:
- Kupata maambukizi ya vimelea vya magonjwa,
- Kudumaa
- Kuchelewa katika hatua za ukuaji
- Kufa
Ulishaji wa watoto waliozaliwa na uzito pungufu Ili kupunguza athari za kiafya kwa mtoto aliyezaliwa na uzito pungufu ni vyema kufanya yafuatayo;
- Mtoto aliyezaliwa na uzito pungufu ambaye hana dalili za maambukizi ya vimelea vya magonjwa, anapumua vizuri na ngozi yake ina rangi ya kawaida awekwe kwenye titi la mama mara tu baada ya kuzaliwa ili aweze kunyonya.
- Mtoto mwenye uzito pungufu ambaye hawezi kunyonya apewe maziwa yaliyokamuliwa ya mama yake.
- Maziwa hayo apewe kwa kikombe na SIYO CHUPA ya kulishia watoto.
- Watoto waliozaliwa na uzito pungufu ambao mama zao wamekufa au ni wagonjwa mahututi wapewe maziwa ya kopo maalumu kwa watoto wachanga. Wapewe maziwa hayo kwa kutumia kikombe na SIYO CHUPA ya kulishia watoto. Iwapo hawataongezeka uzito wapewe maziwa maalumu ya watoto waliozaliwa na uzito pungufu.
- Mtoto anatakiwa alishwe kadiri atakavyohitaji bila kupangiwa muda na iwapo ikitokea mtoto amelala zaidi ya masaa matatu anatakiwa aamshwe ili alishwe.
- Watoto waliozaliwa na uzito pungufu uliyokithiri wapewe maziwa kwa njia ya mrija.
Hata hivyo ulishaji kwa kutumia mrija ni suluhisho la muda mfupi. Badala yake jitihada zifanyike ili kuanza kumlisha mtoto kwa njia ya kawaida mapema iwezekanavyo
Leave feedback about this