Magonjwa ya ndani ya mwili

MAAMBUKIZI KWENYE NJIA YA MKOJO

maambukizi kwenye njia ya mkojo

Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko

Maelezo ya jumla

Maambukizi kwenye njia ya mkojo (Yutiyai) yanaweza kutokea mahali popote kwenye njia ya mkojo. Maambukizi haya yana majina tofauti, kulingana na sehemu ilioambukizwa. Maambukizi katika kibofu cha mkojo huitwa cystitis, maambukizi kwenye figo moja au zote mbili huitwa pyelonephritis , maambukizo kwenye mirija ya kubeba mkojo kutoka kwenye figo mpaka kwenye kibofu huitwa Ureteritis na maambukizi ya bomba ambalo hutoa mkojo kutoka kwenye kibofu mpaka nje huitwa urethritis

Je, nini dalili za maambukizi kwenye njia ya mkojo?

Dalili za maambukizo kwenye kibofu ni pamoja na:

 • Mkojo mchafu au wenye damu, mkojo unaweza kuwa na harufu mbaya au harufu kali
 • Homa (si kila mtu atakuwa na homa)
 • Maumivu wakati wa kukojoa.
 • Kukaza / kukakamaa kwa misuli ya tumbo au mgongo.
 • Kujihisi unahitaji kukojoa mara kwa mara, na hata baada tu ya kutoka kukojoa.

Ikiwa maambukizi yataenea mpaka kwenye figo, dalili zinaweza kujumuisha:

 • Kuhisi baridi na kutetemeka au kutokwa jasho usiku.
 • Uchovu na kujisikia vibaya
 • Homa juu ya nyuzi 37 C
 • Maumivu kwenye mbavu, mgongo au kwenye kinena.
 • Kuiva uso au wekundu usoni (hii huonekana zaidi kwa watu wenye ngozi nyeupe)
 • Kutokujielewa au kuchanganyikiwa (kwa wazee, mara nyingi dalili hizi ndizo ishara pekee za UTI)
 • Kichefuchefu na kutapika
 • Maumivu makali ya tumbo (wakati mwingine)

Ni nini husababisha Maambukizi kwenye njia ya mkojo?maambukizi kwenye njia ya mkojo

Maambukizi ya njia ya mkojo husababishwa na vijidudu, kwa kawaida bakteria wanaingia kupitia kwenye urethra na kupanda mpaka kwenye kibofu. Hii inaweza kusababisha maambukizi, hasa hasa kwenye kibofu, maambukizi haya yanaweza kuenea mpaka kwenye figo.

Wakati mwingi, mwili wako unaweza kuwaondoa hawa bakteria bila kutumia dawa yoyote. Hata hivyo, hali fulani fulani huongeza hatari ya kuwa na UTIs. Wanawake hupata maambukizi mara nyingi zaidi kwa sababu urethra (mrija wa kutoa mkoja nje kutoka kwenye kibofu) yao ni fupi na iko karibu sana na mkundu kuliko ya wanaume. Kwa sababu hii, wanawake wana uwezekano zaidi wa kupata maambukizo baada ya ngono.  Yafuatayo pia huongeza uwezekano wa kupata UTI:

 • Kisukari
 • Umri mkubwa
 • Matatizo yanayosababisha mtu kushindwa kukojoa mkojo wote ,kiasi fulani cha mkojo kinabaki ndani ya kibofu
 • Unapowekewa mpira wa mkojo hospitalini.
 • Kujinyea kunakosababishwa na kushindwa kuzuia kinyesi
 • Kuwa na tezi dume kubwa (prostate), urethra kuwa nyembamba, au chochote kinachozuia mtiririko wa mkojo .
 • Mawe kwenye figo
 • Kukaa/kulala bila kujongea kwa muda mrefu (kwa mfano, wakati unapokua umelazwa ukisubiri kupona baada ya kuvunjika mguu)
 • Mimba
 • Upasuaji au utaratibu mwingine unaohusisha njia ya mkojo

Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata Yutiyai?

Wanawake hupata zaidi maambukizi kwenye njia ya mkojo ukilinganisha na wanaume. Hii ni kwa sababu vijidudu vinaweza kusukumwa na kuingia kwenye urethra wakati wa kunya, ngono, au hata wakati wa kuingiza/kutumia njia ya uzazi wa mpango kama vile kitanzi.

Watu waliowekewa mpira wa mkojo (catheters) pia huwa katika hatari ya kupata maambukizi kwenye njia ya mkojo, kwa sababu vijidudu vinaweza kusafiri kupitia catheter mpaka kwenye kibofu.   Pia watu ambao kinga ya mwili imepungua wako kwenye hatari.

Utambuzi wa Maambukizi kwenye njia ya mkojo

Sampuli ya mkojo hukusanywa ili kufanya vipimo vifuatavyo:

 • Urinalysis- inafanyika kuangalia seli nyeupe za damu, seli nyekundu za damu, bakteria, na kupima kemikali fulani, kama vile nitrites katika mkojo. Mara nyingi, daktari au muuguzi anaweza kugundua kama una maambukizi kwa kutumia urinalysis.
 • Kuupanda mkojo (culture) – mkojo huchukuliwa na kupandwa katika mazingira maalumu yatakayoruhusu wadudu walio kwenye mkojo kuota ili iwe rahisi kuwatambua,hii husaidia kuhakikisha kuwa dawa unayopewa kwa ajili ya tiba ni sahihi na kama itaweza kukuponya.

Vipimo vifuatavyo vinaweza kufanywa pia ili kugundua kama kuna matatizo katika mfumo wa mkojo, matatizo haya yanaweza kusababisha maambukizi au yanaweza kufanya matibabu ya UTI kuwa magumu zaidi:

 • CT scan ya tumbo –
 • Intravenous Pyelogram (IVP)
 • Kidney scan
 • Kidney ultrasound
 • Voiding cystourethrogram

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?yutiyai

Wasiliana na mtoa huduma wa afya ikiwa una dalili za UTI. Fika kwenye kituo cha afya mara moja ikiwa umepata dalili zifuatazo :

 • Maumivu ya mgongo au sehemu ya ubavuni
 • Kutetemeka
 • Homa
 • Kutapika

Hizi zinaweza kuwa ishara za maambukizi kwenye figo.
Ikiwa tayari umeshagunduliwa kuwa una UTI na dalili zinaanza kurudi muda mfupi baada ya matibabu mwone daktari.

Uchaguzi wa matibabu

Daktari ni lazima kwanza aamue kama maambukizi uliyonayo kwenye kibofu au figo ni makali au sio makali.
Maambukizi yasiyo makali  kwenye Kibofu na figo
Kwa sababu kuna uwezakano wa maambukizi kusambaa mpaka kwenye figo, inashauriwa kumeza Antibiotics (kiua vijasumu).
Kwa maambukizo yasiyo makali ya kibofu, utameza dawa aina ya  antibiotics kwa siku 3 (wanawake) au siku 7 – 14 (wanaume). Kwa maambukizi ya kwenye kibofu yanayotokea wakati wa ujauzito, ugonjwa wa kisukari, au maambukizi yasiyo makali ya kwenye figo , mara nyingi utameza antibiotics kwa siku 7 – 14.

Ni muhimu kumaliza dawa zote hata kama unajihisi umepata nafuu. Kama hautamaliza antibiotics zote, maambukizi yanaweza kurudi tena na inaweza kuwa vigumu kuyatibu. Dawa za antibiotics zinazotumiwa kwa kawaida hujumuisha trimethoprim-sulfamethoxazole, amoxicillin, Augmentin, doxycycline na fluoroquinolones
Daktari pia anaweza kupendekeza madawa ili kupunguza maumivu wakati wa kukojoa- Phenazopyridine hydrochloride lakini bado utahitaji kuendelea kutumia antibiotics. Kila mtu mwenye maambukizi ya  kwenye kibofu au figo anapaswa kunywa maji mengi. Wanawake wengine wana maambukizi yanayojirudiarudia kila mara. Daktari anaweza kupendekeza njia mbalimbali za kutibu hili. Kumeza dozi moja ya antibiotic baada ya tendo la ngono inaweza kuzuia maambukizi ambayo hutokea baada ya ngono.
Maambukizi  kwenye figo
Ikiwa wewe ni mgonjwa sana na hauwezi kumeza dawa au kunywa maji ya kutosha, unaweza kulazwa hospitalini. Unaweza pia kulazwa hospitalini ikiwa:

 • Wewe ni mzee
 • Una mawe kwenye figo au una mabadiliko ya kimuundo (anatomia) kwenye njia ya kupitisha mkojo
 • Hivi karibuni ulifanyiwa upasuaji kwenye njia ya mkojo
 • Una saratani,ugonjwa wa kisukari, umeumia uti wa mgongo, au una matatizo mengine ya kitabibu.
 • Wewe ni mjamzito na una homa au ni mgonjwa sana.

Hospitalini, utawekewa maji na antibiotics kupitia mishipa.
Watu wengine wana maambukizi ya njia ya mkojo ambayo hujirudiarudia au ambayo hayaponi hata baada ya matibabu. Maambukizo ya namna hii ni sugu . Ikiwa una UTI sugu, unaweza kuhitaji dawa za kutumia kwa miezi mingi, au daktari anaweza kukupatia antibiotics kali zaidi. Ikiwa kuna tatizo la kimuundo (anatomia) linalosababisha maambukizi, upasuaji unaweza kupendekezwa.

Nini cha kutarajia baada ya kupata UTI ?

Maambukizi kwenye njia ya mkojo yana kera. Matibabu mara nyingi hufanikiwa na dalili za UTI ya kawaida hupotea ndani ya masaa 24 – 48 baada ya matibabu kuanza. Ikiwa una maambukizi kwenye figo, inaweza kuchukua wiki 1 au zaidi kwa dalili zako kuondoka.
Matatizo yanayoweza kutokea

 • Maambukizi yanaweza kusambaa na kuingia kwenye damu (sepsis) – hii inaweza kuhatarisha maisha, hatari ni kubwa zaidi kwa watoto wadogo, wazee sana, na wale ambao miili yao haiwezi kupambana na maambukizi (kwa mfano, wenye VVU au wagonjwa wa saratani wanaotumia mionzi/tiba kemikali)
 • Kuharibika kwa figo
 • Maambukizi kwenye figo

Kuzuia Maambukizi kwenye njia ya mkojo

 • Kunywa maji ya kutosha na kojoa mara kwa mara. Njia rahisi ya kuzuia maambukizi kwenye njia ya mkojo ni kuwaondoa bakteria kwenye kibofu au njia ya mkojo kabla hawajaweka makazi. Ukinywa maji ya kutosha itakusaidia kukojoa mara kwa mara na kuwaondoa.
 • Jitawadhe kutoka mbele kwenda nyuma. Bakteria wanakaa zaidi karibu na mk*ndu . ukijitawadha kutoka mbele kwenda nyuma, hasa baada ya kupata kinyesi, inapunguza uwezekano wa bakteria kuingia ukeni na kwenye njia ya mkojo
 • Jisafishe kabla ya ngono. Jisafishe vyema kwa maji na sabuni kabla ya kushiriki ngono. Hii husaidia kuwapunguza bakteria karibu na urethra (uwazi mkojo unapotokea).
 • Kukojoa mara baada tu ya kushiriki ngono: Japo hakuna tafiti za kutosha zinazothibitisha swala hili, kukojoa mara baada ya kushiriki ngono husaidia kupunguza uwezakano wa kupata maambukizi kwenye njia ya mkojo. Maambukizi hutokea bakteria wanapoingia kwenye njia ya mkojo kupitia kwenye urethra (uwazi mkojo unapotokea) na kusafiri mpaka kwenye kibofu. Kwa wanawake urethra ipo karibu sana na uke na kwa wanaume ndio hutoa mkojo na shahawa japo si kwa wakati mmoja. Kukojoa baada ya kushiriki ngono husaidia kuondoa bakteria walioingia ndani ya urethra wakati wa ngono. Japo hakuna uhakika ya kwamba njia hii ina ufanisi kwa kila mtu, HAIDHURU kujaribu.
 • Vaa nguo za ndani zilizotengenezwa kwa pamba. Kama unapata maambukizi mara kwa mara, wataalamu wanapendekeza ujaribu kuvaa nguo za ndani zilizotengenezwa kwa pamba na epuka kuvaa nguo zinazobana sana. Japo hakuna tafiti za kutosha, baadhi ya watu inawasaidia.

Vyanzo

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/ency/article/000521.htm

Leave feedback about this

 • Quality
 • Price
 • Service

PROS

+
Add Field

CONS

+
Add Field
Choose Image
Choose Video
X