MAGONJWA YA NGONO

MAGONJWA YA NGONO

 • December 20, 2020
 • 0 Likes
 • 24 Views
 • 0 Comments

Maelezo ya jumla

Magonjwa ya ngono (Sexual transmitted diseases) ni magonjwa yanayoambukiza kwa njia ya tendo la kujamiiana na mtu aliyeambukizwa magonjwa hayo bila kutumia kondomu. Matendo ya kujamiiana hujumuisha kuingiza uume ukeni au kwenye sehemu ya haja kubwa na kunyonyana sehemu za siri, Magonjwa haya huweza kuwapata watu wa rika na jinsi zote hususani wale walio katika umri wa kuzaa (kati ya miaka 15-49)

Vijana wenye umri kati ya miaka 10 hadi 24 wanawakilisha moja ya tatu (1/3) ya idadi ya wakazi wote wa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania. Kundi hili liko katika hatari zaidi ya maabukizi ya magonjwa ya ngono kwa kuwa wanapobalehe wanapata hisia za kupenda na pia hamu ya kufanya tendo la kujamiiana hujitokeza kwa nguvu. Hali hii huchochewa na vichocheo/homoni vilivyomo mwilini ambavyo katika kupanda na kushuka husababisha hisia za kufanya tendo la kujamiiana . Hivyo basi, ikiwa watakosa ufahamu wa kutosha kuhusu miili yao wanaweza kujiingiza katika tabia hatarishi za kujamiiana bila kondomu na mwenzi zaidi ya mmoja.

Aina za magonjwa ya ngono

Kuna aina mbalimbali za magonjwa ya ngono ambayi yamegawanywa katika makundi kutokana na dalili zake kama ifuatavyo:

 • Magonjwa yenye dalili za kutokwa na usaha au majimaji sehemu za siri (ukeni au uumeni) ambayo ni Kisonono, Trikomonas na Kandida
 • Magonjwa yenye dalili za kutokwa na vidonda ambayo ni Kaswende, Pangusa na Malengelenge sehemu za siri
 • Magonjwa yenye dalili za kutokwa na uvimbe ambayo ni Mitoki, Pangusa na Malengelenge sehemu za siri

Ieleweke kwamba, mtu anaweza kuwa na zaidi ya ugonjwa mmoja wa ngono kwa wakati mmoja. Kujitokeza kwa dalili za ugonjwa hutegemea aina ya ugonjwa, jinsi na kinga ya mwili. Hata hivyo, baadhi ya watu hawaonyeshi dalili yoyote. Asilimia 10-15 ya wanaume na asilimia 60-70 ya wanawake wenye kisonono hawaoneshi dalili yoyote. Hivyo basi, ni muhimu kijana unapoelezwa na mwezi wako uliyefanya nae tendo la kujamiiana kwamba ameambukizwa ugonjwa wa ngono usisite kwenda kituo cha huduma ya afya kwa uchunguzi na tiba hata kama huna dalili.

Dalili za Magonjwa ya ngono

Kijana uonapo dalili moja, au zaidi kati ya hizi zifuatazo nenda kwenye kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi

Kwa vijana wa kike

 • Maumivu chini ya kitovu
 • Kutokwa na usaha au majimaji yenye harufu mbaya sehemu za siri
 • Kuwashwa sehemu za siri
 • Vidonda na upele sehemu za siri, mdomoni na sehemu nyingine za mwili
 • Maumivu wakati wa kujamiiana
 • Kuvimba mtoki
 • Kuota sundosundo sehemu za siri
 • Kukojoa mara kwa mara kunakoambatana na ,muwasho au maumivu

Kwa kijana wa kiume

 • Maumivu makali sehemu za siri wakati wa kukojoa
 • Kutokwa na usaha sehemu za siri
 • Vidonda sehemu za siri
 • Vidonda sehemu za mdomoni
 • Kuvimba mtoki
 • Kupata melengelenge
 • Kuota sundosundo (warts) sehemu za siri

Tabia zinazoongeza hatari ya kuambukizwa magonjwa ya ngono

Baadhi ya tabia ambazo zinaweza kuchochea kupata maambukizi ya magonjwa ya ngono kwa urahisi zaidi ni:

 • Kujamiiana bila kondomu-vijana wengi hukosa ujasiri wa kusisitiza matumizi ya kondomu kwa kuhofia kuachwa na wenzi wao
 • Kujihusisha na ukahaba
 • Kujamiiana na wapenzi wengi
 • Kunyonyana sehemu za siri- kwa kuwa vimelea vya magonjwa ya ngono vinapatikana kwenye majimaji ya sehemu za siri ni rahisi mtu mwenye maambukizi ya magonjwa ya ngono kumwambukiza mwenzi wakati wa kunyonyana.
 • Kunyonyana ndimi (kula denda) – baadhi ya vimelea vya magonjwa ya ngono hupatikana mdomoni (Kisonono, Kaswende na virusi vya UKIMWI) hivyo huambukiza kupitia kunyonyana ndimi ikiwa mmojawapo ana maambukizi.
 • Woga wa vijana wa kike kuwashawishi vijana wa kiume kutumia kondomu wakati wa kujamiana kwa sababu ya mfumo dume.
 • Kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazosababisha kufanya ngono bila mpangilio, kwa mfano; makundi yanayokwenda ufukweni, kuangalia filamu za ngono au kushiriki kwenye ngoma za jadi zinazochezwa usiku kucha , disko na matamasha
 • Tamaa ya kupata pesa pamoja na vitu vya thamani kama simu za mikononi, magari kutoka kwa watu mbalimbali
 • Kuhusika na vitendo vya ubakaji
 • Utumiaji wa madawa ya kulevya au pombe ambayo husababisha kijana kukosa ufahamu na hivyo kufanya ngono isiyo salama.
 • Ushoga (wanaume wanaojamiana na wanaume)

Kuwa mwangalifu wakati wote ili usiweze kutumbukia kwenye tabia hizi. Ikibidi kujamiiana tumia kondomu kwa usahihi.

Athari za magonjwa ya ngono

Magonjwa ya ngono yasipotibiwa mapema na kwa usahihi huweza kuleta athari zifuatazo kwa magonjwa:

Kwa kijana wa kike

 • Kuziba kwa mirija ya uzazi ambako kunasababisha aidha mimba kutunga nje ya mfuko wa uzazi au ugumba
 • Maambukizi katika mfuko wa uzazi
 • Kupata magonjwa katika viungo muhimu mwilini
 • Magonjwa ya moyo na mishipa ya damu
 • Kansa ya kizazi
 • Mabadiliko ya hedhi
 • UKIMWI

Kwa kijana wa kiume

 • Maambukizi katika kokwa za mbegu za uzazi
 • Kuziba mirija inayopitisha mbegu za uzazi na kuleta utasa
 • Kupata matatizo ya kukojoa kwa sababu ya kuziba njia ya mkojo
 • Kupata magonjwa katika viungo muhimu mwilini kama ubongo, moyo, na figo
 • Kansa ya uume
 • Kupungua nguvu za kiume
 • UKIMWI

Athari zote hizi zinaweza kuepukika iwapo magonjwa ya ngono yatatibiwa mapema na kwa usahihi. Usiogope! Magonjwa ya ngono yanatibika

Mbinu za kuepuka magonjwa ya ngono

Ili kuepuka magonjwa ya ngono zingatia yafuatayo

 • Usifanye kitendo cha ngono kabisa
 • Jiepushe kufanya tendo la kujamiiana katika umri mdogo
 • Jiepushe na ulevi na madawa ya kulevya
 • Jiepushe na vitendo vya ubakaji
 • Jihadhari na kupiga denda na mwenzi usiyejua hali yake ya afya
 • Jiepushe na vitendo vya kunyonya uume au uke wa mwenza
 • Tumia muda wako mwingi katika masomo, kazi za mikono, michezo na Sanaa
 • Epuka vishawishi kama zawadi na lifti za magari barabarani
 • Epuka kukaa na mpenzi wako peke yenu hasa nyakati za usiku
 • Epuka makundi ya vijana walevi, wazururaji na wavuta bangi au watumiaji wa madawa ya kulevya
 • Ikiwa umeoa au kuolewa, kuwa mwaminifu kwa mwenzi wako katika tendo la kujamiiana

Kinga dhidi ya magonjwa ya ngono

 • Acha ngono kabisa katika umri mdogo
 • Tumia kondomu ya kike au ya kiume kwa usahihi kwa kila tendo la kujamiiana
 • Kuna baadhi ya magonjwa ya ngono yana chanjo za kukukinga kwa hiyo pata chanjo mf: Chanjo ya homa ya ini, malengelenge, HPV n.k.

Mambo ya kufanya ukipata maambukizi ya magonjwa ya ngono

Mambo muhimu ya kuzingatia ukipata maambukizi ya magonjwa ya ngono:

 • Wahi kwenye kituo cha huduma ya afya kilicho karibu nawe kwa uchunguzi na matibabu sahihi
 • Tumia dawa zote kwa kufuata maelekezo ya mtaalam wa afya hata dalili za ugonjwa zimepotea
 • Epuka kujinunulia dawa bila maelekezo ya mtaalam wa afya
 • Usifanye tendo la ngono mpaka utibiwe na kupona kabisa
 • Muarifu mwenzi wako mapema ili wote mkapate matibabu sahihi na ushauri nasaha

Kumbuka kuwa kuwepo kwa magonjwa ya ngono kunaongeza uwezekano wa kuambukizwa virusi vya UKIMWI

Leave Your Comment