MAGONJWA YASIYO YA KUAMBUKIZA: Nini cha kufanya

Maana ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza

Magonjwa Yasiyo ya kuambukiza ni magonjwa ambayo hayasambazwi kwa mtu mwingine kwa kuwa hakuna vimelea mwilini vinavyohusiana na magonjwa hayo. Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza ni kama ya moyo na mishipa ya damu, figo, saratani, kifua sugu, kisukari, magonjwa ya akili na mengine ya kurithi kama vile ugonjwa wa selimundu.

Mwaka 1999, Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza yalikadiriwa kuchangia karibu asilimia 60% ya vifo vyote duniani na asilimia 43% ya ukubwa wa tatizo la magonjwa duniani. Tatizo la Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza linakua kwa kasi katika nchi zinazoendelea, kama Tanzania. Inakisiwa kuwa mwaka 2020 Magonjwa haya Yasiyo ya Kuambukiza yatasababisha asilimia 73% ya vifo vyote duniani na asilimia 60% ya ukubwa wa tatizo la magonjwa duniani.

Moja ya mambo yanayochangia kuongezeka kwa magonjwa haya ni mabadiliko ya taratibu za kimaisha zinazohusisha matendo yanayoweza kusababisha ugonjwa. Kati ya taratibu hizi ni:

 • Kutofanya mazoezi – kukaa darasani, ofisini, kuangalia runinga, kutumia lifti, kupanda magari na kutoshiriki michezo na ngoma za utamaduni
 • Ulaji usiofaa
  • kula chakula kuzidi mahitaji ya mwili na hivyo kunenepa
  • kula mafuta na chumvi zaidi ya mahitaji ya mwili
  • kutokula mbogamboga na matunda kiasi cha kutosha
  • kula nafaka zilizokobolewa
 • Matumizi ya pombe, tumbaku na madawa ya kulevya
 • Msongo wa mawazo.

Kugundua na kuzuia magonjwa yasiyo ya kuambukizaMagonjwa yasiyo ya kuambukiza

Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza yanaweza yakawa bila dalili zozote kwa  miaka kadhaa ya kuwa na ugonjwa huo japokuwa  mwili utakuwa umeshaathirika sana. Kwa mfano mtu anaweza kuishi miaka mingi na shinikizo kubwa la damu bila dalili zo zote hadi pale anapopata kiharusi, moyo unaposhindwa kufanya kazi au figo zinapokuwa zimeharibika kwa sababu ya huo msukumo wa damu. Ugonjwa wa kisukari unaweza usiwe na dalili za kumfanya mtu atafute tiba hadi pale macho, figo, moyo au mishipa ya damu au fahamu inapokuwa imeharibika vibaya na kusababisha dalili.

Katika utafiti uliofanywa mwaka 2012 nchini Tanzania ulioshirikisha watu wenye umri wa miaka 25 na kuendelea, kwa kila watu 14 waliokutwa na shinikizo kubwa la damu, ni mmoja tu kati ya hao ndiye aliyekuwa amegunduliwa tayari. Kwa upande wa ugonjwa wa kisukari, ni chini ya nusu ya wote waliokutwa na ugonjwa ndio waliokuwa wamegunduliwa. Hivyo inashauriwa watu wote kupata uchunguzi wa mara kwa mara ili kugundua kuwepo kwa magonjwa haya. Tiba ya mapema inapunguza uwezekano wa kupatwa na madhara zaidi.  Kwa magonjwa mengine kama vile saratani, tiba ya mapema inaweza kundoa ugonjwa huu moja kwa moja.

Magonjwa ambayo uchunguzi wa mara kwa mara unashauriwa, dalili ambazo mtu akiwa nazo anaweza kuhisi kuwa na moja wapo wa magonjwa haya ili apate tiba mapema na . ajue nini cha kufanya juu ya magonjwa haya ni kama ifuatavyo: –

Magonjwa yanayoshauriwa kuchunguzwa mara kwa mara

 • Ugonjwa wa kisukari
  • Kila mwaka baada ya kutimiza miaka 45
  • Kwa wanawake, katika kupindi cha pili wakati wa ujauzito
 • Shinikizo la damu
  • Kila mwaka baada ya kutimiza miaka 40
  • Kila unapohudhuria kituo cha kutoa huduma za afya
  • Kwa wanawake, kila hudhurio la kliniki za ujauzito
 • Magonjwa ya macho
  • Watoto (miaka 0-15) – Kila mwaka
  • Watu wazima – Kila mwaka baada ya umri wa miaka 40 na Kila unapohitaji leseni ya udereva
 • Ugonjwa wa selimundu
  • Watoto – Wakati wa kuanza na kumaliza primary
  • Watu wazima – Mwaka wa mwisho wa sekondari
 • Saratani ya matiti
  • Kujichunguza mwenyewe matiti kila mwezi baada ya miaka 18

Dalili zinazoweza kuashiria kuwepo kwa magonjwa yasiyo ya kuambukizaMagonjwa sugu

Kwa watu wazima, mara moja kila mwezi pitia orodha hii na pata ushauri wa mtaalamu wa afya ikiwa una dalili mojawapo:

 • Kupungua uzito bila sababu
 • Kuchoka bila sababu
 • Kichwa kuuma
 • Kuona kizunguzungu
 • Kutoona vizuri, kuona giza au kushindwa kusoma
 • Makengeza kwa watoto chini ya miaka sita
 • Ganzi ya meno, meno kucheza/kung’oka, kutoka damu kwenye fizi
 • Ganzi au maumivu (kuwaka moto) kwenye mikono au miguu
 • Maumivu ya kifua hasa wakati unajishughulisha
 • Kupumua kwa shida au kukosa pumzi baada ya kujishughulisha tu kidogo
 • Kukosa pumzi usiku wakati umelala
 • Moyo kwenda haraka
 • Kubadilika tabia ya choo (kufunga choo)
 • Kukojoa mara kwa mara au mkojo kuchelewa kutoka
 • Kutokwa damu sehemu yo yote (pua, makohozi, choo kikubwa, mkojo, ukeni)
 • Kutoka damu nje ya mzunguko wa hedhi, wakati wa tendo la ndoa, au baada ya kufunga hedhi
 • Kutokwa na maji maji au ute ukeni, uwe au usiwe na harufu/rangi yo yote
 • Kutokuwa na hamu ya tendo la ndoa
 • Vidonda visivyopona
 • Kujisikia huzuni/mpweke, woga, wasi wasi
 • Hasira nyingi
 • Kushindwa kutimiza wajibu
 • Kunywa pombe kwa wingi
 • Kuvuta sigara kwa wingi
 • Kusikia au kuona vitu ambayo watu wengine hawavioni.

Kumbuka

 • Ajali nazo ni magonjwa yasiyoambukiza
 • Usiendeshe gari kama umekunywa muda si mrefu na pombe bado mwilini
 • Vaa mkanda kila unapokuwa kwenye gari
 • Vaa kofia ngumu kila unapanda pikipiki
 • Zima na usiinue simu wakatii unaendesha
 • Pima macho yako kila mwaka na kila unapohitaji kupata leseni ya udereva.

Vyanzo

Tanzania Diabetes Association

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi