MAKUNDI YA VYAKULA: Unachopaswa kufahamu

Makundi ya vyakula

Vyakula vyenye virutubishi vingi vinavyofanana huwekwa katika kundi moja. Ili kuweza kupata virutubishi vyote muhimu vinavyohitajika mwilini, inashauriwa kula vyakula kutoka katika makundi mbalimbali. Makundi ya vyakula husaidia kupanga mlo kamili kwa urahisi na kuwezesha vyakula vyote muhimu kuwepo. Ikumbukwe kwamba hakuna chakula cha aina moja ambacho kinaweza kuupatia mwili virutubishi vyote vinavyohitajika isipokuwa maziwa ya mama kwa miezi 6 ya mwanzo ya maisha ya mtoto.

Makundi ya vyakula hutumika badala ya aina au kazi za virutubishi katika kujifunza ulaji bora. Makundi ya vyakula ni pamoja na:

Vyakula vya nafaka, mizizi na ndizimakundi ya chakula

Vyakula hivi ndivyo vinavyochukua sehemu kubwa ya mlo na kwa kawaida ndivyo vyakula vikuu. Vyakula katika kundi hili ni pamoja na mahindi, mchele, mtama, ulezi, ngano, uwele, viazi vikuu, viazi vitamu, muhogo, magimbi, viazi mviringo na ndizi.

Makapi- mlo

Makapi-mlo ni aina ya karbohydreti ambayo mwili hauwezi kuiyeyusha. Makapimlo yanasaidia: ­

  • Mfumo wa chakula kufanya kazi kwa ufanisi, kulainisha choo na hivyo husaidia mtu kupata haja kubwa kwa urahisi ­
  • Kupunguza kiwango cha lehemu na aina nyingize za mafuta (tryglycerides) katika damu, hivyo kuukinga mwili dhidi ya maradhi ya moyo, shinikizo kubwa la damu, kisukari na saratani ­
  • Kupunguza hatari ya mtu kupata saratani ya utumbo mpana, ugonjwa wa moyo na matatizo mengine ya mfumo wa njia ya chakula ­
  • Kudhibiti kiwango cha sukari katika damu kwa watu wenye kisukari ­
  • Katika kupuguza uzito kwani chakula chenye makapi-mlo kwa wingi hujaza tumbo kwa urahisi, hivyo kumfanya mtu ajisikie kushiba kwa haraka.

Vyakula vyenye makapi mlo kwa wingi ni pamoja na nafaka isiyokobolewa, mbogamboga, matunda freshi na yale yaliokaushwa, jamii ya kunde na aina mbalimbali za mbegu na njugu kama karanga, ufuta, korosho na alizeti.

Vyakula vya jamii ya kundeMakundi ya chakula

Vyakula vya jamii ya kunde ni pamoja na maharagwe, njegere, kunde, karanga, soya, njugu mawe, dengu, njegere kavu, choroko na fiwi.

Vyakula vyenye asili ya wanyama:

Vyakula vyenye asili ya wanyama ni pamoja na nyama, samaki, dagaa, maziwa, mayai, jibini, maini, figo, senene, nzige, kumbikumbi na wadudu wengine wanaoliwa.

Mboga-mboga

Kundi hili linajumuisha aina zote za mboga-mboga zinazolimwa na zinazoota zenyewe. Mboga-mboga ni pamoja na mchicha, majani ya maboga, kisamvu, majani ya kunde, matembele, spinachi, mnafu, mchunga. Aina nyingine za mboga-mboga ni pamoja na karoti, pilipili hoho, biringanya, matango, maboga, nyanya chungu, bamia, bitiruti, kabichi na figiri.

Matunda

Kundi hili linajumuisha matunda ya aina zote kama papai, embe, pera, limau, pesheni, nanasi, peasi, chungwa, chenza, zambarau, parachichi, ndizi mbivu, fenesi, stafeli, mabungo, madalansi, pichesi na topetope. Aidha ikumbukwe kuwa matunda pori au yale ya asili yana ubora sawa na matunda mengine. Matunda hayo ni kama ubuyu, ukwaju, embe ng’ongo, mavilu, mikoche na zaituni.

Mafuta

Mafuta ni muhimu lakini yanahitajika kwa kiasi kidogo mwilini. Mafuta yanaweza kupatikana kutoka kwenye mimea kama mbegu za alizeti, ufuta, pamba, korosho, karanga na mawese. Mafuta pia yanaweza kupatikana kutoka kwa wanyama, kwa mfano: siagi, samli, nyama iliyonona na baadhi ya samaki.

Sukarimakundi ya chakula

Sukari hupatikana kwenye sukari ya mezani, miwa na asali na inashauriwa itumike kwa kiasi kidogo.

Maji

Maji kwa kawaida hayahesabiwi kama kundi la chakula, lakini yana umuhimu mkubwa katika afya na lishe ya binadamu. Inapaswa kunywa maji safi na salama ya kutosha, angalau lita moja na nusu (au glasi nane) kwa siku. Inashauriwa kunywa maji zaidi wakati wa joto kali ili kuzuia upungufu wa maji mwilini. Vile vile unaweza kuongeza maji mwilini kwa kunywa vinywaji kama

Vyanzo

https://www.tfnc.go.tz/publications/9

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi