MALARIA

MALARIA

 • November 18, 2020
 • 0 pendwa
 • 11 Wameona
 • 0 Maoni

Maelezo ya jumla

Malaria ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea wanaoambukizwa na mbu aina ya anofelesi. Dalili za awali za ugonjwa huu ni pamoja na: uchovu, homa, kuhisi baridi, kutokwa jasho, maumivu ya kichwa, kichefuchefu na kutapika. Dalili zinazofuta zinaweza kuwa mbaya na hata kutishia maisha ya mgonjwa. Mgonjwa huanza kupata shida kupumua, kuchanganyikiwa, na hatimaye koma. Kuna aina tano za vimelea wanaoweza kusababisha malaria, Plasmodium falciparum, P. vivax, P. oval, P. malariae, na P. knowlesi. Mtu yeyote anaweza kuambukizwa malaria. Hata hivyo, watu fulani wako kwenye hatari zaidi ya kuambukizwa, hii ni pamoja na wanaoishi katika nchi zenye malaria kwa wingi mf: nchi zilizo katika ukanda wa kitropiki kama Tanzania, Kenya na Uganda. Ugonjwa huu unaweza kutambuliwa kwa kuangalia dalili na vipimo vya maabara, kama vile darubini au vipimo vya kutambua antijeni. Malaria inaweza kutibiwa kwa muunganiko wa madawa kadhaa (kila nchi inao muunganiko maalumu unaokubalika na kuaminika). Watu wanaosafiri kwenda katika nchi zenye kiwango kikubwa cha malaria wanapaswa kutumia dawa za kujikinga na kuchukua hatua kujikinga dhidi ya mbu. Mfano; kwa kutumia dawa za kufukuza mbu (mosquito repellents) na kuvaa nguo za kufunika mikono na miguu. Kesi nyingi za malaria hupona vyema bila matatizo baada ya kutibiwa vyema.

Je, nini dalili za Malaria?

Dalili za kawaida za malaria ni pamoja na:

 • Uchovu wa mwili
 • Homa
 • Baridi
 • Kutokwa jasho
 • Maumivu ya kichwa
 • Kichefuchefu na kutapika
 • Maumivu ya mwili
 • Manjano

Baada ya kuumwa na mbu aina ya anofelesi mwenye vimelea vya malaria, muda kidogo hupita kabla ya dalili za kwanza kuonekana (incubation period). Kwa kesi nyingi dalili za kwanza huonekana siku 7 hadi 30 baada ya kuumwa na mbu.

Ni nini kinachosababisha Malaria?

Malaria husababishwa na vimelea wanaoenezwa na aina fulani ya mbu wanaokunywa damu ya mwanadamu. Ugonjwa huu huenezwa toka kwa mtu mmoja mpaka mwingine kwa kuumwa na mbu aina ya anofelesi.

Aina nne za vimelea wa malaria hujulikana kwa kusababisha maambukizi kwa wanadamu:

 • Plasmodium falciparum
 • vivax
 • ovale
 • malariae
 • knowlesi – hii ni aina ya vimelea wa malaria iliyogunduliwa hivi karibuni, inayosababisha maambukizi kwa nyani (macaque) na wandamu huko Asia kusini. Aina hii ya malaria inaweza kuhama toka kwa wanyama na kuwaambukiza wanadamu (zoonotic malaria).

Malaria inayotokana na Falciparum, huathiri kiasi kikubwa cha chembe nyekundu za damu kuliko aina nyingine, sababu hii huifanya aina hii ya malaria kuwa na matokeo mabaya na inaweza kusababisha kifo masaa machache tu baada ya kuanza kwa dalili za awali.

Malaria inaweza pia kuambukizwa kwa njia zifuatazo

 • Mtoto aliye-tumboni kwa mama anaweza kuambukizwa malaria
 • Utaambukizwa malaria ukiongezewa damu yenye malaria.

Nani aliye kwenye hatari zaidi?

 • Mtu yeyote anaweza kuambukizwa malaria.
 • Matukio mengi ya malaria hutokea kwa watu wanaoishi katika nchi zenye kiwango kikubwa cha uambukizo wa malaria
 • Watu wasioishi kwenye nchi zenye uambukizo mkubwa wa malaria wanaweza kuambukizwa wakisafiri kwenda kwenye nchi zenye uambukizo mkubwa au kwa kuongezewa damu.
 • Mtoto anaweza kuambukizwa malaria toka kwa mama kabla au wakati wa kujifungua.

Ni nani aliye katika hatari zaidi ya Kufa kwa Malaria?

 • Watu wanaoumwa na mbu wengi ambao wameambukizwa vimelea vya falciparum (vimelea hawa husababisha malaria kali na hatari) wako katika hatari kubwa ya kufa kwa malaria.
 • Watu wanaoishi katika nchi Afrika zilizo kusini mwa jangwa la sahara – vimelea aina ya falciparum ni kawaida
 • Watu wasio na kingamwili ya kutosha kupambana na malaria, kama vile watoto wadogo, wanawake wajawazito, na wasafiri wanaotoka katika maeneo yasio na uambukizo mkubwa wa malaria.
 • Watu masikini, wanaoishi vijijini na wasio na uwezo wa kuzifikia huduma za afya

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Unapaswa kutafuta huduma ya matibabu haraka kama:

 • Kama unaanza kuona dalili za malaria na unaishi katika maeneo yenye uambukizo mkubwa malaria mf; Tanzania, Kenya, Uganda.
 • Unaona dalili za malaria ukiwa safarini katika nchi yenye uambukizo mkubwa wa malaria.
 • Unaona dalili za malaria baada ya kutembelea eneo lenye uambukizo mkubwa malaria (hata baada ya mwaka mzima baada ya kurejea nyumbani)

Utambuzi

Uchunguzi hutegemea dalili za mgonjwa na matokeo ya uchunguzi wa mwili. Dalili za awali za malaria hufanana na magonjwa mengine (mfano: “mafua” na maambukizi mengine ya virusi).

Kwa malaria kali, Ishara zake huwa kali na kusababisha utambuzi kuwa rahisi. Ishara hizi ni pamoja na:

 • Kuchanganyikiwa
 • Koma
 • Upungufu mkubwa wa damu (Anemia)
 • Matatizo ya kupumua

Ishara hizi zinapaswa kuthibitishwa kwa kufanya kipimo cha malaria. Vipimo hivi vya malaria hujumuisha:

 • Uchunguzi kwa kutumia darubini
 • Kugundua antijeni
 • Serolojia

Mbali na vipimo vya malaria vilivyotajwa hapo juu, daktari anaweza kuagiza vipimo vifuatavyo ili kuangalia hali ya mwili wako.

Kama umepimwa na kuundulika kuwa una malaria, daktari anaweza kuagiza vipimo vya ziada ili kutambua kama malaria yako ni kali au la?. Vipimo hivi huchunguza kama kuna:

 • Upungufu mkubwa wa damu –Anemia
 • Kushuka kwa kiwango cha sukari kwenye damu –Hypoglycemia
 • Kushindwa kwa fio kufanya kazi-Renal failure
 • Kiwango kikubwa cha bilirubin kwenye damu- hii huashiria kuwa malaria inavunja na kuziharibu seli nyekundu za damu kwa wingi na kwa kasi sana –Hyperbilirubinemia

Uchaguzi wa matibabu

Malaria ni ugonjwa mkali na unaweza kuua (hasa kama umesababishwa na Plasmodium falciparum). Matibabu yake yanapaswa kuanzishwa haraka iwezekanavyo.

Matibabu ya malaria hutegemea mambo mengi ikiwa ni pamoja na:

 • Ukali wa ugonjwa
 • Aina ya vimelea vya malaria vilivyosababisha maambukizi

Wagonjwa ambao wana malaria kali ya P. falciparum, au ambao hawawezi kumeza dawa, wanapaswa kutibiwa kwa sindano.

Kuna dawa nyingi zinazotumika kutibu malaria katika pembe zote za dunia

 • Chloroquine
 • Atovaquone-proguanil
 • Artemether-lumefantrine– ALU
 • Mefloquine
 • Quinine
 • Quinidine
 • Doxycycline (hutumiwa pamoja na quinine)
 • Clindamycin (hutumiwa pamoja na quinine)

Uchaguzi dawa ya kutumia hutegemea eneo ulipo, na daktari wako atakupatia dawa itakayofaa kwa eneo lako.

Pamoja na kutumia dawa mgonjwa atapaswa kupewa huduma nyingine za kitabibu ili kupata nafuu. Atahitaji kuongezewa damu kama imepungua, ataongezewa maji mwilini kama amepungukiwa maji baada ya kutapika sana, anaweza pia kuhutaji kuwekwa kwenye mashine ya kumsaidia kupumua kama anapata shida kupumua n.k.

Kuzuia

 • Watu wengi wanaoishi katika maeneo yenye uambukizo mkubwa wa malaria kama vile Tanzania hutengeneza kingamwili (usugu) dhidhi ya ugonjwa wa malaria- hawaugui mara kwa mara.
 • Wageni, wasio na kinga yoyote, wanapaswa kutumia dawa za kujikinga wakitembelea eneo lenye uambukizo mkubwa wa malaria. Ni muhimu kumwona mtoa huduma ya afya mapema kabla ya kusafiri, matibabu yanaweza kuanza wiki 2 kabla ya safari na kuendelea mpaka mwezi mmoja baada ya kurejea kutoka katika eneo hilo.
 • Dawa zinazotumiwa na wasafiri wanaoelekea Marekani ya kusini, Afrika, Asia, India, na Pasifiki ya Kusini ili kujikinga ni pamoja na:
 • Mefloquine
 • Doxycycline
 • Chloroquine
 • Hydroxychloroquine
 • Malarone- Atovaquone / Proguanil
 • Wanawake wajawazito wanapaswa kutumia dawa za kujikinga dhidi ya malaria- hii hupunguza uwezekano wa mtoto kuambukizwa malaria akiwa tumboni
 • Watu wanaotumia dawa za kutibu malaria wanaweza kuambukizwa malaria tena. Jikinge dhidi ya mbu kwa kuvaa nguo zinazofunika miguu na mikono, tumia dawa za kufukuza mbu (repellant), lala chini ya chandarua, weka skrini kwenye madirisha yako na tumia dawa ya mbu.
 • Kwa miaka mingi Chloroquine imekuwa ikitumiwa kama dawa ya kujikinga dhidi ya malaria. Lakini kwa sababu ya kuongezeka usugu dhidi ya dawa hii , kwa sasa inashauriwa kutumika kukinga malaria katika maeneo yenye malaria inayosababishwa na Plasmodium vivax, P. oval, na malariae pekee.
 • Kwa wasafiri (wageni) wanaosafiri kwenda maeneo yenye malaria inayosababishwa na falciparum, wanaweza kutumia moja ya zifuatazo ili kujikinga:
 • Mefloquine
 • Atovaquone / Proguanil -malarone
 • Doxycycline

Nini cha kutarajia?

Mara nyingi, Ugonjwa malaria hupona kama matibabu sahihi yatatolewa haraka na kwa wakati.

Matarajio huwa si mazuri sana kwa malaria kali inayosababishwa na falciparum.

Matatizo yanayoweza kutokea

Matatizo mbalimbali yanaweza kusababishwa na malaria kali. Malaria kali husababisha baadhi ya viungo mwilini kushindwa kufanya kazi, husababisha uharibifu wa damu ya mgonjwa na kuvuruga  mfumo wa kimetaboliki. Ishara za malaria kali ni pamoja na;

 • Malaria kupanda kichwani –cerebral malaria
 • uvimbe wa tando za uti wa mgongo na ubongo- meningitis
 • Upungufu mkubwa wa damu –Anemia
 • Kushindwa kupumua kunakotokana na mapafu kujaa maji
 • Kuvuja damu ovyo kunakotokana na damu kushindwa kuganda
 • Kushindwa kwa moyo kufanya kazi – heart failure
 • Kushindwa kwa figo kufanya kazi – renal failure
 • Kushindwa kwa ini kufanya – Liver failure
 • Kupasuka kwa wengu kunakosabaisha damu kuvujia ndani ya mwili- Spleen rupture

 

Vyanzo

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/ency/article/000621.htm

Leave Your Comment