Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maumivu wakati wa kukojoa ni nini?
Maumivu wakati wa kukojoa ni hali ya kuhisi maumivu wakati wa kukojoa inayotokana na sababu mbalimbali
Maumivu wakati wa kukojoa yanasababishwa na?
Sababu kubwa zaidi ya maumivu wakati wa kukojoa ni maambukizi, kama vile maambukizi kwenye kibofu au kwenye njia ya mkojo (yutiyai). Maambukizi ukeni ndio sababu kubwa zaidi kwa wanawake. Kwa wanaume, maambukizi kwenye tezi dume ndio sababu kubwa. Kwa wanawake na wanaume, maambukizi ya magonjwa ya ngono yanaweza kusababisha tatizo hili. Kwa baadhi ya nyakati, matumizi ya sabuni, dawa za povu za kupanga uzazi (spermacides) au lotion kwenye via vya uzazi zinaweza kusababisha harara na maumivu. Baadhi ya magonjwa ya ngozi yanaweza kusababisha maumivu ya kukojoa. Zipo pia sababu nyingine za nadra sana zinazoweza kusababisha tatizo hili.
Dalili za maambukizi kwenye njia ya mkojo?
Kama una maambukizi kwenye njia ya mkojo, kuta za ndani za kibofu huwa nyekundu na zenye harara (zilizovimba). Hali hii inaweza kusababisha maumivu kwenye tumbo na sehemu ya nyonga. Unaweza kujihisi kukojoa mara kwa mara. Unaweza kujaribu kukojoa lakini mkojo ukatoka matone machache tu au ukahisi kama unaungua mkojo unapokua unatoka. Unaweza kujikojolea wakati mwingine. Mkojo unaweza kuwa na harufu mbaya na unakua kama una ukungu.
Kwa mara chache maambukizi ya njia ya mkojo yanaweza kusambaa kwenda kwenye figo. Maambukizi kwenye figo yanaweza kusababisha homa, kutetemeka, kutokwa jasho na maumivu ya mgongo. Maambukizi ya aina hii yanapaswa kutibiwa haraka inavyowezekana kabala hayajasambaa kwenda kwenye damu na kutishia Maisha.
Nifanye nini nikiwa na maumivu wakati wa kukojoa?
Wanaume wenye maumivu wakati wa kukojoa wanapaswa kumwona daktari. Wanawake wenye homa, maumivu ya mgongo, kutokwa uchafu ukeni, au harara au vidonda kuzunguka eneo la uke wanapaswa kumwona daktari. Wanawake wenye maumivu ya kawaida wakati wa kukojoa wanaweza kujaribu kwanza kunywa maji ya kutosha ili kusafisha njia ya mkojo. Unaweza kumeza dawa za kupunguza maumivu kama vile ibuprofen, paracetamol au acetaminophen zikasaidia. Wanawake wanapaswa kumwona dakatari kama maumivu wakati wa kukojoa yataendelea kuwepo, yanazidi kuwa mabaya Zaidi au kama homa au dalili nyingine za maambukizi makali zinaanza kujitokeza.
Daktari atafanya nini nikiwa na maumivu wakati wa kukojoa?
Daktari atakuuliza maswali kuhusu dalili ulizonazo ili kutambua sababu ya maumivu uliyonayo. Kama una maambukizi, daktari atakupatia cheti cha dawa kwa ajili ya antibiotiki. Kwa wagonjwa wengi, uchunguzi wa mwili unahitajika. Mara nyingi, kipimo cha mkojo kitahitajika – kinaweza kufanyika hapo hapo ofisini kwa daktari au mkojo ukatumwa maabara kwa jili ya uchunguzi.
Wakati mwingine, vipimo vya ziada vinahitajika kama sababu haijapatikana bayana au kama kuna dalili za ugonjwa mkali zaidi. Vipimo hivi vinajumuisha vipimo vya damu, vipimo vya kupiga picha na vipimo vya kuchukua sampuli kutoka kwenye uke au uume. Baadhi ya wagonjwa wanaweza kuhitajika kuonana na daktari bingwa wa figo (nephrologist), dakatri bingwa wa mfumo wa mkojo (urologist) au daktari bingwa wa wanawake (gynecologist).
Leave feedback about this