Magonjwa ya mifupa & misuli

MAUMIVU YA NYONGA:Sababu,matibabu,kuzuia

Maelezo ya jumla

Sababu kubwa zaidi ya mkazo au maumivu ya nyonga ni kulika na kuisha kwa maungio ya nyonga kwa sababu ya yabisi kavu ‘’arthritis’’. Tatizo hili huwapata zaidi wazee; kama unalo, utahisi maumivu ya paja, makalio au kwenye kinena pamoja na nyonga.

Sababu nyingine ni ‘’bursitis’’, hili ni tatizo linalotokana na kuvimba kwa mfuko uliojaa majimaji ambao husaidia kupunguza msuguano kwenye maungio ya nyonga. Kuvimba kwa mfuko huu hutokana na matumizi makubwa sana ya maungio ‘’oversuse’’ au kuumia. ‘’Bursitis’’ husababisha maumivu sehemu ya nje ya paja, ambayo yanaongezeka makali unapojaribu kupanda ngazi au unapojaribu kulalia upande wenye matatizo.

Maumivu ya nyonga
Kushoto ni kifuko kilichovimba “Bursitis”

Maumivu ya nyonga -mwone daktari haraka kama

Ni vyema kutafuta usaidizi wa kitabibu haraka

 • Kama unapata maumivu ya nyonga baada ya kuanguka au kupata ajali
 • Kama unapata shida kutembea au kama unashindwa kusimama kwa mguu ulioathirika
 • Kama una homa na una maumivu kwenye nyonga
 • Ni vizuri kuonana na daktari atambue nini sababu ya maumivu yako

Unachoweza kufanya mwenyewe ukiwa na maumivu ya nyonga

Kama unapata maumivu ya nyonga, jaribu kufanya mambo yafuatayo ili kupunguza karaha unayopata

 • Tumia dawa za maumivu. Madawa kama vile ‘’acetaminophen’’yanapunguza maumivu na ‘’ibuprofen’’ inapunguza uvimbe pia
 • Tumia madawa ya kuchua ‘’counterirritant’’, madawa ya kuchua yanaapoza na kuongeza mzunguko wa damu mahali palipoathirika
 • Jaribu kuendelea na shughuli zako kama kawaida kadri unavyoweza, kumbuka kupumzisha nyonga na miguu yako kila unapohitaji. Epuka shughuli au mazoezi yanayoleta maumivu au yanayosababisha maumivu kuzidi
 • Kama una ‘’bursitis’’, jaribu kuweka barafu sehemu inayouma (unaweza kutwanga barafu iliyo kwenye kifuko ukaifunga na kitambaa chepesi kisha ukaitumia). Iweke hapo kwa dakika 10. Rudia utaratibu huu mara 2-3 kwa siku kwa masaa 48 ya mwanzo
 • Kama maumivu yanatokana na kulika au kusagika kwa maungio ‘’yabisi kavu’’, chukua chupa yenye maji ya moto, ifunike na kitambaa chepesi kisha weka kwenye nyonga.
 • Lala kwenye godoro gumu. Jitahidi usilalie nyonga yenye shida
 • Unaweza pia kutumia madawa ya virutubisho vya nyongeza kama vile ‘’glucosamine’’ na ‘’chondroitin’’. ‘’Glucosamine’’ na ‘’chondroitin’’ zinapatikana kwa asili kwenye gegedu za nyonga na kuzitumia inaweza kupunguza uvimbe na taratibu kupunguza mkazo wanyonga na yabisi kavu.

Kuzuia maumivu ya nyoga

Baada ya maumivu kupungua unaweza kufanya mambo yafuatayo ili kuhakikisha hayajirudii

 • Punguza uzito wa mwili, uzito mkubwa wa mwili unaongeza shinikizo kwenye nyonga
 • Endesha baiskeli au ogelea mara kwa mara ili kujenga misuli inayotegemeza maungio ya kwenye nyonga

Mwone daktari kama

Panga kumwona daktari  akupatie ushauri

 • Kama maumivu ya nyonga yako hayapoi baada ya wiki 1 au kama unaona maumivu yanaongezeka
 • Kama unaanza kuhisi maumivu kwenye maungio ya sehemu nyingine mwilini

Vyanzo

https://medlineplus.gov/ency/article/003179.htm

Leave feedback about this

 • Quality
 • Price
 • Service

PROS

+
Add Field

CONS

+
Add Field
Choose Image
Choose Video
X