MBINU ZA KUPUNGUZA UWEZEKANO WA KUPATA SARATANI

Maelezo ya jumla

Mtindo wa maisha usiofaa huchangia kwa kiasi kikubwa aina nyingi za saratani. Kufuata kwa makini ulaji na mtindo bora wa maisha kutakuwezesha kupunguza uwezekano wa kupata saratani. Huu ni uamuzi ambao kila mmoja anaweza kuufanya. Yafuatayo ni muhimu:saratani

Tumia zaidi vyakula vitokanavyo na mimea

Tafiti zimeonesha kuwa, vyakula hivi vinaweza kupunguza uwezekano wa kupata karibu aina zote za saratani.

  • Kula mbogamboga na matunda kwa wingi kila siku;
  • Kula mbogamboga za kijani, njano, nyekundu, zambarau na rangi nyingine zilizopikwa angalau ujazo wa kikombe kimoja katika kila mlo. Kutumia pia mboga zisizopikwa, kama vile saladi, nyanya, matango na kuchanganya mboga au matunda ya rangi mbalimbali kwani huongeza ubora wake;
  • Kula matunda ya aina mbalimbali (kama topetope, mastafeli, zambarau, embe, pera, chungwa, ubuyu, nk,) angalau tunda moja katika kila mlo. Kula tunda ni bora kuliko kunywa juisi;
  • Kujenga tabia ya kutumia nafaka zisizokobolewa kama vile unga wa dona, mchele wa brauni, unga wa ngano usiokobolewa, pia ulezi, mtama au uwele katika kila mlo;
  • Kutumia vyakula mbalimbali vya jamii ya kunde kama vile maharagwe, kunde, njugu mawe, dengu, choroko na mbaazi.

Kunyonyesha watoto

Wanawake wawe na tabia ya kunyonyesha watoto kwani tafiti zimethibitisha kuwa mwanamke anayemnyonyesha mtoto anapunguza uwezekano wa kupata saratani ya matiti na ovari. Pia mtoto aliyenyonya maziwa ya mama kama inavyoshauriwa anapunguza uwezekano wa kuwa na uzito wa mwili unaozidi kiasi (unene) utotoni, na hivyo kupunguza uwezekano wa unene ukubwani, kwa maana hiyo anapunguza uwezekano wa kupata saratani.

Inashauriwa mtoto anyonyeshwe maziwa ya mama pekee bila kupewa kitu kingine chochote (hata maji) katika miezi sita ya mwanzo. Baada ya miezi sita aendelee kunyonyeshwa na kupewa chakula cha nyongeza hadi atimize umri wa miaka miwili au zaidi.

Kuwa na uzito wa mwili ulio sahihi

Uzito wa mwili uliozidi unachangia kupata saratani hasa zile za kinywa, koo, matiti, utumbo mpana, ini, kongosho na kizazi. Unene pia huongeza hatari ya uvimbe wa saratani kurudi tena hata pale ambapo ulishatolewa.

Fanya mazoezi ya mwili

Tafiti zimeonesha kuwa kufanya mazoezi ya mwili husaidia kupunguza uwezekano wa kupata saratani hasa zile za matiti, tezi dume, utumbo mpana, mapafu, kongosho na kizazi. Kufanya mazoezi pia huchangia kuzuia au kupunguza unene ambao pia unahusishwa na saratani za aina nyingi. Pia mazoezi huusaidia mwili kuwa mkakamavu na husadia chakula kufanya kazi vizuri mwilini na kuwezesha mwili kutumia nishati – lishe ya ziada.

Punguza matumizi ya nyama nyekundu

Utumiaji wa nyama nyekundu kwa wingi umeonekana kuongeza uwezekano wa kupata saratani hasa za utumbo mpana, kinywa, koo, mapafu na kongosho. Kama unatumia nyama nyekundu hakikisha isiwe zaidi ya nusu kilo kwa wiki. ­

Epuka matumizi ya nyama zilizosindikwa

Tafiti zimethibitisha kwamba nyama iliyosindikwa, hata inapoliwa kwa kiasi kidogo huongeza sana uwezekano wa kupata saratani hasa zile za utumbo mpana, kinywa, koo, mapafu na tezi ya kiume. Nyama zilizosindikwa ni pamoja na zile zilizohifadhiwa kwa kuongezwa chumvi, mafuta, kemikali au kukaushwa kwa moshi. Nyama hizo ni pamoja na nyama za kopo, soseji, bekoni, salami n.k.

Punguza matumizi ya chumvi

Chumvi huongeza uwezekano wa kupata saratani hasa ya tumbo. Mahitaji ya chumvi kwa siku ni wastani wa gramu 5 (kijiko kimoja cha chai). Vyakula vingi huwa na chumvi ya asili. Jaribu kuongeza ladha kwenye chakula kwa kutumia viungo mbalimbali badala ya chumvi. Gundua chumvi iliyojificha kwenye vyakula vilivyosindikwa na usiongeze chumvi kwenye chakula wakati wa kula.

Epuka vyakula vilivyoota fangasi au ukungu

Vyakula vilivyoota fangasi au ukungu vimeonekana kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya ini. Vyakula hivyo hutoa sumu iitwayo aflatoxin ambayo inahatarisha afya na pia huweza kuongeza uwezekano wa kupata saratani.

Epuka utumiaji wa tumbaku au sigara

Utumiaji wa tumbaku au sigara huongeza hatari ya kupata saratani hasa zile za mapafu, kinywa na koo. Uvutaji wa sigara pia huingilia na kudhoofisha mfumo wa kinga ya mwili. Kumbuka hata unapokuwa karibu na mtu anayevuta sigara wewe pia unavuta ule moshi hivyo unapata madhara pia.

Epuka matumizi ya pombe

kupita kiasi Matumizi ya pombe aina yoyote huongeza uwezekano wa kupata saratani hasa zile za kinywa, koo, utumbo mpana, matiti na ini. Pombe huweza kuingilia umeng’enywaji wa chakula na ufyonzwaji wa virutubishi mwilini. Pia huingilia uhifadhi wa baadhi ya vitamini na madini mwilini.

Vyanzo

https://www.tfnc.go.tz/publications/9

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi