Last Updated on October 13, 2023 by Dr Mniko
Maelezo ya jumla
Mdomo wazi au mdomo sungura (cleft lip and palate) ni kasoro ya kuzaliwa nayo inayoathiri mdomo wa juu wa kinywa na kaakaa au paa la kinywa.
Mdomo wazi
Kama ni midomo ya juu pekee iliyoathirika, hii hujulikana kama mdomo wazi – cleft lip. Mdomo wazi ni uwazi mdogo, pengo au mbonyeo kwenye mdomo wa juu na unaweza kuendelea mpaka kwenye pua. Mdomo wazi unaweza kutokea upande mmoja wa mdomo wa juu au pande zote mbili.
Uwazi kwenye kaakaa
Kaakaa lilipasuka –cleft palate, ni hali inayotokana na kutokuungana vyema kwa sehemu mbili za kaakaa /sehemu ngumu inayounda paa la kinywa.
Kama kuna uwazi kwenye kaakaa kuna uwezekano mkubwa kuwa kimeo (uvula) pia kimepasuka au kina uwazi. Uwazi kwenye kaakaa/paa la kinywa hutokana na kushindwa kuungana kwa vipande viliwili vinavyoliunda wakati wa ukuaji wa mtoto tumboni.
Uwazi unapotokea kwenye kaakaa/paa la mdomo husababisha kuwepo na tundu/muunganiko kati ya mdomo na uwazi wa pua.
Dalili za mdomo wazi au kaakaa?
Mtoto anaweza kuwa na moja ya hali hizi au anaweza kuwa na zote kwa pamoja wakati wa kuzaliwa.
Mdomo wazi unaweza kuonekana kama mbonyeo tu kwenye mdomo wa juu. Inaweza pia kuwa ni uwazi ambao umegawanya mdomo katika sehemu mbili na kuendelea mpaka kwenye pua.
Uwazi kwenye kaakaa unaweza kuwa kwenye upande mmoja au pande zote za paa la kinywa. Uwazi huu unaweza kutoboa kabisa paa la kinywa.
Dalili zingine ni kama vile:
- Meno yaliyopangika vibaya
- Umbo la pua lisilo la kawaida
Matatizo yanayoweza kutokea kwa sababu ya uwepo wa mdomo wazi au uwazi kwenye kaakaa ni pamoja na:
- Kushindwa kuongezeka kwa uzito wa mwili
- Matatizo wakati wa kula
- Kutokea kwa maziwa puani wakati wa kunyonya
- Meno yaliyopangika vibaya mdomoni
- Ukuaji usioridhisha/duni
- Maambukizi ya mara kwa mara kwenye masikio
- Ugumu au matatizo ya kuongea/kuzungumza
Nini husababisha mdomo wazi na uwazi kwenye kaakaa?
Kuna sababu nyingi za kutokea kwa mdomo wazi au uwazi kwenye kaakaa. Matatizo kwenye jeni zinazorithiwa toka kwa mzazi mmoja au wote, madawa, virusi au sumu zingine zinazoweza kusababisha kasoro hizi za kuzaliwa nazo. Mdomo wazi unaweza kutokea sambamba na kasoro zingine za kuzaliwa nazo.
Tatizo hili linaweza kusababisha mwonekano wa mtu kuwa mbaya au usioridhisha na unaweza kusababisha matatizo wakati wa kuongea na maambukizi kwenye masikio. Matatizo yanaweza kuwa madogo tu, kama vile mbonyeo/ufa au yanaweza kuwa makubwa na kugawanya kabisa paa la kinywa na pua.
Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata mdomo wazi?
Sababu zinazoongeza hatari ni pamoja na:
- Kuwepo kwa historia ya kuwa na mdomo wazi au uwazi kwenye kaakaa kwa mwanafamilia
- Kuwepo kwa kasoro nyingine za kuzaliwa nazo
1 kati ya watu 2,500 huwa na uwazi kwenye kaakaa
Utambuzi wa mdomo wazi
Uchunguzi na ukaguzi wa mdomo, pua, na kaakaa huthibitisha uwepo wa uwazi kwenye mdomo au kaakaa. Vipimo vingine vinaweza kufanyika ili kuhakikisha hakuna kasoro nyingine za kuzaliwa nazo au matatizo mengine ya kiafya
Wakati gani utafute matibabu ya haraka?
Uwazi kwenye mdomo au kaakaa hutambuliwa pindi tu baada ya mtoto kuzaliwa. Fuata maelekezo utakayopewa na daktari, zingatia miadi ya kumpeleka kwa daktari kufuatilia maendeleo ya mtoto. Mrudishe mtoto hosipitali kama tatizo lolote litaibuka katikati ya miadi-appointment.
Uchaguzi wa matibabu
Upasuaji hufanyika ili kufunga uwazi uliopo kwenye mdomo mtoto anapokuwa na umri kati ya wiki 6 mpaka miezi 9. Upasuaji unaweza kuhitajika baadae kama tatizo hili litaathiri kwa kiasi kikubwa eneo la pua.
Mara nyingi upasuaji kwa ajili ya kurekebisha uwazi ulipo kwenye kaakaa (paa la kinywa) hufanyika ndani yam waka mmoja wa maisha ya mtoto, ili mtoto aweze kuongea vizuri. Kwa wakati mwingine, kifaa maalumu kinaweza kuwekwa ili kuziba uwazi huo kabla ya upasuaji ili kupunguza matatizo au ugumu wa kula na kukua mpaka siku ya upasuaji itakapofika.
Mtoto anahitaji kuendelea kufuatiliwa na anaweza pia kuhitaji msaada wa mtaalamu wa lugha (speech therapist) ili aweze kuzungumza vizuri.
Kuzuia
Japo kesi nyingi za mdomo wazi na uwazi kwenye kaakaa hazitabiriki, unaweza kufanya mambo kadhaa kupunguza uwezekano wa kutokea kwake
- Ushauri wa kijenetiki: Upimaji wa kijenetiki unaweza kukuambia una historia kwa kiasi gani inayoongeza uwezekano wa kupata mdomo wazi kwenye familia. Inaweza kukuambia pia kama damua au vinasaba vya DNA vina kasoro zozote zinazoongeza uwezekano wa kupata mdomo wazi.
- Kutumia vitamini wakati wa ujauzito: Watafiti wameonesha kuwa upungufu wa madini ya folic acid aua aina nyingine za vitamin huongeza uwezekano wa kupata mdomo wazi na uwazi kwenye kaakaa. Kwa kutumia vitamin wakati wa ujauzito hupunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kupata mtoto mwenye uwazi kwenye mdomo au kaakaa.
Nini cha kutarajia?
Ingawa matibabu yanaweza kuendelea kwa miaka kadhaa na kuhitajika kufanyiwa upasuaji mara kadhaa, watoto wengi wenye tatizo hili hufikia kuwa na mwonekano wa kawaida, kuzungumza kama watoto wengine na kula bila shida yoyote. Hata hivyo, baadhi yao wanaweza kuendelea kuwa na matatizo au shida wakati wa kuzungumza.
Matatizo yanayoweza kutokea
- Meno yaliyokaa vibaya
- Kuwa kiziwi
- Mwonekano wa mdomo usiopendeza/usioridhisha
- Mwonekano wa pua usipendeza/usioridhisjha
- Maambukizi ya mara kwa mara ya masikio
- Matatizo au ugumu kuzungumza
Leave feedback about this