MKAMBA

MKAMBA

 • August 17, 2020
 • 1 Like
 • 149 Views
 • 0 Comments

Maelezo ya jumla

Mkamba (bronchitis) ni kuvimba kwa njia kuu ya kupitisha hewa kwenda kwenye mapafu. Mkamba unaweza kuwa wa muda mfupi tu (acute) au sugu (chronic),hii inamaanisha kuwa mkamba hudumu kwa muda mrefu na mara nyingi hujirudia rudia.

Nini dalili za mkamba?

Dalili za mkamba ni iamoja na:    

 • Kujisikia vibaya kifuani   
 • Kikohozi chenye kutoa makohozi, ikiwa ni ya kijani-manjano kuna uwezekano mkubwa wa kuwepomaambukizi ya bakteria    
 • Uchovu
 • Homa – kwa kawaida homa huwa sio kali   
 • Kupata shida kupumua kunakoongezeka mgonjwa akifanya kazi/shughuli ndogo tu.
 • Kukorota (wheezing)

Hata baada ya mkamba kupona, unaweza bado kuwa na kakikohozi kakavu, kanakoendelea kukusumbua kwa wiki kadhaa.

Dalili za ziada za mkamba sugu (chronic bronchitis) ni pamoja na:    

 • Kuvimba kwa vifundo vya miguu na miguu
 • Midomo yenye rangi ya bluu kwa sababu ya kukosa oksijen ya kutosha     
 • Maambukizi ya mara kwa mara kwenye njia ya hewa (kama vile mafua)

Ni nini husababisha mkamba?

Mkamba wa muda mfupi (acute bronchitis) hutokea baada ya maambukizi ya virusi kwenye njia ya hewa. Mwanzoni huathiri pua, uwazi ndani ya fuvu unaowasiliana na mianzi ya pua (sinuses) na koo na kisha huenea kwenye mapafu. Wakati mwingine, baada ya maambukizi hayo unaweza kupata maambukizi mengine ya bakteria kwenye njia ya hewa. Hii ina maana kwamba mgonjwa huwa na maambukizi ya bakteria na virusi kwa pamoja.

Mkamba sugu ni hali ya muda mrefu. Mgonjwa huwa na kikohozi kinachozalisha makohozi mengi. Ili kutambuliwa kuwa una mkamba sugu,lazima uwe na kikohozi kinachotoa makohozi kwa siku nyingi za mwezi kwa angalau miezi 3.

Mkamba sugu ni moja ya magonjwa yaliyo katika kundi la magonjwa sugu yanayosababisha kuziba kwa njia ya hewa (chronic obstructive pulmonary disease).

Mambo yafuatayo yanaweza kufanya hali ya mgonjwa wa mkamba kuwa mbaya zaidi

 • Uchafuzi wa hewa    
 • Mzio (allergies)
 • Kazi fulani fulani (kama vile uchimbaji wa makaa ya mawe, viwanda vya nguo, au utunzaji wa nafaka)    
 • Maambukizi

Nani yuko kwenye hatari zaidi?

Watu walio katika hatari zaidi ya kupata mkamba (bronchitis) ni pamoja na:    

 • Wazee, watoto wachanga, na watoto wadogo    
 • Watu wenye magonjwa ya moyo au mapafu    
 • Wavutaji wa sigara

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Mwone daktari kama:    

 • Una kikohozi cha siku nyingi au una kikohozi kinachorudi mara kwa mara    
 • Unakohoa damu    
 • Una homa kali au kutetemeka   
 • Una homa ya kadri kwa siku 3 au zaidi    
 • Unatoa kohozi lenye harufu mbaya, zito na lenye rangi ya kijani hivi
 • Unapata shida kupumua au unapata maumivu
 • Kama una ugonjwa wa moyo au mapafu

Utambuzi

Mtoa huduma ya afya atasikiliza mapafu yako kwa stethoscope. Sauti isiyo ya kawaida katika mapafu inayoitwa rales au sauti nyingine zisizo za kawaida zinaweza kusikika.

Vipimo vingine ni:    

 • Eksirei ya kifua 
 • Vipimo vya mapafu kujua jinsi yanavyofanya kazi (lung function tests) hutoa taarifa ambazo ni muhimu kwa ajili ya utambuzi na kubashiri matarajio ya mgonjwa.    
 • Pulse Oximetry husaidia kupima kiasi cha oksijeni kwenye damu. Kipimo hiki hutumia kifaa kinachowekwa kwenye kidole, ni cha haraka na hakisababishi maumivu yoyote. Arterial blood gases ndicho kipimo bora zaidi kinachoweza kupima oksijeni na kaboni dioksaidi kwenye damu kwa usahihi kabisa ,lakini kinahitaji kumchoma mtu sindano na kusababisha maumivu.
 • Sampuli za makohozi zinaweza kuchukuliwa ili kuchunguza kama kuna alama za uvimbe au maambukizi ya bakteria.

Uchaguzi wa matibabu

Hauhitaji kutibiwa kwa viuavijasumu (antibiotics) ukiwa na mkamba wa muda mfupi kwa sababu mara nyini husababishwa na virusi. Maambukizi haya yatapona yenyewe ndani ya wiki moja. Fanya mambo yafuatayo ili kupata nafuu mapema.

 • Usivuta sigara    
 • Kunywa maji mengi    
 • Pumzika    
 • Tumia aspirini au paracetamol ikiwa una homa. USIMPE mtoto aspirin    
 • Tumia humidifier au mvuke ukiwa bafuni

Ikiwa dalili zako hazipungui, daktari wako anaweza kuagiza upewe inhaler ili kusaidia kufungua njia ya hewa kama unakorota (wheezing).Kama daktari wako anafikiria kuwa umepata maambukizi ya bakteria,anaweza kuagiza upewe antibiotics. Lakini mara nyingi antibiotics hazihitajiki na hazipendekezwi.

Kwa aina yoyote ya mkamba (bronchitis) , hatua muhimu zaidi unayoweza kuchukua ni KUACHA KUVUTA sigara. Kama mkamba ukigunduliwa mapema inaweza kuzuia uharibifu wa mapafu.

Nini cha kutarajia (Prognosis)?

Kwa mkamba wa muda mfupi (acute bronchitis), dalili huondoka ndani ya siku 7 hadi 10 kama hauna shida nyingine ya mapafu. Hata hivyo kakikohozi kakavu ,kanakosumbua kanaweza kuwepo kwa miezi kadhaa.

Uwezekano wa kupona kwa watu wenye mkamba sugu ni mdogo. Utambuzi wa mapema na matibabu, pamoja na kuacha kuvuta sigara, kwa kiasi kikubwa husaidia kuleta matokeo bora.

Matatizo yanayoweza kutokea

Nimonia inaweza kutokea baada ya mkamba wa muda mfupi au mkamba sugu.Unawaweza kupata maambukizo ya mara kwa mara kwenye njia ya hewa kama una mtamba sugu. Unaweza pia kupata:

 • Emphysema (ni hali inayotokea baada ya vifuko vinavyochuja hewa kwenye mapafu kuharibiwa na kusababisha shida ya kupumua). 
 • Kushindwa kusukama damu kwa sehemu ya kulia ya moyo baada ya kuharibika mapafu (cor pulmonale/Right sided heart failure)    
 • Shinikizo la juu la damu kwenye mapafu (pulmonary hypertension)

Kuzuia    

 • Usivute sigara.    
 • Punguza uchafuzi wa hewa.    
 • Osha mikono yako (na mikono ya watoto wako mara kwa mara) ili kuepuka kuenea kwa virusi na maambukizi mengine.

Vyanzo

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/ency/article/001087.htm

 • Share:

Leave Your Comment