Last Updated on October 12, 2023 by Dr Mniko
Lishe kwa watoto wachanga hadi umri wa miezi 6
Kuna mambo ya kuzingatia katika lishe kwa watoto wachanga hadi umri wa miezi 6. Maziwa ya mwanzo yenye rangi ya njano ni mazuri kwa ajili ya mtoto wako. Maziwa haya humkinga mtoto dhidi ya magonjwa. Maziwa ya mama ndiyo chakula pekee ambacho mtoto anahitaji katika miezi 6 ya mwanzo. Maji au vinywaji vingine na vyakula vinaweza kumfanya mtoto apate magonjwa.
Wanawake waliogundulika kwamba wameambukizwa VVU nao wanashauriwa kunyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo.
Katika kipindi hiki chote, mama na mtoto wenye maambukizi ya VVU wanashauriwa kuendelea kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU kama walivyoshauriwa na wataalamu wa afya.
Lishe kwa watto wenye umri wa miezi 6 hadi miaka 2
Mtoto anapotimiza umri wa miezi 6 apewe vyakula vya nyongeza ili kukidhi mahitaji yake ya kilishe yanayoongezeka kadri anavyokua kwa kuwa maziwa ya mama pekee hayawezi kutosheleza mahitaji ya kilishe ya mtoto. Vile vile anapaswa kuendelea kunyonyeshwa kila anapohitaji usiku na mchana kwani maziwa ya mama bado ni sehemu muhimu katika ukuaji wa mtoto. Vyakula anavyopaswa kupewa mtoto mwenye umri huu ni pamoja na:
- Maziwa ya mama hadi atimize umri wa miaka miwili au zaidi
- Vyakula vya nafaka, mizizi na ndizi kuchanganywa na vyakula vingine vyenye virutubishi kwa wingi kama maziwa, karanga au mafuta ili kumpatia mtoto virutubishi vya kutosha
- Mchanganyiko wa angalau chakula kimoja kutoka katika makundi makuu matano ya vyakula (vyakula vya nafaka, mzizi na ndizi, vyakula vya jamii ya kunde na vile vyenye asili ya wanyama, mboga mboga, matunda na mafuta na sukari)
- Vyakula vilivyo tayarishwa na kuhifadhiwa vizuri ili kuzuia maambukizi yanayoweza kusababisha magonjwa kama vile kuharisha
- Maji safi na salama
- Vyakula vilivyo andaliwa kwa kutumia chumvi yenye madini joto
Usimulazimishe mtoto kula. Tumia mbinu shirikishi za ulishaji ili mtoto aweze kukubali kula.
Kumbuka kumpeleka mtoto kliniki kwa ajili ya ufuatiliaji wa maendeleo, kupewa chanjo zote kama miongozo ya kitaifa inavyoelekeza.
Lishe kwa watoto wenye umri wa miaka 3–5
Watoto katika umri huu wana mahitaji makubwa ya virutubishi kwa sababu wapo katika kipindi cha ukuaji wa haraka. Pia katika kipindi hiki huwa hakuna uangalizi mzuri wa watoto, na hivyo kuwaacha watoto wale chakula peke yao au kula na watoto wakubwa hivyo kushindwa kupata virutubishi vya kutosha ili kukidhi mahitaji ya miili yao. Katika umri huu mtoto anaweza kuachishwa kunyonya na kuendelea kula chakula cha familia katika uwiano wa makundi matano ya vyakula ili kupata virutubishi vya kutosheleza mahitaji yake ya mwili kilishe. Vyanzo vingine vyenye virutubishi vingi kwa mfano vyakula vya asili ya wanyama kama vile maziwa ya ng’ombe lazima yajumuishwe katika mlo wa mtoto hadi miaka mitano. Walezi wa watoto wenye umri wa miaka 3–5 wanatakiwa:
- Kuendelea kupewa maziwa, kwa mfano ya ngo’mbe, kama sehemu ya chakula cha mtoto.
- Kuwapa chakula mchanganyiko kutoka katika makundi yote matano ya vyakula.
- Kuwapa milo mitatu kwa siku.
- Kuwapa asusa angalau mara mbili kwa siku (katikati ya mlo na mlo) kwa mfano uji, maziwa, kipande cha mhogo uliochemshwa au viazi vitamu kulingana na mazingira na kinaweza kuwa chakula kilichobaki kutoka katika mlo wa familia.
- Wasilazimishe mtoto kula. Tumia mbinu shirikishi za ulishaji ili mtoto aweze kukubali kula.
- Kuhakikisha mtoto anapewa maji na chakula safi na salama.
- Kuhakikisha vyakula anavyopewa mtoto vinatayarishwa na kuhifadhiwa vizuri ili kuzuia maambukizi yanayoweza kusababisha magonjwa kama vile kuharisha.
- Kuwapeleka watoto kliniki kwa ajili ya ufuatiliaji wa maendeleo, kupewa chanjo zote kama miongozo ya kitaifa inavyoelekeza.
- Kutumia chumvi yenye madini joto wanapoandaa chakula cha mtoto.
Lishe kwa watoto wenye umri wa miaka 6–10
Watoto katika umri huu wana mahitaji makubwa ya virutubishi kwa sababu bado wanaendelea kukua na bado wanawategemea watu wengine kuwalisha. Pia kipindi hiki watoto hawa hufanya shughuli nyingi zinazohusisha mwili kama kucheza michezo mbalimbali pamoja na ukuaji wao ambavyo kwa pamoja huongeza mahitaji ya virutubishi ili kukidhi mahitaji ya miili yao. Vilevile katika kipindi hiki watoto wengi huwa wameanza shule na hivyo wanaweza kukosa mlo wa mchana lakini pia wanakabiliwa na hatari ya kupata magonjwa yanayotokana na kutumia maji yasiyo safi na salama. Hali hizi zote huchangia uwezekano wa kupata utapiamlo.
Watoto wenye umri wa miaka 6–10 wanatakiwa:
- Kulishwa kwa kutumia mwongozo wa mbinu za ulishaji.
- Kupewa chakula mchanganyiko kutoka katika makundi yote matano ya vyakula.
- Kupewa kifungua kinywa kabla ya kwenda shule. Kama hakuna kifungua kinywa wapewe matunda au asusa zilizobora kilishe zinazopatikana katika mazingira anayoishi kama mihogo, viazi na ndizi.
- Kupewa milo kamili mitatu na asusa mara mbili au tatu kwa siku.
- Kupewa chakula ili wale wakati wa mchana.
- Kupewa vyakula vilivyoongezewa virutubish.
- Kuzingatia kanuni za usafi ikiwa ni kunawa mikono nyakati zote muhimu na kutumia choo.
- Kupewa dawa za minyoo kila baada ya miezi sita.
- Kutumia chumvi yenye madini joto wakati wa kuandaa chakula chao.
- Kunywa maji safi na salama.
- Kuzingatia usafi na usalama wa chakula na maji.
- Kunawa mikono nyakati zote muhimu.
Lishe kwa watoto wagonjwa
Mtoto anapokuwa mgonjwa huhitaji chakula kingi zaidi ili aweze kukidhi mahitaji ya kilishe yaliyoongezeka, kuuwezesha mwili kukabiliana na maradhi aliyo nayo, kuzuia kupungua uzito na kuweza kupona mapema.
Mpeleke mtoto katika kituo cha kutoa huduma ya afya mapema kwa ajili ya matibabu. Watoto wagonjwa wanatakiwa:
- Kunywa maziwa mara nyingi zaidi.
- Kula milo midogo midogo mara nyingi.
- Kula chakula laini kilicho rahisi kumeza.
- Kunywa vinywaji kama maji safi na salama, juisi halisi ya matunda, madafu au maziwa.
- Kula matunda na mboga mboga kwa wingi hususan zenye rangi ya kijani na njano. kwani husaidia kuboresha kinga ya mwili.
Leave feedback about this