MLO/LISHE WAKATI WA MAJANGA

Majanga na Dharula

Majanga na dharura ni matukio ambayo yanatokea kwa ghafla na kuharibu mfumo mzima wa maisha na mali za mtu, watu au jamii nzima. Pia matukio hayo yanaweza kusababisha watu kuumia na hata kupoteza maisha. Kuna makundi mawili ya majanga ambayo ni majanga ya asili na majanga yanayosababishwa na binadamu wenyewe.Majanga

Majanga ya asili:

 • Tetemeko la ardhi
 • Upepo mkali
 • Mawimbi makubwa ya baharini
 • Kimbunga
 • Mlipuko wa volkano
 • Mlipuko wa magonjwa
 • Maporomoko ya theluji kwenye milima
 • Mafuriko
 • Joto lililozidi
 • Ukame

Majanga yanayosababishwa na wanadamu:

 • Vita
 • Ajali za moto
 • Uchafuzi wa mazingira
 • Mlipuko wa magonjwa

Majanga na Dharura Yanavyoathiri Lishe ya Jamii

Wahanga wa majanga wanakuwa katika uwezekano mkubwa wa kupata matatizo ya kiafya na lishe kutokana na:

Upungufu wa chakula unaoweza kusababishwa na:

 • Kuaribika kwa mazao
 • Kufa kwa mifugo
 • Kukosa soko
 • Sababu za kiuchumi

Mabadiliko ya ulaji katika jamii kwa sababu ya:

 • Kuharibika kwa mfumo wa maisha ya kila siku
 • Kutegemea mgao wa chakula cha msaada
 • Kupungua kwa upatikanaji wa vyakula vya aina mbalimbali
 • Uhaba wa nishati ya kupikia mfano mkaa na kuni

Ongezeko la magonjwa ya kuambukizwa:

 • Kuishi katika mazingira machafu
 • Kukosa maji safi na salama
 • Kuishi kwenye maeneo yenye msongamano wa watu
 • Mazingira duni ya kuishi

Afua za Lishe Wakati wa Majanga

Kutokana na athari za majanga waathirika wanakuwa katika hatari ya kupata matatizo mbalimbali ya kilishe. Matatizo hayo ni pamoja na Utapiamlo wa muda mfupi hasa kwa watoto na upungufu wa vitamini na madini mbalimbali mwilini. Zifuatazo ni afua muhimu za lishe ambazo zinapaswa kutekelezwa wakati wa majanga:

Kuzingatia taratibu sahihi za ulishaji wa watoto wachanga na wadogo

Uzoefu unaonyesha kwamba kulinda, kuendeleza na kusaidia unyonyeshaji watoto maziwa ya mama na ulishaji sahihi wa vyakula vya nyongeza ni mkakati mkuu wa kulinda uhai wa watoto wakati wa majanga. Kwa hiyo wakati jamii inapoathiriwa na majanga ni muhimu kuzingatia yafuatayo:

 • Kusaidia wanawake wenye watoto wa umri chini ya miezi sita wanyonyeshe watoto wao maziwa ya mama pekee.
 • Kusaidia wanawake wenye watoto wa umri wa miezi sita wawalishe watoto wao vyakula vya nyongeza pamoja na kuendelea kunyonyesha maziwa ya mama hadi wafikishe miaka miwili au zaidi.
 • Kuwasaidia wanawake walioacha kunyonyesha kutokana na maziwa kuacha kutoka kwa sababu ya uchovu, msongo wa mawazo au sababu nyingine ili waweze kuanzisha unyonyeshaji tena.
 • Kuepuka ugawaji wa maziwa mbadala kwa wanawake wenye watoto chini ya umri wa miaka miwili kwa kuwa maziwa hayo yanaweza kutolewa iwapo mama wa mtoto hajulikani alipo au amefariki.
 • Kutenga eneo maalum kwa ajili ya wanawake wanaonyonyesha.
 • Kuepuka uvunjifu wa kanuni za kitaifa na za kimataifa zinazodhibiti matumizi holela ya maziwa mbadala na vyakula vya watoto wachanga na wadogo.

Usafi na Usalama wa Maji na Mazingira

Majanga mara nyingi huaribu mfumo wa maji safi na salama kusababisha jamii iliyoathirika janga kukosa maji safi na salama. Pia huishi kwenye maeneo ya msongamano wa watu na hivyo hali duni ya usafi wa mazingira. Haya yote huongeza uwezekano wa kuambukizwa magonjwa hasa ya mlipuko mfano kuhara, homa ya uti wa mgongo na kipindupindu. Kwa hiyo ni muhimu kuchukua hatua za haraka za kuboresha usafi wa mazingira na upatikanaji wa maji safi na salama wakati wa majanga kwa kufanya yafuatayo:

 • Kugawa na kuhamasisha matumizi ya dawa za kutibu maji kwa waathirika
 • Kutenga maeneo maalum yenye miundombinu ya kunawa mikono
 • Kujenga vyoo bora vya dharula na kuhamasisha matumizi yake.
 • Kuweka vifaa na maeneo maalum ya kutupa taka.
 • Kutoa elimu ya usafi wa mwili na mazingira kwa waathirika.
 • Kutenga maeneo ya kutolea huduma za matibabu hususani ya magonjwa ya mlipuko.
 • Matibabu ya magonjwa ya mlipuko yafuate taratibu zilizoainishwa kwenye miongozo mbalimbali ya kitaifa

Huduma za Msingi za Afya

Waathirika wa majanga wanahitaji kupewa huduma za msingi za afya kama watu wengine. Huduma hizo ni pamoja na:

 • Chanjo mbalimbali zinazotolewa kwa watoto wachanga na wadogo na wanawake wajawazito kwa kufuata miongozo ya kitaifa.
 • Vidonge vya madini chuma na asidi ya foliki kwa wanawake wajawazito na waliojifungua kufuata miongozo ya kitaifa.
 • Dawa za minyoo kwa watoto kwa kufuata miongozo ya kitaifa.
 • Uzazi wa mpango.

Vyanzo

https://www.tfnc.go.tz/publications/9

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi