MLO/LISHE YA WATOTO WENYE ULEMAVU:Mtindio wa ubongo, usonji

Lishe ya watoto wenye ulemavu

Utapiamlo kwa watoto wenye ulemavu unatokana na kutokula chakula cha kutosha na/au ulaji mbaya unaopelekea upungufu wa virutubishi kwa watoto wenye ulemavu. Upungufu wa virutubishi kwa watoto wenye ulemavu husababisha matatizo mbalimbali ya kiafya hususani utapiamlo na upungufu wa kinga ya mwili. Hivyo watoto watoto wenye ulemavu wanahitaji uangalizi wa karibu juu ya masuala ya lishe ili kuepuka matatizo ya kiafya yasio ya lazima.

Changamoto za ulishaji wa watoto wenye ulemavuulemavu

Ulemavu wa viungo na tabia zisizofaa za ulishaji vinaweza kusababisha matatizo ya ulishaji wa watoto wenye ulemavu. Matatizo hayo ni;

 • Kinywa kushindwa kufanya kazi: Mtoto mwenye ulemavu anaweza kushindwa kunyonya, kuwa na uwezo mdogo wa chakula kukaa mdomoni, kutafuna na kumeza.
 • Kushindwa kukaa: Ni vigumu kumlisha mtoto mwenye ulemavu anayeshindwa kukaa wima hivyo kupelekea mtoto kutokupata chakula cha kutosha
 • Kushindwa kushika chakula: Ni vigumu kumlisha mtoto ambaye hana uwezo wa kushika chombo au kula chakula mwenyewe. Hii mara nyingi hupelekea mlishaji kupata wakati mgumu na kuamua kumlisha kwa haraka iwezekanavyo na wakati mwengine kumlisha chakula kidogo.
 • Tabia za ulishaji: Tabia za ulishaji ambao si mzuri zinasababisha ulaji duni kwa watoto wenye ulemavu. Sababu mlishaji hupunguza umakini au kutojali uhitaji wa mtoto mwenye mlemavu.

Afua za ulishaji wa watoto wenye ulemavu

Hizi ni hatua muhimu ambazo zinapaswa kuzingatiwa ili kuwezesha mtoto mwenye ulemavu kula chakula cha kutosha na kuwezesha mwili kupata virutubishi vya kutosha. Ni muhimu kuzingatia mambo yafuatayo katika ulishaji wa watoto wenye ulemavu;

 • Chakula:
  • Zingatia ulaji unaoafaa kwa kutumia vyakula kutoka kwenye makundi matano ya chakula ili kuwezesha mwili kupata virutubishi vyote.
  • Ongeza ulaji wa vyakula vyenye vitamini na madini vinavyopatikana kwenye jamii husika kwa wingi. Mfano, mbogamboga (mchicha, matembele na mgagani) na matunda (machungwa, maembe, zambarau na ndizi mbivu).
  • Kama mtoto atakuwa na tatizo la kushindwa kutafuna na kumeza chakula apelekwe kwenye kituo cha kutolea huduma za afya.
  • Fuata taratibu sahihi za unyonyeshaji wa maziwa ya mama na mtoto anyonyeshwe kama invyoshauriwa kitaalamu.
  • Mpe mtoto chakula kilicho pondwa pondwa, kusagwa, au kilichokatwakatwa vipande vidogo vidogo.
 • Matunzo:
  • Epuka kumtelekeza mtoto mwenye ulemavu.
  • Mtoto mwenye ulemavu anahitaji upendo na huduma zote sawa na watoto wengine
  • Fanya tathimi ya hali ya lishe ya mtoto mara kwa mara ili kutambua kama anapungua uzito au anapata tatizo la uzito uliozidi.
  • Tumia muda wa kutosha kumlisha mtoto.
  • Tambua mkao unaomfaa mtoto wakati wa kula.
  • Mpeleke mtoto akapate huduma nyingine za kijamii sawa sawa na watoto wengine. Huduma hizo ni pamoja na chanjo, ufuatiliaji wa ukuaji na maendeleo ya watoto, utoaji wa vitamini na madini ya nyongeza, elimu, michezo na matibabu anapokuwa mgonjwa.
  • Mpeleke mtoto akapate huduma maalumu kwa walemavu mfano mazoezi maalumu ya viungo na viungo bandia.

Ulishaji wa mtoto mwenye mtindio wa ubongo

Watoto wenye mtindio wa ubongo wanahitaji matunzo mahususi wakati wa kuwalisha.  Hii ni kwa sababu umakini ukikosekana wakati wa ulishaji wanaweza kupaliwa kutokana na chakula au kinywaji kuingia kwenye mfumo wa hewa na kusababisha athari kwenye mfumo wa upumuaji na maambukizi kwenye mapafu.  Jambo la msingi la kuzingatia ni kurekebisha mkao wa mtoto wakati wa kula ili kuhakikisha anameza chakula vizuri kupunguza uwezekano wa kupaliwa na kumwezesha ale kiasi cha kutosha cha chakula. Ili kuhakikisha mkao unaofaa wakati wa kula inapaswa kuzingatia yafuatayo:

 • Kichwa cha mtoto kiwe kimenyooka kwa kuangalia juu kwa kiasi kidogo.
 • Shikilia kidevu na taya la mtoto taratibu.
 • Mlishe kiasi kidogo cha chakula kwa kutumia kijiko.

Mambo mengine ya kuzingatia ni:

 • Mlishe mtoto chakula chenye kiasi kikubwa cha nishati lishe, utomwili, vitamini na madini.
 • Mlishe mtoto katika mazingira tulivu. Acha shughuli zingine wakati wa kumlisha mtoto ili umlishe kwa umakini na kupunguza uwezekano wa kupaliwa.
 • Msaidie mtoto ajilishe mwenyewe kama ana uwezo. Mwangalie na kumsimamia kwa umakini wakati anakula mwenyewe.
 • Mpe mtoto vipande vidogo vidogo vya chakula ambacho anaweza kukimeza.
 • Hakikisha amemeza vizuri kabla ya kumpa chakula kingine.
 • Usimlazimishe mtoto kula. Kama amechoka, acha kumlisha ili kupunguza uwezekano wa kupaliwa.

Ulishaji wa watoto wenye usonji

Vifuatavyo ni vipengele vinavyosaidia ulishaji wa watoto wenye usonji:

 • Fuata ratiba ya ulaji wa mtoto
 • Usimpe asusa katikati ya mlo
 • Mlishe mtoto katika mazingira tulivu. Acha shughuli zingine wakati wa kumlisha mtoto ili umlishe kwa umakini na kupunguza uwezekano wa kupaliwa.
 • Muhusishe mtoto kwenye uchaguzi na maandalizi ya chakula
 • Fuata taratibu za usafi na usalama wa maji na chakula wakati wa kuandaa
 • chakula na kumlisha mtoto.
 • Mhamasishe ale chakula zaidi kwa kumsifia na kuongea naye wakati wa kula.
 • Mtengee mtoto chakula katika hali ya mvuto kama vile chakula
 • kidogo kwenye sahani au chombo chenye maua au rangi ya kuvutia

Vipaumbele vya ulishaji wa watoto wenye ulemavu

Watoto wenye ulemavu huwa na sababu mbalimbali zinazopelekea ulaji wao kushindwa kufikia mahitaji yao ya kilishe mfano wazazi/walezi kutotenga muda wa kutosha kuwalisha, kutoweza kula wenyewe na maradhi. Kuepukana na matatizo haya kuna baadhi ya mambo ya ulishaji yanayopewa vipaumbele yakizingatia maeneo yafuatayo;

 • Lishe ya kutosha
 • Maji ya kutosha
 • Kuboresha afya
 • Kuepuka kupaliwa

Umuhimu wa usafi kwa watoto wenye ulemavu

Usafi wa chakula, maji na mazingira husaidia kuboresha afya na hupunguza uwezekano wa kupata maambukizi ya magonjwa na matatizo mengine yanayoweza kujitokeza kwa mtoto. Familia nyingi hupata changamoto ya kuwaweka watoto hawa kutokana na matatizo yao ya ulemavu. Ni muhimu sana kuwahimiza wazazi na walezi kufanya bidii kuhakikisha kuwa watoto:

 • Wanakuwa katika hali ya usafi wa mwili na mavazi.
 • Wanakaa katika na mazingira safi na salama
 • Wanakunywa maji safi na salama
 • Wanatumia vyombo visafi kwa ajili ya maji na chakula
 • Wanapata huduma za afya.
 • Wanapata msaada pale inapohitajika.

Vyanzo

https://www.tfnc.go.tz/publications/9

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Jiunge Nasi