Msaada wa Haraka! 255 759 07 960
Kwa Kina
Tafuta
 1. Home
 2. MSHTUKO WA MOYO

MSHTUKO WA MOYO

 • August 14, 2020
 • 0 pendwa
 • 58 Wameona
 • 0 Maoni

Maelezo ya jumla

Shambulizi la moyo (heart attack) hutokea pindi tu mtiririko wa damu kuelekea kwenye misuli ya moyo unapokatishwa.Ikiwa mtiririko wa damu haukurejeshwa haraka misuli ya moyo huharibika/kufa kutokana na ukosefu wa oksijeni.
shambulio la moyo linaongoza kwa kusababisha vifo kwa wanaume na wanawake nchini Marekani. Lakini kwa bahati nzuri, siku hizi kuna matibabu bora ya mshtuko wa moyo ambayo yanaweza kuokoa maisha na kuzuia ulemavu. Matibabu haya ni yenye ufanisi zaidi  yakianzishwa ndani ya saa 1 baada ya kuanza kwa dalili. Ikiwa unadhani wewe au mtu ulienaye anapata shambulio la moyo, tafuta msaada haraka afikishwe kituo cha afya.

Je! Nini dalili za shambulio la moyo?

Ni muhimu kujua dalili za mshtuko wa moyo.

Dalili hizo ni pamoja na:

 • Kujisikia vibaya kifuani– kifua kubana au kuuma. Dalili ya kawaida ya shambulio la moyo ni maumivu ya kifua au kuijisikia vibaya.Shambulio la moyo husababisha maumivu katikati ya kifua kwa dakika chache na kisha kutoweka ,maumivu haya yanaweza kurejea tena baada ya kitambo kidogo. Mgonjwa hujisikia kama anakandamizwa kifuani,anabanwa na wakati mwingine huhisi mauamivu makali au ya kadri. Wakati mwingine maumivu yanayosababishwa na shambulio la moyo hufanana na yale ya kuvimbiwa au kiungulia.
 • Kupumua kwa shida – Kupumua kwa shida mara nyingi hutokea kabla mgonjwa hajaanza kujisikia vibaya kifuani.
 • Kujisikia vibaya kwenye mkono mmoja au mikono yote,mgongo, shingo, taya, au tumbo. 
 • Kichefuchefu, kutapika, kizunguzungu na jasho.

Sio mashambulizi yote ya moyo huanza kwa ghafla na kusababisha maumivu makali kifuani kama ambavyo mara nyingi huoneshwa kwenye runinga(TV) au katika sinema. Ishara na dalili za shambulio la moyo hazifanani kwa kila mtu. Mashambulizi mengi ya moyo huanza polepole kama maumivu ya kawaida au kujisikia vibaya tu. Watu wengine hawana dalili kabisa (hii inaitwa shambulio la moyo la kimyakimya).

Ni nini kinasababisha mshtuko wa moyo?

Mshtuko wa moyo hutokea mara nyingi kama matokeo ya magonjwa yanayoathiri ateri za moyo. Ugonjwa unaoathiri ateri za moyo husababishwa na utando wa mafuta ambao hujengeka taratibu, kwa miaka mingi ndani ya ateri za moyo (ateri hizi ndizo hutiririsha damu na oksijeni kwenye moyo),hatima yake ni kuwa sehemu ya ateri yenye utando mwingi huchanika na kusababisha damu kuganda juu ya utando. Kama donge la damu iliyoganda litakua na kuwa kubwa sana, litaziba kabisa ateri na kuzuia mtiririsho wa damu yenye oksijeni kufika kwenye misuli ya moyo.

Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata mshtuko wa moyo?

 • Kuna mambo kadhaa yanayoongeza hatari ya kupata magonjwa ya ateri za moyo na kuongeza uwezekano wa kupata mshtuko wa moyo. Baadhi ya sababu hizi zinazoongeza hatari ya shambulio la moyo zinaweza kudhibitiwa na wakati mwingine haziwezi kudhibitiwa.
 • Sababu kubwa zinazoongeza hatari ya shambulio la moyo zinazoweza kudhibitiwa ni pamoja na:   
  • Kuvuta sigara
  • Shinikizo la juu la damu
  • Kiwango kikubwa cha mafuta (Cholesterol) kwenye damu
  • Kupunguza uzito na kitambi
  • Kutofanya mazoezi
  •  Kisukari
 • Sababu kubwa zinazoongeza hatari ya kupata shambulio la moyo zisizoweza kudhibitiwa ni pamoja na:
  • Umri: Hatari ya kupata shambulio huongezeka mara dufu kwa wanaume wenye miaka zaidi ya 45 na kwa wanawake wenye umri  wa miaka zaidi ya 55 (au baada ya kukatika kwa damu ya hedhi).
  • Kuwepo kwa historia ya kupata magonjwa ya ateri za moyo kwenye familia ya mtu kunaongeza maradufu hatari ya kupata mshtuko,hatari huongezeka zaidi kama baba au kaka yako aligundulika kuwa na ugonjwa wa ateri za moyo kabla ya miaka 55,au ikiwa mama au dada yako amegunduliwa kuwa na ugonjwa wa ateri za moyo kabla ya miaka 65.

Mambo fulani yanayoongeza hatari ya kupata ugonjwa wa ateri za moyo yanaweza kujitokeza kwa pamoja. Kwa ujumla, mtu mwenye mambo mawili au zaidi yanayoongeza hatari ya kupata magonjwa ya ateri huwa kwenye hatari mara mbili ya kupata mshtuko wa moyo na mara tano zaidi kupata ugonjwa wa kisukari.

Utambuzi kuwa una shambulio la moyo

Utambuzi wa shambulizi la moyo unategemea dalili, historia binafsi ,historia ya familia, na matokeo ya vipimo vya uchunguzi vitakavyofanyika.

 • EKG (Electrocardiogram):

Kipimo hiki hutambua na kurekodi shughuli za umeme katika moyo. Baadhi ya mabadiliko katika mawimbi ya umeme kwenye EKG ni ushahidi thabiti washambulizi la moyo. EKG pia inaweza kuonesha kama una mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida.

 • Vipimo vya damu:

Wakati wa shambulizi la moyo, seli za misuli ya moyo hufa na kupasuka, na kumwaga protini fulani katika damu. Vipimo vya damu hufanyika kupima kiasi cha protini hizi katika damu. Viwango vya juu kuliko kawaida vya protini hizi katika damu ni ushahidi wa shambulio la moyo.

 • Baadhi ya vipimo vya damu vinavyofanyika ni pamoja na:
  • Vipimo vya Troponin,
  • Uchunguzi wa CK au CK-MB
  • Viwango vya myoglobin ya Seramu katika damu.

Vipimo vya damu mara nyingi hurudiwa mara kwa mara ili kuchunguza mabadiliko ya vipimo kadri muda unavyoenda.   

 • Coronary Angiography:
  Coronary Angiography ni kipimo maalum cha x-ray ya moyo na mishipa ya damu. Mara nyingi hufanyika wakati wa shambulizi la moyo ili kusaidia kujua kwa uhakika mahali/sehemu ya mishipa ya damu ya moyo iliyoziba.
  Wakati wa kufanya Coronary angiography,daktari hupitisha catheter (bomba nyembamba) kwenye ateri ya mkono wako au ateri ya kwenye paja la mguu ,na kisha kuisukuma catheter taratibu,akifuatisha mfumo wa mzunguko wa damu mpaka catheter itakapofika kwenye moyo.baada ya catheter kufika kwenye moyo rangi maalumu inayoweza kuonekana kwa x-ray huwekwa ndani ya damu kupitia ncha ya catheter,rangi hii husafiri katika ateri na veni za moyo,na humpatia fursa daktari kujifunza/kuchunguza mtiririko wa damu katika moyo na mishipa yake.

Wakati gani utafute matibabu haraka?

Unapaswa kutafuta huduma za matibabu ikiwa unapata maumivu ya kifua au unajisikia vibaya kifuani, kwenye mkono mmoja au mikono yote miwili, mgongo, shingo, taya, au tumbo, kupata shida kupumua, kichefuchefu, kutapika au kupata kijasho chembamba.

Uchaguzi wa matibabu.

 • Matibabu fulani huanza mara moja ikiwa kuna wasiwasi wa kuwepo shambulizi la moyo, hata kabla utambuzi huo haujathibitishwa.
 • Matibabu haya ni pamoja na:
  • Aspirin ili kuzuia damu kuganda zaidi.
  • Okisijeni
  • Nitroglycerin, huupunguzia mzigo moyo na kuboresha mtiririko wa damu damu kwenye mishipa ya moyo.
  • Matibabu ya maumivu ya kifua
 • Mara baada ya ugunduzi wa shambulio la moyo kuthibitishwa au kama kuna sababu za kuelemea zinazoashiria kuwa ni mshtuko wa moyo, matibabu ya kujaribu kurejesha mtiririko wa damu kwenye moyo huanza haraka iwezekanavyo.

Madawa:

Aina mbalimbali za madawa zinaweza kutumiwa kutibu mashambulizi ya moyo.Madawa hayo ni pamoja.

Thrombolytic medicines: Dawa hizi hutumiwa kuyeyusha madonge ya damu yaliyoganda na kuzuia mtiririko wa damu katika mishipa ya damu ya moyo. Dawa hizi zinapaswa kutolewa ndani ya saa 1 baada ya dalili za shambulio la moyo kuanza.

Beta Blockers: Dawa hizi hupunguza mzigo na kurekebisha mapigo ya moyo. Beta blockers hupunguza maumivu ya kifua na kusaidia kuzuia shambulio lingine.

Angiotensin-Converting Enzyme inhibitors: Madawa haya hupunguza shinikizo la juu la damu na kupunguza mgandamizo katika moyo wako. Pia husaidia kupunguza kudhoofika zaidi kwa misuli ya moyo.

Anticoagulants: Madawa haya husababisha damu  kuwa nyepesi na kupunguza uwezekano wa damu kuganda katika ateri za moyo.

Antitiplatelet medicines: Dawa hizi (kama vile aspirin na clopidogrel)huzuia damu kuganda kwenye ateri za moyo kwa kuzuia chembe sahani (aina ya seli ya damu) kuungana na kusababisha madonge ya damu.

Madawa mengine: Dawa zingine zinaweza pia kutolewa ili kupunguza maumivu na wasiwasi, na kutibu arrhythmias (mapigo ya moyo yasiyo sawa), ambayo mara nyingi hutokea wakati wa shambulizi la moyo.

Utaratibu wa kimatibabu:

Ikiwa dawa pekee haiwezi kuzuia shambulio la moyo, taratibu za kimatibabu- upasuaji au zisizo za upasuaji-zinaweza kutumika. Taratibu hizi ni pamoja na.

Angioplasty: Utaratibu huu unaweza kutumika kufungua/kuzibua mishipa ya damu ya moyo Wakati wa kufanya angioplasty, catheter (bomba nyembamba) yenye puto mwishoni, huingizwa  kwenye mshipa wa damu wa mkononi au pajani na kisha kusukumwa mpaka kuifikia sehemu ya mshipa wa moyo iliyoziba. Kisha,puto hupulizwa na kuukandamizia utando uliouziba mshipa ukutani mwa ateri ili kuruhusu damu kutiririka tena.

Kipindi cha angioplasty, kimrija kidogo(stent) hubakizwa kwenye sehemu ya mshipa iliyotanuliwa ili kuzuia kuziba tena.

CoronaryArtery Bypass Grafting: Ni upasuaji unaohusisha kuchukua ateri au veni toka sehemu moja ya mwili na kuipandikiza katika sehemu ya moyo ambayo mishipa yake imeziba ,hii husaidia kurudisha mtiririko wa damu kupitia njia nyingine baada ya ile ya mwanzo kuziba.

Matibabu baada ya kutoka hospitalini

Watu wengi hutumia siku kadhaa hospitalini baada ya shambulizi la moyo. Unapoondoka hospitalini, matibabu hayakomi. Nyumbani, matibabu yako yanaweza kuwa madawa ya kila siku na ukarabati wa moyo (rehab). Daktari anaweza kupendekeza mabadiliko ya mfumo wa maisha, kama kuacha uvutaji wa sigara, kupunguza uzito, kubadilisha mlo , na kuongeza mazoezi ya mwili, ili kupunguza uwezekano wa kupata shambulio jingine la moyo

Cardiac Rehabilitation(Ukarabati wa moyo):

Daktari anaweza kuagiza ufanye ukarabati wa moyo ili kukusaidia kupona na kupunguza uwezakano wa kupata shambulio jingine. Karibu kila mtu aliyepata shambulizi la moyo anaweza kufaidika na ukarabati wa moyo. Moyo umeundwa kwa misuli, na mazoezi sahihi huuimarisha.

Ukarabati wa moyo,hauhusishi mazoezi tu,pia hujumuisha elimu, ushauri, na kujifunza jinsi ya kupunguza hatari ya kupata shambulio jingine. Rehab itakusaidia kujifunza njia bora ya kujitunza baada ya shambulizi la moyo.

Timu ya ukarabati wa moyo inaweza kujumuisha madaktari (daktari wa familia, daktari bingwa wa moyo, na / au upasuaji), wauguzi,wataalamu wa mazoezi, wataalam wa mwili na kazi, wataalamu wa mlo, na wanasaikolojia au wataalamu wengine wa tabia na mwenendo.

Madawa ya kuepuka kama una shambulio la moyo

Wagonjwa waliogundulika kuwa wamepata shambulio la moyo,wanapaswa kuepuka madawa yafuatayo;

 • Aliskiren
 • Anti-inhibitor coagulant complex
 • Eletriptan
 • Ethynodiol diacetate and ethinyl estradiol
 • Fingolimod
 • Gilenya
 • Sitagliptin And Metformin Hydrochloride
 • Levothyroxine
 • Frovatriptan

Ikiwa umegunduliwa kuwa umepata mshtuko wa moyo, wasiliana na daktari kabla ya kuanza au kuacha dawa yoyote.

Magonjwa yenye dalili zinazofanana na mshtuko wa moyo

Dalili za shambulizi la moyo zinaweza kuchanganywa na hali zifuatazo[1]:

 • Kuvimbiwa
 • Gastric reflux (tumbo kupwa)
 • Anxiety attack (Mshtuko/Shambulio la wasiwasi)
 • Panic attack (Mshtuko/shambulio la hofu )
 • Panic disorder (Ugonjwa wa hofu)
 • Nimonia
 • Bronchitis (mkamba-ugonjwa wa kuvimba koo)
 • Kiungulia

Jinsi ya kuzuia mshtuko wa moyo

 • Kupunguza hatari ya kupata ugonjwa wa mishipa ya damu ya moyo (coronary artery disease (CAD)) inaweza kusaidia kuzuia shambulio la moyo. Hata kama tayari una CAD, bado unaweza kuchukua hatua za kupunguza hatari yako ya kupata shambulio la moyo.

Uchaguzi wa mtindo wa maisha:

Kupunguza hatari ya shambulio la moyo humaanisha kufanya uchaguzi wa afya bora.

Uchaguzi bora wa mtindo wa maisha hujumuisha:

 • Kupunguza mafuta na chumvi kwenye mlo na kuongeza matunda na mboga mboga. Mabadiliko haya yanaweza kusaidia kupunguza shinikizo la damu na mafuta kwenye damu.
 • Kupunguza uzito.
 •  Kuacha uvutaji sigara.
 • Kufanya mazoezi ya mwili huimarisha misuli ya moyo. Muulize daktari wako kiasi gani na aina gani ya mazoezi, moyo na mwili unaweza kuhimili.

Tibu hali na magonjwa yanayohusiana na shambulio la moyo:

Mbali na kufanya mabadiliko ya mtindo wa maisha, unaweza kusaidia kuzuia shambulizi la moyo kwa kutibu hali ambazo zinaongeza uwezekano wa shambulio la moyo:

 • Kiwango kikubwa cha mafuta (cholestrol) katika damu. Unaweza kuhitaji dawa ili kupunguza cholesterol ikiwa chakula na mazoezi havitoshi.
 • Shinikizo la juu la damu:Unaweza kuhitaji dawa ili kudhibiti shinikizo la damu.
 • Ugonjwa wa kisukari: Ikiwa una ugonjwa wa kisukari, unatakiwa kudhibiti viwango vya sukari katika damu kwa njia ya chakula ,mazoezi na kama itahitajika tumia dawa kama unavyoagizwa na daktari.

Kuwa na mpango wa dharura:

Hakikisha kuwa una mpango wa dharura, ikiwa wewe au mtu mwingine katika familia yako atapata shambulio la moyo. Hii ni muhimu hasa ikiwa uko katika hatari kubwa au tayari umeshawahi kupata shambulizi la moyo.

Ongea na daktari wako kuhusu ishara na dalili za shambulizi la moyo, na hatua ambazo unaweza kuchukua wakati unasubiri msaada.

Nitarajie nini baada ya kupata mshtuko wa moyo?

Kila mwaka, watu milioni 1.1 nchini Marekani hupata shambulizi la moyo, na karibu nusu yao hufa. Magonjwa yanayoathiri ateri za moyo, mara nyingi husababisha shambulizi la moyo na huongoza kwa kusababisha vifo kwa wanaume na wanawake nchini Marekani.

Watu wengi zaidi wanaweza kupona baada ya shambulizi la moyo ikiwa watapata msaada haraka. Kati ya watu ambao hufa kutokana na shambulizi la moyo, karibu nusu yao hufa ndani ya saa moja baada ya dalili kuanza na kabla ya kufika hospitalini.

References

 1. “Misdiagnosis of Heart attack”.
 • Shirikisha:

Leave Your Comment